ZIARA YA MWANASHERIA MKUU TUNDU LISSU (MB) ULAYA NA MAREKANI Mwanasheria Mkuu wa Chama Mhe. Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili za Ulaya na Marekani kuanzia Jumatatu, Januari ...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KWA KAULI YA DKT. MWAKYEMBE, SERIKALI IONESHE MFANO ISIFUNGIE TENA CHOMBO CHA HABARI
Kupitia kwa Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa, Dkt. Harrison Mwakyembe leo bungeni, serikali ya awamu ya tano imedhihirisha wazi imekuwa na ‘ndimi mbili’ (double standards) katika maamuzi yake ya kuvifungia vyombo vya habari nchini, jambo ambalo linaashiria kuwa uamuzi huo umekuwa ukisukumwa na dhamira ya kuvionea baadhi ya vyombo hivyo na kukandamiza uhuru wa habari na maoni nchini.
Akijibu hoja za baadhi ya wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Waziri Mwakyembe amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa wale wote wanaochukizwa na magazeti yanayochochea ukabila na udini kupitia habari zake, waende kushtaki mahakamani na wizara yake itakuwa shahidi nambari moja.
Katika majibu yake hayo, Waziri Mwakyembe ameenda mbali zaidi na kuyataja kwa majina magazeti mawili ya Tanzanite na Jamvi la Habari, yaliyotolewa mfano na baadhi ya wabunge, ambayo pia kwa siku za hivi karibuni yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa habari, kuwa mbali ya kutozingatia maadili na weledi wa uandishi wa habari, yamekuwa yakiandika habari zenye kuibua hisia na kuchochea uhasama wa ukabila na udini ndani ya jamii ya Watanzania.
Tungependa Waziri Mwakyembe awaambie Watanzania kama inajua umuhimu wa mahakama katika kuamua masuala ya namna hiyo, kwanini siku zote Serikali imekuwa ikichukua hatua ya kufungia vyombo vya habari kinyume cha sheria, hata pale ambapo yenyewe ndiyo inakuwa mlalamikaji na haijawahi kwenda mahakamani kushtaki dhidi ya madai ya namna hiyo hiyo na wizara yake ingelikuwa shahidi nambari moja?
Waziri Mwakyembe anajua kuwa hatua hiyo ya Serikali kufungia vyombo vya habari imekuwa ikikiuka misingi ya utoaji haki, kwa sababu Serikali imekuwa ikijigeuza mlalamikaji, polisi (mkamataji), mwendesha mashtaka, jaji (wa kesi yake mwenyewe) na kisha magereza.
Kama hiyo haitoshi, waziri huyo anajua vyema kuwa hata Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, ambayo waziri huyo ameshaitumia vibaya mara kadhaa sasa, kuyaweka vifungoni magazeti, haimpatii mamlaka ya kuchukua hatua kama hiyo.
Kutokana na majibu hayo yaliyotolewa leo bungeni, tunatarajia kuwa kuanzia sasa Serikali itaacha mara moja kujichukulia sheria mkononi kwa kufungia vyombo vya habari kwa madai ya uchochezi, uongo, uzushi, kumsingizia Rais na badala yake itakuwa ikienda mahakamani kufungua mashtaka ili sheria ichukue mkondo wake kwa usahihi. Au kwa chombo kingine huru kinachoweza kushughulikia kesi za namna hiyo kwa kadri ya taratibu zilizowekwa. Jambo ambalo limekuwa ni rai ya wadau wa habari kwa muda mrefu ili Serikali iache kuwa jaji wa kesi zake yenyewe.
Vinginevyo, majibu ya Waziri Mwakyembe yatatafsiriwa kuwa ilikuwa ni namna ya kukwepa kuchukua hatua dhidi ya uandishi hatari wa magazeti hayo, hivyo kuhalalisha tuhuma zilizopo kuwa baadhi ya mamlaka na vyombo vya Serikali vina ‘mikono’ yake katika habari hizo, zikiyatumia kwa mikakati hatarishi na michafu dhidi ya wakosoaji wa Serikali.
Tukiwa wadau wa habari, uhuru wa habari na uhariri unaozingatia uwajibikaji kwa jamii, tukiwa taasisi pekee ya kisiasa iliyotia saini Tamko la Dar es Salaam Kuhusu Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji, tunasisitiza kuwa Serikali kama mdau wa habari isitumie tena mamlaka yake vibaya kufungia vyombo vya habari bali ioneshe njia kama ilivyo kauli yake iliyotolewa leo.
Ni rai yetu pia kuwa vyombo vya habari nchini vitaendelea kuzingatia maadili na weledi wa taaluma hiyo adhimu, katika shughuli zao za kila siku, wakiweka mbele haki na wajibu kwa jamii wanayoitumikia.
Imetolewa leo Jumanne, Juni 26, 2018 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA