ZIARA YA MWANASHERIA MKUU TUNDU LISSU (MB) ULAYA NA MAREKANI Mwanasheria Mkuu wa Chama Mhe. Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili za Ulaya na Marekani kuanzia Jumatatu, Januari ...
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) tumepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za tukio la shambulizi linalohusishwa na ugaidi, lililofanyika kwenye eneo lenye shughuli mbalimbali za kijamii, katika Hoteli ya DusitD2, Nairobi, nchini Kenya, siku ya Jumanne, Januari 15, mwaka huu.
Kipekee Chadema inatuma salaam za pole kwa watu wote walioathiriwa na tukio hilo, kwa kupoteza maisha ya wapendwa wao na wengine waliojeruhiwa. Tunawatakia majeruhi wote uponaji wa haraka.
Halikadhalika tunatoa pole kwa Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Wananchi wa Kenya, katika wakati huu mgumu wa kukabiliana na tukio hilo ambalo taarifa za awali pia zinasema kuwa limegharimu maisha na uhai wa raia wa mataifa mengine waliokuwa eneo hilo lilipofanyika shambulizi.
Hivyo tunatoa pia pole kwa mataifa na mashirika ya ndani na nje ya nchi yaliyoguswa na tukio hilo baya.
Tunalaani vikali tukio hilo na wote waliohusika kuliandaa na kulitekeleza. Ni tukio jingine la kikatili dhidi ya binadamu na aibu kubwa kubwa kutokea katika ardhi ya nchi za Afrika Mashariki, likihusishwa na mikakati ya kigaidi. Hii haiwezi kuwa namna sahihi na bora ya kutatua matatizo ya kisiasa, kiuchumi au kijamii tuliyonayo katika nchi zetu za Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla.
Aidha, kupitia taarifa hii, Chadema tunaitaka Serikali ya Tanzania, kupitia Ubalozi wetu nchini Kenya kufuatilia kwa makini iwapo kuna Watanzania walioathirika katika tukio hilo la jana na kutoa msaada kadri inavyohitajika, huku pia tukizikumbusha mamlaka zinazohusika nchini kwetu kuchukua tahadhari zinazotakiwa na kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao muda wote.
Tunatoa pia rai kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika utangamano wake kuendeleza juhudi za kuimarisha usalama katika ukanda huu.
*Imetolewa leo Jumatano, Januari 16, 2019 na;*
*Tumaini Makene*
*Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano*
*Chadema*