ZIARA YA MWANASHERIA MKUU TUNDU LISSU (MB) ULAYA NA MAREKANI Mwanasheria Mkuu wa Chama Mhe. Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili za Ulaya na Marekani kuanzia Jumatatu, Januari ...
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO MHE. DAVID SILINDE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
_______________
Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee, naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali, kwa Mwaka wa Fedha 2018/19
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuwalinda viongozi wa Upinzani katika ngazi mbalimbali nchini na kuwaepusha na hila mbaya za ibilisi, na pia kwa kuwatia nguvu na ujasiri wa kukabiliana na dhoruba mbalimbali zinazowakabili katika juhudi zao za kutetea haki za wanyonge wa taifa hili.
Mheshimiwa Spika, pili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwashukuru na kuwapongeza sana viongozi wote wa CHADEMA pamoja na viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA kwa ujasiri wao wa kuendelea kuchapa kazi bila woga licha ya mazingira magumu ya kufanya siasa hapa nchini. Aidha, Kambi Rasmi inawatia moyo wale wote waliokamatwa na kutiwa magerezani; walioumizwa na kujeruhiwa kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki shughuli za kisiasa. Tunapenda kuwaambia wasikate tamaa kwani mateso wanayoyapata sasa ni kielelezo cha ukombozi wa watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia hadhara hii kwa niaba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo; kuwashukuru sana wananchi wote walioguswa na tukio la kushambuliwa kwa kupigwa risasa kwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Tundu Lissu na kumwombea pamoja na kutoa michango yao ya hali na mali katika jitihada za kuokoa maisha yake. Napenda kuwahakikishia kuwa michango yao ilitumika vizuri; na dua zao zilipokelewa na Mwenyezi Mungu; na ndio maana kwa neema zake Mwenyezi, Mheshimiwa Lissu ni mzima na anaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda pia kuchukua nafasi hii kutoa pole nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa viongozi wa vyama vya upinzani na wananchi wote kwa ujumla kwa kuondokewa na ndugu zao waliouwawa wakitekeleza majukumu yao. Kipekee tunamkumbuka Marehemu Daniel John, Katibu wa CHADEMA – Kata ya Hananasifu katika Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam; aliyeuwawa kinyama kwa kunyongwa na kupigwa kichwani na vitu vyenye ncha kali; Marehemu Akwilina Akwilini, Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Dar es Salaam; aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati polisi wakisambaratisha mkutano halali wa kampeni za uchaguzi wa marudio wa Ubunge katika jimbo la Kinondoni – Dar es Salaam. Ikumbukwe kwamba mwanafunzi huyu hata hakuwa sehemu ya mkutano, bali alikuwa akisafiri katika daladala. Tunamkumbuka pia marehemu Godfrey Lwena, Diwani wa Kata ya Namawala katika Jimbo la Mlimba – Wilaya ya Kilombero huko Morogoro; aliyeuwawa kikatili na watu wasiojulikana. Aidha, tunamkumbuka marehemu Aramu Kaigwe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi –Kata ya Nyarugusu katika Jimbo la Kasulu Vijijini mkoani Kigoma, aliyeuwawa kikatili kwa kukatwa katwa mapanga na watu wasiojulikana. Mauaji yote haya yametokea kati ya Feburuari na Machi mwaka huu wa 2018.
Mheshimiwa Spika, Tanzania iliyosifika duniani kote kama kisiwa cha amani ndiko ilikofika sasa – ambapo viongozi wa upinzani wanauwawa kinyama kila uchwao; wanafunguliwa kesi za ugaidi na mkakati ulioko sasa ni kuwafungulia kesi za uhaini ili wanyongwe; watu wanazidi kutekwa; maiti zinazidi kuokotwa fukweni na mitoni; vyama vya siasa vinatishiwa kufutwa na msajili nk.
Mheshimiwa Spika, mwenendo huu sio mzuri hata kidogo. Taifa limechafuka damu ya watu wasio na hatia; na ardhi ya Tanzania imelaanika kwa kumwagikiwa na damu ya watu wasio na hatia. Natoa wito kwa Serikali, kutafakari jambo hili kwa makini na kuchukua hatua ya kurejesha tena imani iliyopotea kwa wananchi na Jumuiya ya Kimataifa; kwamba; Tanzania bado ni sehemu salama ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa nitoe maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Mheshimiwa Spika,tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikiwasilisha bajeti isiyotekelezeka jambo ambaolo linaifanya bajeti hiyo kuwa BAJETI HEWA.
Mheshimiwa Spika, nitatoa sababu za Bajeti Hewa:-Sababu ya kwanza ya Bajeti kuwa hewa: ni kuweka makisio makubwa ya makusanyo ya fedha; na kushindwa kukusanya kiasi hicho. Kile kiasi kilichoshindikana kukusanya kinakuwa ni makusanyo hewa. Kwa mfano:-
Mheshimiwa Spika, Sababu ya pili ya Bajeti kuwa hewa; ni kutotekeleza kikamilifu bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika sekta mbalimbali. Nitatoa mifano katika wizara tatu zinazogusa maisha ya watu wengi moja kwa moja kwa miaka miwili (2016/17 na 2017/18):-
Mheshimiwa Spika, Sababu ya tatu inayoifanya Bajeti ya Serikali kuwa Hewa ni Utovu wa Nidhamu ya Matumizi ya Fedha kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 na Sheria ya Fedha.Kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 41(1) ni kwamba; Ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya Serikali “Serikali itatakiwa kuwasilisha Bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa”. Aidha, utaratibu huu unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma wa mwaka 2001( Public Finacne Act, 2001)ambapo kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka Serikali kuleta Bungeni bajeti ya nyongeza (mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huo wa kisheria umekuwa ukivunjwa na Serikali kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge jambo ambalo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali; lakini pia kunatoa mwanya uwa wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Ikiwa matumizi yanafanyika nje ya bajeti; bajeti ya namna hiyo inakuwa hewa kwa kuwa haina Baraka za Bunge.
Mheshimiwa Spika, upotevu wa fedha wa shilingi trilioni 1.5 uliobainika na CAG yamkini unatokana na matumizi ya fedha kiholela yanayofanywa na Serikali bila kuidhinishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, ipo mifano mingi ya mtumizi ya Serikali yaliyofanywa nje ya Bajeti iliyodhinishwa na Bunge. Mifano hiyo ni pamoja na:-
Aidha, zipo Wizara zilizopewa fedha zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali kwenye Kamati ya Bajeti ya Bunge kuhusu matumizi ya serikali kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 na mwelekeo hadi juni 2018 inaonyesha kwamba baadhi ya wizara zilipatiwa fedha zaidi ya bajeti iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Matumizi yote haya ambayo hayakujumuishwa kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Bunge yanaifanya Bajeti ya Serikali kuwa hewa kwa kuwa haizingatiwi katika kufanya matumizi.
Mheshimiwa Spika, nimetoa mifano hiyo michache lakini ukifanya uchambuzi wa fedha za maendeleo zilizoidhinishwa kutekeleza miradi mbalimbali utakuta kwamba zaidi ya asilimia 60 ya fedha hizo hazikutolewa; na kwa maana hiyo zilikuwa ni fedha ewa. Kwa mantiki hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuota maelezo mbele ya Bunge hili; ni kwa nini inawahadaa wananchi kwa kutoa makisio makubwa ya bajeti ambayo kwa mika mitatu mfululizo imekuwa ikishindwa kuyafikia? Aidha, ni kwani nini inashindwa kutekeleza bajeti iliyoidhinishwa na Bunge; na wakati huo huo inafanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge kutekeleza shughuli ambazo hazipo katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa?
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Fedha anawasilisha mapendekezo ya bajeti ya serikali hapa Bungeni alisoma kwa mbwembwe nyingi mambo kumi aliyoyaita kuwa ni mafanikio katika utawala wa Rais John Pombe Magufuli ndani ya miaka miwili na nusu toka aingie madarakani. Pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kusisitiza kuwa na taasisi imara kwa ajili maendeleo endelevu ya nchi yetu, ni aibu kwa Waziri wa Fedha kutumia muda mrefu kumsifu mtu mmoja na kudhani kuwa yeye binafsi ndiye anaweza kuijenga nchi na kuipeleka mbele kimaendeleo! Anajidanganya!
Mheshimiwa Spika, ni lazima tufike kwamba serikali na nchi hii sio mali ya Rais Magufuli, ni lazima tujenge na kuimarisha taasisi imara ikiwemo Bunge kwa ajili ya kuisimamia serikali kwa ustawi wa nchi yetu. Hizi kauli za “Serikali ya Magufuli” ni kumtukuza mtu na kamwe hiyo haiwezi kuwa dira ya taifa letu. Lazima ieleweke kuwa – Rais hayupo juu ya Sheria; na anawajibika kwa wananchi. Cheo alichopewa ni dhamana tu!
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 8 (1) inasema kwamba; “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo-
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii
(b)lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi
(d)wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.”
Mheshimiwa Spika, nimenukuu ibara hiyo Katiba ili Waziri wa Fedha ajue kuwa Serikali inapata mamlaka yake kwa wananchi na sio kutoka kwa mtu binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Waziri wa Fedha alieleza mambo 10 aliyoyaita mafanikio ya “Serikali ya Rais Magufuli” naomba kueleza mambo mabaya ishirini (20) ambayo Serikali hii imeyafanya kwa kipindi cha miaka miwili na nusu tangu iingie madarakani ambayo yameirudisha nchi hii nyuma kiuchumi, kisiasa, na kijamii kuliko wakati wowote tangu uhuru. Kimsingi mambo hayo yameturudisha katika enzi za ujima – kipindi ambacho hakukuwa na ustaarabu wowote katika maisha ya mwanadamu. Mambo hayo mabaya ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ni katika utawala huu wa Rais Magufuli ambapo Serikali yake ilipiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa matangazo ya mijadala ya Bunge kupitia Runinga na Redio kwa kigezo dhaifu kwamba wananchi hawapati nafasi ya kufanya kazi wanaangalia tu mijadala Bungeni. Aidha sababu nyingine nyepesi iliyotolewa kuhalalisha marufuku hiyo ni gharama kubwa kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja. Pamoja na kuwa Bunge ni chombo kinachowawakilisha wananchi, wananchi wamenyimwa fursa na utawala huu ya kuona moja kwa moja kazi zinazofanywa na wawakilishi wao Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Hata pale baadhi ya wadau walipotoa nafasi ya kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kwa gharama zao walizuiwa. Lakini cha ajabu shughuli anazofanya Rais hata za kukata utepe wa kuzindua mradi wowote zimekuwa zikipata live coverage kwa vituo karibu vyote vya redio na televisheni kana kwamba hakuna gharama zozote zinazotumika kurusha live kazi zake. Kinachoonekana hapa ni ubinafsi wa kutaka aonekane yeye tu; na kuwaziba watanzania wasione upande mwingine wa shilingi. Huku ni kuirudisha nchi kwenye ujima ambapo habari na matukio katika nchi hayakuwa mambo ya msingi kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia isiyokuwa na dini na yenye mfumo wa Vyama vingi vya Siasa. Kupitia Bunge hili ilitungwa Sheria namba 5 ya mwaka 1992 ambayo inatoa haki kwa vyama vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli nyingine za kisiasa.
Mheshimiwa Spika, ni katika awamu ya tano chini ya Rais Magufuli utaratibu huo umepigwa marufuku kinyume na matakwa ya Katiba na Sheria za nchi.
Mheshimiwa Spika, ni katika awamu ya tano ambapo tumeshuhudia kuporomoka kwa kasi kwa uhuru wa kutoa na kupokea habari ambapo Sheria ya Makosa ya Mtandao pamoja na Sheria ya huduma za habari kutumika kama mkuki na ngao kuminya uhuru wa habari ikiwa ni pamoja na kufungia magazeti, kuzipa adhabu idhaa za radio mbalimbali pamoja na Televisheni.
Mheshimiwa Spika, idadi kubwa ya vijana hasa wa upinzani kupewa kesi za makosa ya mtandao kwa sababu tu ya kutumia uhuru wao kupaza sauti pale wanapoona serikali haifanyi masuala kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na sheria.
Mheshimiwa Spika, zipo shughuli nyingi ambazo zinatekelezwa na serikali ambazo hazikuwa kwenye Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako tukufu ikiwemo ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Chato, Kuhamia Dodoma, Ujenzi wa Hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam n.k. yanaweza kuonekana kuwa mambo mema lakini ni lazima kama nchi tukubaliane kuwa upo utaratibu ambao umekubalika na unaotakiwa kufuatwa.
Mheshimiwa Spika, ni katika utawala huu wa Rais Magufuli ambapo tumeona ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu unaofanywa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini, mathalani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alias Daudi Albert Bashite kuvamia kituo cha Televisheni cha Clouds akiwa na ulinzi wa vyombo vya dola na hakuna chochote kilichofanyika dhidi yake, Mkuu huyo huyo wa Mkoa kutangaza moja kwa moja watuhumiwa madawa ya kulevya bila kufuata mfumo wa kisheria, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti kusema kuwa hawezi kufanya kazi na Madiwani wa Upinzani, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kuvamia na kuharibu mashamba ya Mheshimiwa Freeman Mbowe pamoja na kumuadhibu Mwalimu kwa kushindwa kujua jina lake, Wakuu wa Wilaya cum Mikoa kudharau na kuwadhalilisha Wabunge. Haya yote yanafanywa bila wasiwasi na viongozi wa serikali wanaona kawaida.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa Katiba ulitumia fedha nyingi za wananchi pamoja na kuwa uligubikwa na mapungufu makubwa lakini ni katika utawala huu Rais ametangaza kwa umma kuwa ananyoosha nchi na hivyo Katiba si kipaumbele chake. Kambi ya Upinzani inahoji kama nchi inanyooshwa kwa Katiba au matakwa ya mtu binafsi?
Mheshimiwa Spika, katika utawala huu tumeshuhudia misingi ya kidiplomasia ambayo tulijiwekea kukiukwa ikiwemo msimamo wa Tanzania kusimama na kuzitetea nchi au watu ambao wanaonewa na mataifa au watu wengine. Mathalani leo Morocco ni marafiki zetu huku tukijua mpaka leo inaikalia kimabavu Sahara Magharibi, leo tumefungua Ubalozi Israeli huku tukijua toka enzi za Mwalimu tulisimama kuwatetea Wapalestina.
Mheshimiwa Spika, Watanzania katika maeneo mbalimbali hawana uhakika na kesho yao kwa sababu ya kuongezeka kwa matukio ya watu waliovikwa kilemba cha “watu wasiojulikana” ambao wamekuwa wakiendesha mauaji na utekaji na kuwapiga risasi wale ambao wanaikosoa serikali hii. Kuongezeka kwa matukio ya mauaji, utesaji na utekaji ni ishara kuwa nchi ina hali mbaya kiusalama.
Mheshimiwa Spika, kutotabirika kwa mifumo ya kodi, utendaji mbovu wa TRA na kuigeuza TRA kama polisi kukusanya mapato kimabavu kumefanya biashara nyingi kufungwa ndani ya utawala huu na kukosa vyanzo muhimu vya mapato.
Mheshimiwa Spika, hakuna asiyejua kuwa sekta ya benki na fedha imeyumba katika utawala huu ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chechefu (non-performing loans) jambo linaloashiria kuwa uchumi wa nchi unadumaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kujinasibu kuwa Tanzania ya Viwanda, taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa nchi imeporomoka vibaya kwenye masuala ya uwekezaji nchini. Na sababu kubwa ni hofu kutokana na hali ya kisiasa nchini kutotabirika. Nchi imekuwa inaongozwa kwa matamko ya kisiasa zaidi kuliko sheria. Hivyo wawekezaji wanaogopa kuwekeza mitaji yao kutoakana nan chi kuendeshwa kwa amri za rais bila kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Spika, ni katika utawala huu ambao tumeona watumishi wa umma wakitukanwa hadharani na kufukuzwa kazi kwenye mikutano ya hadhara kwa kinachitwa “kutumbua majipu” jambo linaloonyesha kuwa sheria za utumishi wa umma na taratibu zake zimewekwa kapuni.
Mheshimiwa Spika, Mahakama imekuwa ikitoa amri kadhaa lakini serikali imekuwa mara kadhaa ikikiuka amri hizo, mathalani amri ya kusitisha bomoabomoa katika barabara ya Morogoro ambapo Wakala wa Barabara aliendelea na zoezi hilo bila kujali amri ya Mahakama, Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kutoa ruzuku kwa kundi la Lipumba bila kujali amri ya kumzuia kufanya hivyo mpaka Mahakama itakapotanzua mgogoro wa Chama hicho.
Mheshimiwa Spika, ni katika kipindi cha utawala huu wa awamu ya tano ambapo Rais alitamka wazi kwamba; Katiba sio kipaumbele chake, ananyoosha nchi kwanza:- Jambo la kujiuliza ni kwamba; ananyoosha nchi akiongozwa na nini? Bila shaka anangozwa na utashi wake mwenyewe. Na kwa kuwa anaongozwa na utashi wake mwenyewe tumeshuhudia akitoa amri na matamko ambayo ni kinyume na Katiba na Sheria. Kwa mfano, amefukuza watu kazi bila kuzingatia sheria ya utumishi wa umma ambayo inatoa haki ya mtuhumiwa kusikilizwa; ameagiza matumizi ya fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina kutekeleza miradi ambayo haipo kwenye mpango wa Taifa wa Maendeleo na pia ametumia fedha hizo bila idhini ya Bunge n.k Mambo yote hayo ni kinyume na utawala bora na kwa maneno mengine ni utawala wa kimabavu – udikteta.
Mheshimiwa Spika napenda watanzania watambue kwamba kama Taifa tumekamilisha Bajeti ya pili ya Utawala wa awamu ya tano chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli. Ni wazi kwamba mwenendo wa Serikali baada ya utekelezaji wa bajeti yake ya kwanza na ya pili unatosha kutoa picha kamili juu ya aina gani ya Uongozi tulionao kama Taifa katika usimamizi wa Uchumi, Siasa na Maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla. Sitegemei kama bado kuna mtanzania anahitaji muda zaidi aweze kutafsiri Uongozi wa sasa.
Mheshimiwa Spika, Nathubutu kusema kwamba Taifa linapita kwenye kipindi kigumu cha utawala wa mtu mmoja, usioheshimu Katiba, Sheria, Taratibu na wala tamaduni zetu kama watanzania. Tunapita kwenye kipindi kigumu cha utawala wa mtu mmoja asiyeamini katika nguvu ya taasisi za dola, Tunapita kwenye Utawala wa mtu mmoja asiyeamini katika Uhuru wa mihimili mingine kwa maana ya Bunge na Mahakama. Kwa kifupi ni utawala wa Kiongozi mmoja aliyejikusanyia mamlaka yote mkononi na mwenye kupenda kila kitu kwenye nchi hii awe yeye. Waingereza wanaita POPULIST LEADERSHIP.
Mheshimiwa Spika, Tabia ya Utawala wa namna hii umechambuliwa vizuri katika Makala ya Mwandishi na Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti Chuo Kikuu cha Central Europe university, Dr Milkoz Harasz kwenye Jarida maarufu duniani la Washington Post la Disemba 28, 2016, ambapo kwa kifupi naomba ninukuu maneno yake kuhusu tabia za populist leaders kwa faida ya Bunge lako na watanzania;
Mheshimiwa Spika, Mwandishi na Mtafiti na Milkoz Harasz, anasema “ “Populists govern by swapping issues as opposed to resolving them. They don’t mind being hated.Their two basic postures of defending and triumphing are impossible to perform without picking enemies.Populist can turn into peace nicks or imperialist depending on what they think could yield good spin that boost their support. Hypocrisy is in the genes of populists, in many countries they betray expectations of selfless strongman nd have lead to civic awekeny”..
Mheshimiwa Spika, Kwa tafsiri isiyo rasmi, Dr Miltoz anasema “ Kiongozi mpenda sifa na mwenye kujikweza hutawala kwa kufunika matatizo ya msingi badala ya kuyatafutia ufumbuzi, watawala hawa hawaoni shida kuchukiwa.Dhamira zao mbili za kulinda utawala wao na kuwashinda wapinzani wao wanaamini hazitafanikiwa bila kutengeneza maadui. Watawala wapenda sifa na wenye kijikweza huweza ama kuwa wahubiri wa Amani ya uongo ama wakawa mabeberu madikteta kutegemea wanachodhani kinaweza kulinda matakwa yao.Unafiki ndio asili yao, hata hivyo katika nchi nyingi watawala wa namna hii hudhihirisha utawala wenye maslahi binafsi, na mwishowe wananchi huwaelewa, huzinduka na kuasi’
Mheshimiwa Spika, Tabia hizo za viongozi wapenda sifa mara nyingi hutumia muda na akili nyingi kuzuia au kukabiliana na wakosoaji ndani na nje ya vyama vyao. Wanaposhindwa kukidhi matarajio waliyoyajenga kwa Umma hugeuka na kutumia mbinu za kikatili kwa mkono wa dola kutawala,na mara nyingi hukanyaga demokrasia na kuvunja katiba kama inavyonekana hapa nchini kwasasa ambapo kama Taifa tunashuhudia utawala wa Rais wetu ukikanyaga Katiba na misingi yake sambamba na kuminya demokrasia kwa hoja za kuleta maendeleo yasiyonekana.
Mheshimiwa Spika, Tawala za namna hii hutumia muda mwingi kutaka umma uamini kwamba demokasia ni kikwazo cha Maendeleo na kwamba Udikteta unaweza kuleta maendeleo (kitu ambacho hakijawahi kuonekana kwenye tafiti yoyote kuhusu maendeleo Tanzania).Ni vema Rais wetu akaelewa na kuamini kwamba tawala anazochukulia mfano zina historia tofauti na Taifa letu, mataifa anayochukulia mfano watawala wake waliingia madarakani kwa mkono wa chuma, na sio sanduku la kura. Ni huzuni kuona Rais aliyetafuta madaraka kwa kuomba kura nchi nzima mpaka anapiga ‘push up’ jukwaani kushawishi achaguliwe leo anatamani kutawala kwa mkono wa chuma. Mwenendo wa mambo kwasasa unabainisha dalili zote za utawala anaozungumzia Dr milkoz Sarasz,
Hivyo, Tusigawanyike kwa misingi ya itikadi za vyama katika vita hii kwani Taifa linaelekea kuparanganyika tusiposimama na kukataa kwa sauti moja. Lazma wanasiasa, viongozi wa dini, wafanyabiashara, wanazuoni, wakulima na wafanyakazi wote kwa pamoja tusimame kama watanzania kupinga Taifa hili zuri kupelekwa kusikojulikana ambako Demokrasia inaelekezwa kuzimu, biashara zinapukutika, ukata unazidi na watanzania wanazidi kuzama kwenye lindi la umasikini na hofu ya dhidi ya utawala wao.
Mheshimiwa Spika, Haya ni maisha ambayo watanzania hawakutarajia, na hii ndio changamoto kuu kwa Bunge hili lenye dhamana ya mwisho kuhusu mustakabali wa Taifa hili kikatiba. (Parliament is the supreme organ of the state).
Mheshimiwa Spika, Ni jambo lisilobishaniwa tena kuhusu kuongezeka kwa ukali wa maisha kwa kila mtanzania. Kwa muda mrefu, Serikali ya CCM imekua ikitumia kigezo cha ukuaji uchumi kupotosha kuhusu hali halisi ya uchumi wa taifa letu. Serikali ya awamu ya tano inatumia dhana ya ukuaji uchumi kwa asilimia 7% kama hoja ya kukaririsha watanzania waamini kwamba hali ya uchumi ni shwari na kwamba kiwango chetu cha ukuaji uchumi ni kikubwa ukilinganisha na nchi washindani wetu hususani Kenya ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 6%.
Mheshimiwa Spika, Kwanza, nivema tukafafanua kwamba uchumi wa Kenya ni zaidi ya dola 65 billioni, hivyo unapokua kwa asilimia6% ni sawa na ongezeko la dola 4 bilioni , wakati uchumi wa Tanzania wa dola 45billion, unapokua kwa asilimia 7% ni sawa na ongezeko la dola 3bilioni. Hii ni tafsiri muhimu sana kujulikana kwa watanzania kwamba kwa mwaka uchumi wa Kenya unaongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko uchumi wetu badala ya kuwadanganya na takwimu za asilimia bila kuzingatia ukubwa wa uchumi wa kila nchi.
Mheshimiwa Spika, ni vema ikaeleweka pia kwamba ukuaji huu wa uchumi kwa asilimia 7% haukuanza leo baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani. Ukuaji huu umekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, kwa maana tangu awamu ya tatu(rejea hotuba ya bajeti ya 2005/06), chini ya Benjamini Mkapa, uchumi ulikua kwa kiwango hicho cha asilimia7%, na ifahamike tu kwamba mwaka 2011, Ukuaji huo ulifikia asilimia 7.9.
Mheshimiwa Spika, Nivema ikafahamika kwamba changamoto tuliyonayo kama taifa kuhusu uchumi sio ukuaji tena, bali namna ya kufanya ukuaji huo utafsiri maisha ya watanzania. Ilitegemewa tangu kuingia awamu ya nne na sasa ya tano, kazi kubwa ingekuwa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unapunguza umasikini, badala yake imekua kinyume chake kwani awamu ya nne imeshindwa kupunguza idadi ya masikini, na mbaya zaidi awamu hii ya tano inafanya vibaya zaidi kuliko awamu ya nne katika mkakati wa kupunguza umasikini kama inavyojipambanua kwenye ripoti mbalimbali za kiuchumi za kimataifa na kitaifa sanjari na hali halisi wanayopitia wananchi kwasasa.
Mheshimiwa Spika, Bado Uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unakuzwa na sekta zilezile, za Utalii, Madini, Huduma ya fedha,Mawasiliano, ambazo kwa hakika zinabeba watu wachache na ndio sababu ya uchumi kuendelea kukua bila kupuguza umasikini.Kwa zaidi ya muongo mmoja, Taasisi maarufu nchini inayohusika na tafiti za kiuchumi ijulikanayo kama Research on Poverty Alleviation(REPOA) imebainisha wazi kwamba ili kupunguza umasikini ni sharti kukuza sekta ya kilimo katika dhana pana(mazao, uvuvi na ufugaji) kwa asilimia 8% mpaka 10%, na kwamba tukikuza Kilimo kwa kiasi hicho kwa miaka mitatu3 mfululizo tutakata umasikini kwa asilimia 50%.
Mheshimiwa Spika, Ni bahati mbaya kwamba tangu awamu ya tatu mpaka awamu ya nne kilimo kiliendelea kukua chini ya asilimia 4% na mbaya zaidi, katika mwaka wa kwanza wa serikali ya wamu ya tano inayojinasibu kama serikali ya masikini, kilimo kimekua kwa asilimia 1.7%, kiwango ambacho ni hafifu kupata kutokea tangu Utawala wa Mkapa na Kikwete.
Mheshimiwa Spika, Ndio sababu Kambi rasmi ya upinzani bungeni tunapenda watanzania watambue kuwa Rais John Pombe Magufuli ni adui wa wakulima wa nchi hii kwa kuwa bajeti yake ya kwanza ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2016/17 ruzuku ya mbolea ilikuwa shilingi billioni10; na katika Bajeti yake ya pili katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali Ilipanga kutumia shilingi billion 15 kama ruzuku ya pembejeo ukilinganisha na shilingi billion 78 ya mwaka wa mwisho wa Kikwete. 2015/16. Na safari hii 2018/19, hali ni mbaya zaidi kwa kuwa hata fedha ya ruzuku ya mbolea haijatajwa kwenye randama ya Wizara ya Kilimo. Ni vema ikaeleweka kwamba moja ya tatizo kubwa katika sekta ya kilimo Tanzania ni matumizi duni ya mbolea kwani imesisitizwa kwenye ripoti mbalimbali za tafiti za uchumi na kilimo.Kwa mujibu wa Ripoti ya Umasikini na Maendeleo ya Binadamu 2014(Poverty and Human Development 2014), Matumizi ya Mbolea Tanzania ilikuwa ni 9kg kwa ekari1 wakati nchi zenye chumi ndogo kama Malawi, wakulima wamewezeshwa kiasi cha kutumia 29kg kwa ekari1 na nchi zilizpiga hatua zaidi kwa kilimo kama China, ekari 1 wanatumianzaidi ya 260kg.
Kama tathimini hii ya matumizi ya 9kg kwa ekari1 Tanzania ni utafiti wakati ambapo serikali ya awamu ya nne walau ilikuwa ikitenga fedha kiasi cha kuonekana kwenye ruzuku ya mbolea, watanzania na hususan wakulima wanapaswa kujiuliza leo, ambapo Serikali inatenga shilingi bilioni 10 kutoka shilingi bilioni 78 hali itakuwaje?.
Mheshimiwa Spika, Ni vigumu kwa Serikali ya Tanzania kufanya mapinduzi makubwa kiuchumi yenye kupunguza umasikini bila kukuza kilimo katika dhana pana(mazao,ufugaji na uvuvi). Kwa mujibu wa Ripoti ya USAID ya 2014, asilimia 70% ya watanzania wanategemea Kilimo, na kati yao asilimia 75% ni wanawake. Hivyo masikini wakubwa Tanzania ni wanawake ambao ni asilimia 75% ya watu wote wanaotegemea kilimo, hivyo mwenendo wa sasa ambapo Bajeti ya Miradi ya kilimo inatekelezwa kwa asilimia 2 – 3 ni rekodi mbaya ambayo haijapata kutokea tangu Uhai wa Taifa hili na ni ishara tosha kwamba Serikali hii haina mpango na masikini watanzania, na tabia ya Mhe Rais kujinasibu kuwa ni Rais wa wanyonge(masikini) ni dhihaka kwa watanzania masikini.
Mheshimiwa Spika, imekuwa changamoto kubwa hata miongoni mwa wachumi kuhusu hali ya uchumi nchini hasa inapoonekana biashara nyingi zinafungwa, walipa kodi wakubwa kama TBL, Benki za biashara , Kampuni za simu zote zinatangaza hasara. Manunuzi ya nje(imports) kuzidi kushuka, sekta ya nyumba(real estate) inazidi kuporomoka, kampuni zinazidi kupunguza wafanyakazi, soko la mitaji(stock market) linazidi kufanya vibaya, ukata kwenye uchumi (decline in liquidity) unazidi kuongezeka, lakini bado serikali inatangaza uchumi kuwa ni imara.
Mheshimiwa Spika, Ipo haja ya kuchunguza uhalisia wa takwimu zetu kuepuka kujenga uchumi hewa kwa takwimu za kupika , ndio sababu IMF hivi karibuni wametahadharisha kuwa mwenendo mbovu wa sera za kibajeti na kutokutabirika kwa utawala huu kutasababisha kuzorota kwa uchumi katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, katika tathmini ya saba ya hali ya uchumi wa Tanzania iliyotokewa tarehe (11/01/2018 na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ni kwamba hali ya uchumi wa Tanzania imekuwa ikipanda na kushuka na kwamba matazamio ya mwenendo huo yanaonyesha mashaka.Tathmini hiyo IMF imetaja baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri kiuchumi. Imesema kiwango cha ukuaji wa uchumi kimeendelea kupanda taratibu; upandaji wa bei za bidhaa muhimu umekuwa wa wastani; akiba ya fedha za kigeni imekuwa nzuri, na utekelezaji wa Mpango wa Sera ya Misaada (PSI) kwa miezi ya Julai hadi Septemba 2017 umekuwa wa kuridhisha, na takwimu za maendeleo ya kujamii inaridhisha, ingawa utekelezaji wa maboresho ya sera yanakwenda polepole.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, IMF imetaja maeneo mengi ambayo kiuchumi Tanzania imefanya vibaya katika kipindi hiki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shirika la Fedha Duniani (IMF) linahitimisha kwa kuitaka Serikali ya Tanzania kutekeleza yafuatayo ili uchumi wa nchi usididimie mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na maangalizo hayo ya IMF, taarifa za BOT zinaonesha kwamba zinaonesha wazi kwamba kushuka huko kwa ujazo wa fedha kwenye uchumi kunatokana na kushuka kwa kiwango cha mikopo kutoka Benki za biashara kwa sekta binafsi, na hivyo kuyumba kwa sekta binafsi ambayo kimsingi ndio injini ya uchumi.Na ndio sababu Benk Kuu ya Tanzania, kama msimamizi wa sera ya fedha, ikachukua hatua mbili kama namna ya kutafuta ufumbuzi wa ukata wa fedha kwenye uchumi(liquidity tightness). Hatua ya kwanza ni ile ya tangazo la kupunguza riba(credit discount) kwa mikopo ya Bank kuu kwenda bank za biashara kutoka riba ya asilimia 16% mpaka riba ya silimia 12%. Ikafuatiwa na tangazo la Benki Kuu la kupunguza dhamana za Benki za biashara zinazowekwa benki kuu kutoka asilimia 10% mpaka asilimia 8%
Mheshimiwa Spika, Hatua zote hizo zilichukuliwa kwa lengo la kukabili ukata kwenye uchumi kwa kuhakikisha sekta binafsi zinapata mikopo na kuchangamsha biashara kwenye uchumi na hivyo kukabili ukata mkali unaokabili uchumi kwasasa.Hata hivyo, pamoja na juhudi zote hizo za Benki Kuu kwa kutumia sera ya fedha(Monetary Policy), bado ukata umebaki kuwa tatizo kwenye uchumi ikiwa ni kielelezo kwamba mzizi wa tatizo la uchumi kwa sasa chimbuko lake sio sera ya fedha( monetary policy)bali sera ya bajeti na mazingira ya biashara kwa ujumla (Fiscal Policy&Business environment).
Mheshimiwa Spika, Tatizo la uchumi kwasasa sio benki kukosa fedha kukopesha sekta binafsi, tatizo ni Serikali imeshindwa kujenga mazingira rafiki kwa biashara na wawekezaji kwa ujumla.wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje kwa ujumla wanakabiliwa na mazingira magumu kibiashara ndio sababu kiwango cha mikopo isiyolipika(Non Performing loans-NPL) kimezidi kuongezeka kwa kiasi ambacho hakijawahi kutokea kwa zaidi ya miongo miwili.Kwa mujibu wa ripoti ya BoT, kiwango cha mikopo isiyolipika kimefikia zaidi ya asilimia 10 ambapo wastani ni asilimia 5
Mheshimiwa Spika, Hii ni ishara mbaya sana kwa sekta binafsi ambayo ndio inapaswa kuwa injini ya uchumi katika uchumi wa soko.Sio kwamba wafanya biashara hawa wanapenda kushindwa kulipa mikopo hiyo bali mazingira ya biashara ni mabovu na hivyo kusababisha wafanyabiashara kuogopa kukopa kwa ajili ya biashara na pia mabenki kuongeza urasimu wa kutoa mikopo kwa hofu ya mikopo isiyolipika kutokana na mazingira mabovu ya kibiashara ambayo msingi wake ni sera duni za kodi na utawala unaoendesha nchi kwa amri zaidi ya sheria. Na ndio maana hata ripoti ya mwaka 2017 kuhusu urahisi wa kufanya biashara(EASY OF DOING BUINESS) inayotolewa na Bank ya Dunia, Tanzania bado iko nyuma ya Kenya, Uganda na Rwanda ambao ndio washindani wetu kibiashara.
Mheshimiwa Spika, Tangu awamu ya tatu chini ya Benjamini Mkapa kiliundwa chombo kinaitwa Tanzania National Business Council-TNBC, Chombo hiki ni jukwaa muhimu kati ya Serikali na wafanyabiashara nchini, na kimuundo kinaongozwa na Rais kama Mwenyekiti.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na umuhimu wa chombo hiki kwajili ya kukutanisha na kugonganisha fikra kuhusu majibu ya uchumi na biashara nchini, Mhe Rais hakuwahi kuitisha chombo hiki kwa zaidi ya mwaka mmoja, na hata baada ya kuitisha baada ya shinikizo kubwa, bado maoni ya wawekezaji na wafanyabiashara yameendelea kupuuzwa. Ni wito wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kumtaka Mheshimiwa Rais na wataalamu wake atumie jukwaa hili kusaka majawabu ya hali mbovu ya kibiashara inayoendelea nchini kwa kuchanga mawazo ya bongo za pande zote, wafanyabiashara na wataalamu wake. badala ya kusikia upande mmoja wa watendaji wake ambao wengi ni wanataaluma kutoka vyuo vikuu ambao kwa kiasi kikubwa hawajawahi kuwa practioners.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuachana na Sera na Mipango ya kubahatisha au majaribio kwenye Uchumi. Itambukwa mwaka 2016 mwanzoni Serikali ilifanya uamuzi wa kuondoa fedha zake zote zilizokuwa zikiwekwa kwenye benki za biashara na kuzipeleka benki kuu BoT kwa hoja kwamba benki za biashara zinafaidi fedha hizo za serikali kwa kuzifanyia biashara.
Mheshimiwa Spika, Baadaye tena, Serikali hiyohiyo imehamasisha benki za biashara zikakope fedha benki kuu kwa riba punguzo kutoka asilimia 16% mpaka asilimia 12%. Kambi rasmi ya upinzani tunajiuliza, hivi ni akili gani iliyoamua kuondoa fedha za serikali kwenye benki za biashara ambako zilikuwa zinazalisha riba ya mpaka asilimia 15% na kuzipeleka benki Kuu ambako hazizalishi chochote? Kama awali Serikali ilikuwa inaweka fedha zake benki za biashara kwa riba ya asilimia 15% ni sawa na kusema serikali ilikuwa inazikopesha benki za biashara fedha yake kwa riba ya asilimia 15% lakini sasa imeamua kuzikopesha kwa mlango mwingine benki hizo hizo kwa riba ya asilimia 12%. Kwa utaratibu wa uliofutwa ni serikali ilikuwa inapata riba ya asilimia 15 na sasa umeletwa utaratibu unaoitwa bora ambapo sasa serikali itapata riba ya asilimia 12%. Akili iko wapi katika jambo hili?
Mheshimiwa Spika, Jukumu la kujadili na kuamua kuhusu Bajeti ni moja ya majukumu muhimu kabisa ya Bunge hili tukufu ambalo tumepewa kikatiba. Jukumu la Serikali katika Bajeti ni utekelezaji tu. Na ndio maana mwaka 2015, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Bajeti kwa lengo la kuhakikisha nidhamu na ufanisi katika kupanga, kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa Bajeti.
Mheshimiwa Spika, Ni bahati mbaya sana, kama nilivyoeleza awali kwamba Utawala huu unaongoza kwa kutokuheshimu sheria na Katiba, makosa hayo yanajidhihirisha pia katika utekelezaji wa bajeti hii ya kwanza katika utawala wa awamu ya tano.Serikali kwa agizo la Mhe Rais imetumia fedha za bajeti hii kutekeleza baadhi ya mambo ikiwemo kuhamishia Serikali Dodoma,mambo ambayo hayakupitishwa naBunge kwenye Mpango wa Bajeti.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani haina tatizo na dhamira njema ya Serikali kuhamia Dodoma au utekelezaji wa mpango wowote kwajili ya huduma kwa wananchi. Tunachosisitiza ni kwamba uendeshaji wa Serikali lazma ufuate sheria na taratibu. Uendeshaji wa Serikali usiofuata Sheria na taratibu ni utawala wa fujo.Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015( The Budget Act 2015, Sect 34), inasisitiza wazi kwamba Serikali haitaruhusiwa kutekeleza mradi wowote ambao hakupitishwa na Bunge kwenye Mpango wa bajeti.Maamuzi ya namna hii yanapora mamlaka ya Bunge letu, na ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa Serikali hii kwa Muhimili wa Bunge ambao kikatiba ndio Muhimili Mkuu wa dola (Supreme organ of the State).
Mheshimiwa Spika, Naomba kwa msisitizo, nitumie maneno yaliyotumiwa na Jaji Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya arusha aliyetoa dhamana kwa Mhe Godbless lema , akionekana kukemea tatizo la Mahakama kuingiliwa, alisema “Ni lazma Mahakama zionee wivu mamlaka yake”.
Mheshimiwa Spika, Hilo ndilo neno ningependa Bunge pia tulitumie kama sote tunajitambua bila kujali tofauti zetu: Kwamba ni lazma Bunge lionee wivu Mamlaka yake . Na lisikubali Mamlaka yake yapokonywe na Serikali au Mamlaka nyingine ya dola. Ni lazma tuhakikishe Serikali inatekeleza majukumu yake ndani ya ukomo wa mamlaka yake na sio vingineyo kwani kuacha Serikali ifanye maamuzi ya Bunge, itafanya pia ya Mahakama na kuingiza taifa hili kwenye kile waingereza wanaita ‘Kangaroo Governance”. Kwa maana ya Utawala usio na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Bajeti ndio kipimo cha uwezo wa uongozi kutimiza wajibu wake kwani ni bajeti inayotafsiri ahadi za Ilani ya Chama kilichopo Madarakani katika kufikia Dira ya Taifa, sanjari na ahadiMgombea Urais. Mafanikio ya Rais yeyote yanapimwa katika namna anavyomudu kutekeleza bajeti na sio idadi ya purukushani au ziara za kushtukiza na matamko yasiyo na ukomo kila kukicha na yasiyo ya kimkakati kuweza kutolewa na Ofisi kuu ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti 2016/17, inaonesha wazi kwamba miradi ya maendeleo iliyotekelezwa ni asilimia 38% ya makadirio ya Bajeti. Kwamba, wakati makadirio ya matumizi kwa miradi ya maendeleo yalikuwa billion 11,820,503, Serikali imefanikiwa kutekeleza kwa kutoa billion 3,647.7 na fedha za nje billioni907. Mwaka 2017/18 bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa ilikuwa shilingi trilioni 11.9 lakini iliyotolewa hadi kufikia Aprili, 2018 ilikuwa ni shilingi trilioni 5.123[1]sawa na asilimia 42.7 ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge. Ukitafuta wastani kwa miaka yote miwili utapata kuwa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ni wa takriban asilimia 40. Ni wazi kwamba huu ndio msuli wa Rais wa awamu tano unapoishia, na bila shaka Mhe Rais atakuwa amejua kipimo cha uwezo wake kuwa ni kati ya asilimia 38 na 40, tofauti na mafikirio makubwa aliyokuwa nayo kuhusu uwezo wake wa kutekeleza mipango katika Taifa hili kulinganisha na watangulizi wake.Utekelezaji huu wa asilimia 38 mpaka 40 unamfanya Rais wetu atambue nafasi yake kuwa yeye ni rais wa kawaida sana ukilinganisha na watangulizi wake kwani miradi ya maendeleo tangu awamu ya tatu imekuwa ikitekelezwa kwa takriban asilimia 40% Na hii ndio changamoto kwake.
Mhe shimiwa Spika, Uchambuzi wa Bajeti hii unaonesha wazi kwamba chini ya CCM Taifa hili litasafiri zaidi ya karne bila kufikia uwezo wa kujitegemea. Kwa mfano, katika Bajeti ya 2016/17 , Makusanyo ya Kodi yalikuwa trilioni 11.6 dhidi ya makisio ya trilioni 15, na makusanyo yasiyo ya kodi yalikuwa trilioni 1.6 dhidi ya makisio ya trilioni 2.69 na makusanyo toka serikali za mitaa yalikuwa billion 399 dhidi ya makisio ya billion 665.
Mheshimiwa Spika, Wakati uwezo wa Serikali yetu yenye umri zaidi ya nusu karne ukiwa kiasi hicho, kiasi cha deni lililoiva mwaka 2016/17 ilikuwa trilioni 8 wakati msahahara peke yake ikiwa trilioni trilioni7?. Hii maana yake katika mwaka uliokwisha, makusanyo yetu jumla ya ndani trilioni 13.5 wakati hitaji la mshahara na deni peke yake likifika trilioni 15. Ni mazingira haya Rais Uhuru wa Kenya ataendelea kutukujeli kuwa Tanzania bado tuna serikali ambayo sio tu inakopa kugharimia miradi yote ya maendeleo bali inakopa kujiendesha kwa matumizi ya kawaida na hata mishahara ya walimu na watumishi haijimudu bila kukopa.
Mheshimiwa Spika, Hali ni hiyo pia katika Bajeti ya 2017/18, kwani Bajeti hii imekosa ubunifu wa vyanzo vya mapato, na hivyo itaendeleza aibu ya kushindwa kujimudu hata kugharamia mishahara ya watumishi kwani hakuna ubunifu wowote katika vyanzo vya mapato. Ni Bajeti iliyojaa rhetorics. Imekosa ubunifu katika vyanzo vya mapato, imekosa mkakati wa kuchochea sekta binafsi iweze kuchochoa uchumi, haisemi kwa utekelezaji wa bajeti hii itatengeneza ajira ngapi wala haisemi bajeti hii itapunguza umasikini kwa kiasi gani ili iweze kupimika mwisho wa siku.Kifupi ni bajeti ya mazoea, iliyojielekeza kwenye vyanzo vya mapato kwa mazoea na hivyo kukosa nyongeza ya ubunifu.
Mheshimiwa Spika, Nasisitiza kuwa Bajeti hii ni ya mazoea kwasababu maeneo yaliyongezwa kodi ni yaleyale ya miaka yote. Bajeti hii haisemi lolote kuhusu mkakati wa kumwinua wakulima ambao ni70% ya watanzania hasa katika mazingira ya sasa ambapo kilimo kimeporomoka kufikia ukuaji wa 1.7%, zaidi kwenye kilimo imebaki na msimamo wa kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka 78bn ya mwaka 2015 mpaka 15bn ya mwaka 2017/18.Haina chochote kuhusu bank ya wakulima, iliyoanzishwa mwaka 2015 kwa kusudio la mtaji wa 1trilioni na kukopesha wakulima 200,000 kwa mwaka lakini sasa imeishia kukopesha wakulima 3700 na mtaji wa billion 60 tu kwa miaka3.
Mheshimiwa Spika Bajeti hii haisemi lolote kuhusu kujenga na kuimarisha wajasiliamali wadogo na wakati ambao ni asilimia 40% ya ajira zote.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania imekuwa kinara wa kupata misaada na mikopo nafuu toka nje kuliko Serikali zote ukanda huu wa kusini na Mashariki ya afrika. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Official Development Aid (ODA) ya mwaka 2013. Kwa mujibu wa Ripoti hii, Tanzania tunayokaririshwa kuwa nchi ya Amani na Utulivu imekuwa ikipata misaada (Grants) kuliko nchi zilizo vitani au zisizo na usalama kabisa duniani kama Kongo DRC na Sudan. Hii ni moja ya aibu kubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mwenendo huo wa miongo kadhaa ya Taifa hili kupata upenedelo huo wa misada zaidi ya kiwango cha nchi zilizo vitani, bado misaada hiyo haijaweza kuleta tija ya maana kiuchumi zaidi ya kujenga Serikali yenye akili tegemezi badala ya kujitegemea.
Serikali hii ya awamu ya tano, kuanzia kwenye hotuba ya Rais bungeni pamoja na hotuba ya wizara ya Bajeti 2016/17 lisisitiza kwa kiasi kikubwa dhana ya kutotegemea nje ingawa bajeti yake ni tegemezi kuliko ile ya awamu ya nne.
Kwa mfano, Katika Bajeti ya mwisho ya awamu ya nne, kiwango cha misaada na mikopo nafuu toka nje ilikuwa trilioni 2.6, wakati bajeti ya kwanza ya Rais John Pombe Magufuli anayejitangza kutotegemea nje, misaada na mikopo nafuu ilikuwa 3.6trilioni. Huu ni ushahidi wazi kwamba serikali hii inategemea nje kuliko Serikali iliyopita.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Transparency Inernational kwa mwaka 2016 kuhusu tathimini ya hali rushwa na ufisadi duniani,Tanzania ni miongoni mwa nchi tano katika Afrika ambazo ziliguswa mahususi katika Ripoti hiyo, Kwa kifupi, ushauri wa jumla kuhusu nchi hizo za Kenya, Nigeria, Afrika ya Kusini, Ghana kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi, ripoti hiyo inasema kwamba: “African Leaders that come to Office on an anti corruption ticket, will need to live up their pledges to deliver corruption free services to their citizen, they must implement their commitments to their principles of governance, democracy and human rights. This includes strengthening the insitutions that hold government accountable as well as electoral systems that allow citizens to either re elect them or freely chose an alternative.
Mheshimiwa Spika, Kwa tafsiri isiyo rasmi, Ripoti hiyo inasema kwamba “ Viongozi wa Afrika walioingia madarakani kwa tiketi ya vita dhidi ya ufisadi wanapaswa kuishi ahadi zao kuhakikisha rai wanapata huduma bila rushwa,na ili kufikia hatua hiyo ni lazma Viongozi hao wahakikishe wanatimiza wajibu huo kwa misingi ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu. Hii ni pamoja na kuhakikisha Taasisi zinazosimamia uwajibikaji wa serikali zinaimarishwa pamoja na mifumo ya uchaguzi inaimarishwa kuhakikisha wananchi wanaweza kuirudisha serikali hiyo madarakani au kuchagua serikali mbadala kwa hiari yao”
Mheshimiwa Spika, Hii ni ripoti Muhimu sana kwa utawala huu na ni vema Serikali hii ijenge tabia ya kusikiliza taasisi za kitaalamu zinasema nini kuhusu utawala wake. Kambi rasmi ya Upinzani inaunga mkono ripoti hii kwamba ili vita dhidi ya ufisadi iwe endelevu na yenye mafanikio ni lazma kama nchi tujenge taasisi imara za kuisimamia Serikali likiwemo Bunge.
Mheshimiwa Spika, Hali ya sasa ambapo Serikali inadhoofisha bunge kwa kuliweka gizani na kwa miongozo isiyokwisha toka Ikulu, Hali ya sasa ambapo Ofisi ya CAG inabanwa kibajeti ishindwe kutimiza majukumu yake ya ukaguzi ili kulisaidia Bunge kuisimamia Serikali, Hali ya sasa ambapo vyombo vya habari vinabanwa kuhakikisha vinaandika habari tamu kwa serikali, Ni mfano mbaya kabisa na ni kielelezo tosha kwamba serikali haipo serious katika vita dhidi ya Ufisadi nchini kwani kinachoendelea ni serikali inaharibu yenyewe na inataka ijikosoe yenyewe na kujisimamia yenyewe.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu msingi ya Wizara ya fedha ni pamoja na jukumu la kusimamia deni la Taifa. Wizara imeonyesha udhaifu mkubwa katika kusimamia Deni la Taifa, kwa kuwa Deni hili limeendelea kuwa kubwa kila mwaka jambo ambalo limekuwa na athari kubwa katika bajeti ya Serikali na hivyo kuathiri uchumi wetu na maisha ya wananchi kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania kuhusu tathmini ya nusu mwaka ya mwenendo wa uchumi (Mid-Year Review) katika mwaka wa fedha 2017/18 iliyotolewa mwezi Februari, 2018 ni kwamba; deni la taifa liliongezeka kwa dola za kimarekani milioni 1,054.6 (sawa na shilingi trilioni 2, bilioni 320 na milioni 120)[2] kutoka dola za kimarekani milioni 19,957.6 (sawa na shilingi trilioni 43 , bilioni 906 na milioni 720) mwezi Juni 2016; hadi kufikia dola za kimarekani milioni 21,012.2 (sawa na shilingi trilioni 46 , bilioni 226 na milioni 840) mwisho wa mwezi Desemba, 2017. Deni hilo linajumuisha deni Serikali la nje na deni la sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo; Deni la ndani liliongezeka kwa asilimia 8.6 na kufikia shilingi 12,810,300,000,000/= (trilioni 12, bilioni 810, na milioni 300). Kwa hiyo, ukijumlisha deni la nje na la ndani utapata jumla ya deni la taifa kuwa ni shilingi 59,037,140,000,000/= (trilioni 59, bilioni 37, na milioni 140)
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa inayoelezwa ya kuongezeka kwa deni ni mikopo mipya pamoja na mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha (exchange rate fluctuations). Katika nusu ya kwanza ya mzunguko wa bajeti ya 2017/18, Serikali ilikopa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 556.0 (sawa na shilingi trilioni 1, bilioni 223, na milioni 200) ambapo kati ya fedha hizo dola za kimarekani milioni 471.1 (sawa na shilingi trilioni 1, bilioni 36 na milioni 420) zilipokelewa kama fedha taslimu na kiasi kilichobakia cha dola za kimarekani milioni 84.9 (sawa na shilingi bilioni 186 na milioni 780) zilingia kwa mfumo wa ugharamiaji wa moja kwa moja wa miradi ya maendeleo (direct project financing)
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho hicho cha nusu ya kwanza ya mzunguko wa bajeti ya 2017/18; Serikali ililipa kiasi cha dola za kimarekani milioni 453.7 (sawa na shilingi bilioni 998 na milioni 140) kama marejesho ya mkopo wa nje. Kati ya fedha hizo, dola za kimarekani milioni 315.2 (sawa na shilingi bilioni 693 na milioni 440) zilikuwa ni marejesho ya deni msingi (principal repayments) na kiasi kilichobakia cha dola za kimarekani milioni 138.5 (sawa na shilingi bilioni 304 na milioni 700) kilikuwa ni malipo ya riba (interest payments).
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kulazimika kulipa riba ya shilingi bilioni 304 na milioni 700 ni matokeo ya kiburi cha Serikali hii ya CCM cha kutotaka kupokea na kuufanyia kazi ushauri wa muda mrefu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa kutochukua mikopo yenye masharti ya kibiashara. Fedha hii tunayolipa kama riba ni fedha ambayo ingetumika kugharamia huduma za jamii kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maangalizo yote ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiipatia Serikali hii kuhusu kupunguza kwa kadri iwezekanavyo au kuacha kabisa kuchukua mikopo yenye masharti ya kibiashara; safari hii Serikali imepanga kukopa jumla ya shilingi trilioni 8 bilioni 904, na milioni 727[3] katika mwaka wa fedha 2018/19. Aidha, ukiangalia sura ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19 utaona kwamba Serikali imetenga shilingi trilioni 10, bilioni 4, na milioni 840 kwa ajili ya kulipa deni la taifa.
Mheshimiwa Spika, hatua tuliyofikia ya kukopa shilingi trilioni 8 yenye masharti ya kibiashara na kulipa madeni kwa shilinigi trilioni 10 ni mbaya sana. Hii haina tofauti na kuwa kwenye mzunguko wa madeni yasiyoisha (vicious cycle of debts). Tukishakubali kuwa katika mzunguko wa madeni maana yake tuko katika mzunguko wa umasikini pia (viscious cycle of poverty).
Mheshimiwa Spika, mikopo ya masharti nafuu ambayo Serikali inatarajia kukopa kwa mawaka wa fedha 2018/19 ni jumla ya shilingi trilioni 2.676. Hiki ni kiasi kidogo na kimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka. Tafsiri ya kushuka kwa mikopo yenye masharti nafuu ni kwamba nchi yetu haikidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya masharti nafuu. Na hii ni kwa sababu deni la taifa halijafanyiwa uhakiki (credit rating) ili kujiridhisha Serikali inakopesheka kwa kiwango gani. Kwa sababu hiyo; mashirika mengi ya fedha duniani yamejitoa kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa nchi yetu kwa kuwa hakuna uhakika kama mikopo hiyo itaweza kurejeshwa. Matokeo ya jambo hilo, Serikali imekosa namna nyingine ya kumudu gharama za kuendesha nchi, badala yake imekimbilia kwenye mikopo ya masharti ya kibiashara jambo ambalo linaendelea kudidimiza uchumi wan chi.
Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi kwamba kukua kwa deni la Taifa kunaisababishia serikali kuendelea kuwa tegemezi na hivyo kushindwa kutatua kero za kiuchumi za wananchi. Jambo la kusikitisha ni kwamba pamoja na ukweli huo, serikali imeendelea kukopa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara hali ambayo inazidi kufanya hali ya maisha kwa wananchi yaendelee kuwa ngumu kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kulipa madeni hayo badala ya kuzitumia fedha hizo kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishatoa rai kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum (Special Audit) katika kitengo cha deni la Taifa (Fungu 22) ili tuweze kujua mikopo tunayoichukua kila mwaka inatumika kufanyia nini, atoe taarifa ya miradi iliyotekelezwa kutokana na mikopo hiyo kama ni ya miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa Maendeleo. Halikadhalika ukaguzi huu maalum utatuwezesha kama Taifa kujua kiwango halisi cha deni la Taifa ambalo tunadaiwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilishatoa ushauri kwa Serikali hii kutenganisha deni halisi la Taifa na matumizi mengineyo yanayohusu Mfuko Mkuu wa Hazina ili kuziba mianya ya ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kisingizio cha Deni la Taifa. Katika muktadha huo huo, ili kudhibiti Serikali kukopa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara, ambayo hatimaye yanaliingiza taifa kwenye mzigo wa madeni; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza pia kwamba; Kabla Serikali haija kopa; ilete pendekezo la mkopo huo Bungeni pamoja na orodha ya miradi itakayotekelezwa kwa kutumia mkopo huo ili Bunge liidhinishe. Pendekezo hili lilizingatia msingi kwamba Bunge ndicho chombo cha uwakilishi wa wananchi, na kwa kuwa mikopo hii inakuja kulipwa na wananchi kupitia kodi zao, ni vema wananchi wakashirikishwa kupitia wawakilshi wao juu ya mikopo ambayo Serikali inachukua kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa za Fedha za Taasisi za Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2017, inaonyesha kwamba kiwango cha deni la taifa kimeshushwa kwa kiasi cha shilingi 4, 588,390,000,000/= (trilioni 4, bilioni 588, na milioni 390)
Mheshimiwa Spika, CAG anasema kwamba, mapitio yake ya deni la taifa yalibaini kwamba kiwango cha deni la taifa kilifikia shilingi 46,081,430,000,000/= (trilioni 46, bilioni 81 na milioni 430) kufikia Juni, 2017; lakini kiwango hicho hakikujumuisha madeni ya shilingi bilioni 4,588,390,000,000/=, ikiwa ni madeni ya mifuko ya pensheni kiasi cha shilingi 4,421,750,000,000[4] na shilingi 166,640,000,000/= ikiwa ni dhamana zilizokiukwa masharti chini ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Spika, ukichukua kiwango cha deni la taifa kilichoshushwa cha shilingi 4, 588,390,000,000/=; ukajumlisha na kiwango cha jumla ya deni la taifa cha shilingi 59,037,140,000,000/= kilichotolewa na BOT, utakuta kwamba jumla ya deni la Taifa ni shilingi 63,625,530,000,000/= (trilioni 63, bilioni 625, na milioni 530).
Mheshimiwa Spika, ukirejea hotuba ya Waziri Mkuu aliyoitoa hapa Bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi katika Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19; tarehe 4 Aprili, 2018; alisema kuwa deni la Taifa hadi kufikia Desemba, 2017 lilikuwa Dola za Kimarekani milioni 25,419.6[5]. Ukibadili dola hizi kuwa shilingi za Tanzania kwa ‘exchange rate’ ya shilingi 2,200/= kwa dola moja ya Marekani utapata jumla ya shilingi 55,923, 120,000,000/= (trilioni 55, bilioni 923, na milioni 120).
Mheshimiwa Spika, kiwango hiki cha deni la taifa cha takriban shilingi trilioni 63 ni sawa na asilimia 59.43 ya Pato la Taifa ambalo kwa sasa ni shilingi trilioni 106.867 kwa mujibu wa taarifa ya CAG.
Mheshimiwa Spika, kuna mkanganyiko kuhusu uhimilivu wa deni la taifa dhidi ya pato la taifa. Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Fedha ni kwamba pato la taifa kwa sasa ni shilingi trilioni 50.5 Na kwa mujibu wa hotuba hiyo; uhimilivu wa deni kwa sasa ni asilimia 34 ya pato la taifa wakati ukomo wa uhimilivu ni asilimia 56 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia takwimu za uchambuzi wa deni la taifa uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – ambapo deni la taifa limefikia shilingi trilioni 63; ni kwamba deni la taifa si himilivu tena. Takwimu zinazotolewa na Serikali haziwezi kuaminika tena kwa kuwa Serikali hiyo hiyo ina takwimu tofauti kuhusu deni la taifa; na pia kuhusu pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa fedha, anasema kuwa pato la taifa ni shilingi trilioni 50.5; taarifa iliyowasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge inaonyesha kuwa pato la taifa ni shilingi trilioni 86. Wakati huo huo, CAG anasema kuwa pato la taifa kwa sasa ni shilingi trilioni 106. Katika Mazingira hayo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapata mashaka juu usahihi wa deni la taifa na pia pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika; pamoja na ukengeufu huo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashukuru kwa Serikali kujiumbua yenyewe kwamba deni la taifa si himilivu tena kwa kutumia kigezo cha deni dhidi ya pato la taifa. Hotuba ya Waziri wa Fedha kuhusu hali ya uchumi ukurasa wa 9 aya ya 16 inasema kwamba; “Pato halisi la taifa kwa mwaka 2017, lilifikia shilingi milioni 50,525,087 (trilioni 50.5). Kwa hiyo, ukilinganisha na deni la taifa ambalo kwa sasa ni shilingi trilioni 63 ni wazi kwamba nchi iko rehani.
Mheshimiwa Spika, kuwa deni la taifa limefikia zaidi ya nusu ya pato la taifa; na ukomo wa kukopa ni asilimia 50 ya pato la Taifa ambayo tumeshaivuka kwa mujibu wa takwimu alizotoa Waziri Mkuu. Hivyo kuendelea kusema kuwa deni ni himilivu ni kujivika kilemba cha ukoka, na kujitoa ufahamu, mambo ambayo hayakubaliki katika kanuni za uchumi. Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalisihi Bunge kuazimia kuunda Kamati Teule kuchunguza uhalisia wa deni la Taifa na Pato la Taifa.Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kushikilia msimamo wake wa kuitaka Serikali kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya uchunguzi maalumu (Special Audit) ya mwenendo wa deni la taifa na kushauri hatua za kuchukua ili taifa liepukane na athari za deni hilo katika uchumi wan chi.
Mheshimiwa Spika, Ujasiri wa kusema deni letu ni himilivu, lazima uendane sambamba na uwezo wetu wa kiuchumi wa kukusanya KODI. Deni linaweza kuwa himilivu kama uwezo wa nchi kukusanya kodi unafikia japo 36% ya Pato la Taifa. Kwa mantiki hiyo,kwa pato letu la Taifa la shilingi Trillion 106, tulitakiwa kwa mwaka tuwe tunakusanya kodi isiyopungua shilingi Trillion 38 kwa mwaka. Kwa makusanyo haya tutakuwa na uwezo wa kulipa deni ,mishahara kwa watumishi wetu na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa hali ilivyo sasa uwezo wetu wa kukusanya ni 14% tu ya pato la Taifa. Taarifa ya Wizara ya Fedha kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti inaonyesha kwamba Kati ya shilingi Trillion 17.3 zilizopangwa kukusanywa na TRA katika mwaka wa fedha 2017/18. Mpaka Mwezi Machi 2018 kiasi kilichokusanywa ni shilingi trillion 10.7 tu. Kwa “makusanyo ya Trillion 1.3 kwa mwezi kama tunavyoambiwa na TRA” inatarajiwa mpaka mwaka wa fedha unaisha makusanyo ya Kodi yatafikia shilingi Trillion 14tu!
Mheshimiwa Spika, Kutokana na uwezo mdogo wa kukusanya mapato unaokwenda sambamba na mzigo mkubwa wa deni la Taifa. Utekelezaji wa Bajeti unadhihirisha hilo kwani ¾ ya fedha inayokusanywa inakwenda kwenye kulipa deni la Taifa na Mishahara kwa watumishi.
Mheshimiwa Spika, Kwa uchambuzi huu utaona kwamba kuna tofauti ya takwimu za deni la taifa zilizotolewa na Benki Kuu; zilizokaguliwa na CAG na zilizotolewa na Waziri Mkuu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni takwimu zipi sahihi kati ya hizo?
Mheshimiwa Spika, ukengeufu huu wa takwimu unatokana na udhaifu uliopo katika mfumo mzima wa usimamizi wa deni la taifa. Mfumo huo, umepitwa na wakati. Mkakati wa Taifa wa Madeni (NDS) wa mwaka 2002 uliandaliwa kwa mazingira ya sheria ya Mikopo ya serikali , Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 (Miaka 43 iliyopita). Hali ya uchumi na mazingira ya kuanzishwa kwa sheria na mkakati wa NDS yamebadilika mno kutokana na mabadiliko ya kiuchumi ambayo yametokea.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kupanuka kwa wigo wa deni la Taifa katika suala la vipengele na mikopo mikubwa ambayo imefanyika, sheria na miongozo inayosimamia deni la Taifa haiko sambamba na maendeleo hayo na vyombo vinavyotumika vimepitwa na wakati na kwa sababu hiyo kufanya usimamizi wa deni la taifa kuwa changamoto.
Mheshimiwa Spika, Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali anabainisha [6] katika ripoti yake ya Machi, 2017 kwamba: mfumo uliopo sasa unaongeza uzembe katika uendeshaji,uratibu duni na kutokuwa na taarifa za kutosha katika vitengo na taarifa sahihi kupitia taasisi na kusababisha kuwa na rekodi zisizosahihi na zisizojitosheleza kuhusiana na deni. Alishauri mfumo mzima wa usimamizi wa deni la taifa ufanyiwe maboresho (reform); ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo sasa; na hivyo kuweza kuwa na usimamizi mzuri (management) ya deni la taifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza; maboresho hayo yaliyopendekezwa na CAG yalishafanyika?
Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba iliyowasilishwa Bungeni kuhusu hali ya uchumi na mpango wa serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 pamoja na hotuba ya bajeti kuhusu vipaumbele vya serikali ni vitu viwili tofauti vinavyotoka kwenye serikali moja. Mheshimiwa Spika, Wakati hotuba ya mpango na hali ya uchumi ukurasa 27 ukiweka vipaumbele vya serikali kuwa ni viwanda, kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuimarisha utekelezaji wa mpango, hotuba ya bajeti ukurasa wa 38 na 39 inaeleza vipaumbele vya bajeti ya serikali kuwa ni kilimo, viwanda, huduma za jamii na miundombinu hasa ya umeme pamoja na sekta zingine.
Mheshimiwa Spika, Hili ni jambo la kushangaza kwa sababu wakati wa asubuhi serikali inatoa kauli tofauti na jioni wakati wa kuwasilisha bajeti. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Serikali inawahadaa wananchi.
Mheshimiwa Spika, licha ya vipaumbele kutofautiana kwenye Mpango wa Maendeleo na Hotuba ya Waziri; hata fedha zilizotengwa kwenye sekta hizo ambazo Serikali inasema ni za kipaumbele haziendani na hadhi ya kipaumbele. Kwa mfano ukiangalia sekta ya Kilimo; Serikali imetenga shilingi bilioni 64.105 kama fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/19.Kiasi hiki ni pungufu ya zaidi ya asilimia 100 ukilinganisha na miaka miwili iliyopita ambapo Serikali ilitenga shilingi bilioni 100.527 kwa mwaka 2016/17 na shilingi bilioni 150.253 kwa mwaka 2017/18 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Kilimo.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye sekta ya viwanda; ambayo Serikali imesema ni sekta ya kipaumbele; fedha iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni shilingi bilioni bilioni 100.024. Pamoja na fedha hii kuonekana kuongezeka ukilinganisha na shilingi bilioni 35.387 iliyotengwa kwa mwaka 2015/16 na shilingi bilioni 73.840 iliyotengwa mwaka 2017/18 lakini utekelezaji wa bajeti hizo zilizopita ulikuwa asilimia 5 na 9 kwa mfuatano. Utekelezaji huo hauendani kabisa na sekta ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huo, Serikali inawafurahisha wananchi kwa kutaja sekta hizo kuwa ni za kipaumbele wakati haijatenga fedha zinazoendana na sekta za kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, ili halmashauri ziwe na uwezo wa kuleta maendeleo endelevu mbali na mgawo unaotoka Serikali kuu, ni lazima na muhimu kwa halmashauri kuwa na vyanzo vya ndani vya mapato na fedha hizo kuzitumia kulingana na mahitaji na mipango inayopangwa kuanzia Serikali za vijiji.
Mheshimiwa Spika, Vyanzo vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vimeainishwa katika vifungu Na. (6) hadi (9) vya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka 1982 yaani (The Local Government Finance Act, No. 9 of 1982).Kulingana na Sheria ya Fedha Na. 9 ya mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa iliyorekebishwa na Sheria ya Fedha Na. 15 ya mwaka 2003 yaani (The Finance Act No. 15 of 2003), Serikali za Mitaa hazitozi kodi ya Mapato bali kodi hiyo hutozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA). Ni muhimu sana Serikali kuu hasa awamu ya tano iache utaratibu wake iliouanzisha tangu iingie madarakani wa kupora vyanzo vya mapato vya halimashauri.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa ardhi ndiyo rasilimali pekee ambayo kila Halmashauri katika nchi inaimiliki. Ardhi ndiyo chanzo cha mapato cha uhakika kwa kila Halmashauri ya nchi hii, hivyo kitendo chochote cha Serikali Kuu kupora au kujaribu kupora chanzo hiki ni kuifanya halmashauri kushindwa kabisa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zinatakiwa kuchukua 30% ya kodi ya Ardhi, hivyo inapotokea kuwa Serikali Kuu inachukua fedha hizo na urejeshaji wake unakuwa ni pale itakapojiridhisha kuwa zinahitajika, hilo sio sahihi kwa maendeleo ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Chanzo hicho cha mapato ya halimashauri kinachotokana na kodi ya ardhi kama makusanyo ya ndani (own source) ni muhimu sana katika kuzifanya halimshauri zikabiliane na changamoto mbali mbali za kuhudumia wananchi. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri serikali kuziruhusu halimashauri ziendelee kukusanya hiyo asilimia 30 ya kodi ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kupitia Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, Hotuba ya Bajeti ya Wizara Fedha na Mipango, Hotuba ya Waziri OR-TAMISEMI, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano II, Taarifa ya Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali 2015/16, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025;
Mheshimiwa Spika, kwa ufahamu ni kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na majukumu yake kuainishwa katika Ibara ya 146, na kwamba mamlaka hizi zimetambuliwa na Agenda ya Maendeleo Endelevu Duniani ya 2030 (Sustainable Development Goals 2030) kuwa vyombo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu na kuondoa umaskini, na kwamba;
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 katika kifungu namba 3 cha Utawala Bora na Utawala wa Sheria kinachozungumzia demokrasia na ushiriki wa wananchi inatambua umuhimu wa kuziwezesha Serikali za Mitaa katika kuwahudumia wananchi ndani ya mamlaka hizo.
Mheshimiwa Spika, Tunatambua juhudi kubwa za Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa malengo haya na kwamba, Serikali Kuu kupitia Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi ya Mwaka 1998 imeazimia kuzipa Serikali za Mitaa uhuru na mamlaka ya kutoa huduma na kuleta maendeleo katika maeneo yao. Hii ni pamoja na kuzipa mamlaka ya kupanga kukusanya na kutumia mapato yake ya ndani katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17-2020/21 umejielekeza katika kuongeza mapato ya ndani kutoka vyanzo vipya. Serikali kupitia mpango huu imetambua umuhimu wa kodi ya majengo kama chanzo kikuu cha mapato ya ndani ya Serikali za Mitaa na kusisitiza kuwa itaziwezesha
Mamlaka hizi katika ukusanyaji wa kodi. Hata hivyo uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umedhihirisha kuendelea kuongezeka kwa hali ya utegemezi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Serikali Kuu, jambo ambalo hata mwelekeo wa bajeti ya mwaka ya Mwaka 2016/17 na ya Mwaka huu 2017/18 umeziacha Serikali za Mitaa kwenye njia panda pale ambapo imeamua kuziondolea baadhi ya vyanzo vyake vya mapato. Mfano, tathmini iliyofanyika mwaka 2012 na TACINE (Mtandao wa Majiji na Miji Tanzania) ilionyesha miji imekuwa tegemezi kwa Serikali Kuu kwa 73% kinyume na Sheria ya Mipango Miji ambayo inataka Manispaa zijitegemee kwa 70% na Majiji 95%;
Mheshimiwa Spika, pamoja na sera nzuri ya ubia wa Serikali na sekta binafsi kama ambavyo imeelezwa vyema na Waziri wa Fedha na Mipango, miradi mingi ya ubia inayoonekana kufanikiwa ni ile inayotekelezwa na Serikali Kuu. Nafasi ya Serikali za Mitaa kupata miradi hiyo inakuwa ngumu kwa kuwa inahitaji uwezo mkubwa wa kifedha wakati Halmashauri nyingi hazina na kuna ushahidi kuwa tayari zimenyang’anywa baadhi ya vyanzo vya mapato.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha na Mipango ya 2017/18, Serikali za Mitaa zimeondolewa mamlaka ya kukusanya baadhi ya vyanzo vyake muhimu vya mapato ya ndani ikiwemo Kodi ya Majengo na Kodi ya Mabango. Jambo hili linaenda kinyume na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano II, ambao umetambua Kodi ya Majengo yaani “Property Tax” kama chanzo kikuu na muhimu cha mapato ya ndani ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwani inachangia kati ya 30% hadi 60% ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Miji.
Mheshimiwa Spika, kuondolewa kwa kodi hizi yaani kodi ya majengo na ile ya mabango, kutapelekea athari zifuatazo;
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali;
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa bajeti ya serikali unakumbwa na changamoto kadhaa ambazo huathiri utekelezaji wa bajeti hiyo hata baada ya kupitishwa na Bunge. Tunatambua kuwa maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha unaofuata huanza mapema baada ya kuanza mwaka wa fedha mpya.
Mheshimiwa Spika, inatambulika pia kuwa bajeti hutakiwa kuanzia kwenye ngazi za Vijiji na Mitaa kwa mfumo wa kuibua fursa na changamoto katika maendeleo (Opportunities and Obstacles to Development “O- and OD”) na baadae kwenda Halmashauri pamoja na ngazi ya Mkoa. Hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa mambo yamekuwa yakipangwa kuanzia ngazi ya Halmashauri pekee na sio shirikishi kama inavyotakiwa na sera na maelekezo ya serikali.
Mheshimiwa Spika, hata utofauti wa takwimu kwenye vitabu vya bajeti ambao Kambi Rasmi ya Upinzani ilionyesha kwa miaka miwili mfululizo huenda unasababishwa na utaratibu wa Halmashauri kujipikia takwimu na miradi bila kushirikisha ngazi za chini katika mipango.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya serikali kwa namna moja ama nyingine imekua ikiathiriwa na maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wa Serikali. Mathalani kama Halmashauri ilipanga kukusanya kodi kupitia kwenye masoko au mazao inaathiriwa na agizo linalotolewa katikati ya mwaka wa fedha kuwa vyanzo hivyo visiendelee kutozwa kodi. Taarifa zilizopo ni kuwa Halmashauri kama ya Wilaya ya Mvomero inayumba kimapato kwa sababy agizo la Rais kufuta tozo kwenye mazao kulingana na kiasi alichonacho mkulima au mfanyabiashara lilitolewa katikati ya mwaka wa Bajeti jambo lililopelekea Halmashauri kukosa mapato ya ndani ambayo walishajipangia. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuacha kutoa maelekezo ambayo yanaathiri bajeti za Halmashauri na wakati huo huo ni Serikali hiyo hiyo iliyokubali mipango ya Halmashauri hizo kabla ya kupitishwa na Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zinazozikabili Halmashauri nchini kutokana na maelekezo ya serikali, kumekuwa na tatizo la maelekezo kutoka Hazina kuhusu vipaumbele vya bajeti. Ofisi ya Katibu Mkuu Hazina imekuwa ikitoa maelekezo kuhusu vipaumbele vya mpango na ukomo wa bajeti bila kwanza kupitia na kuchambua mapendekezo ya mamlaka za serikali za mitaa.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu huu wa serikali unazifanya Halmashauri kusubiri na kupokea maelekezo kutoka serikali kuu na ndiyo maana serikali imekua na audacity ya kuondoa hata vyanzo vya mapato ya Halmashauri katikati ya mwaka wa bejeti kama wanavyotaka kinyume na utaratibu wa kibajeti. Hali hii inamaanisha kuwa serikali inavunja sheria kwa sababu bajeti ya serikali ikishapitishwa na Bunge inapitishwa pamoja na sheria ya fedha pamoja na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali ambapo sheria hiyo inayotoa ruhusa kwa serikali kutumia mafungu ya bajeti kama yalivyopitishwa na Bunge (The Appropriation Act).
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha ameamua kujipangia utaratibu wake binafsi wa kuhakiki tena maombi ya fedha za Wizara, Idara na Wakala wa serikali hata baada ya Bunge lako tukufu kuipitisha kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti. Waziri wa fedha anajitetea kwa kifungu cha 10 cha Sheria ya Bajeti ambacho kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hakiondoi mamlaka ya Bunge kuchambua, kujadili na au kurekebisha bajeti ya serikali.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bajeti kifungu cha 27 kinamtaka Waziri kuhakikisha kuwa anaandaa vizuri matumizi ya serikali kwa usahihi kwa ajili ya kupitishwa na Bunge. Kitendo cha Waziri wa Fedha kuweka tena utaratibu wa kuhakiki maombi ya fedha ambazo zimeidhinishwa na Bunge kama ambavyo ameendelea urudia kauli yake kuhusu utaratibu huo inathibitisha kuwa yeye anaona anayo mamlaka makubwa kuliko Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, katika hili sio tu kuwa Waziri anadharau mamlaka ya Bunge lako tukufu kwa kuhakiki tena maombi ya fedha ambazo zimepitishwa na Bunge bali pia anakiuka maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambao kwa mujibu wa kifungu cha 19(1)(e)(f) cha Sheria ya Bajeti ambalo hujadili na kuridhia masuala yote ya mapato na matumizi ya serikali kabla ya kuwasilishwa katika Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, athari wa kile Waziri wa Fedha na Mipangp anachokiita “uhakiki” kinaonekana kwenye utoaji wa fedha za maendeleo katika Wizara mbalimbali ambapo miradi mingi inasuasua na wakandarasi na au watoa huduma wamekuwa wakidai fedha zao kwa muda mrefu bila mafanikio na wanachoelezwa ni kuwa wanatakiwa kusubiri uhakiki ukamilike.
Mheshimiwa Spika, jambo hili la uhakiki linamfanya Waziri wa Fedha kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kama hisani na sio kwa mujibu wa Sheria na taratibu tulizojiwekea. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwa Bunge kupitia Kamati ya Bajeti kuingilia kati utaratibu huu na ikiwezekana kupendekeza azimio la Bunge kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango kuacha mara moja utaratibu huu ambao unaenda kinyume na Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Haiwezekani Bunge lako tukufu kama muhimili liidhinishe bajeti alafu kuwe na mamlaka nyingine tena ambayo inafanya kazi hiyo hiyo, hii maana yake ni kuwa Bunge halina haja ya kuichambua na kuipitisha bajeti kama kuna mamlaka nyingine ambayo hufanya tena kazi ile ile pengine tofauti na kile kilichoidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia au utaratibu wa kuzuia wananchi, vyombo vya habari au hata Wabunge kuhoji baadhi ya masuala ambayo yana harufu au tuhuma za ufisadi kwa kigezo kuwa jambo husika linahusiana na masuala ya ulinzi na usalama ambayo ni masuala yanayotakiwa kuwa ya siri kwa ajili ya usalama wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa pia kuwa hata wakati wa kashfa za Makampuni ya TANGOLD, MEREMETA, KAGODA, DEEP GREEN, baadhi ya viongozi wa serikali wakati huo walinukuliwa na vyombo vya habari wakidai kuwa masuala mengine yanayohojiwa na Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla hayatakiwi kujibiwa kwa sababu yanahusiana na ulinzi na usalama wa nchi.
Mheshimiwa Spika, kama ulinzi na usalama ni kuchota fedha za umma au kuingia mikataba mibovu inayoligharimu taifa, ni wazi kuwa sio ulinzi na usalama wenye tija kwa manufaa kwa wananchi bali ni mzigo mkubwa kwa walipa kodi na pia ni kwa manufaa ya wachache.
Mheshimiwa Spika, Naomba kurejea suala la Kivuko cha MV DAR-ES-SALAAM. Itakumbukwa kuwa tarehe 17 Novemba, 2014 aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati huo John Pombe Magufuli alizindua kivuko cha majini (MV DAR-ES-SALAAM) kwa alichokiita mkakati wa kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam ambapo Kivuko hicho kilitarajiwa kutoa huduma ya usafiri wa majini kwa wakazi wanaoishi katika mwambao wa Bahari ya Hindi hasa kutoka Dar-es-Salaam hadi Bagamoyo Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Spika, wakati wa uzinduzi Waziri wa Ujenzi wa wakati huo John Pombe Magufuli alinukuliwa akieleza kwa mbwembwe sifa za Kivuko hicho ikiwa ni pamoja na uwezo wa kubeba abiria 309 hadi 400 wakiwa wamekaa, speed kubwa kuliko vivuko vyote Afrika Mashariki na kuwa kilikuwa kinatumia teknolojia ya kisasa kwa kuwa kimetengenezwa na mkandarasi kutoka Denmark na kiligharimu Tshs. bilioni 7.9.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi tulieleza kuwa pamoja na gharama hizo za kivuko za takribani bilioni 8 na sifa alizoeleza Waziri, ukweli ni kuwa Kivuko kilikuwa hakina speed kama ilivyokuwa imeelezwa na ukweli ni kuwa kilikuwa kinatumia masaa matatu kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam jambo lililowafanya wananchi kukataa kukitumia.
Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani ulionyesha kuwa Kampuni ya Azam inamiliki Boti za mwendo wa haraka ambapo kutoka Dar hadi Zanzibar zinatumia muda wa dakika 90, abiria 500 na bei zake ni kuanzia bilioni 4 hadi 5.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tuliliomba Bunge lako tukufu kuunda Tume kwenda kuchunguza ununuzi wa kivuko hicho ambacho iliaminika kuwa ni kibovu na cha kizamani kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kwa siku kikiweza kwenda Dar es Salaam mara moja tu na kurudi Bagamoyo mara moja tu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na taarifa kuhusu Kivuko cha MV Dar-es-Salaam kutolewa katika Bunge lako tukufu Rais John Pombe Magufuli aliamua kukitoa Kivuko hicho kwa Jeshi la Wananchi ili kitumike katika doria za majini na Rais alionya wale waliokuwa wanaendelea kuhoji kuhusu kivuko hicho kuacha kwa sababu sasa ni kifaa cha Kijeshi.
Mheshimiwa Spika, pamoja kitisho hicho cha Rais, Kambi Rasmi ya Upinzani katika hotuba yake ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/18 ilieleza kuwa Kivuko hicho kilikuwa hakiwezi kutumiwa hata na Jeshi letu kwa sababu kilitengenezwa kinyume na makubaliano hasa suala la speed.
Mheshimiwa Spika, kwa agizo la Rais kuwa suala la Kivuko cha MV Dar-es-Salaam lisijadiliwe kwa sababu kimekuwa kifaa cha kijeshi ni ishara kuwa hata majibu yanayotolewa na serikali kuwa yapo masuala mengine hayatolewi ufafanuzi kwa sababu za kiusalama ni mkakati wa serikali kujificha katika kivuli cha ulinzi na usalama ili kulea ufisadi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule kuchunguza sakata la Kivuko cha MV DAR-ES-SALAAM ili kuhakikisha kuwa ukweli kuhusu gharama na tuhuma za Kivuko hicho kuwa kibovu zinafanyiwa kazi na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa Sheria. Ni wazi kuwa serikali hii inayojinasibu kuwa ni ya waadilifu watafurahia uchunguzi wa Bunge na kuyafanyia mapendekezo ya Kamati Teule.
Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja uliopita tulipozungumza juu ya suala la makinikia na utapeli wa ccm tulitukanwa na kupewa majina mengi sana kwamba sisi si wazalendo, tukaambiwa sisi ni mawakala wa mabeberu, tumehongwa na tukaambiwa kwamba Serikali inaidai kampuni ya Accasia ya kodi inayofikia trilioni 423 na tukaambiwa kwamba fedha hiyo inatosha kumnunulia kila mtanzania gari aina ya Noah Mwaka mmoja baadaye, Waziri wa Sheria na Katiba anatoa kauli bungeni kwamba Serikali haiwezi kuweka hadharani mapato yaliyotokana na makubaliano na makampuni ya madini baada ya Serikali kudai kuwa inatapeliwa.
Mheshimiwa Spika, Tulimsikia Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Dr. Palamagamba Kabudi akiliambia Bunge kwamba Serikali ya Rais John Magufuli haitatoa hadharani, taarifa zinazohusu fedha tulizolipwa na makampuni ya kigeni ya madini. Serikali ya Magufuli inahofu kwamba fedha hizo zikitangazwa hadharani basi wadai wetu mbalimbali watatufungulia kesi nyingi za madai, kwa sababu watajua sasa tuna fedha.
Mheshimiwa Spika, Aidha, fedha hizo hazitalipwa kama maduhuli ya Wizara ya Madini. Maana yake ni kwamba taarifa ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini inayotolewa Bungeni kila mwaka, haitaonyesha mapato yanayotokana na madini.
Mheshimiwa Spika, Kwenye suala hili na kwa kauli hii ya Waziri Kabudi, sasa ni wazi kwamba Serikali ya Magufuli haina nia njema na umakini katika usimamizi wa rasilimali za nchi yetu hasa madini na hivyo kutokuwa tofauti na serikali zilizotangulia ambazo zimetufikisha hapa leo. Hii ni kutokana na sababu mbalimbali kadiri tutakavyofafanunua;
Mheshimiwa Spika, Mosi, Usiri ulitawala masuala yote ya leseni, mikataba na malipo serikalini yaliyotokana na uchimbaji madini wakati wote wa tawala za Rais Kikwete na Mkapa. Bunge lilinyimwa kuangalia na kuchunguza mikataba ya madini kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Spika, Pili, Usiri huu ulitengeneza mazingira yaliyozaa mikataba mibovu na ufisadi mkubwa katika sekta ya madini, ulioligharimu taifa letu mabilioni ya fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, Kwa kauli ya Prof. Kabudi, usiri huu sio tu utaendelea, bali sasa utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu leseni za uchimbaji madini zitatolewa na Baraza la Mawaziri, badala ya watendaji wa serikali. Kama inavyojulikana, majadiliano na maamuzi ya Baraza la Mawaziri ni siri kwa mujibu wa sheria zetu na Mawaziri wote hula kiapo cha kutunza siri hizo. Usiri unaopigiwa upatu na Prof. Kabudi unavunja wazi wazi Sheria za Rasilmali za Nchi zilizopitishwa kwa mbwembwe kubwa na majidai mengi Bungeni mwaka jana. Mpiga Mbwembwe Mkuu alikuwa Prof. Kabudi mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 12 cha Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali za Asilia ya 2017 kinaruhusu Bunge kupitia mikataba yote inayohusu uchimbaji (extraction), utumiaji (exploitation) au upataji (acquisition) wa utajiri na rasilmali asilia kupitiwa na Bunge. Sasa, kwa kauli ya Prof. Kabudi, haitawezekana tena kwa Bunge kuipitia mikataba hiyo na hivyo kuiweka hadharani kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Wakati Prof. Kabudi akidai mbele ya Bunge lako tukufu kwamba itakuwa ni marufuku kwa Serikali kuingia mikataba ya uendelezaji madini (Mineral Development Agreements – MDAs) kwa sababu mikataba hiyo imetuletea matatizo mengi sana, vifungu vyote muhimu vya Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali Asilia vinahusu utaratibu wa ‘mikataba’ ya utajiri na rasilmali asilia, ikiwemo madini. Angalia tafsiri ya maneno ‘arrangements or agreement’ katika kifungu cha 3. Vifungu vingine husika vinavyohusika na mikataba ni 5(4), 6, 7, 8, 9, 10(1), 11(3) na 12.
Mheshimiwa Spika, Ni sahihi kusema kwamba Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilmali Asilia imeweka utaratibu mpya wa ‘mikataba’, wakati Prof. Kabudi anadai mbele ya Bunge hili kwamba kuanzia sasa ni marufuku kuingia mikataba ya uendelezaji madini.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 5(2) cha Sheria hii kinasema kwamba “utajiri na rasilmali asilia zitashikiliwa na Rais kama dhamana kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano.” Haya pia ni masharti ya kifungu kipya cha 5(1) cha Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa mwaka uliopita.
Mheshimiwa Spika, mbali na Sheria ya Ardhi ya 1999, hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kujitwalia kisheria umiliki wa utajiri na rasilmali asilia zote za nchi yetu, ikiwemo madini. Ukijumlisha na kauli kwamba sasa leseni zote za madini na, by extension, utajiri na rasilmali asilia nyingine zote zitatolewa na Baraza la Mawaziri, kuna mashaka kuwa sasa madili yote ya kifisadi yatahamia Ikulu na hatutayajua, kwa sababu tukiyajua wadai wetu watatushtaki mahakamani!
Mheshimiwa Spika, Utaratibu huu wenye sura ya kifisadi kwenye masuala ya rasilmali asilia za nchi yetu haukuwepo kabisa wakati wa Rais Kikwete na Mkapa, ambao ndio wanaowajibika kwa kiasi kikubwa na hali aliyoikuta Magufuli alipoingia madarakani.
Mheshimiwa Spika, Msimamo wa sasa wa Serikali unakinzana moja kwa moja na matakwa ya Sheria ya Kupitiwa na Kujadiliwa Upya kwa Masharti Yasiyofaa ya Mikataba ya Utajiri na Rasilmali Asilia ya 2017 (The Natural Wealth and Resources Contracts (Review na Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017). Wakati Prof. Kabudi akisema mbele ya Bunge hili kwamba itakuwa ni marufuku kwa Serikali kuingia mikataba ya uendelezaji madini, Sheria hii yote inahusu kupitiwa na kujadiliwa upya kwa mikataba iliyopo sasa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ikiwa haitaki mikataba hii na fedha zinazopatikana kwa mujibu wake zijulikane kwa wananchi kupitia kwa wabunge wao, kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinasema: “Kwa ajili ya utekelezaji kwa ufanisi wa kazi zake za usimamizi na ushauri zilizotajwa chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba, Bunge linaweza kupitia taratibu zozote au makubaliano yaliyoingiwa na Serikali kuhusiana na utajiri na rasilmali asilia.”
Mheshimiwa Spika, Aidha, Kifungu cha 5(1) kinaitaka Serikali kupeleka Bungeni mikataba yote ya utajiri na rasilmali asilia iliyoingiwa na Serikali ndani ya siku sita za Mkutano wa Bunge unaofuata kuingiwa kwa mikataba hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kwa vile Prof. Kabudi amekiri kwamba Serikali imekwishaingia makubaliano ya msingi na Barrick Gold kuhusu makinikia ya Bulyanhulu na Buzwagi; na pia na Tanzanite One kuhusiana na tanzanite ya Mererani, Serikali inawajibika kisheria, na wabunge wanatakiwa kudai, kuwasilishwa mikataba hiyo Bungeni katika Mkutano huu wa Bunge, ili Bunge liweze kuipitia na, ikihitajika, kuishauri Serikali kuanzisha majadiliano mapya kuhusu mikataba hiyo, kama inavyotakiwa na vifungu vya 5(2) na (3) vya Sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kutofanya hivyo ni kuendeleza ufisadi na usanii ule ule wa miaka ya Rais Kikwete na Mkapa ambao serikali hii inajidai kuwa inapambana nao.
Mheshimiwa Spika, Prof. Kabudi amesema ndani ya Bunge hili kwamba kuanzia sasa leseni zote za uchimbaji madini zitatolewa na Baraza la Mawaziri. Itambulike kuwa Baraza la Mawaziri halijatajwa mahali popote katika Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa mwaka jana. Badala yake, wajibu wa kutoa leseni zote za uchimbaji madini umekabidhiwa kwa Tume ya Madini, kwa usimamizi wa Waziri wa Madini. Angalia kifungu kipya cha 19(f) cha Sheria ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini ndiyo yenye uwezo wa kusimamisha au kufuta kabisa leseni yoyote ya madini. Angalia kifungu kipya cha 24(m) cha Sheria ya Madini. Itakuwa maajabu ya Tanzania kwa Tume iliyoteuliwa na Rais kufuta leseni iliyotolewa na Baraza la Mawaziri linaloongozwa na Rais.
Mheshimiwa Spika, Haya ndiyo mambo ya awamu ya tano na watu wao wanaojifanya kwa wananchi kuwa ndio watetezi wa madini na rasilmali asilia za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa huu ni utaratibu wa kuwahadaa wananchi na unaweza kuwa ni usanii mtupu. Ni ukiukaji mkubwa wa sheria walizozipitisha wenyewe na wanazozipigia debe kila kukicha. Ni maandalizi ya ufisadi mkubwa zaidi; au mwendelezo wa ufisadi wa miaka ya Rais Kikwete na Mkapa kwenye sekta ya madini. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa Bunge na Waheshimiwa wabunge na Watanzania wanatakiwa kuyaelewa haya na kuyachukulia hatua haraka kabla nchi yetu haijaingia kwenye hasara kubwa.
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Machi 2, 2017, Wizara ya Nishati na Madini iliandika barua kwa umma kuwajulisha wafanyabiashara na makampuni yanayojishuhulisha na shughuli za uvunaji wa madini kuacha mara moja shughuli za usafirishaji wa makinikia (concentrates) na mawe yenye madini ya metaliki kama vile dhahabu, shaba, nikeli na fedha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na katazo hili Rais aliunda kamati mbili za uchunguzi wa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Pamoja na mambo mengine ripoti zote zilizungumzia hasara kubwa tunayoipata kama taifa kutokana na sheria mbovu za madini na mikataba mibovu iliyoingiwa baina ya serikali ya ccm na wawekezaji. Ripoti zote mbili zilijikita zaidi katika kubaini viwango vya madini vilivyopo katika makinikia na mikataba ya uchenjuaji ambayo haikuwa wazi.
Mheshimiwa Spika, sakata la makinikia lilikuwa ni sakata la kisiasa lililojawa na ahadi nyingi hewa ambapo mpaka sasa linaigharimu serikali kutokana na maamuzi hayo ya kukurupuka. Kwa takribani miaka zaidi ya 20 Wabunge kutoka vyama vya upinzani walikuwa wakidai uwepo wa uwazi katika mikataba ya madini na ubovu wa mikataba mingi ikiwemo mkataba wa Buzwagi, Resolute, Bulyanhulu n.k. Katika awamu tofauti za serikali Mawaziri ambao ndio watendaji wakuu wa serikali walikuwa walilifumbia macho pamoja na kupigiwa sana kelele.
Mheshimiwa Spika, katika tume ya Jaji Bomani, iliainisha mapungufu makubwa katika mikataba ya madini ambayo iliruhusu upenyo wa ukwepaji kodi na ikiwemo ukwepaji wa mrabaha, usiri katika uendeshaji wa biashara ya madini nchini na rushwa. Japokuwa Sheria zilikuwepo, tatizo kubwa lilikuwa katika mikataba ambayo serikali iliingia na makampuni ya madini. Mfano Mwaka 1997 mpaka 2009 hakuna kampuni hata moja iliyolipa kodi ya mapato. Mathalani kampuni ya Resolute iliyokuwa inachimba dhahabu katika mgodi wa Lusu iliyochimba dhahabu kwa takribani miaka 14 ililipa kodi kwa kipindi cha miaka 2 tu kabla ya kufunga mgodi. Pamoja na hilo katika ripoti ya Makinikia ya mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagwi unaonyesha kuwa kampuni ya Acacia ambayo ndiyo mmiliki wa migodi hiyo ilikuwa ilkidaiwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kiasi cha dola za Marekani 190 bilioni sawa na zaidi ya trilioni 424 ambayo ni kodi iliyokuwa ikikwepwa pamoja na riba
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kiasi hiki cha fedha kiliwafanya watanzania kuwa na matumaini makubwa wengi wao wakiamini kila Mtanzania ataweza kumiliki gari aina ya Naoh na wengine wakiamini huduma za kijamii zitapatikana bure. Katika sakata zima la makinikia lililoihusisha kampuni ya Acacia serikali imeendelea kuyafanya yale yale ambayo iliifanya Mwaka 2007. Hii ni kutokana na kwamba Acacia waliikana taarifa iliyotolewa na serikali kuwa haijawahi kukwepa kodi na huilipa serikali 4% ya mirahaba ya dhahabu, shaba na fedha kwenye makinikia kama ilivyo kwenye makubalino baina ya serikali na Acacia.
Mheshimiwa Spika, tutakumbuka Mwaka 2007, kampuni hii ilituhumiwa kukwepa kodi na hivyo kuzua mtafaruku mkubwa na serikali wakati huo. Katika makubaliano Barrick iliilipa serikali kiasi cha dola milioni 700 kama kishika uchumba wakati mazungumzo zaidi yakiendelea ili kuona ni namna gani nchi itanufaika. Kuanzia kipindi kile matatizo na lawama za ukwepa kodi zimeendelea. Katika sakati hili la makinikia serikali imefanya yale yale kwani imepokea kiasi cha dola milioni 300 tenakama kishika uchumba. Hii ni pungufu ya mil 400 iliyopatikana mwaka 2007.Kwa maana hiyo timu ya makubaliano (negotiation team) imeshindwa hata kufikia kiwango cha milioni 700 kilichotolewa takribani miaka 10 iliyopita. Madhaifu haya ya kufanya majadiliano ya dili za kibiashara yanashindwa kutoa majibu chanya kutokana na kwamba watu waliolitengeneza tatizo hao hao ndio wanaotumwa kwenda kutafuta suluhu ya tatizo.
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika ripoti ya makinikia ilianisha takribani aina 11 za madini yaliyopo katika makinikia , serikali ilikubalina na Acacia kulipa asilimia 4 ya mrabaha tu bila kuangalia aina nyingine za madini yaliyo katika makinikia. Hii yote ni kutokana na mikataba mibovu na utendaji kazi uliokosa ufanisi katika taasis mbalimbali za serikali zinazojishughulisha na madini. Mpaka sasa serikali inazungumzia madini ya dhahabu, fedha na shaba pekee. Kamati ya makinikia ilianisha aina nyingine za madini kutoka kwenye nyaraka za usafirishaji wa makontena yaliyokamatwa bandari ikiwa ni pamoja na Sulfur, Chuma na madini mkakati (strategic metals) yaani iridium,rhodium,ytterbium,beryllium,tantalum na lithium)
Mheshimiwa Spika, kabla ya serikali kutoa zuio la kusafirisha makinikia nje ya nchi, kulikuwa na mazungumzo yanayoendela baina ya kampuni ya Acacia na kampuni ya Endeavour Mining kutoka nchini Canada. Mazungumzo hayo yaliyoanza mwezi January 2017, yalikuwa kuhusu kuuza kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara. Katika hatua za awali za majadiliano hayo kampuni ya Endeavour ilitaka kuinunua Acacia kwatakribani paundi bil 3, sawa na dola bil 4.4.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na mauziano hayo (Transfer of shares) Tanzania ingeweza kupata capital gain tax. Kutokana na zuio lililowekwa na serikali ya Tanzania dhidi ya kampuni ya Acacia iliilazimu kampuni ya Endeavour kusitisha majadiliano. Hivyo nchi ilipoteza takribani dola 880 mil sawa na shiling trilioni 1.8 ambayo ni 20% ya mauziano kama mpango huo wa mauziano ungefanikiwa. Hivyo kauli za kisiasa na maamuzi yasiyopimwa yamelisababishia taifa kukosa 1.8 trilioni ambayo ni zaidi ya bajeti ya kilimo ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, baada ya kutolewa kwa ripoti ya makinikia tarehe 22/09/2017 kampuni ya Acacia ilitoa tangazo kuhusu kubadilisha mfumo wa uchenjuaji mbale, .Hii ni kutokana na utafiti uliofanywa na Wakala wa Jiolojia (GST) katika mgodi wa Buzwagi ili kuhakiki ufanisi wa mfumo huo mpya (mbale) wa kuchenjua dhahabu ili kubaini kama serikali inapata faida au hasara.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa GST 2018, wakati mgodi wa Buzwagi ukiwa unazalisha makinikia mgodi huo ulikuwa unazaisha dhahabu kilo 28, fedha kilo 5 na shaba tani 18.9 kwa siku. Baada ya kubadili mfumo wa uchenjuaji kwa sasa unazalisha dhahabu kilo 23.5,fedha kilo 0.24 na shaba kilo 1.6 pekee kwa siku. Baada ya kutumia mfumo huu mpya uzalishaji wa dhahabu umepungua kutoka asilimia 97 mpaka asilimia 87 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu mpya wa uchenjuaji unasababisha kupotea kwa madini ya fedha na shaba . Hivyo kwa mfumo huu serikali inapata hasara kubwa tofauti hapo awali. Mauzo ya dhahabu hapo awali ilikuwa ni 95% ya mapato ya jumla,na 70% ni kutoka kwenye mauzo ya tofali za dhahabu, na 25% hutoka kwenye dhahabu iliyomo ndani ya makinikia. Iliyobaki 5% ya mapato ni kutokana na shaba iliyomo katika makinikia na kiasi kidogo tu cha fedha. Kwa maana hiyo kwa sasa kampuni inapoteza 30% ya jumla ya mapato. Na karibia 50% ya mapato ya pamoja ya Bulyanhulu na Buzwagi.Kwa katazo la kusafirisha makinikia tunapoteza mapato ya zaidi dola mil 1 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, kwa mfumo huu mpya wa uchenjuaji unasababisha pia mabaki ya fedha na shaba kuchanganywa na mabaki ya zamani ambayo hayakuwa yanasafirishwa kwa kuwa hayakuwa na madini yoyote au kiwango kidogo sana cha madini. Mchanganyiko huo (dilution) unasababisha serikali kupata hasara kwa kuwa mali iliyopo katika makinikia inapotea.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Bunge lilipitisha Sheria mpya ya Mamlaka ya Nchi kuhusu umiliki wa Maliasili (The natural Wealth and Resources –Permanent Sovereignity 2017), iliyoletwa kwa hati ya dharura ndani ya Bunge na kujadiliwa kwa dharura katika kifungu cha 9 (1) kimeweka masharti kuwa shughuli zote za uzinduaji, uchimbaji na upatikanaji au utumiaji wa rasilimali utahakikisha kuwa hakuna rasilimali ghafi itakayosafirishwa nje ya Tanzania. Maana yake ni kuwa hata makinikia yasisafirishwe nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, maana yake ni kuwa nchi inapaswa kuwa na uwezo wa kufanya uchenjuaji hapa hapa nchini. Kuanzia mwaka 2011 serikali kupitia TMAA ilifanya upembuzi yakinifu(visibility study) ya uwezekano wa kujenga kinu cha uchenjuaji (smelting) hapa nchini. Baada ya upembuzi huo serikali ilitoa ripoti kuwa kujenga kinu cha uchenjuaji hakina faida ya kibiashara kwa nchi. Mwaka jana (2017) Waziri Mkuu alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mbeya, alitembelea mgodi wa Sunshine Group uliopo Chunya. Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji ili kuona namna ya kujenga mitambo ya kuchenjulia makinikia.
Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza ni kuwa,kama serikali ilifanya tathimini Mwaka 2011 na ikaja na majibu kuwa makinikia hayana faida hivyo hakukuwa na sababu ya kujenga kiwanda hapa nchini na kwa sasa tunaona serikali inaweza kupata faida kupitia makinikia, Je, serikali imechukua hatua gani ya kuwawajibisha wataalamu wale waliolisababishia hasara Mwaka 2011 kwa kuishauri serikali vibaya? Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama serikali imefanya tena upembevu yakinifu juu ya kujenga kiwanda cha uchenjuaji nchini na ripoti ya upembuzi huo inasemaje. Pamoja na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua mazungumzo baina ya serikali na Kampuni ya Sunshine Group yamefikia wapi?
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 60,000 za makinikia. Kwa kawaida viwanda vya uchenjuaji (refinery) huhitaji takribani tani 150,000 za makinikia. Hivyo, mpaka sasa bado hatujawa na utoshelevu wa malighafi ya makinikia kama ambavyo wataalamu mbalimbali wameainisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni aina gani mbadala ya teknolojia mbayo serikali itaitumia ili kuweza kufanya uchenjuaji wa kiwango hicho ambacho kinazalishwa nchini. Vilevile, ni muhimu kutambua kwamba uchenjuaji hufanyika kutokana na aina ya miamba.Kila aina ya miamba hutegemea aina fulani ya uchenjuaji.mfano, uchenjuaji unaofanyika mkoani Mara na maeneo ya Geita hatua zote huweza kufanyika mgodini na kuzalisha matofali ya dhahabu hii ni tofauti na Buzwagi na Bulyanhulu ambapo dhahebu yenyewe ndio bidhaa muhimu.
Mheshimiwa Spika,vilevile, ili kuweza kuendesha mitambo ya uchenjuaji ni lazima nchi iwe na umeme wa uhakika. Mpaka sasa tuna takribani megawati 1,500 ambazo hazitoshelezi mahitaji hususani mahitaji ya viwandani. Mpaka sasa serikali haijachukua mbinu mbadala katika uzalishaji wa umeme. Umeme unaotegemewa zaidi nchini unatokana na maji (hydro power). Hivyo serikali ni lazima ifanye uwekezaji wa kutosha katika vyanzo vingine vya umeme ikiwemo umeme wa upepo. Mpaka sasa upepo unaoweza kuvunwa katika maeneo ya Same, Singida na Makambako tuna uwezo wa kuzalisha takribani megawati 5,000 ambao utaweza kutusaidia katika viwanda kwa kuanzia. Hata hivyo, ni muhimu zaidi kuwekeza katika umeme wa jua (solar power) ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo vyanzo vingi vya maji vinakauka kutokana na kukata miti na kuongezeka kwa hewa ya ukaa.
Mheshimiwa Spika, Ni aibu kwamba ingawa Washirika wa Maendeleo toka nje wameendelea kupunguza kwa kasi kiasi chao cha mikopo na misaada, bado bajeti za Serikali ya CCM zimendelea kuongeza kiasi cha utegemezi wa mikopo na misada toka huko bila kutatua msingi wa tatizo la kukwama huko. Tangu mwaka 2014/15 Nchi za Ulaya zimekuwa kwenye mahusiano mabovu na taifa letu kutokana na Serikali kushindwa kusimamia misingi ya utawala bora na Demokrasia kama sharti lao muhimu katika ushirikiano. Ni katika msingi huo Tanzania imekosa fedha toka Millenium Challenge Accounts (MCC II) zaidi ya 1trilion, ambapo nchi kama Ghana wamendelea kupata.
Mheshimiwa Spika, Kwasababu ya kuharibu uchaguzi mkuu zanzibar, Sheria mbovu ya makosa ya mitandao, kuliweka bunge gizani, Kuzuia mikutano ya kisiasa kwa vyama kinyume cha Katiba, yote hii imesababisha mahusiano mabovu kati ya Tanzania na nchi washirika wa maendeleo na ndio sababu ya kukwama kwa mikopo nafuu kutoka mataifa hayo pamoja na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, Kibaya zaidi wakati Serikali ikikwama kupata mikopo nafuu kutokana na udikteta, bado pia imeshindwa kupata mikopo ya kibiashara kwasababu ya uzembe na kutojipanga. Nchi za Kenya na Rwanda imekuwa rahisi kupata mikopo ya kibiashara toka nje kupitia Eurobond/International Bond kwasababu zimeshakikiwa kuhusu uwezo wake wa kukopa.
Mheshimiwa Spika, Tanzania tangu zama za Mhe Mkulo kama waziri wa fedha mpaka Mgimwa na baadae Saada Mkuya na sasa Dr Mpango inapiga stori za kufanyiwa uhakiki wa uwezo wake kukopesheka(CREDIT RATING).Huu ni mfano wa namna tulivyo na Serikali isiyo na akili ya kibiashara. Duniani kote kuna Agency tatu zinazofanya kazi hii, ambazo ni Moodys, Standard&Poor na Fitch, kwa muda mrefu kumekuwa na mazungumzo yasiyokwisha kuhusu kampuni ya Moodys kufanyia uhakiki uchumi wetu lakini hakuna kinachoendelea. Ni vema Serikali ikakamilisha mazungumzo hayo yasiyokwisha kwani uwezekano wa Tanzania kuendelea kupata mikopo ya kawaida toka nje umezidi kufifia.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza hili kwani hata ripoti ya IMF ya Januari 9,2017, kuhusu mwenendo wa uchumi wetu imesisitiza hili, kwamba ni lazma Serikali ihakikishe inapata mikopo toka nje ili kutekeleza miradi mikubwa ya kibajeti kwakuwa ukosefu wa fedha hizo kwenye miradi hiyo ni moja ya sababu za ukata kwenye uchumi kwani imepunguza mzunguko wa fedha kwa kiasi kiubwa nchini.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kiasi kikubwa cha rasilimali lakini kwasababu ya ukosefu wa uongozi wenye maono bado rasilimali hizo hazijaweza kuliondoa taifa kwenye lindi na umasikini. Idadi ya watanzania masikini imezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka badala ya kupungua.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Poverty &human Development, inaonesha kwamba tangu kama taifa tuanze marekebishoya Uchumi (economic restructuring) katika miaka ya 1990, umaskini Tanzania ulikuwa asilimia 39% wakati idadi ya watu ilikuwa milioni 25, sawa na masikini milioni 9.750,000 na sasa kiasi cha umasikini ni asilimia 28, wakati idadi ya watu imefikia milioni 48, sawa na masikini milioni13.44.
Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa ya kuendelea kuongezeka kwa masikini ni sera mbovu mtazamo finyu wa CCM katika kujua mahitaji ya Taifa na namna ya kuweka vipaumbele ili kufikia malengo. Badala yake imebaki chama kilekile kinabadilisha majina ya awamu na watawala bila kubadili mbinu zenye kuleta majawabu ya matatizo ya umasikini wetu watanzania. Moja ya Agenda kwa Afrika kwenye mwaka huu kwenye World Economic Forum, ilikua ni “AFRICA FORGET ABOUT NATURAL RESOURCES BUT TECHNOLOGY”.
Mheshimiwa Spika, Naamini kama Mhe Rais angeshiriki mkutano huu wa kimkakati angeweza kupata mawazo zaidi ya dunia imefikia wapi na inahitaji nini kwasasa. Dunia kwasasa inahitaji tuwekeze zaidi kwenye kujenga rasilimali watu zaidi ya vitu. Ni utawala wa ajabu unaweza kuacha kuboresha elimu ya vijana wake ikatumia fedha hizo kununua ndege au kujenga barabara. Ndio maana sisi kama CHADEMA/UKAWA tulisistiza na tunaendelea kusisitiza kuwa Mradi pekee wa kimkakati kukwamua Taifa hili hapa ni kusuka mfumo wa elimu na kuhakikisha vijana wanapata elimu bora itakayowawezesha kushiriki dunia ya ushindani kama wadau sio watazamaji. Tunapaswa kujenga Taifa la watu ambao wanaweza kukabili maisha hata nchi hii ikigeuka kuwa jangwa lisilo na rasilimali yoyote kama ilivyo Israel. Inasikitisha kwamba huduma ya elimu nchini kuanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu imebaki vurugu tupu. India ambayo miaka ya 1970tulikuwa nayo sawa kiuchumi, sasa inauza wataalamu wake nchi za Ulaya na marekani, wakati sisi bado tunauza mchanga, tumbaku na ngozi.
Mheshimiwa Spika, eneo la Liganga linakadiriwa kuwa na makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 428 kiwango ambachi kinaweza kutumika kwa takribani miaka 500 (Kwa mujibu wa utafiti wa NDC),na chuma tani milioni 126.
Mheshimiwa Spika, Tangu awamu ya tatu mpaka ya nne kumekuwa za masimulizi yasiokwisha kuhusu namna kuvuna utajiri huu wa makaa ya mawe na chuma.Lakini kwasababu ya mtazamo finyu kibiashara, awamu zote zimekuja na kuondoka na kuacha masimulizi hayo. Awamu ya tano, kwenye bajeti 2016/17, iliahidi kufanyia kazi suala hili, lakini ni bahati mbaya sana, maelezo kwenye kitabu cha utekelezaji wa bajeti, yanatoa picha kwamba hakuna jipya zaidi ya mwendelezo wa masimulizi.
Mheshimiwa Spika, Akiba hiyo ya chuma na makaa ya mawe ni biashara kubwa na kama Serikali ingeweka mkazo kukamilisha utaratibu wa kukamilisha miradi hiyo miwili kwa pamoja Tanzania ingeweza kufikia kiwago cha kuuza nje sio chini ya tani milioni 2 za chuma na makaa ya mawe, na kuvuna dola za kutosha kuendesha nchi hii. Ilikuvuna chuma, inahitajika umeme zaidi ya 250MW, wakati mradi uliokwama wa kuzalisha makaa ya mawe Liganga unaweza kuzalisha kwa kuanzia zaidi ya 600MW, kiasi ambacho kingetosha kuendesha mtambo wa kufua chuma na kubaki na ziada ya umeme ya 350MW.
Mheshimiwa Spika, Laiti kama tungekuwa na Uongozi makini, miradi hii miwili ilipaswa kuwa ya kwanza na yenye kupewa kipaumbele kabla hata ya kujielekeza kwenye ujenzi wa reli. Hii inatokana na ukweli kwamba ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa zaidi ya 2,400km itakayogharimu zaidi ya dola million 7,000, utahitaji mamilion ya tani za chuma, kiasi ambacho kama tungekuwa tumekamilisha mradi huo wa chuma tungeweza kupunguza gharama hizo kwa kiasi kikubwa na mradi huo ungekuwa soko kubwa kwa mradi wa chuma, kuliko sasa ambavyo Serikali itakapoanza ujenzi wa reli na kuhitaji kutumia fedha za kigeni kuagiza chuma nje na kwa bei ambayo ni kubwa ukilinganisha na kama ingenunua chuma nchini
Hivyo ni ushauri wa Kambi rasmi ya upinzani kwamba serikali ikamilishe miradi hii ya Liganga na Mchuchuma ili kupunguza gharama kubwa za ujenzi wa reli ya kati.
Mheshimiwa Spika, Tangu miaka ya 2011, Serikali ya CCM ilitangaza kwa matangazo makubwa kuhusu ujenzi wa uchumi wa gesi baada ya kuvumbuliwa kiasi kikubwa cha gesi nchini kinachozidi futi za ujazo trilioni 55. Mategemea makubwa katika biashara hii ya gesi yalitegemea sana uwekezaji mkubwa katika mradi huu ambao unakadiriwa kufikia dola billion 30, uwekezaji ambao kama ungeanza mwaka huu inakadiriwa ungesababisha uchumi kukua kwa asilimia 7.2 kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu wenye uwekezaji wa dola 30billion ni mradi wa kihistoria katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, na kwakweli katika historia ya Tanzania kwani dola billion 30 ni karibu asilimia 75% ya uchumi wa Tanzania ambao kwasasa ni takribani dola billion 45. Uwekezaji wa dola billion 30 ni zaidi ya theluthi moja ya uchumi wa Kenya, Dola billion 30, ni karibu sawa na uchumi wote wan chi ya Uganda unaokadiriwa kuwa dola billion 30.
Mheshimiwa Spika, Ni uchungu kusema kwamba ingawa taarifa ya utekelezaji wa bajeti serikali inasema mradi huu utaanza mwaka 2019/20 ,Ukweli ni kwamba wawekezaji katika mradi huu ambao ni kampuni za State Oil, BG/Shell, Exxon Mobile na Orphir , wamekwishamua kuahirisha uwekezaji huu. Kwa mujibu wa Jarida la Reuters, la Novemba16, Meneja wa kampuni ya Sate amekaririwa akisema kwamba kutokana na kutoeleweka kwa Serikali ya Tanzaia, wao wameamua watafanya uamuzi kuhusu uwekezaji huo miaka mitano 5 kutoka 2016, yaani 20 kusisitiza kwamba ikiwa hivyo, wataingiza mtaji miaka mitano5 kutoka mwaka huo 2021, ikimaanisha kwamba ratiba ya kampuni hizi kuleta mtaji ni mwaka 2026.
Mheshimiwa spika, Huu ndio ukweli ambao Serikali haiusemi na badala yake inatoa maelezo yaliyojaa simulizi kwa suala muhimu na la kimkakati kama hili. Kifupi ni kwamba Serikali ya awamu tano haiaminiki, haitabiriki kwa wafanyabiashara wa ndani nanje kama IMF iliyosisitiza hivi karibuni. Na kwakuwa mitaji inatafutwa duniani, wawekezaji hawahawa ambao wameahirisha mradi huu hapa kwetu wanaendlea kuwekeza nchini Mozambique, na watakapomaliza, ni wazi Mozambique yenye gesi kuliko Tanzania, ikiwa na LNG Plant, itatawala soko lote la gesi kusini na mashariki ya Afrika, wakati Tanzania ikiendelea na utawala wake wa purukushani sio na maono wala mkakati.
Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba mipango mbali mbali ya serikali imekuwa ikigonga mwamba kwa sababu mipango inakuwa mingi, fedha kidogo na hakuna mwendelezo (consistency). Jambo likipangwa kutekelezwa kwa miaka mitano , lisipofanikiwa tunarukia jambo lingine hata kama hatukufanya uwekezaji wakutosha, Matokeo yake hakuna kinachofanikiwa!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kwamba huwezi kuondoa umasikini bila kuigusa sekta inayoajiri watanzania walio wengi! TUNARUDIA Kama Kilimo hakitaendelezwa, ina maana kwamba, itakuwa ni ndoto kuondoa 75% ya Wananchi wetu katika lindi la umasikini. Sekta ya Kilimo imedumaa si kwa sababu nyingine yeyote zaidi ya Ukweli kwamba hakuna uwekezaji wa maana unaofanyika!
Mheshimiwa Spika, Ripoti zinaonyesha kwamba Shughuli za kiuchumi za kilimo zilikuwa kwa kasi ndogo ya asilimia 3.5 mwaka 2014/15 ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwaka 2025/16 .Mwaka 2017 kimezidi kudidimia kufikia 1.7%…tusishangae mwaka 2018 tukiambiwa ukuaji wa sekta hii imefikia 0.5%!! ni wazi kwamba hakuna miugiza inayoweza fanyika kama serikali inatenga shilingi bilioni 3.3 kuhudumia watanzania milioni 30 , wakati huo huo shilingi Trillion 1 zimelipwa ‘CASH’ kununua ndege ambazo zinahudumia watanzania 10,000[7].
Mheshimiwa Spika, Licha ya kupuuzwa, bado sekta hii imeendelea kuongoza kwa kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa kuchangia kwa asilimia 29.0 ya pato la Taifa ikifuatiwa na shughuli za ujenzi (13%), biashara na matengenezo (10.7%) na ulinzi na utawala 6.4%.
Mheshimiwa Spika, hata hotuba wa waziri [8]I naonyesha ni kwa namna gani serikali ya CCM haina mpango kabisa na wakulima wan chi hii (75% ya watanzania) kwa miradi inayopewa msukumo wa KIPEKEE kwa mwaka 2016/17-2020/21 kati ya vipaumbele 8, suala la KILIMO limezungumziwa katika kamradi kamoja ka uanzishwaji wa shamba la miwa nakiwanda cha sukari,na pesa zilizotengwa ni shilingi bilioni mbili tu!! HII NI ZAIDI YA MZAHA!
Mheshimiwa Spika,
ILI Kilimo kiweze kupiga hatua:-
Mheshimiwa Spika, Uchumi imara wa Brazil leo,unategemea KILIMO NA VIWANDA[10] Pamoja na mambo mengine ulianzia katika uwekezaji wa zao la KAHAWA .Brazil ilitambulika Duniani kwa zao husika, hata mtikisiko wa uchumi ulipotokea miaka ya 1930 serikali ilihakikisha inafanya uwekezaji kupitia program maalum kuhakikisha zao husika halitetereki. Kilimo kilikwenda sambamba ya viwanda vidogo na vya kati vya kuongezea thamani . Hii ilikwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya Barabara na reli kwa ajili ya kuunganisha maeneo ya uzalishaji (yaliyotambulika kimkakati) na masoko.
Mheshimiwa Spika, Kukosekana kwa umakini kunaonekana kwenye hotuba wa waziri wa fedha na mipango juu ya jukumu la Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB)[11]. Waziri anasema katika mwaka 2017/18 Benki ya Maendeleo ya Kilimo itaboresha huduma za kibenki kwa kuanzisha mazao maalum kwa wakulima wadogowadogo kulingana na mnyororo husika wa thamani kulingana na vipaumbele vya Mikoa husika.. Na kwamba Benki imepanga kufanya maandalizi ya kutoa Mikopo ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yaliyoainishwa na Tume ya Taifa ya umwagiliaji.. vilevile benki imepanga kuwa jengea uwezo wakulima wadogowadogo, Wafanyakazi wa Benki, benki nyingine na Wadau mbalimbali wa kilimo nk.
Mheshimiwa Spika, mbali na kwamba haijulikani hivyo vipaumbele vya mikoa vina uhusiano gani na Malengo Mapana ya Taifa ili kuelekeza Mikopo kwenye maeneo husika ni Ukweli usiopingika kuwa benki hii ni MFU.
Mheshimiwa Spika, Kwa wasiofahamu uanzishwaji wa benki hii mwaka 2009 , Benki hii ilikuwa shughuli ya pili kwa umuhimu (Baada ya shughuli ya 1 ya “kuongeza bajeti ya Serikali kwa ajili ya Kilimo kwanza “)Kati ya shughuli 15 za nguzo ya pili ya Kilimo Kwanza. Ilidhamiriwa TADP ianzishwe ikiwa na mtaji wa dola za kimarekani milioni 500 (kipindi kile shilling bilioni 800, sasa hivi Trilion 1.1)….Fedha hizo zingepatikana iwapo serikali ingetenda bilioni 100 kila mwaka …. Lengo likiwa ni kukopesha wakulima wadogo wadogo kwa masharti na riba nafuu!! Benki hii muhimu iliishia kuambulia shilingi bilioni 60 tu mwezi April 2015.
Mheshimiwa Spika, Kwa nini tunaogopa kufanya utambuzi wa KITAALAM , kuwekeza, hatimaye kurekebisha pale ambapo tunakosea pasipo kuchoka mpaka pale azma ya NCHI ikakapotimia?
Mheshimiwa Spika, Kwa hili, tuna la kujifunza kutoka India. Mapinduzi ya viwanda India ni Matokeo ya mkakati/mpango maalum wa miaka mitano mitano wa toka mwaka 1951 unaoendelea mpaka sasa, huku Mkakati mahsusi wa Maendeleo ya viwanda ukianza mwaka 1970. Iliwachukua zaidi ya muongo mmoja kwa India kugundua kwamba walikosea ‘kutaka kuanzisha viwanda vikubwa’ wakati rasilimali watu(ndani ya nchi) ya kuviendesha viwanda hivyo haipo. Kuziba mwanya huo wenzetu walianzisha mkakati maalum wa kutumia DIASPORA ambao wamekuja kuwa na mchango chanya sana katika mapinduzi ya Uchumi na viwanda![12]
Mheshimiwa Spika, Natambua kwamba kila nchi ina mazingira tofauti na fursa tofauti. Sisi kama Taifa tunajipambanua vipi? Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inasisitiza ,UKUAJI SHIRIKISHI wa uchumi hauwezi kuacha Maendeleo ya KILIMO .Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) akitoa utangulizi katika semina ya waheshimiwa wabunge kuhusu kuanzishwa kwa TADB alisema: “ili Tanzania ifanikiwe katika kupunguza umasikini na kujenga uchumi wa viwanda , ni lazima ifanye mapinduzi kwenye sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Ni ukweli unaouma kwamba, viwanda haviwezi kuwepo bila malighafi. Lakini vilevile viwanda (kama vitajengwa ) havitakuwa na msaada katika kupunguza tatizo la AJIRA nchini kama hatuna rasilimali watu ya ndani ya kutosha kuweza kuviendesha..Korea ya Kusini ilikuwa na POTENTIAL toka miaka ya 1970 ya kuanzisha viwanda vya magari (automotive industries),lakini iliwachukua miongo miwili kabla ya nchi kuibuka kama moja ya wazalishaji wa magari toka bara la Asia. Waliwekeza katika rasilimali watu mahsusi kwa ajili ya viwanda husika kwa zaidi ya miaka 20. Walipoibuka walipenya kiurahisi kabisa na kuwa washindani wakubwa katika uzalishaji wa magari!
Mheshimiwa Spika, Somo la Korea ya Kusini na India linatuambia kwamba BAJETI inayozingatia UKUAJI SHIRIKISHI wa uchumi unatutaka tuwekeze katika ELIMU na mafunzo kwa VITENDO. Na sio elimu kiujumla wake, bali mkazo uwekwe (toka ngazi ya msingi) kwenye maeneo ya kimkakati ambayo TAFITI zinaonyesha kwamba tukiwekeza ,tutapenya kwenye SOKO! Hivi Tanzania ya viwanda ambayo ndio Wimbo wa TAIFA wa kila mmoja wetu tumeihuisha vipi katika mipango yetu mbalimbali ya nchi ? Hivi nikiiuliza serikali leo, kiwanda cha chuma cha liganga na mchuchuma kinatarajiwa kuendeshwa na nani?? Kwa manufaa ya nani?? Na kwa maandalizi gani?? Au ndio yale ya dhahabu, zinavunwa na wageni sisi tunaishia kugombana sababu ya MCHANGA
Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya sekta moja inategemea ukuaji wa sekta nyingine. Viwanda sio mbadala (Substitutive ) wa Kilimo , bali ni sekta mbili zinazotegemeana. Viwanda /Kilimo haviwezi kukua bila kukuza / kuboresha sekta hizi mbili kwa pamoja . Kama Kilimo kitachukuiwa kuwa ni ‘ moyo’ wan chi, basi viwanda itakuwa ni ‘ubongo’.
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yoyote unategemea hali ya utulivu wa kisiasa pamoja na uzingatiwaji wa misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu. Ni dhahri kuwa mambo hayo yakikosekana kutakuwa na athari za moja kwa moja za kiuchumi katika taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza kuhusu uchumi shirikishi ambao unalenga kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unaendana na kuboresha maisha ya wananchi. Malengo haya hayawezi kufikiwa kama bado hali ya nchi kisiasa sio nzuri kutokana na baadhi ya makundi kuminywa kupaza sauti yao na kutoa maoni juu ya masuala yanayoendelea katika taifa.
Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo ningependa kugusia masuala yafauatayo ambayo yanahitaji majibu na hatua za Serikali;
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalo jukumu la kuilinda Katiba ya nchi kwa kutekeleza matakwa ya kikatiba juu ya haki ya wananchi kushiriki katika uchaguzi kwa kupiga kura. Aidha Serikali inalo jukumu la kuhakikisha kuwa matakwa ya kisheria kuhusu masuala ya uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanazingatiwa ikiwemo maandalizi ya daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba: “Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, Ili kuhakikisha kuwa haki ya wananchi ya kupiga kura inalindwa, Ibara ya 5(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria ya uchaguzi na kuweka masharti ya kuanzisha daftari la kudumu la wapiga kura na kuweka utaratibu wa kuboresha daftari hilo.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi sura namba 343 toleo la mwaka 2015 kifungu cha 15(5) inaelekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuboresha daftari la kudumu mara mbili ikiwa na maana ya mara tu baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi mkuu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni toka Bunge la kumi imekuwa ikiitaka Serikali kutekeleza takwa hilo la kisheria lakini Serikali imekuwa ikiziba masikio.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili toka uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulipofanyika lakini hakuna dalili yoyote inayoonesha kuwa daftari la kudumu la wapiga kura litaboresha kama ambavyo sheria inataka. Ukisoma kwa makini Fungu 61 Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina kifungu ambacho kimetengewa fedha kwa ajili ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Spika, Hii maana yake ni kuwa tunaelekea mwaka wa tatu bila kuboresha daftari la wapiga kura. Huu ni ukiukwaji wa taratibu za kisheria ambazo kama taifa tumejiwekea. Ikumbukwe kuwa lengo la kuboresha daftari ni muhimu kwa sababu kumekuwa na chaguzi ndogo za Udiwani na Ubunge ambazo zote zimefanyika kwa kutumia daftari la wapiga kura lililoboreshwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ili kuepuka malalamiko ya wadau wa siasa nchini kwa kuboresha daftari la wapiga kura ili kukidhi matakwa kikatiba na kisheria kama ambavyo tumeeleza.
Mheshimiwa Spika, kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura haiondoi hoja ya hitaji la kuwa na Tume huru ya uchaguzi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa na madai ya muda mrefu ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi. Majibu ya Serikali kwenye hoja hii yamejikita kusubiri mchakato wa Katiba mpya kukamilika.
Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanajua kuwa mchakato wa Katiba mpya umekwama na Rais ameshasema hadharani kuwa wakati wa kampeni hakutamka popote kuhusu Katiba mpya na hivyo inaonekana si kipaumbele chake. Hii maana yake ni kuwa majibu ya hoja ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi itasubiri Katiba mpya hayatakuwa na mantiki baada kauli ya Rais.
Mheshimiwa Spika, ili kuwe na mwelekeo mzuri wa huko tunakoelekea Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwe na mabadiliko ya Katiba iliyopo ili kukidhi masuala ya kidemokrasia nchini na kuondoa malalamiko ya wadau wa siasa nchini. Ikumbukwe kuwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 kulikuwa na majadiliano ambayo hayakufikia mwisho yaliyokuwa yanasimamiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambayo yalipendekeza kuwe na marekebisho ya mpito ya Katiba iliyopo ya mwaka 1977 kwa ajili ya kuepuka mambo ambayo yanaweza kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Mheshimiwa Spika, Ili kuwa Taifa linaloheshimu misingi ya kidemokrasia nchini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kurudia baadhi ya mapendekezo ya Kamati ya Kituo cha Demokrasia Tanzania ili kuwe na marekebisho ya Katiba ya mpito katika masuala yafuatayo yanayohusu Tume ya Uchaguzi;
Mheshimiwa Spika, demokrasia ikishamiri vizuri katika nchi uchumi utakua na kufanya nchi yetu kuendelea. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha inalichukulia kwa uzito jambo hili kwa ajili ya mustakabali mwema wa yetu.
Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Machi, 2016 Shirika la MCC lilifikia uamuzi wa kusitisha misaada yake kwa Tanzania[13]. Sababu za kusitishwa kwa misaada hiyo pamoja na mambo mengine ni kutokana na kufutwa kwa uchaguzi halali wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 pamoja na Serikali kutumia sheria ya makosa ya kimtandao kuzuia uhuru wa kutoa maoni.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kusisitiza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi feki wa Zanzibar wa tarehe 20 Machi, 2016 hakujawa dawa ya kutatua mkwamo wa kisiasa Zanzibar. Wananchi wa Zanzibar walifanya maamuzi yao tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad lakini sauti yao haikusikika kwa sababu kuna kikundi cha watu ambao hawaheshimu misingi ya demokrasia nchini.
Mheshimiwa Spika, Aidha tunasisitiza kuwa marudio ya uchaguzi Zanzibar hayajawa dawa kwa wanachama wa Chama cha Wananchi CUF walioteswa na kupigwa na Mazombi huku vyombo vya dola vikishuhudia kama ambavyo ambavyo tulieleza kwa kirefu kwenye hotuba ya Kambi ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.
Mheshimiwa Spika, marudio ya uchaguzi wa Zanzibar hayajafanyika kwa mujibu wa Katiba wala Sheria bali kwa matakwa ya mtu mmoja ambaye aliamua kufuta uchaguzi huo bila kuwa na mamlaka ya kisheria wala Katiba.
Mheshimiwa Spika, thamani ya fedha zilizozuiliwa na MCC ni takribani 1.5 Trilioni[14], Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haishangai kuona miradi ya REA ikisuasua kutokana na ukosefu wa fedha. Hata bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini imeshuka (kutoka 1,056,354,669,000 hadi 938,632,006,000) tofauti na mwaka wa fedha uliopita. Ikumbukwe kuwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji suala hili Serikali ilijinasibu kuwa itagharamia miradi ya REA kwa fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba fedha za MCC zilikuwa muhimu kwa nchi lakini kutokana na kukiukwa kwa misingi ya demokrasia na kuwaziba wananchi midomo kunakofanywa na Serikali ya CCM fedha hizo zikazuiwa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 01 Juni, 2017 Balozi Msaidizi wa Marekani hapa nchini, alitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini[15].
“At this same crossroads, however, is another path. One which leads to a Tanzania where people are afraid to use their voice, and where development stagnates. Down this road, entrepreneurs hang back from starting new business due to stifling or inconsistently applied regulations. Government institutions remain susceptible to corruption and inefficiencies. Schools and medical centers do not have the resources they need. And are unable to serve those who need them. The security forces are feared and operate outside the rule of law. People distrust their neighbors and wonder where their loyalties lie. Citizens are afraid to offer their views – limiting the debate that is so often needed to come up with the best way forward. In this direction, the efforts of millions of hard-working, talented Tanzanians – especially young Tanzanians – will see a less certain future”.
Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi maoni haya yanaweza kujengwa katika dhana zifuatazo;
Mheshimiwa Spika, Hii ndiyo hali ya siasa katika nchi yetu kwa jicho la kimataifa. Huu ndio ukweli ambao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliuweka wazi katika hotuba zake kwa Wizara mbalimbali. Japo mengine yalifutwa na kutoingia ndani ya Bunge lakini ukweli utabaki palepale kuwa hali sio nzuri ndani ya nchi yetu kwa sasa kwa sababu imejengwa hofu kubwa miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Rais anapenda kusisitiza kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kuhoji kuwa ni ukweli upi ambao Serikali yake inapenda kuusikia? Hii ni kutokana na juhudi za kila namna ya kuzuia mawazo mbadala kusikika kwa wananchi. Ukweli upi ambao Rais anapenda kuusikia wakati amezuia kinyume na sheria mikutano ya vyama vya siasa? Ukweli ni upi anaopenda kuusikia wakati wananchi hawawezi kusikia na kuona moja kwa moja mijadala ya wawakilishi wao ndani ya Bunge?
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Act) imekuwa mwiba wa uhuru wa kujieleza nchini. Hii inatokana na vyombo vya dola kujizolea sifa ya kuendelea kuwakamata vijana mbalimbali na kuwafungulia mashitaka ya uchochezi au makosa ya kimtandao kutokana na kuamua kutumia uhuru wao wa kikatiba kutoa maoni na kujieleza.
Mheshimiwa Spika, wapo vijana wengi ambao wamekuwa wakikamatwa na kuteswa hasa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi na Kituo cha Polisi cha Oysterbay Jijini Dar Es Salaam, kutokana na kuandika na kutoa maoni yao mtandaoni ambayo huonekana ikikosoa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni alikamatwa kijana kutoka Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe Mdude Nyagali pamoja na Nicas David, ambapo baada ya Mdude kukamatwa huko Mbozi aliteswa bila kupelekwa hospitali na baadae kusafirishwa kwenda Dar es Salaam ambapo pia alipata mateso akiwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay bila ya kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, ni baada ya Wakili na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Mhe. Tundu Lissu (Mb) kuwaeleza Polisi kuwa angepeleka maombi Mahakama Kuu ya Habeas Corpus ndipo aliporudishwa tena Mbozi na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi ambapo mwezi wa Aprili mwaka 2017 Mahakama imemkuta bila hatia yoyote.
Mheshimiwa Spika, mwendelezo wa Serikali kutumia Sheria ya Makosa ya Kimtandao “Cyber Crime Act” ya mwaka 2015 umekuwa mwiba mchungu kwa watu kutoa maoni yao ndani ya nchi. Ni ishara kuwa Serikali haipendi matumizi ya mitandao ya kijamii na ndiyo maana Mkuu wa nchi wakati anapokea ndege za Bombadier Jijini Dar es Salaam alisema kuwa anatamani malaika washuke kuizima mitandao hiyo na kusahau kuwa wakati wa uchaguzi mkuu 2015 alitumia mitandao hiyo hiyo kujinadi na kutafuta kura.
Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa Sheria hiyo inatumika kama malaika kuzuia uhuru wa kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii. Mamlaka makubwa waliyopewa Polisi kukamata computer au simu za mikononi tuliyaeleza kwa kirefu wakati sheria hiyo ilipokuwa inapitishwa Bungeni kwenye Bunge la kumi.
Mheshimiwa Spika, Ndiyo maana mpaka sasa nchi washirika wa maendeleo na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Umoja wa Ulaya na Shirika la Millenium Challenge Corporations (MCC), wameikosoa sheria hiyo kuwa inakiuka misingi ya demokrasia na utawala bora kwa sababu inazuia uhuru wa raia wa kujieleza; na kwa sababu hizo Shirika la MCC iliamua kuinyima Tanzania fedha za misaada katika miradi ya umeme kutokana na Serikali kutumia sheria hiyo kuzuia uhuru wa kujieleza.
Mheshimiwa Spika, kuna orodha ndefu ya vijana wa Kitanzania ambao tayari walishapandishwa kizimbani kutokana na Sheria hii ya Makosa ya Kimtandao kwa kuikosoa Serikali ya awamu ya Tano na hususani Mkuu wa Nchi, orodha hiyo ya vijana ni kubwa kuliko matumizi ya vifungu vingine vya Sheria hii, jambo linaloifanya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iamini kuwa uwepo wa Sheria hii ulilenga kuzuia uhuru wa kujieleza ili Serikali hii iendelee na vitendo vya ukandamizaji wa haki nyigine na ikose kabisa watu wa kuikosoa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao ni ya kibaguzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wapo makada wa Chama cha Mapinduzi wanaotoa matusi mpaka ya nguoni kwa viongozi wa Vyama vya Upinzani lakini sheria hiyo haitumiki kuwachulia hatua. Kutokana na hali hiyo, mtu yeyote anaweza kujenga hoja kuwa sheria hiyo wametungiwa wapinzani pekee na si upande mwingine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta marekebisho ya sheria hiyo ili kuondoa vifungu kandamizi ambavyo vinalalamikiwa na wadau na wananchi kwa ujumla.
14.MAMBO MUHIMU YALIYOIBULIWA NA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2017/18 AMBAYO HAYAJAFANYIWA KAZI NA SERIKALI MPAKA SASA
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18, Kambi Rasmi ya Upinzani iliibua matatizo ya msingi yaliyokuwa yanahitaji kutatuliwa haraka ili kujenga mshikamano na mustakabali mzuri wa Taifa lakini jambo la kushangaza ni kwamba masuala hayo hayajafanyiwa kazi na Serikali mpaka sasa. Miongoni mwa masuaa hayo ni pamoja na haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, hali ya maisha ya wananchi bado ni ngumu, na mzunguko wa fedha bado ni mdogo. Kuhusu mahusiano na sekta binafsi; ni hivi majuzi tu Serikali imeanza kutafuta suluhu na sekta binafsi, na hii ni kutokana na Serikali kuanza kukwama kutokana na makusanyo madogo ya kodi kutoka sekta binafsi. Serikali ingechukua ushauri wetu mapema pengine mzunguko wa fedha ungekuwa umerejea katika hali yake na hali ya maisha ya wananchi ingekuwa nzuri na makusanyo ya Serikali yangeongezeka.
Mheshimiwa Spika, ni vema Waziri Mkuu atakapokuwa anahitimisha hoja yake, akalieleza bunge hili, utekelezaji wa masuala hayo umefikia wapi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ina utaratibu wa kuibua Kaulimbiu (theme) kila mwaka Bunge linapojadili Bajeti ya Serikali kwa lengo la kuchagiza mwelekeo wa Bajeti ya Serikali na kutoa mawazo mbadala kwa mustakabali mwema wa uchumi wa Taifa. Kwa mwaka wa fedha 2016/17 kauli mbiu yetu ilikuwa ni “Ukuaji wa Uchumi Vijijini (Rural Growth)” kama chanzo cha ukuaji imara wa uchumi wa Taifa. Mwaka wa fedha 2017/18, kauli mbiu yetu ilikuwa ni “Ukuaji wa Uchumi Shirikishi (Inclusive Economic Groth)” tukilenga kwamba; ili ukuaji wa uchumi uwafikie wananchi wote na kila mmoja apate kufaidi matunda ya uchumi, ni lazima uchumi huo uwe shirikishi. Na tulieleza kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo; unatokea katika maeneo ambayo watu masikini wanaishi kwa mfano maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali; unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo kwa mfano nguvukazi isiyo ya kitaalamu; na unapunguza bei za bidhaa ambaombazo watu masikini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo. Ninatoa changamoto kwa Serikali ijipime, kama ukuaji wa uchumi wetu unakidhi vigezo hivyo.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha 2018/19, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea na Kauli Mbiu ile ile ya Ukusaji Shirikshi wa Uchumi isipokuwa tutaweka msisitizo katika “Kujenga Taasisi Imara kwa Maendeleo Endelevu (Building Strong Institutions for Sustainable Development)” Sababu kubwa ya kuweka msisitizo huo ni kutokana na ukweli kwamba ili kuwa na uendelevu (sustainability) katika jambo lolote ni lazima kuwe na mifumo imara ya kitaasisi, kanuni, taratibu na sheria zitakazofuatwa juu ya namna ya kutekeleza jambo hilo; na sio kufuata matakwa ya mtu au kikundi cha watu katika kufanya hivyo kwa kuwa watu ni wa kupita lakini taasisi na mifumo itabaki.
Mheshimiwa Spika, tunahitaji taasisi imara zinazozingatia misingi ya utoaji haki, ulinzi wa amani na zinazojali uwajibikaji wa pamoja ili kujenga jamii jumuishi kwa maendeleo endelevu. Tunahitaji jamii ya watu huru wanaoishi bila hofu ya kutekwa, kutengwa na wapendwa wao, kuuawa, au vitisho vya namna yoyote. Tunahitaji kuwa na mahakama zilizo huru, zinazoweza kutoa maamuzi yanayozingatia sheria na haki bila mashinikizo ya mtu yoyote. Tunahitaji kuwa na tume huru ya uchaguzi inayofanya kazi kwa uhuru bila shinikizo la mtu au kikundi cha watu, tunahitaji kuwa na bunge lenye uwezo wa kuikosoa serikali na kuiwajibisha serikali, tunahitaji jeshi la polisi linalozingatia sheria, usawa na haki za binadamu. Tunahitaji Jeshi la Wananchi lisiloegemea upande wowote na linalowajibika kwa wananchi wote wa Tanzania na tunahitaji taasisi zote na idara za Serikali zifuate sheria na kanuni na sio maelekezo au matakwa ya viongozi.
Mheshimiwa Spika, ili taasisi nilizotaja ziweze kuwa imara ni lazima tuwe na Katiba Bora itakayoweka utaratibu wa jinsi taasisi hizo zinapaswa kuendeshwa. Aidha, katika kujenga taasisi imara tunahitaji kuwa na viongozi wanaoheshimu katiba na sheria za nchi. Katika ulimwengu wa sasa hatuhitaji kumjenga mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu kwa kuwa hao watapita ila taasisi zitabaki. Katika historia; mifumo ya nchi iliyomjenga mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu imesambaratika na kuziacha nchi hizo katika migogoro mikubwa na udikteta wa kutisha.
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana kwamba taasisi tulizo nazo zimekuwa dhaifu sana na udhaifu huo umesababishwa na vingozi wanaopenda kutawala kwa kutumia njia za mkato – wasiopenda kufuata taratibu za kisheria za kitaasisi. Tumeshuhudia sheria zikivunjwa na viongozi kwa kutoa kauli au matamko ambayo ni kinyume na sheria; watu wananyimwa haki zao za kikatiba na kisheria lakini taasisi husika zinazotakiwa kukemea mambo hayo zimekaa kimya.
Mheshimiwa Spika, nikitoa mfano mdogo tu wa uchaguzi wa marudio wa kata 43 za udiwani na ubunge. Ule haukuwa uchaguzi bali ni unyanganyi wa kimabavu kwani kulikuwa na uporaji wa wazi wa karatasi za matokeo ambapo vyombo vya dola vilitumika vibaya kuingilia uchaguzi huo. Lakini Tume ya uchaguzi ambayo ndiyo taasisi yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi huo haikutimiza wajibu wa kusimamia chaguzi hizi ipasavyo na hili linatia shaka na kujenga hisia kwamba chombo hiki pengine kinafuata maelekezo kutoka kwa mtu au chombo fulani. Udhaifu kama huo, upo katika taasisi nyingi ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa anayeshabikia migogoro ya vyama vya siasa badala ya kuwa msuluhishi.
Mheshimiwa Spika, Ni muda mwafaka sasa kama taifa kuunda taasisi imara zenye uwezo wa kujisimamia na kufanya kazi kwa ufanisi. Mfano; Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) ni lazima iweze kujitathimini na kutathiminiwa katika utendaji wake ili kuzuia taasisi hiyo kufanya kazi kwa visasi,uwepo wa taasisi inayotathimini utendaji wa Jeshi la Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nk.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na udhaifu wa taasisi zetu, tumeshuhudia vyombo vya dola kama polisi vikivunja sheria kwa makusudi na watendaji wake wakuu wakijinasibu hadharani kwamba wanafuata maelekezo.Utendaji wa namna hii unajulikana kabisa ni kinyume cha sheria. Lakini hoja ya msingi ni kuwepo na chombo huru inachotathimini utendaji kazi na uwajibishaji wa taasisi hizi ili kupunguza utovu mkubwa wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya watendaji wakuu kwa kivuli cha maelekezo kutoka juu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na taasisi ya kuangalia maadili ya watumishi wa umma, lakini kwa bahati mbaya sana taasisi hii inakosa nguvu ya kufanya kazi kutokana na mashinikizo kwani watendaji wake wakuu ni wateule wa Ikulu. Jambo hili liko wazi kwa kuwa taasisi imeshindwa kuwachukulia hatua wateuliwa wa Ikulu kwenye sakata zima la kuhusu vyeti feki. Pia, tumeshuhudia watendaji wa Serikali ambao ni wateuliwa wa Ikulu wakifanya kazi za uenezi wa Chama cha Mapinduzi. Masuala kama haya yanapelekea wananchi kukosa imani na taasisi hii ya kushughulikia maadili ya viongozi wa umma.
Mheshimiwa Spika, bila kuboresha utendaji kazi wa taasisi zetu haitawezekana kamwe kuwa na maendeleo endelevu ndani ya nchi yetu. Ni jukumu letu sote kulitazama jambo hili kwa kina na kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kunusuru nchi yetu kuingia katika mipasuko inayotokana na ubaguzi, chuki na visasi na hata kuingia katika majanga yakiwemo machafuko ambayo kimsingi yanaweza kugharimu maisha ya watu wetu, kuporomosha uchumi wetu na kuharibu jina zuri la taifa letu lililolinda misingi ya amani na utulivu tangu uhuru.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Serikali iliahidi kutoa ajira 71,496 ikiwa ni ajira mpya na kufidia ajira za watumishi 13,008 walibainika kuwa na vyeti feki au cheti kimoja kutumiwa na watumishi zaidi ya mmoja. Ahadi ya Waziri aliyekuwa na dhamana ya utumishi aliliambia Bunge kuwa mwaka huu 2018/19 Serikali inatarajia kutoa ajira mpya 52,436. Na wakati huo huo liyekuwa Waziri wa Tamisemi Mheshimiwa George Simbachawene, alipokuwa anahitimisha Hotuba ya Bajeti katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa fedha 2017/18 alisema kuwa Serikali ina upungufu wa watumishi 96,000.
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo huu wa Serikali ni kwamba dhana ambayo imekuwa ikitengenezwa kwa miaka yote ya Serikali kupunguza matumizi kwa kupeleka ajira katika sekta binafsi na Serikali kuu kubaki kama mamlaka ya uratibu tu imeshindikana na badala yake Serikali ndiyo sasa inakuwa mtoaji wa ajira mkubwa badala ya Sekta binafsi au Taasisi zake zenye ubia na Sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na International Finance Corporation (IFC) kwa nchi zilizoendelea ni kwamba; katika ajira 10 mpya, 9 zinatengenezwa na sekta binafsi. Pamoja na utafiti huo kubaini hivyo, takwimu hizo hazina uhalisia katika nchi yetu. Hii ni kwa sababu sekta binafsi hapa nchini imebanwa sana kuweza kutengeneza ajira, hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano. Mazingira ya kufanya biashara Tanzania ni magumu sana kiasi kwamba waliokuwa nazo sasa wanazifunga na wale wanataka kuanzisha masharti ni magumu mno kiasi kwamba wanashindwa kuanzisha.
Mheshimiwa Spika, Ukitaka kuanzisha biashara Tanzania unakumbana na utitiri wa masharti na kodi kama ifutatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukijaribu kuuza bidhaa nje (export) hali ndio inakuwa ngumu zaidi; na hapo bado michango ya Halmashauri kama vile madawati, ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, maabara na mchango wa mwenge nk.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ya namna hii, Sekta Binafsi haipumui na ukizingatia hali ya kiuchumi iliyo sasa ambapo mzunguko wa fedha haupo na purchasing power imepungua; biashara nyingi zimefungwa na wanaojaribu kufungua hawawezi kutokana na vizingiti nilivyovitaja hapa juu. Katika mazingira hayo, sekta binafsi haiwezi kuajiri tena kuweza kukidhi vile viwango vya utafiti kwamba katika kila ajira 10 mpya, 9 zinatoka sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, si jambo la kubishaniwa kwamba Kilimo ni lango kuu la uzalishaji mkubwa wa mazao ghafi yanayohitajika katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Kwa sababu hiyo, mapinduzi ya viwanda lazima yaende sambamba na mapinduzi ya Kilimo ili viwanda viweze kupata malighafi ya kutosha kufanya uzalishaji. Licha ya ukweli huo, kilimo pia ni sekta pekee inayotoa ajira nyingi kwa watanzania zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, ili kilimo chetu kiweze kubeba dhana nzima ya uchumi wa viwanda ni lazima uwekezaji mkubwa katika sekta hii ufanyike; na Uwekezaji huo ni lazima uwe wa rasimali watu na rasilimali fedha. Ni bahati mbaya sana kwamba hakuna uwekezaji wa maana uliofanywa katika sekta ya Kilimo hapa nchini. Nasema hivi kwa sababu kwa mujibu wa tamko la Maputo “Maputo Declaration on Agriculture and Food Security in Africa” kuhusu Kilimo na usalama wa Chakula kila nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) inatakiwa kutenga angalau asilimia10 ya bajeti ya Taifa, na kuilekeza kwenye sekta ya Kilimo ili kusaidia ukuaji wa sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, toka kusaini tamko hilo mwaka 2003, Tanzania haijawahi kutenga bajeti kwa sekta hiyo zaidi ya 6% ya bajeti ya Taifa. Kwa mfanomwaka wa fedha 2016/17 fedha za maendeleo zilizotolewa zilikuwa ni chini ya asilimia 3 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge ya Tshs bilioni 101.5 Kwani hadi Kambi Rasmi inawasilisha Maoni yake zilikuwa zimetolewa shilingi bilioni 2.25 sawa na asilimia 2.22 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya maendeleo katika sekta ya kilimo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili; ni muujiza gani utatendeka ili kilimo kiweze kusukuma uchumi wa viwanda ikiwa haitengi fedha za kutosha katika sekta hiyo?
Mheshimiwa Spika, ili kuonyesha msisitizo wa wa umuhimu wa sekta ya kilimo Umoja wa Afrika ulikutana tena Malabo, Equatorial Guinea tarehe 26-27 Juni, 2014 na kuweka vigezo vya upimaji wa ukuaji wa Sekta ya Kilimo katika nchi wanachama. Moja ya azimio la Malabo ni kilimo kuchangia au kukua kwa angalu 6% kwenye pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na azimio hilo, Tanzania bado imeshindwa kutekeleza. Takwimu zinaonyesha kwamba; kwa miaka miwili 2015 na 2016 ukuaji wa kilimo nchini Tanzania ulikuwa ni 2.3% na 1.7% kwa mfuatano.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Raslimali watu inayotakiwa kwa sekta ya kilimo, watumishi wenye sifa mbalimbali katika kilimo wanaohitajika ni 19,228 lakini waliopo ni 8,756 sawa na 45.4%. Hii ni kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na Jukwaa la Wadau wa Kilimo wasio wa Kiserikali (Agricultural Non – State Actors Forum – ANSAF). Utafiti huo unaonyesha kwamba; watumishi wenye taaluma kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea mahitaji halisi ni 2,746 lakini waliopo ni 1,530 ambao ni sawa na 55.7%. Wakati wenye taaluma ngazi ya Cheti na Diploma mahitaji ni 16,542 lakini waliopo ni 7,226 sawa na 43.7%
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maafisa ugani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2013 waliokuwepo ni 7,974 wakati Tanzania ina vijiji vilivyo sajiliwa 15,082. Wakati kuna upungufu huo; Muongozo wa Serikali maafisa ugani ni kila kijiji kimoja kuwa na afisa ugani mmoja.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya Mifugo na Uvuvi hali ya upungufu wa rasilimali watu ni vivyo hivyo kama kwenye kilimo. Hapa watumishi wenye taaluma ya kuanzia shahada na kuendelea wanaohitajika ni 1,936 waliopo ni 867 sawa na 44.8%. Ngazi ya cheti na Diploma wanaohitajika ni 15,000 waliopo ni 3,904 sawa na 26%. Kwa ujumla sekta inahitaji watumishi wataalam 16,936 lakini waliopo ni 4,771 sawa na 28.1%
Mheshimiwa Spika, fursa kwenye uvuvi ni nyingi sana kwa vijana na kuongeza pato la Taifa, lakini fursa hizo bila kuwa na wataalam wa kutoa ushauri wa karibu kwa wajasiriamali ni kuwatumbukiza wahusika kwenye shimo, kwani watapata hasara na watachukia sekta hiyo. Ni vyema kuhakikisha rasilimali watu ya kutosha ipo ili iweze kukabiliana na mahitaji na changamoto za kitaalamu kwa wawekezaji katika sekta husika.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana sekta ya kilimo imekuwa haipewi umuhimu kama ule ilionao katika uchumi wa nchi. Ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha Ukomo wa Bajeti ya mwaka 2018/19 na kutoa mrejesho wa matumizi kwa bajeti ya mwaka 2017/18; alisema yafuatayo:-
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgao wa bajeti ni pamoja na: kulipa deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma; kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia elimu-msingi bila ada; utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa tiba”.
Mheshimiwa Spika, kwa nukuu hiyo; Kilimo sio kipaumbele kwa Serikali. Vipaumbele ni kulipa madeni (kwa kifupi bajeti ya mwaka huu tunaweza kuiita ni bajeti ya madeni). Si vibaya kulipa madeni lakini lazima pia kuzingatia uwekezaji katika sekta muhimu za uzalishaji kama kilimo ili sekta hizo ziweze kuzalisha fedha ambazo zitatumika kulipa hayo madeni. Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa na Serikali hii kujinasibu kuwa inajenga uchumi wa viwanda wakati sekta ya kilimo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa malighafi za viwandani si kipaumbele chake. Ninapata wasiwasi sana na uwezo wa watendaji wa Serikali wanaoandaa sera za Serikali na kupanga vipaumbele vya bajeti ikiwa kuna mkinzano mkubwa namba hii kati ya Sera na vipaumbele. Sera ya Serikali ni Tanzania ya Viwanda; lakini vipaumbele vya bajeti ni kulipa deni la taifa na madeni ya watumishi!!! (where is the relationship?).
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi shirikishi kwa kiasi kikubwa unategemea uimara wa taasisi za fedha. Kwa kipindi cha miaka mitatu toka mwaka 2015; tasnia ya fedha (Banking Industry) imekumbwa na msukosuko mkubwa ambao umepelekea kuyumba kwa sekta nyingine za uzalishaji hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mei, 2015, Benki Kuu ya Tanzania iliongeza kiwango kinachotakiwa kuwekwa kama dhamana (Statutory Minimum Reserve -SMR) kutoka 8% hadi 10%. Mwaka 2016 uhaba wa fedha kwenye mzunguko wa biashara ulizidisha makali kwenye tasnia ya benki kutokana na masharti yasiyotabilika yanayowekwa na Benki Kuu, makali hayo yanayowekwa na benki kuu yanaathiri moja kwa moja mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi. Jambo hilo lilipelekea mikopo kwa sekta binafsi kukua kwa 7.2% mwaka 2016 kulinganisha na kiwango cha ukuaji wa 24.8% mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2015-2017 faida kwa tasnia ya benki ilipungua kwa 32% kutoka shilingi bilioni 676 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 459 mwaka 2017. Mikopo chechefu kwa upande mwingine imeongezeka kutoka shilingi bilioni 675 mwaka 2014 hadi shilingi trilioni 1.8 mwaka 2017. Hii ikiwa ni ongezeko la 160%, uwiano wa mikopo chechefu umezidi kuongezeka kutoka 6.83 mwaka 2014; 10.3% mwaka 2016 na 11.7% mwaka 2017. Japokuwa kiwango cha chini cha mikopo chechefu kilichowekwa na Benki kuu ni chini ya 5%.
Mheshimiwa Spika, ongezeko hili la mikopo chechefu na kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi ni kiashiria kuwa uchumi kwa sekta mbalimbali za uchumi unazidi kurudi nyuma. Chanzo kikuu cha fedha kwa wajasilimali wadogo ambao ndio wengi katika kuanzisha na kuendeleza biashara, ni kutoka na mikopo ya familia au marafiki.
Mheshimiwa Spika, mbali na utendaji huo usioridhisha wa tasnia ya Benki ambao kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya udhibiti usiokuwa na tija wa Serikali kupitia Benki Kuu, tasnia ya benki inaathirika sana na kodi zinazotozwa katika hasara ambayo inatokana na biashara za kila siku za benki.
Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa “provision for loan losses” hii ni katika kutayarisha vitabu vya mahesabu ya benki inakadiriwa uwezekano wa kupata hasara katika mikopo inayotolewa. Jambo hili la uwezekano wa kupata hasara umekuwa ni jambo ambalo linapunguza faida kwa benki. Lakini TRA wanatoza kodi mahesabu hayo ya uwezekano wa kupata hasara katika mikopo.
Mheshimiwa Spika,kuna hizi “interest in suspense”, haya ni mapato tarajiwa lakini kutokana na mikopo chechefu au mikopo isiyolipika, maana yake ni kuwa riba hii iliyotarajiwa kuwa faida kwa benki haiwezi kupatikana kutokana na mikopo kutokulipika, japokuwa kwenye vitabu inasomeka. Hivyo riba hii kukatwa kodi ni kuzikamua benki kwa kuzipa hasara mara mbili, takwimu zinaonesha kuwa riba ya mikopo chechefu, takriban 98% ya riba hizo inafutwa kwenye vitabu na kuwa hasara kwa benki, lakini kodi kwenye riba hizo tayari imelipwa. Hili ni tatizo kubwa ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona linatakiwa kupatiwa ufumbuzi mapema ili tasnia ya benki iweze kuendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha TRA kushurtisha benki kulipa kodi kwa mikopo chechefu ambayo inamatarajio ya kulipika hata ikiwa ni kwa miaka kadhaa ijayo. Mikopo ikishakuwa chechefu na uwepo wa “defaulters” ni sawa na Serikali inapopanga bajeti na mwisho kushindwa kutimiza kupeleka fedha katika miradi. Hoja ni je fedha hizo zinapelekwa wakati mwaka wa fedha husika unapomalizika?
“Banks are required to provide for tax liability of a defaulter and pay TRA any tax due before they recover their outstanding amounts”
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuongelea uchumi bila kuangalia utendaji wa taasisi za fedha, kwani taasisi hizi ndio nguzo ya uchumi kwa kutoa mitaji kwa biashara mpya pamoja na zile zilizopo. Takwimu zinaonesha kuwa mikopo chechefu au mikopo isiyolipika (Non perfoming Loans) imeongezeka hadi 11.2% ya mikopo yote inayotolewa na taasisi za fedha kutoka 9.1% mwaka jana. Hii maana yake ni kwamba biashara hazifanyiki na kama biashara hazifanyiki, ajira zinazidi kupotea na mwisho hali ya uchumi kwa wananchi inazidi kuwa mbaya.
Mheshimiwa Spika, Aidha, kuongezeka kwa mikopo chechefu kunapunguza faida kwa taasisi za fedha, na hivyo kupunguza uwezo wake katika utoaji wa mikopo na pia kuongeza ukali wa vigezo (masharti) vya utoaji wa hiyo mikopo kwa wafanyabiashara na mwisho wajasiriamali watashindwa kuendeleza au kuanzisha biashara. Kwa mfano viwango vya riba za mikopo ya hadi mwaka mmoja viliongezeka kufikia asilimia 18.2 Desemba 2017 kutoka wastani wa asilimia 12.9 Desemba 2016. Hii ilitokana na mabenki kuchukua tahadhari kubwa kwa wateja wanaoshindwa kurejesha mikopo.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu mwaka 2017 ilizifunga benki za FBME na Mbinga Community Bank kutokana na utendaji mbaya wa benki hizo na Mwaka huu 2018 imetangaza kuzifunga benki tano za Covenant, Efatha, Njombe Community Bank, Kagera Community Bank na Meru Community Bank na kuzifutia leseni na kuziweka chini ya Mufilisi. Kufutwa kwa benki hizo ni kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mtaji wa kuwa na akiba ya shilingi Bilioni mbili tu.
Mheshimiwa Spika, Benki nyingine tatu zimewekwa kwenye uangalizi wa miezi sita mpaka Juni mwaka huu ikiwemo Benki ya Chama cha Ushirika Kilimanjaro, Benki ya Wanawake TWB na Tandahimba Community Bank. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ishara hii ya benki kuanza kufilisika ni ishara mbaya sana kwa uchumi ambao tunaambiwa unafanya vizuri na kukua kwa kasi .
Mheshimiwa Spika, Benki za wananchi ndizo zilizokuwa na mitandao rahisi ya kuwahudumia wananchi walio katika mazingira ya kutokupata mitaji toka kwa taasisi za fedha na pia benki hizo zilikuwa ndicho kiungo kikubwa na muhimu kati ya wananchi na taasisi nyingine za huduma kama vile bima kwa kilimo na mifugo yao na huduma ya hifadhi za jamii kwa familia zao. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua umuhimu na nguvu kubwa ya wananchi pamoja na Serikali za awamu zilizotangulia kuhakikisha kuwa benki hizo zinatoa huduma kwa wananchi, lakini Serikali ya awamu hii ina kasi bila muelekeo jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa uchumi wa taifa hili.
Mheshimiwa Spika,bajeti mbadala ya KRUB, ni yenye kuleta matumaini yenye heri kwa Watanzania. Kwa ushahidi wa wazi ambao Kambi Rasmi ya Upinzani inao katika kuongoza Majiji na Halmashauri kwa kipindi ambacho imeanza kufanya kazi hiyo (Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri zake, Halmashauri ya Mbeya, Jiji la Arusha, Halmashauri ya Mji wa Tunduma n.k) Mfano, Halmashauri ya Kinondoni kabla ya kuwa chini ya UKAWA ilikuwa inakusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 7, lakini mwaka mmoja chini ya UKAWA ikakusanya zaidi ya shilingi bilioni 70; Halmashauri ya Mji wa Tunduma ilikuwa inakusanya shilingi milioni 300-400 kwa mwaka lakini baada ya kuwa chini ya CHADEMA ikaweza kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 3 hadi bilioni4 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, hii ni kuonesha kuwa kuna fedha nyingi mno ambazo haiingii katika mfumo rasmi wa makusanyo ya mapato. Hivyo basi, UKAWA tunaamini kuwa tatizo la makusanyo bado ni kubwa mno na mapato halisi ambayo tunaweza kuyakusanya ni asilimia 25 zaidi ya yale yanayokusanywa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, mbali na wizi ulipo katika mfumo wa utendaji wa Serikali, kuna suala ambalo Serikali inaamua kukaa kimya katika kukusanya mapato. Mfano ni kwenye uvuvi wa bahari kuu, kutokuweka mazingira mazuri katika ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na madini ya vito; ukusanyaji wa maduhuli kwenye sekta ya mifugo n.k
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ni ukweli ulio wazi kwamba; tukiweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipa kodi, tukipanua wigo wa kodi, tukiwa na sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, ufanisi ukiongezeka TRA kwa asilimia 50[16],(Mazingira mazuri ya uwazi na haki na sio kuuunda vikosi kazi vya kutoa vitisho kwa walipa kodi).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka wa fedha 2017/18 makusanyo halisi ya Serikali yalikuwa ni shilingi trilioni 21.89, hivyo basi kutokana na mazingira ya serikali na uwezo mdogo wa kukusanya kutokana na mkanganyiko wa kiutawala. Mambo ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa inaweza kuyakabili na kuweza kukusanya mapato hayo kwa ziada ya asilimia 25.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo Kambi Rasmi ya Upinzani bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani itakuwa ya shilingi trilioni 27.363
Mheshimiwa Spika, ni nadharia na uzoefu wa kawaida kwamba; taifa lolote linalotaka kujitegemea na kujinasua kwenye dimbwi la utegemezi na umasikini linajitahidi sana kuwajengea watu wake uwezo wa ki-elimu, ki-ufundi na maarifa ili kuweza kukabiliana changamoto mabalimbali na hivyo kuweza kuyamudu mazingira yao. Kwa sababu hiyo; taifa la namna hiyo, huwekeza sana katika elimu ili kuandaa wataalamu (rasilimali watu) wa kutosha wenye weledi wa kuendesha sekta mbalimbali za uchumi.
Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu hiii, Serikali ya awamu ya kwanza ilikuja na sera ya Elimu ya Msingi kwa Wote – Universal Primary Education na kujikita sana kwenye elimu ya kujitegemea ambayo iliwapatia wengi maarifa ya kujiajiri na kuendesha maisha yao. Hata elimu ya juu iligharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Licha ya nchi yetu kuwa bado kwenye dimbwi la umasikini; na licha ya kuwa bado nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa rasilimali watu, Serikali hii ya awamu ya tano imechagua kuwekeza katika vitu badala ya watu. Ni kweli tunahitaji maendeleo ya vitu kama tunavyoona Serikali ikijenga reli ya kisasa, viwanja vya ndege, kununua ndege mpya ingawa hatuoni zikifanya kazi; ujenzi wa mabarabara nk. lakini nachelea kusema kwamba vitu hivyo vinaweza kudumu kwa muda mfupi mno kama hatutawajengea watu wetu uwezo wa kuvifanya wenyewe na kuviendesha. Kambi Rasmi ya Upinzani ingefurahi kuona makandarasi wa kujenga reli ya kisasa; na hata mabarabara yetu wakiwa ni watanzania wenzetu. Lakini tathmini fupi inaonyesha kuwa miradi mikubwa ya maendeleo hapa nchini iko mikononi mwa makandarasi wageni. Watu wetu wanaambulia kazi za kuchimba mitaro, kubeba mizigo na kufanya kazi zile ambazo hazihitaji ujuzi na matokeo yake hata ujira wao ni ule wa mboga tu.
Mheshimiwa Spika, Katika ulimwengu wa utandawazi, ufunguo wa mafanikio ya kiuchumi unategemea sana uwezo wa nchi kupata na kutumia ujuzi/maarifa kwa ufanisi na kwa faida katika sekta za kipaumbele na ambazo zinaweza kukua.Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu, kwa kuwa watu wenye ujuzi ndio msingi mkuu wa kuwepo kwa mfumo wa viwanda unaochochea ukuaji wa uchumi. Uwekezaji katika vitu na katika taasisi ni vikamilisho muhimu vya rasilimali watu; kwani rasilimali (vitu) haitatumiwa vizuri, iwapo itakosa ujuzi wa kiufundi na kiuongozi.
Mheshimiwa Spika, mpango wa maendeleo wa miaka mitano ndiyo dira inayotuongoza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotakiwa kutekelezwa na serikali kwa kipindi cha kuanzia bajeti ya mwaka 2016/17 hadi 2020/21
Mheshimiwa Spika, katika mpango huo umetoa mwelekeo ambavyo miradi yote ya maendeleo kwa kipindi hicho itakavyopatiwa fedha za maendeleo na kwa kiwango gani Serikali inatakiwa ichangie na Sekta binafsi inatakiwa kuchangia. Mpango wa maendeleo wa miaka mitano ulihitaji jumla ya shilingi za kitanzania trilioni 107 na kati ya fedha hizo Serikali serikali ilitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi trilioni 59(fedha za ndani,mikopo na misaada), ambazo zinatakiwa kila mwaka Serikali itenge kwenye bajeti yake wastani wa shilingi trilioni 11.8 na sekta binafsi ilitakiwa kuchangia shilingi trilioni 48 kwa wastani wa shilingi trilion 9.6 kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, kitabu cha Mpango wa miaka mitano kinaonesha kuwa bajeti za Serikali kwa miaka mitano ili kutekelezwa kwa ukamilifu mipango ya kila mwaka ilikuwa ni kama ifuatavyo:-Mwaka 2016/17 bajeti ilitakiwa kuwa trilioni 29.5396; mwaka 2017/18 bajeti ilitakiwa kuwa trilioni 30.4424; mwaka 2018/19 bajeti ilitakiwa kuwa trilioni 31.6129; mwaka 2019/20 inatakiwa kuwa shilingi trilioni 32.4701 na mwaka wa mwisho wa mpango, 2020/21 bajeti inatakiwa kuwa trilioni 33.7010
Mheshimiwa Spika, Mpango unaeleza kuwa Serikali ilikwisha fikia mwafaka wa kutenga asilimia 30-40 katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kambi rasmi ya Upinzani inauliza kama kweli uamuzi huo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mujibu wa mpango bado upo au umetupwa?
Mheshimiwa Spika, mpango umeeleza vizuri kuwa miradi yote ambayo ni “commercially viable projects should be left to the private sector, unless there is strong justification for doing otherwise”. Miradi hiyo ambayo ni commercially viable imeorodheshwa na gharama utekelezaji wake, ambayo ni ujenzi wa SGR, Ujenzi wa kiwanda cha LNG, Liganga Mchuchuma Industrial Park, Mtwara Petrochemical Special Economic Zone na Bagamoyo Special Economic Zone.[17]
Mheshimiwa Spika, kubadilika kwa Serikali kutoka katika mpango ambao ulipitishwa na Bunge hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ni sababu zipi za msingi ambazo Bunge halikupewa taarifa?
Mheshimiwa Spika, Katika bajeti ya serikali 2018/2019 imeainisha sekta ya kilimo kama kipeumbele cha serikali lakini haijaonyesha ni kwa namna gani hasa inalenga kufanya Mapinduzi ya Kilimo (Agrarian Revolution) ili kuweza kusisimua na sekta ya viwanda
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Mpango ya Waziri inaonesha kuwa mchango katika sekta za kiuchumi katika Pato la Taifa kilimo kilichangia asilimia 30.1 mwaka 2017 huku Sekta hiyo inachangia hutoaji wa ajira kwa asilimia 66, lakini ukuaji wake ni wa wastani wa asilimia 3.7. Katika kujiuliza sekta hiyo ambayo inatoa ajira asilimia 66 inachangia mapato ya kodi kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba mapato ya kodi kutokana na sekta hiyo ya kilimo ni kidogo sana. Kwa bahati mbaya sana katika hotuba ya Mpango wa Maendeleo uk. 38 aya ya 54 sekta ambazo zinaimarishwa ili kufangamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, sekta ya kilimo haipo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuangalia unyeti wa sekta hii katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati na uchumi wa viwanda ni lazima sekta ya kilimo iwe ndiyo ingine ya kutupeleka huko. Hivyo basi, pamoja na mambo mengine Kambi Rasmi ya Upinzani italenga kuondoa kodi zote kwenye uwekezaji katika sekta ya kilimo(kilimo,uvuvi na mifugo).
Mheshimiwa Spika, hii ni pamoja na kuondoa kodi kwenye uingizaji wa mashine mbalimbali zinazoingia katika mnyororo wa uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vinavyotengeneza na kukarabati mashine na zana nyingine za kilimo kama vile matrekta, pampu za umwagiliaji, mashine za uvunaji, viwanda vya kutengeneza madawa, mbolea, mbegu,na vifungashio, zana za uvuvi kama vile mitumbwi, nyavu, na zana nyingine za uvuaji. Katika mifugo itahakikisha kodi za mifugo zinaondolewa, na kodi za viwanda vinavyotengeneza madawa na chanjo mbalimbali za mifugo, pamoja na kupunguza kodi katika viwanda vya kuongeza thamani za mazao.
Mheshimkiwa Spika, katika kutimiza azma hiyo ya kukifanya kilimo kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Tanzania, Kambi Rasmi ya Upinzani itaondoa fedha zote zilizokuwa zimetengwa shilingi 700,000,000,000/- kwa ajili ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa maji katika mto Rufiji wa Stieglers Gorgi na zile zinazojenga Reli kwa kiwango cha Kati (SGR) pamoja na ununuzi wa ndege Boeing 787-8 na kuziweka kwenye sekta ya Kilimo na uendelezaji wa matumizi ya bomba la gesi asilia katika uzalishaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa kumezuka ubadhirifu mkubwa wa taasisi za Serikali kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi kadhaa wakati huo utekelezwaji wa miradi hiyo hakuna uhakika wa kupata fedha. Au miradi ambayo inatakiwa kutumia fedha nyingi katika utekelezaji wake hadi kukamilika inapatiwa fedha kidogo sana kiasi ambacho haiwezi kukidhi hata robo ya mahitaji.
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni matumizi mabaya ya rasilimali zetu chache tulizonazo, kwani fedha hizo ni sawa na kuchimba shimo na kuzifukia badala ya kuziweka kwenye mzunguko wa kibiashara. Mfano ni,RAHCO ilitumia zaidi ya Shilingi bilioni 20.1 kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi iliyopangwa kutekelezwa ambayo ni (i) Arusha-Musoma, (ii) Mtwara-Songea-Mbambabay, (iii) Uvinza-Musongati-Mpanda-Karema, na (iv) Tabora-Kigoma-Kaliua-Mpanda. Hata hivyo, miradi hiyo haikutekelezwa kutokana na changamoto za kifedha licha ya kutumia gharama za awali za Shilingi bilioni 20.1 kufanya upembuzi huo.
Mheshimiwa Spika, Malipo ya Riba Yatokanayo na Kucheleweshwa kwa Malipo ya Wakandarasi Shilingi 3,889,404,110.00 zililipwa kama riba kutokana na kutolipa madai ya wakandarasi kwa wakati yaliyohusisha miradi ya Programu ya Msaada katika Sekta ya Barabara Awamu ya Kwanza (RSSP I), RSSP II na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili (WSDP II). Ucheleweshwaji wa malipo ya wakandarasi ulitokana na Hazina kutopeleka fedha za miradi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, katika ukaguzi ilibainika kuwa wakala wa barabara nchini (TANROADS) pamoja na wakala wa majengo TBA kwa ujumla walilipa kiasi cha shilingi 587,226,567.00 kama adhabu ya kuchelewesha kulipa madai ya wakandarasi na marejesho ya mkopo.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, jumla ya fedha za Serikali zilizopotea kwa kulipa riba inayotokana na uzembe wa kutokuwepo kwa mipango madhubuti ni shilingi 4,476,630,677.00
Mheshimiwa Spika, Serikali kushindwa kuunda Bodi za Wakurugenzi za Mashirika ya Umma maana yake ni kuwa mashirika hayo yafanye kazi bila kukaguliwa na CAG, Kutokuwepo kwa Bodi ya Wakurugenzi na Wadhamini kunazorotesha shughuli za kiutendaji za mashirika hayo. Taarifa ya CAG inaonesha kuwa Kwa mwaka huu wa ukaguzi, kulikuwa na Bodi za mashirika 20 ambazo zimemaliza muda wake. CAG anasema kwamba hadi anakamilisha ukaguzi wake Mwezi Machi, 2018; hakukuwa na Bodi mpya za kusimamia mashirika hayo zilizochaguliwa. Baadhi ya taasisi zimekuwa zikiendelea na utendaji wa kazi bila ya Bodi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bunge ilipendekeza na kupitisha sheria kwa ajili ya kutoza tozo mbalimbali ili kuunda mifukoya kuendeleza sekta mbalimbali za uchumi.Kwa mujibu wa taarifa ya CAG inaonesha kuwa makusanyo ya tozo hizo yamekuwa yanakwamba. Taarifa hiyo inaeleza kuwa TRA ilishindwa kuwasilisha Ushuru wa Maendeleo ya Reli ya Shilingi Bilioni 194.31 kwa RAHCO kulingana na matakwa ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo TRA imeshindwa kupelekea kwenye mfuko wa barabara “road fund” kiasi cha shilingi 14,828,686,613.55 au bilioni 14.83, na ukweli ni kuwa fedha zilikusanywa na lakini kwa makusudi kabisa hazipelekwe na hivyo kukwamisha miradi ya ukarabati wa barabara kama hitajio la uanzishwaji wa tozo hiyo.
Mheshimiwa Spika, aidha CAG anazidi kutueleza kuwa TRA imeendelea kuhesabu kuwa ni mapato kwa kutorejesha fedha za VAT kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 kwa watekelezaji wa miradi 16. Hizi ni fedha halali za wakandarasi na hivyo hazitakiwi kuonekana kama ni fedha za kodi kwa Serikali. Jambo hili pia linapelekea kuonesha kama TRA inakusanya mapato mengi lakini ukweli sio hivyo.
Mheshimiwa Spika, kukuza makusanyo ya kodi kutoka makusanyo ya asilimia 13 ya pato la taifa na kufikia asilimia 16 ya pato la taifa, inatakiwa mfumo wa kodi kuwa wa haki na uwazi(tax system which is transparent and fair)[18] ili kuondoa uonevu kwa walipa kodi ambao kwa kiwango kikubwa ndio umetawala na hivyo kuwakatisha tamaa walipa kodi na wengine kufunga biashara na pengine kuhamisha biashara zao nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kuwepo kwa mfumouliowazi na wa haki katika kodi, Mamlaka mbalimbali zinazosimamia ubora wa bidhaa kupunguza tozo na kuangalia namna ya kupanua wigo wa ukusanyaji wa kodi ili kupunguza rundo la kodi kwa watu wachache.
Mheshimiwa Spika, mbali na jambo hilo pia mambo yafutayo ni lazima yarekebishwe ili kupanua wigo wa walipa kodi wapya na kutoa motisha kwa walipa kodi kuendelea kulipa kodi(biashara zao kuendelea kukua wakati wakilipa kodi);
Jedwali Na. 1: Sura ya Bajeti mbadala kwa Mwaka Wa Fedha 2018/19
MAELEZO | MAPATO (TZS) | |
JUMLA YA MAPATO YA KODI
|
15,762,500,000,000. | |
MAPATO YASIYO YA KODI | 2,237,500,000,000. | |
MAPATO YA HALMASHAURI | 547,000,000,000. | |
MIKOPO NAFUU+ MIKOPO YAKIBIASHARA | 8,815,500,000,000. | |
JUMLA YA MAPATO | 27,362,500,000,000. | |
MATUMIZI | ||
MATUMIZI YA KAWAIDA | ||
Deni la Taifa | 7,004,480,000,000. | |
Mishahara | 7,409,952,000,000. | |
Matumizi mengineyo | 2,054,244,000,000. | |
JUMLA NYA MATUMIZI YA KAWAIDA | 16,468,676,000,000. | |
MATUMIZI YA MAENDELEO | ||
Fedha za ndani + Nje | 10,893,824,000,000. | |
JUMLA YA FEDHA ZA MATUMIZI | 27,362,500,000,000 | |
Mheshimiwa Spika,katika bajeti yetu mbadala; badala ya kulipa deni la taifa la shilingi trilioni 10 kama ambavyo bajeti ya serikali inaonesha, Sisi tutalipa kiasi cha shilingi trillion 7. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika biashara yoyote kuna nafasi ya majadiliano, hivyo tutafanya majadiliano ya kulipa kiasi hicho.
Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakua na vipaumbele katika sekta zafuatazo;
Jedwali Na. 2 : Mgawanyo wa Fedha katika Sekta za Kipaumbele
Na. | Sekta | Kiasi (Tshs.) | Asilimia (%) |
1. | Elimu | 1,634,073,600,000. | 15 |
2. | Kilimo | 2,178,764,800,000. | 20 |
3. | Viwanda | 1,634,073,600,000. | 15 |
4. | Maji | 1,089,382,400,000. | 10 |
5. | Afya | 1,089,382,400,000. | 10 |
6. | Mengineyo | 3,268,147,200,000. | 30 |
7. | JUMLA | 10,893,824,000,000. | 100 |
Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia hotuba yangu kwa kurejea tena wito wangu kwa Serikali na wananchi wote wenye mapenzi mema; kwamba; “hili taifa ni letu sote” Hakuna Mtanzania zaidi ya mwingine – wote ni watanzania. Hizi kauli za kusema kwamba kuna wazalendo na wasio wazalendo au wapinga maendeleo, ni kauli za kibaguzi na hazilijengi taifa bali zinalipasua.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika hakuna yeyote mwenye hati miliki ya Taifa hili. Kama kuna kiongozi aliyepewa dhamana ya kuliongoza taifa hili kwa kipindi fulani cha muda; atambue kwamba hiyo ni dhamana tu – tena ya muda mfupi, lakini hii nchi sio mali yake. Ana wajibu wa kuliunganisha taifa na sio kulisambaratisha au kuligawa kwa misingi ya aina yoyote ile – iwe ya kidini, kiitikadi au ukanda.
Mheshimiwa Spika, Utangamano katika taifa ni jambo la msingi sana. Umoja na mshikamano wa kitaifa ndio moyo wa taifa lolote duniani linalohitaji kuwepo na kuendelea kuwepo. Inatakiwa Mtanzania mmoja akiumizwa iwe tumeumizwa wote; mmoja akipotea tuhuzunike wote; – lakini yanayoendelea sasa; ya wengine kupotea huku wengine wanafanya sherehe; wengine kuuwawa huku wengine wakiendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna kilichotokea; tunajenga utamaduni na desturi mbaya kuwahi kutokea duniani; na yamkini tukaingia kwenye kitabu cha rekodi za dunia (the guiness book of records) za kuwa taifa la kwanza duniani lisilojali utu wa mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tena; uhalali (legitimacy) hautafutwi kimabavu. Hali kadhalika heshima hailazimishwi bali huja yenyewe kutokana na matendo mema afanyayo mtu na watu wengine kuwiwa kumpa heshima. Ili uheshimike kama kiongozi timiza wajibu wako wa kutenda haki kwa kila mtu – kwa kufanya hivyo Mungu ataiamuru heshima ikufuate – hata kama uko usingizini.“But don’t kill or plan to kill, demanding respect and legitimacy by force; it will backfire”
Mheshimiwa Spika, majibu sahihi ya kuondokana na athari za utukufu binafsi (personal glory) katika kuongoza nchi ni kujenga mifumo na taasisi imara zitakazojisimamia na kujiendesha kwa namna ile ile hata kama atakuja kiongozi mwingine ili tuweze kuwa na uendelevu (sustainability) katika utendaji wa Serikali na pia kuondoa manung’uniko dhidi ya viongozi. Dawa pekee ya kuondoa kufanya kazi kwa upendeleo (subjectivity and bias) ni kuongoza na sheria, taratibu na kanuni na sio utashi wa mtu.Kujenga taasisi imara kwa maendeleo endelevu inawezekana ikiwa tutahuisha mchakato wa Katiba Mpya. Hii ni changamoto kwa Serikali na Taifa lingependa kupata kauli ya Serikali juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Mwisho kabisa, Serikali iache kufanya propaganda katika mambo ya msingi hasa katika bajeti ya Serikali. Tumeeleza kwa kirefu jinsi Serikali inawahadaa wananchi kwa kuweka makisio makubwa ya ukusanyanji wa mapato ambayo inajua kabisa kuwa haiwezi kukusanya na hivyo kuwapa wananchi matumaini hewa! Kwa kuwa Serikali hii ya awamu ya tano ilikuwa bingwa sana kukabiliana na vitu hewa – kuanzia wafanyakazi hewa na madai hewa ya watumishi; ijisafishe na yenywe kwa kuacha kupanga bajeti hewa kwa maendeleo ya taifa hili.
Mheshimiwa Spika,baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
David Ernest Silinde (Mb)
KNY:WAZIRI KIVULI WA FEDHA NA MIPANGO
NA MSEMAJI MKUU WAKAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
18 Juni, 2018
VIAMBATANISHO: UCHAMBUZI WA KISEKTA
HAKUNA SERA KAMILI YA UGATUAJI WA MADARAKA
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana ni kwamba hakuna SERA iliyopo tayari inayotoa mwongozo na uelekeo wa UGATUAJI WA MADARAKA unavyotakiwa kufanyika na kutungiwa sheria na Bunge, badala yake ni mawasilisho ya tafiti mbalimbali tu. Udhaifu huu ndio umepelekea mvurugano unapelekea hata uvunjwaji wa Katiba Ibara ya 146, kuhusu ushirikishwaji wa wananchi katika kujiletea maendeleo yao.
Mheshimiwa Spika kutokana na ukosefu wa Sera hiyo ya ugatuzi kumeanza kutokea upotoshaji kuhusu D by D. Wakati D by D inajulikana kuwa ni Decentralization by Devolution – yaani ugatuaji wa madaraka kamili kwa Serikali za mitaa; sasa wengine wameanza kutafsiri D by D kuwa ni Decentralization by Directives or Delegation. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni lini itatunga Sera ya Ugatuzi wa Madaraka kwa Serikali za Mitaa na kuleta Muswada Bungeni ili Ugatuzi huo utungiwe Sheria?.
FEDHA ZA MRADI YA MAENDELEO KUTOFIKA KWA WAKATI KATIKA HALIMASHAURI
Mheshimiwa Spika,Katika kujiletea maendeleo raslimali fedha toka Serikali kuu ni muhimu sana lakini kuna tatizo la Serikali kushindwa kupeleka fedha zinazopitishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenda kwenye Halmashauri zetu kwa ukamilifu wake na kwa wakati. Hata pale zinapopelekwa kwa ukamilifu kuna tatizo kwamba zinakwenda kwa vipande vipande kiasi kwamba utekelezwaji wa miradi unashindikana, kutokana na mazingira halisi yanayokuwepo kwa wakati huo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kupeleka fedha za miradi katika robo ya mwisho ya mwaka, jambo linalopelekea kushindwa kutumika kwa fedha hizo kutokana na utaratibu mzima wa kufuata sheria ya manunuzi ambayo inahitaji kutimizwa kwa masharti. Hivyo kupelekea fedha hizo kurudishwa Serikali kuu.
KUCHELEWESHWA KWA MIONGOZO YA BAJETI NA UKOMO WA BAJETI
Mheshimiwa Spika, hapa jambo kubwa na haraka linalohitajika ni kuimarisha mifumo yetu ya uwajibikaji, na jambo hili haliwezi kuwa ni suala la watawala tu bila watawaliwa kushirikishwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inamini kwamba Katiba mpya ndiyo suluhisho la utengenezaji wa mifumo mipya ya uwajibikaji ambayo haitachezewa kwa matakwa ya yule atakayepewa ridhaa ya kuisimamia.
UTARATIBU WA BAJETI YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa bajeti ya serikali unakumbwa na changamoto kadhaa ambazo huathiri utekelezaji wa bajeti hiyo hata baada ya kupitishwa na Bunge. Inatambulika kuwa maandalizi ya Bajeti ya mwaka wa fedha unaofuata huanza mapema baada tu ya kuanza mwaka wa fedha mpya. Aidha, inafahamika kuwa bajeti hutakiwa kuanzia kwenye ngazi za Vijiji na Mitaa kwa mfumo wa kuibua fursa na changamoto katika maendeleo (O- and OD) na baadaye kwenda Halmashauri na ngazi ya Mkoa. Hata hivyo uzoefu unaonesha kuwa mambo yamekuwa yakipangwa kuanzia ngazi ya Halmashauri pekee na sio shirikishi kama inavyotakiwa. Hata utofauti wa takwimu kwenye vitabu vya bajeti ambao Kambi Rasmi ya Upinzani ilionesha kwa miaka miwili mfululizo huenda unasababishwa na utaratibu wa Halmashauri kujipikia takwimu na miradi bila kushirikisha ngazi za chini katika mipango.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya serikali kwa namna moja ama nyingine imekua ikiathiriwa na maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wa Serikali. Mathalani kama Halmashauri ilipanga kukusanya kodi kupitia kwenye masoko au mazao inaathiriwa na agizo linalotolewa katikati ya mwaka wa fedha kuwa vyanzo hivyo visiendelee kutozwa kodi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuacha kutoa maelekezo ambayo yanaathiri bajeti za Halmashauri na wakati huo huo ni Serikali hiyo hiyo iliyokubali mipango ya Halmashauri hizo kabla ya kupitishwa na Baraza la Madiwani.
VYANZO VYA MAPATO VYA HALMASHAURI KUCHUKULIWA NA SERIKALI KUU
Mheshimiwa Spika, ili halmashauri ziwe na uwezo wa kuleta maendeleo endelevu mbali na mgawo unaotoka Serikali kuu, ni lazima na muhimu kwa halmashauri kuwa na vyanzo vya ndani vya mapato na fedha hizo kuzitumia kulingana na mahitaji na mipango inayopangwa kuanzia Serikali za vijiji.
Mheshimiwa Spika, Vyanzo vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vimeainishwa katika vifungu Na. (6) hadi (9) vya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka 1982 yaani (The Local Government Finance Act, No. 9 of 1982).Kulingana na Sheria ya Fedha Na. 9 ya mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa iliyorekebishwa na Sheria ya Fedha Na. 15 ya mwaka 2003 yaani (The Finance Act No. 15 of 2003), Serikali za Mitaa hazitozi kodi ya Mapato bali kodi hiyo hutozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA). Ni muhimu sana Serikali kuu hasa awamu ya tano iache utaratibu wake iliouanzisha tangu iingie madarakani wa kupora vyanzo vya mapato vya halimashauri.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa ardhi ndiyo rasilimali pekee ambayo kila Halmashauri katika nchi inaimiliki. Ardhi ndiyo chanzo cha mapato cha uhakika kwa kila Halmashauri ya nchi hii, hivyo kitendo chochote cha Serikali Kuu kupora au kujaribu kupora chanzo hiki ni kuifanya halmashauri kushindwa kabisa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zinatakiwa kuchukua 30% ya kodi ya Ardhi, hivyo inapotokea kuwa Serikali Kuu inachukua fedha hizo na urejeshaji wake unakuwa ni pale itakapojiridhisha kuwa zinahitajika, hilo sio sahihi kwa maendeleo ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Chanzo hicho cha mapato ya halimashauri kinachotokana na kodi ya ardhi kama makusanyo ya ndani (own source) ni muhimu sana katika kuzifanya halimshauri zikabiliane na changamoto mbali mbali za kuhudumia wananchi. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri serikali kuziruhusu halimashauri ziendelee kukusanya hiyo asilimia 30 ya kodi ya Ardhi.
ASILIMIA KUMI YA MFUKO WA VIJANA NA WANAWAKE ITENGEWE AKAUNTI YAKE MAALUM KATIKA HALIMASHAURI
Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na mwongozo wa Serikali unaoelekeza kuwa kila halimashauri kutenga asilimia 10 kutokana na mapato ya ndan kwa ajili ya mfuko wa vijana na wnawake. Jambo hili ni jema sana iwapo litaratibiwa vizuri kwa vile litasaidia ajira kwa wajasiriamali mbali mbali nchini. Hata hivyo, tangu muongozo huu utolewe na Serikali, utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi sana katika halimashauri nyingi kutokana na ufinyu wa bajeti za ndani za halimashauri ukilinganisha na Vipaumbele vya halimashauri hapa nchini pamoja na makusanyo duni ya mapato.
Mheshimiwa Spika, hakuna Sheria rasmi iliyotungwa na bunge inayosimamia mfuko huu, hivyo kuufanya kama mfuko wa hiari unaotegemea matamko na maagizo ya viongozi wenye dhamana na serikali za mitaa. Hakuna Akaunti maalum katika Halmashauri ya kuweka fedha hizo pale zinapokusanywa na pale wakopeshwaji wanaporejesha marejesho yao.
Mheshimiwa Spika, Matokeo yake fedha hii inakaa kwenye mfuko mkuu wa halmashauri hivyo kuwa vigumu kuitenganisha na shughuli nyingine za halimashauri. Aidha, kwa vile fedha hii inazunguka kwa kukopeshwa yaani ni “Revolving fund” inatakiwa baada ya muda fulani wa takribani miaka mitano iwe imekuwa ni mtaji mkubwa ambao utajiendesha wenyewe kibiasharana hivyo kuzifanya halimashauri zijielekeze kwenye shughuli zingine za kijamii.
Mheshimiwa Spika Kambi Rasimi ya Upinzani inashauri mambo matatu makubwa ili kuuboresha mfuko kwa ajili ya kufikia malengo yaliyotarajiwa:
UJIO WA WAKALA WA JUENZI WA BARABARA VIJIJINI-TARURA
Mheshimiwa Spika, Tarura ni wakala iliyoundwa kwa kupitia Tangazo la Serikali (Government Notice na. 211 ya Juni 2017, kwa madhumuni ya kuhudumia barabara zote zilizokuwa zinahudumiwa na Halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Hivyo basi, mfumo mzima wa uanzishwaji wake ukiangalia kwa undani haukuwa wazi kiasi kwamba utaacha maswali mengi sana yasiyo na majibu juu ya utendaji wa Halmashauri zetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwmba ni azimio la buge lako tukufu lilopelekea kuanzishwa kwa TARURA lakini ujio wake umekuwa wa haraka na haukuwa shirikishii, kwa kiwango cha kuridhisha. Mpaka sasa kuna mkanganyiko mkubwa kati ya watendaji wa TARURA na Madiwani pamoja na watendaji wa halimashauri hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, maeneo yenye utata zaidi ni ÷
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haikubaliani na kuanzishwa kwa Chombo hiki cha TARURA kama mambo yafutayo hayatazingatiwa;
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu ni kwamba barabara zilizopo chini ya TARURA ni Kilomita 108, 946.2; mwaka huu TARURA imesimamia matengenezo ya Kilomita 4,183.3 tu. Hii maana yake ni kwamba itachukua muda wa miaka 26 kuweza kukamilisha ujenzi barabara zote zilizopo chini ya TARURA. Kwa uchache huu wa barabara zilizotengenezwa, Serikali ione umuhimu wa kuchukua mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuongeza fedha kwa mamlaka hii ili malengo yake yaweze kufikiwa.
MATAMKO BILA MKAKATI WA UTEKELEZAJI
Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tumesikia tamko la Waziri wa TAMISEMI kuwa kila mkoa ujenge viwanda 100. Hiki ni kitu kikubwa kinachotakiwa kiwe na Sera itakayoonesha wadau watashiriki vipi katika ujenzi huo wa viwanda 100 na sera hiyo itengenezewe Mkakati wake na chini yake Bunge litunge sheria yake pamoja na Kanuni kwa kueleza wazi katika mkoa viwanda vya aina gani vya kimkakati vijengwe na ushiriki wa kila Halmashauri, Kata na Kijiji na namna ya kupata Raslimali za viwanda hivyo 100.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kuwa viwanda hivyo 100 vitatumia teknolojia gani na soko la bidhaa zake litakuwa ni wapi ukizingatia kwamba kuna ushindani mkubwa sana wa soko kikanda na kimataifa na Soko la ndani halitaweza kubeba bidhaa za viwanda hivyo iwapo kweli vitajengwa kama Mheshimiwa Waziri alivyoagiza.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali kwamba dhana hii ya ujenzi wa viwanda lazima iwe shirikishi na usiwe mtazamo wa mtu mmoja ikiwemo kushirikisha wataalamu waliobobea katika sekta hiyo. Aidha, lazima dhana hii iangalie miaka zaidi ya 50 ijayo, hivyo ni muhimu sana kujenga taasisi imara itakayosimamia mpango huu ili uwe endelevu na usije ukashindwa kama ulivyoshindwa miaka ya nyuma.
SERA YA ELIMU BURE/BILA ADA
Mheshimiwa Spika, ukiangalia changamoto zinazotokana na tamko la elimu bure, na sasa imekuwa elimu bila ada ni matokeo ya kutoa sera zitakazo athiri maisha ya watu katika majukwaa ya kisiasa bila kufanya utafiti wa kutosha. Aidha, kumekuwa na mkanganyiko mkubwa katika utekelezaji wa matamko hayo ya viongozi wa juu kwa vile kila mmoja ana uelewa wake juu ya dhana hii ya elimu bure au elimu bila mailipo. Tunafahamu kuwa elimu ya Msingi na Sekondari ipo chini ya TAMISEMI lakini matamko hayo kwakuwa yanatolewa bila maandalizi yanapelekea mipango yote iliyokuwa tayari inaanza kutekelezwa kusitishwa kwa ajili ya matamko kutoka Serikali Kuu; ambo ambalo llinasbabisha kuanguka kwa ubora wa elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasimi ya Upinzani inaendelea kuishauri serikali iwe makini wakati inafanya maamuzi makubwa yanayogusa maisha ya watu hivyo kutoendelea na utaratibu ambao sasa umekuwa ni kawaida wa uendeshaji nchi kuwa ni wa mwendokasi bila ya kuwa na uelekeo,“speed without direction is useless” matokeo yake ni kupelekea raslimali finyu tulizonazo kutotumika kwa ufanisi.Aidha, Serikali lazima itambue kwamba waathirika wakuu wa matamko ya viongozi wakuu ni wananchi ambao wanahitaji Serikali yao iwapatie huduma kutokana na mipango ambayo wanakuwa wameiibua na kuiweka kuwa ni kipaumbele chao.
FEDHA ZA UTEKELEZAJI ELIMU MSINGI
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa muundo wa Serikali ulivyo ndiyo inaratibu na kutekeleza sera na mkakati wa elimu ya msingi na sekondari na pia ndio wamiliki wa shule zote za msingi na sekondari zinazomilikiwa na Serikali na pia ndio waendeshaji wa shule hizo. Hivyo ndio wawajibikaji wakuu wa hali ya elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, takwimu za utafiti wa Haki Elimu zinaonesha kuwa uwiano uliopo sasa wa matundu ya vyoo na wanafunzi wa kike ni 1:53 wakati uwiano unaoshauriwa ni 1:20 na kwa wavulana uwiano uliopo ni 1:56 na unaoshauriwa ni 1:25. Hivyo kufanya upungufu wa mashimo ya vyoo kwa wsichana kuwa 62% na kwa wavulana kuwa 56%. Sambamba na hilo taarifa inaonesha kuwepo kwa upungufu wa nyumba 186,008 za walimu wa shule za msingi sawa na 83.1% majengo ya utawala 10,943 sawa na 83.4%.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya elimu kwa ujumla mwaka wa fedha 2016/17 ilitengewa jumla ya shilingi 4,770.4 billion na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 zilitengwa Tsh. bilioni 4,706.4 kwa matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo[19], hii ikiwa sawa na asilimia 14.8 ya bajeti mzima ya Serikali ya shilingi 31,712 billion. Uchambuzi unaonesha kuwa bajeti ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2015/18 ilikuwa ni 17% ya bajeti ya mwaka huo na 2016/17 ilikuwa ni 16%.
Mheshimiwa Spika, sekta ya elimu inahusisha fedha zinazotengwa TAMISEMI, wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na taasisi zingine zinazohusika na elimu kama vile Tume ya UNESCO, wizara ya afya kwa kuendesha program za afya na usafi mashuleni, Tume ya huduma kwa walimu (Teacher Service Commission) n.k
Mheshimiwa Spika, Ili kufanyakazi zake za kuratibu na kuendesha elimu ya msingi na sekondari Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2016/17 ilitengewa shilingi bilioni 3,069.5 na kwa mwaka wa fedha 2017/18 zilitengwa shilingi bilioni 3,279.6 ambazo ni sawa na asilimia 69.7 ya bajeti yote ya sekta ya elimu. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 3,063.1 sawa na 93.4% zilikuwa ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 216.5 sawa na 6.6% zilikuwa ni za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imechambua taarifa hiyo ya mgawo wa fedha kwa mujibu wa utafiti wa HakiElimu ili kuwataka waheshimiwa wabunge kujadili na kuona kama kweli elimu yetu inatendewa haki kutokana na mgawo huo wa fedha. Haiingii akilini kwamba fedha za maendeleo katika elimu ni asilimia 6 tu halafu Serikali ijigambe kwamba tuna elimu bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kupinga kitendo cha Serikali Kuu kuendelea kupora vyanzo vya mapato vya Serikali za mitaa kwa kuwa vyanzo hivyo ndivyo vilivyosaidia Halmashauri kuwa uwezo wa kutoa huduma bora katika sekta ya elimu ambapo uwezo huo umepungua kutoka na vyanzo vyake kuchukliwa na Serikali Kuu. Ujenzi wa vyoo, nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na ofisi za walimu ni fedha za “own source” zinazotakiwa kufanyakazi hiyo. Sasa vyanzo vikuu hakuna na michango ya wazazi hakuna hapo kuna elimu bora kweli?
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika, mwaka ujao wa fedha Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) italeta bajeti yake ambapo pamoja na mambo mengine sehemu ya bajeti hiyo itahusisha pia maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 Serikali ilikutanisha wadau wanaohusika na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa vikiwemo Vyama vya Siasa Mjini Morogoro kwa ajili ya kupokea maoni yao kuhusu Kanuni za uchuguzi huo. Moja ya changamoto zilizoibuliwa wakati huo ilikuwa ni uchaguzi wa Madiwani kufanyika tofauti na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wakati huo huo Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ambapo Wajumbe wake ni Wenyeviti wa Vijiji au Mitaa katika Kata husika.
Mheshimiwa Spika, aidha ilielezwa pia kuwa ni vema usimamizi wa uchaguzi huo ufanywe na Tume ya Uchaguzi kuanzia kwenye uandikishaji wa wapiga kura mpaka siku ya uchaguzi. Serikali kupitia kwa Waziri wa TAMISEMI wakati huo Mheshimiwa Hawa Ghasia ilikubali na kuahidi kuwa Serikali ingewasilisha muswada Bungeni ili kufanya marekebisho ya utaratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi na pia uchaguzi wa Madiwani kufanyika pamoja na Serikali Mitaa ifikapo mwaka 2019.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mapungufu ya kimfumo na kisheria yaliyopo kwenye Tume ya Uchaguzi ya sasa, ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kutekeleza ahadi yake iliyoitoa kwa Vyama vya Siasa Mjini Morogoro mwaka 2014 ili kuzifanyia kazi changamoto za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwakani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kuwa kimfumo uchaguzi wa nchi hii unasimamiwa na TAMISEMI kwa sababu Tume inawatumia Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi, na ikumbukwe kuwa tulishaeleza kuwa Wakurugenzi wengi wa Halmashauri walioteuliwa na Rais ni makada wa Chama cha Mapinduzi walioshindwa uchaguzi wa mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 (14) inakataza maofisa wanaohusika na uchaguzi kujihusisha na Siasa, licha ya katazo hilo tumeshuhudia Wakurugenzi wengine wakishiriki vikao vya CCM. Katika hili hatushangai Vyama vya Upinzani vikishinda uchaguzi inalazimishwa kutangaza mgombea wa CCM ambaye hajashinda.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni lini Serikali italeta muswada hapa Bungeni kwa ajili ya kupitia upya mfumo wa uchaguzi nchini ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye uchaguzi ukizingatia kwamba uchaguzi ni zoezi muhimu kwa ajili ya demokrasia na utawala bora.
MGOGORO WA HALMASHAURI YA MJI WA TUNDUMA
Mheshimiwa Spika, naomba ieleweke kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 145 na 146, imeunda Serikali za Mitaa na kutamka bayana kuwa Serikali za Mitaa ni vyombo vya wananchi ambavyo vipo katika ngazi za chini za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vyombo hivi huundwa, huendeshwa, husimamiwa na kuwajibika kwa wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 1982 inazungumzia uundaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo ya mijini, ambazo ni Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji. Tunatambua kuwa Halmashauri ya Mji wa Tunduma imeundwa kwa mujibu wa sheria hii.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa katika Bunge lako tukufu kuwa kumekuwa na mgogoro ndani ya Halimashauri ya Mji wa Tunduma ambao chanzo chake ni maagizo yaliyotolewa kwenye waraka wa Mkuu wa Wilaya ya Momba Juma Said Irando yasiyozingatia Sheria za uendeshaji wa Halmashauri. Waraka huo ulitolewa tarehe 18 Septemba, 2017 kwa Watendaji wote wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Waraka huo wa Mkuu wa Wilaya ya Momba uliwaagiza watumishi wote wa Halimashauri kutowapatia ushirikiano wowote viongozi wa kuchaguliwa yaani Wahe. Madiwani pamoja na Mwenyekiti wa Halimashauri ikiwa ni pamoja na kuzuia stahiki zao kama posho, kuzuia kufanyika kwa vikao halali kama vya Baraza la Madiwani na Kamati mbalimbali za Halimashauri.
Mheshimiwa Spika, Waraka wa Mkuu wa Wilaya kwa watumishi wa Halimashauri unakwenda kinyume na Sheria za Serikali za Mitaa namba 7 na 8 za mwaka 1982, kwani Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepewa madaraka mbalimbali ya kisheria ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Baadhi ya madaraka hayo ni pamoja nakufanya Maamuzi.
Mheshimiwa Spika, Chanzo cha mgogoro na Mkuu wa Wilaya ni kutokana na Taarifa za upotevu wa makusanyo ya ushuru wa magari ambayo yalivuka mpaka wa Tunduma katika mwaka wa fedha 2016/17. Madiwani walibaini kuwa Idadi ya magari yaliyovuka Mpaka kwa mujibu wa taarifa rasmi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Halmashauri ilitakiwa iwe imekusanya kiasi cha shilingi 695,450,000 ila fedha inayoonekana kuingizwa Halimashauri ni shilingi 463,445,000 na hivyo kuwa na upungufu wa shilingi 232,000,000.
Mheshimiwa Spika, Katika kikao cha Kamati ya Fedha kilichoketi na kubaini wizi huu wa fedha za Halmashauri, kikao kiliagiza kuwa ufanyike uchunguzi ili kubaini ni wapi makusanyo hayo yalienda, jambo la kushangaza ni kuwa Mkuu wa Wilaya alikataa uchunguzi huo kufanyika na badala yake alielekeza kuwa watumishi waliohusika katika upotevu huo wapongezwe na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Wilaya ya Momba kwa kitendo hiki cha kuzuia uchunguzi ili kubaini upotevu wa fedha za Halmashauri anafanya kosa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na.9 ya mwaka 1982 kifungu cha 14, ambacho kinaitaka kila Halmashauri ya Wilaya na kila Mamlaka ya Mji (Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji) kutoza na kukusanya kodi na mapato mengine ambayo yatatosheleza matumizi yaliyoidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya ya Momba amekuwa na tabia ya kuingilia uendeshaji na utendaji wa Halimashauri. Mkuu wa Wilaya amekuwa akitoa maagizo na maelekezo ambayo yanaenda kinyume na maamuzi yaliyokwisha kufanywa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kuingizwa kwenye bajeti kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, Kwa mfano Mkuu wa Wilaya ameagiza kuwa ujenzi wa Shule ya Msingi ufanyike eneo la Makambini ambalo ni eneo lililoko katikati ya Mahoteli na Bar! za starehe wakati Halmashauri ilishafanya uamuzi kuwa eneo hilo pajengwe stendi na ilishatenga eneo linguine katika kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi na ujenzi ulikua unaendelea .
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika Mkuu wa Wilaya ya Momba amekua akiingilia utekelezaji wa bajeti ya Halmashauri ambayo ilishapitishwa na Baraza la Madiwani. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2017/18 Halmashauri ilitenga Fedha kwenye bajeti yake na kupitishwa na TAMISEMI kiasi cha shilingi Milioni 12.6 kwa ajili ya kuwalipa posho ndogo Wenyeviti wa Mitaa kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya, lakini Mkuu wa Wilaya alimuagiza Mkurugenzi kutolipa fedha hizo kwa Wenyeviti wa Mitaa na badala yake anazipangia matumizi mengine kinyume kabisa na utaratibu wa uendeshaji wa Halmashauri na huku ni kukiuka kwa makusudi sheria na Kanuni za uendeshaji wa Halimashauri.
Mheshimiwa Spika, Vile vile Mkuu wa Wilaya ya Momba amezuia kufanyika kwa vikao halali na vya kisheria vya Halmashauri kinyume na Sheria. Mkuu wa Wilaya baada ya agizo lake la kuwazuia watumishi wa Halmashauri kutokutoa ushirikiano kwa Madiwani mpaka alisababisha Halmashauri kushindwa kutimiza wajibu wake wa kisheria wa kujadili na kufunga taarifa ya fedha ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya kufikishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya Ukaguzi , jambo ambalo lilitishia hata uwepo wa Halimashauri ya Mji wa Tunduma.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inashindwa kuelewa malengo ya Mkuu huyo wa Wilaya dhidi ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Kwa maelekezo yake ya hovyo na kuingilia utendaji wa Halmashauri je Madiwani wanapaswa kulaumiwa? Je ile dhana ya kupambana na ufisadi inatekelezwa kwa hali hii ambayo tumeonyesha?
Mheshimiwa Spika, natambua kuwa yapo maelekezo yaliyotolewa na Waziri mwenye dhamana baada ya kuandikiwa barua kuhusu mgogoro huu na Mwenyekiti wa Halmashauri lakini maelekezo hayo hayajatekelezwa kwa sababu bado Mkuu wa Wilaya na kwa wakati huu akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wanaendelea kusimamia maamuzi yao ya kuwataka Watendaji wa Halmashauri kutowapa ushirikiano Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Spika, kama inafikia hatua Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anashindwa kutekeleza maelekezo ya Waziri, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kuna tatizo kubwa ambalo pengine Bunge lako tukufu linatakiwa kuchukua hatua kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Serikali.
VITEGA UCHUMI VYA HALMASHAURI KUPORWA NA CCM CHINI YA USIMAMIZI WA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, tangu Serikali hii ya awamu ya tano imeingia madarakani kumekuwa na wimbi kubwa kupokonya vitega uchumi vya halmashauri na kukabidhiwa kwa Chama cha cha Mapinduzi kwa kisingizio cha kuhakiki mali za chama hicho. Upokonyaji wa aina hii umetokea katika Halmashauri ya Mji wa Babati ambapo stendi ya mabasi ya mji wa Babati ilikabidhiwa kwa CCM tarehe 13 Januari, 2018 kwaagizo la Mkuu wa Mkoa wa Manyara akidai kwamba stendi hiyo ni mali ya CCM na hivyo Rais ametoa amri kwamba stendi hiyo ikabidhiwa kwa CCM.
Mheshimiwa Spika, Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ameshalalamikiwa kufanya kazi ya uenezi ya CCM huku akiwa ni kiongozi wa umma anayatakiwa kuhudumia wananchi wote kwa usawa na bila kuwabagua kwa itikadi za vyama vyao; aliwaagiza wajumbe wa Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Mji wa Babati , Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Babati na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa wa Manyara kuikabidhi stendi hiyo kwa CCM siku hiyo hiyo.
Mheshimiwa Spika, wajumbe wa Kamati ya fedha walipohoji uhalali wa amri hiyo kwa kutaka kuona barua au waraka wowote kutoka kwa Rais unaoagizi stendi hiyo kukabidhiwa kwa CCM hawakupewa kielelezo chochote; lakini mbaya zaidi baraza la madiwani pamoja na kamati ya fedha wamekataza kabisa na Mkuu huyo wa Mkoa kujadili suala hilo kwa kuwa amri ya rais haijadiliwi bali inahitaji utekelezaji tu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na agizo hilo la Mkuu wa Mkoa; Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati alitekeleza agizo hilo kuikabidhi stendi hiyo kwa CCM kwa barua na kwa kuvunja mkataba wa wakala aliyekuwa anakusanya ushuru wa stendi bila kulishirikisha baraza la madiwani wala wakala aliyekuwa akikusanya ushuru wa Halmasharuri. Baada ya CCM kukabidhiwa stendi, kilichotokea ni kwamba greenguards wa CCM walimfukuza wakala aliyekuwa akikusanya ushuru wa halmashauri huku wakala huyo akiwa hana taarifa yoyote wala barua inayomjulisha kuhusu mabadilko hayo.
Mheshimiwa Spika; Sambamba na hilo wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo waliokuwa waliojenga vibanda vya biashara katika stendi hiyo na ambao walikuwa na mkataba na Halmashauri hadi 2031 wamenyang’anywa vibanda vyao na kukabidhiwa CCM na CCM wamewakabidhiw watu wapya kumiliki vibanda hivyo jambo ambalo limezua mgogoro mkubwa katika stendi hiyo baina ya wafanyabiashara na CCM na Halmashauri jambo ambalo linahatarisha amani na usalama kwa wafanyabiashara hao na mali zao.
Mheshimiwa Spika, mgogoro huo umesababisha wafanyabiashara hao; wakala wa ushuru wa stendi pamoja na wananchi wa Mji wa Babati kupeleka notisi ya siku 30 ya kuishtaki Halmashauri kwa kushindwa kusimamia mktaba baina yao.
Mheshimiwa Spika, kwa kifupi Mji wa Babati unafukuta moshi wa machafuko kutokana na siasa za kibaguzi za itikadi za vyama na mbinu chafu za kutaka kudhoofisha Halmashauri zinazoongozwa na Upinzani. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli katika Bunge hili inachukua hatua gani ya kusuluhisha mgogoro huo wa Babati na halmashauri nyingine zenye migogoro ya namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa namna hii pia uko katika Halmashuri ya Wilaya Mbulu kata ya Hydom kijiji cha Basonyagwe ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Selestino Mofuga amewaweka ndani viongozi wa Serikali ya kijiji kwa kukataa amri ya Mkuu wa Wilaya ya kukabidhi kwa CCM shamba la kijiji hicho lenye ukwa wa zaidi ekari 20.
Mheshimiwa Spika, wajumbe wa halmashauri ya kijiji walipohoji uhalali wa amri hiyo ya DC wakati yeye sio mamlaka ya kugawa amri DC huyo amekuwa akiagiza polisi kuwakamata na kuwaweka mahabusu kila siku toka Novemba mwaka 2017 bila kuwafikisha mahakamani. Huu ni unyanyasaji wa hali ya juu na ni njia haramu ya kuipatia CCM rasilimali bila ridhaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utendaji kazi usiofaa wa baadhi ya wakuu wa Wilaya na Mikoa; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kufanya upya uchunguzi juu ya mienendo (verting)ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa ili kuokoa rasilimali za nchi zinazotumika vibaya kutokana na matumizi mabaya ya madaraka ya wakuu hao na pia kurejesha imani ya wananchi kwa Seriali yao ambayo kwa sasa imeporomoka sana.
UTA RATIBU WA KUTEUA WAKURUGENZI NA WAKUU WA IDARA WA HALIMASHAURI
Mheshimiwa Spika pamoja na nguvu ya kikatiba aliyonayo Rais au waziri mwenye dhamana ya kuteua Wakurugenzi na wakuu wa idara wa Halmashauri ni muhimu kuwepo na utaratibu sahihi wa kikanuni unaoongoza uteuzi huo ikiwemo usaili wa wateule haokwa vigezo vya uwezo wao kitaaluma na kiweledi.
Mheshimiwa Sipika Kambi Rasimi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Serikali za mitaa ni muhimili muhimu sana katika kuchochea maendeleo ya nchi hivyo inapaswa kusimamiwa na watendaji wenye weledi mkubwa ili kuleta ustawi wa wananchi.
MFUKO WA WATU WENYE ULEMAVU NA WATU WENYE MAHITAJI MAALUMU
Mheshimiwa Spika, lazima kuwe na sheria inayozielekeza halimashauri kutenga kiasi kinachotajwa cha aslimia 2 ili kwa makundi ya watu wenye ulemavu na asilimia 2 kwa watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wagonjwa wa ukimwi ambao wana hali duni ya maisha.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa makundi haya katika jamii mifuko hii ni ya lazima na inatakiwa kutungiwa sheria na bunge lako tukufu ili utekelezaji wake usitegemee utashi wa kiongozi anayekuwa madarakani. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini makundi haya yakiwezeshwa yanauwezo mkubwa wa kuchangia uchumi wa Taifa.
POSHO ZA WENYEVTI WA MITAA
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya 2017/18 Kambi Rasmi ya Upinzani ilishauri Serikali kuzielekeza halimashauri zipandishe viwango vya posho za wenyeviti wa mitaa,vijiji na vitongoji kufika shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa mwezi pamoja na kuanzisha posho ya mkono wa kwaheri wa shiling laki tano pale wanapomaliza muda wao. Hii inatokana na ukweli kwamba kundi hii la uwakilishi linafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi katika ngazi za chini kabisa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani ilishauri kuanzishwa kwa posho ya shilingi elfu 30 kwa wajumbe wa vijiji,vitongoji na mitaa ili kuwapa ari ya kutetekeza majukumu yao ambayo ni magumu sana ya kuwahudumia wananchi wa kada ya chini kabisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kusisitiza umuhimu na ulazima wa kupandisha posho hizo pamoja na kuanzishwa kwa posho hizo zingine. Aidha, Wizara yenye dhamana izielekeze halimashauri zilipe hizo posho kwa wakati ili uwepo wake uwe na maana kwa viongozi wetu hao.
UHUSIANO WA TAMISEMI NA SEKTA ZINGINE ZA UZALISHAJI
Mheshimiwa Spika, unaposema TAMISEMI maana yake ni taasisi ambayo inahusika moja kwa moja kuinua hali ya maisha kwa watanzania wote hususani waishio vijijini ambao ni zaidi ya asilimia 85. Aidha, asilimia 75 ya idadi hiyo ni nguvukazi inajishughulisha na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kwamba; Sekta ya kilimo ambayo inahusisha, mazao, mifugo na uvuvi ilikuwa ilikua kwa asilimia 2.3 mwaka 2015, na asilimia 2.1 mwaka 2016. Ni dhahiri kuwa ukuaji huu wa asilima 2.1 hauwezi kuwa na matokeo chanya katika kuondoa umasikini kwa watanzania wanaotegemea sekta hii.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo za Ofisi ya Taifa ya Takwamu ni kujaribu kuonyesha tu umuhimu wa sekta hiyo kwa maisha ya watanzania na Tanzania kwa ujumla. Sasa kama sekta hiyo ingepata umuhimu wa kutosha kama vile, Sera ya kilimo ya mwaka 1997 kabla ya kuhuishwa mwaka 2013 kwamba huduma za ugani (EXTENSION SERVICE) kwa sekta ya kilimo ni jukumu la Halmashauri zetu (TAMISEMI), ni wazi kuwa kilimo kingeweza kukua kwa zaidi ya asilimia 4 na mchango wake katika mauzo nje ya nchi yangeongezeka maradufu na mchango wake katika pato la Taifa ungeongezeka na hivyo kuwa kwenye mwelekeo sahihi wa kuondoa umasikini wa kipato kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya uvuvi ambayo kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya uvuvi[20] inaonesha kuwa Tanzania ina wavuvi wapatao 183,800, na watu wapatao 4,000,000 wanategemea kuendesha maisha yao kutokana na sekta hii. Sambamba na hilo ni kuwa Tanzania inaukanda wa bahari upatao kilometa 1,424 kwa mikoa ya (Tanga,Pwani, Dar, Lindi na Tanga), kwa takwimu za mwaka 2015 ni kuwa samaki wanaovuliwa ni tani 51,912 sawa na 14% na maziwa yote kwa pamoja yenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,500(Kagera,Mwanza,Geita,Simiyu,Mara, Kigoma,Sumbawanga, Ruvuma, Mbeya na Njombe), samaki wanaovuliwa ni tani 314,062 sawa na 85%. Wahusika wakuu wa samaki hizi na wavuvi wadogo wadogo lakini hatuwaheshimu na kuwalea ili wawe ni wavuvi wakubwa, hii ni aibu kubwa sana kwa walio na dhamana kwa kuhakikisha nchi inakuwa ya uchumi wa kati
Mheshimiwa Spika, maeneo yote hayo, Halmashauri husika zinapata mapato yake ya ndani kwa kutegemea shughuli zinazofanywa kutokana na uvuvi, lakini wavuvi hasa wadodgo wanapata madhia makubwa sana ambayo yanawafanya badala ya kuondoa umasikini yanawaongezea umasikini na hivyo mapato ya halmashauri yanapotea kutokana na kukosa taasisi imara za kusimamia sekta hii.
Mheshimiwa Spika, operation iliyoendeshwa na bad inaendelea katika ziwa viktoria ya kukamata wavuvi ambao wanatumia nyavu ambazo kikosi kazi cha Operation hiyo kinahisi sio mwafaka imeleta kilio kikubwa sana kwa wavuvi na kuwaletea umasikini wa ghafla.
Mheshimiwa Spika, sheria inasema nyavu zitakazotumika kuvulia ziwani ni lazima ziwe na matundu yenye inchi 6 na kuendelea, lakini katika ziwa Viktoria kuna samaki wadogo chini ya inchi 6. Mfano; Furu, Gogogo(ngore) na Ningu. Hawa ni samaki maarufu sana katika ziwa Viktoria. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hawa wanavuliwa na Nyavu za inchi ngapi?
Mheshimiwa Spika, kutokuwepo au kupatikana kwa nyavu zinazokubalika kisheria kwa ajili ya uvuaji wa dagaa imekuwa ni usumbufu mkubwa sana na hivyo kutoa mwanya kwa watendaji kudai rushwa na kuwabambikizia kesi wavuvi.Mfano dhahiri ni walioendesha Operation katika visiwa vya Irugwa-Ukerewe kudai fedha nyingi kuliko thamani halisi ya mali walizonazo wavuvi na wakishindwa wanakamatwa na kufunguliwa kesi za uvuvi haramu.
Mheshimiwa Spika,ukweli ni kuwa zaidi ya 60% ya wavuvi wa dagaa wameshindwa kuendelea na shughuli zao kwa sababu nyavu zilizopo hazina ubora wa kuweza kuhimili kazi za kila siku. Jambo hilo linazidi kupunguza mapato kwa halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wavuvi wa Ukanda wa Pwani, nao wanapata madhila makubwa sana kutokana na makatazo ambayo hayaangaliii hali halisi ya ukuaji wa sekta hii na hivyo kuongeza mapato kwa halmashauri zilizo katika ukanda wa Bahari. Wavuvi wengi wadogo wanatumia uvuvi wa Mtanda “ring net” na ni lazima uzame ukiwa na mtungi wa gesi ya Oxygen.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya watendaji wasiofahamu uvuvi unafanyikaje wanashindwa hata kukaa na wahusika ili wajifunze, matokeo yake ni kuwafanya wavuvi kuwa masikini kwa kuteketeza mitungi na kupora engine za boat na wavuvi kukamatwa. Kwa upande wa Nyavu wanasema nyavu zenye ukubwa wa mm 38 au Inchi 2 ndizo zinazotakiwa. Sasa dagaa watavuliwa na nyavu zenye matundu ya ukubwa huo?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za mapato kama yalivyotolewa na “kundi la Fungamano la vyama na vikundi vya sekta ya uvuvi”katika soko la samaki Magogoni/Ferry na maeneo mengine, ni kwamba Wastani wa mapato yanayochangiwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa Taifa kwa soko la samaki Magogoni/Feri kwa mwaka mmoja niTshs. 8,663,294,000/- hizi ni stahiki za Serikali peke yake bado mzunguko wa biashara kwa wananchi. Aidha, vyombo vikubwa vinavyotumika katika mwambao wa Dar na Pwani ni vikubwa 3000 na vidogo 650, lakini wamiliki wanashindwa kufanyakazi kutokana na mazingira magumu wanayowekewa na Watendaji na hivyo kupelekea Halmashauri zetu na Serikali kukosa stahiki za mapato kwa maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuiangalia vizuri sekta hii ya uvuvi hasa wavuvi wadogo, wasinyanyaswe ili waweze kuzalisha zaidi na mapato kwa Serikali hususani halimashauri yaweze kuongezeka.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO 2017/18 NA MAOMBI YA UTEKELEZAJI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/19
Mheshumiwa Spika, kwa mujibu wa Randama, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imegawanyika katika maeneo yafutayo; OR-Tamisemi na Taasisi zake (Chuo cha Serikali za Mitaa(LGTI)-Hombolo, Shirika la Elimu Kibaha-(KEC), DART, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa(LGLB). 2. OR-Tamisemi Makao Makuu, 3. Tume ya Utumishi wa Waalimu, 4. Fungu 26 kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia fungu la OR-TAMISEMI na Idara zake kwa mwaka wa fedha 2017/18 ilikuwa imepangiwa jumla ya shilingi 449,278,985,671/= na kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 417,256,688,000. Kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 inaomba kiasi cha shilingi 387,455,020,714/=, kati ya hizo shilingi 344,586,778,001/= ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Aidha, fedha za ndani ni shilingi 283,642,430,000 na fedha za nje shilingi 60,944,348,001 ambazo zimepungua kutoka shilingi 108,691,778,000/= sawa na punguzo la 43.9% ya zile mwaka 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu za punguzo hilo la asilimia 43.9 la bajeti.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Fungu 26 la Mikoa na Mamlaka za Serikali za mitaa inaonesha kuwa, fedha za maendeleo zilizotolewa kwa mwaka wa fedha 2017/18, toka Serikali kuu zilikuwa shilingi 529,646,004,000 na zile za “own source” zilikuwa shilingi 412,383,996,000/= hizi zikilinganishwa na kwa mwaka 2018/19 zinazoombwa, toka Serikali Kuu shilingi 56,677,370,500. Hapa kunaongezeko la shilingi 37,127,266,500/= Kwa upande wa fedha za vyanzo vya ndani “own source” mwaka 2017/18 zilikuwa shilingi 412,383,996,000/- zimepungua kwa makadirio ya mwaka 2018/19 kuwa shilingi 345,726,629,000/= ikiwa ni punguzo la shilingi 66,657,367,000/= sawa na 16%.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinatuonesha kuwa Serikali badala ya kuiimarisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili ziweze kujitegemea katika kuhakikisha kuwa zina uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo bila ya utegemezi wowote kulingana na vyanzo vyake vya mapato; Serikali Kuu inazidhoofisha kwa kutenga bajeti ndogo
HOJA ZA ELIMU
Mheshimiwa Spika, licha ya sarakasi za kisiasa zinazofanywa na Serikali hii ya CCM za kushusha viwango vya ufaulu ili ionekane kwamba wanafunzi wengi wamefaulu; kubadili mfumo wa upangaji madaraja kutoka divisheni kwenda GPA na baadaye kutoka GPA kwenda divisheni; kuwatisha kuwafukuza kazi wakuu wa shule ambao shule zao hazitakuwa na ufaulu mzuri nk; tafiti zimebaini kwamba bado ubora wa elimu uko chini.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wa UWEZO wa mwaka 2017; uwezo wa kusoma na kuhesabu miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi bado uko chini ya kiwango kinachohitajika na mtaala. Hali hii imesababishwa na uwezo mdogo wa walimu kufundisha. Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2014, walimu wengi wanakosa ujuzi na mbinu za kielimu za kufundisha. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ni moja ya tano (1/5) tu ya walimu wanaoweza kumudu mtaala wanaofundisha.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kukosa ujuzi na mbinu za kufundisha, bado walimu wengi hawavutiwi na kazi ya kufundisha jambo ambalo linawafanya kutofundisha kwa bidii na hivyo kupelekea kushuka kwa ubora wa elimu. Utafiti ulifanywa na Haki Elimu 2016 ulibaini kwamba ni asilimia 37.8 tu ya walimu ndio waliokuwa wanaipenda kazi yao ya ualimu. Hii ina maana kwamba, zaidi ya asilimia 60 ya walimu hawaipendi kazi hiyo; na kwa maana hiyo hawaifanyi kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, changamoto zote hizi zimepelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya kuhitimu. Uchambuzi wa matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili na cha nne mwaka 2017; unaonesha kuwa wastani wa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo walipata daraja la nne na sifuri.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira hayo; Serikali inatakiwa kujikita kwenye kushughulikia tatizo hilo badala ya kufanya siasa za kubadili michakato ili hali ya elimu ionekane kuwa nzuri wakati kiuhalisia hali ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita imekuwa ikiikumbusha Serikali hii ya CCM kwamba; hakuna elimu bila walimu. Sarakasi na mbwembwe zote za kisiasa za elimu bure; elimu bila malipo na sasa elimu bila ada hazitasaidia chochote kama hakuna idadi ya kutosha ya walimu wenye weledi na motisha wa kufanya kazi ya kufundisha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016 na 2017; idadi ya walimu kwa shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 179,291 mwaka 2017 ikiwa ni anguko la asilimia 6.5 na kufanya uwiano wa mwalimu na wanafunzi kuwa 1:50. Aidha, katika shule za awali, idadi iliyopungua ni walimu 1948 na kufanya uwiano wa mwalimu na wanafunzi kuongezeka kutoka 1:135 mwaka 2016 hadi kufikia 1:159 mwaka 2017 badala ya 1:25 ambao ni uwiano unaokubalika.
Mheshimiwa Spika, katika shule za Sekondari kuna uhaba mkubwa wa walimu kwa baadhi ya masomo kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za Elimu Msingi za Mikoa (BEST Regional Data, 2017); walimu 7, 743 wanatarajiwa kustaafu kati ya mwaka 2018 na 2019. Aidha, takriban walimu zaidi ya 30,000 wana umri wa zaidi ya miaka 51ya kuzaliwa; hivyo na wao wanatarajiwa kustaafu muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Spika; kwa kuzingatia ukweli kwamba bila walimu hakuna elimu; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu katika maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika; mazingira bora ya kufundisha na kujifunza yanategemea sana uwepo wa miundombinu rafiki na wezeshi. Ni jambo ambalo haliwezekani kutegemea kupanda kwa ubora wa elimu ikiwa hakuna jitihada zozote za kuboresha miundombinu itakayosaidia zoezi la kufundisha na kujifunza kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika, kuna uhaba mkubwa sana wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari za umma, jambo linalopelekea mazingira magumu ya kufundisha na kujifunza na hivyo kushusha viwango vya ubora wa Elimu. Kwa mujibu wa takwimu za BEST, 2016 na 2017; ni kwamba uhaba wa maktaba katika shule za msingi umeongezeka kutoka asiliia 88 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 91.1 mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinaonyesha pia kwamba; upungufu wa maabara katika shule za sekondari unatofautiana kulingana na masomo husika. Kwa mfano upungufu wa maabara za somo la Bailojia ni asilimia 51.5, Fizikia ni asilimia 54.3 na Kemia ni asilimia 43.3
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha pia kwamba kuna upungufu wa nyumba za walimu 186,008 sawa na asilimia 83.1 na upungufu wa majengo ya utawala 10,943 sawa na asilimia 83.4. Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2016 inaonyesha kwamba; ni asilimia 41 tu ya shule za msingi na sekondari nchini Tanzania zenye miundombinu inayokidhi viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inafahamu upungufu huu kwa kuwa takwimu zilizotumika ni za Serikali. Swali ni je; kwanini upungufu huu umekuwa ukiongezeka? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge; imepunguza tatizo la uhaba wa miundombinu mashuleni kwa kiwango gani hadi sasa? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza imetenga bajeti kiasi gani katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mashuleni ili kukabiliana na uhaba ulipo sasa?
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/18, Bunge liliidhinisha matumizi ya shilingi bilioni 4,706.4 kwa ajili sekta ya elimu, bajeti ambayo ilikuwa imepungua kwa asilimia 1.3 ikilinganishwa na bajeti ya 2016/17 ambayo ilikuwa bilioni 4,770.4. Kwa mantiki hiyo, bajeti ilipungua kwa kiasi cha shilingi bilioni 64.
Mheshimiwa Spika, Upungufu huu wa asilimia 1.3 (shilingi bilioni 64) umepunguza mgao wa bajeti ya sekta ya elimu kutoka katika bajeti ya kuu ya serikali kutoka asilimia 16 iliyoidhishwa mwaka 2016/17 hadi asilimia 14.9% iliyoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya mwaka wa fedha 2017/18.
Mheshimiwa Spika, upangaji huu wa bajeti ya sekta ya elimu chini ya asilimia 20 ya bajeti kuu unakwenda kinume na makubaliano ya kikanda na kimataifa ambayo nchi imeridhia ikiwemo Dakar Framework for Action on Education for All, 2000 na Incheon Declaration and Framework for Action, 2015; ambapo ilikubaliwa kwamba nchi wanachama watenge angalau asilimia 20 ya bajeti zao za taifa kwa ajili ya elimu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa imeonekana dhahiri kwamba nchi yetu badala ya kutenga bajeti inayokaribia asilimia 20; sasa kumekuwa na mwendendo wa kushusha bajeti hiyo mwaka hadi mwaka; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali si tu kuheshimu makubaliano ya kimataifa ya kutenga asilimia 20 ya bajeti yake kwenda kwenye elimu; bali ijali mustakabali wa nchi yetu na malengo makubwa ya maendeleo ya nchi kwa kuwekeza vya kutosha katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na uwiano kinzani (inversely proportion) kati ya bajeti ya matumizi ya kawaida na bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu. Wakati bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikiongezeka katika sekta hii, bajeti ya maendeleo imekuwa ikipungua.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa uchambuzi wa bajeti ya Elimu uliofanywa na Haki Elimu, 2018; ni kwamba; Katika mwaka wa fedha 2017/18 kwa mfano, kati ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya sekta ya elimu (shilingi bilioni 4,706.4), kiasi cha shilingi bilioni 3,582 (76%) ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 1,134 (24%) ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo. Uchambuzi unaonyesha kwamba; katika miaka miwili ya nyuma mathalani, 2016/17 na 2017/18 bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kutoka shilingi bilioni 3,069.5 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 3,572 mwaka 2017/18 sawa na ongezeko la asilimia 16.4; wakati fedha za maendeleo zimeshuka kutoka shilingi bilioni 1,700.5 mwaka 2016/17 hadi kufikia shilingi bilioni 1,134 mwaka 2017/18 sawa na anguko la asilimia 33.3
Mheshimiwa Spika, bajeti hafifu ya maendeleo ya sekta ya elimu ina athari kubwa kwenye Elimu Msingi, na imeathiri kwa sehemu kubwa mgawo wa fedha unaokwenda TAMISEMI kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya elimu msingi. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18, TAMISEMI ilitenga kiasi cha asilimia 7 (shilingi bilioni 198) na asilimia 6.6 (shilingi bilioni 216) tu kwaajili ya shughuli za miradi ya maendeleo kwa elimu msingi. (Uchambuzi wa sekta wa Wizara ya Fedha, 2017/18).
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu, utekelezaji wa bajeti ya maendeleo umekuwa hafifu. Wakati Waziri wa Fedha, alipokuwa akihutubia bunge mwezi Aprili 2017 alikiri kuwa serikali imetekeleza bajeti ya maendeleo kwa asilimia 34 tu hadi kufikia mwezi Aprili, 2017. Aidha, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Aprili 2018 imeonesha kuwa, serikali imetekeleza bajeti ya maendeleo kwa asilimia 51% tu katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, mwenendo huu wa utekelezaji umeathiri bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu pia. Katika mwaka wa fedha 2016/17 shilingi bilioni 897.6 ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo shilingi bilioni 427 ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya Bodi ya Mikopo na shilingi bilioni 470 kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo ya wizara. Hata hivyo, ni asilimia 31tu ya shilingi bilioni 470 tu ndiyo iliyopelekwa wizarani hadi kufikia Aprili, 2017. Kutokana na ufinyu wa bajeti hiyo ya maendeleo; iko miradi ya maendeleo ambayo iliathirika. Miradi hiyo ni pamoja na:-Programu ya kuimarisha mafunzo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ambapo bajeti iliyoidhinishwa ilitekelezwa kwa asilimia 27 tu hadi kufikia Aprili 2017 ; Programu ya Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni ambayo ilitekelezwa kwa asilimia 29 tu na mraddi wa Uthibiti Ubora wa Shule ambao ulitekelezwa kwa asilimia 16 tu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/18 ambapo bajeti ya wizara ya elimu iliyoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilikuwa shilingi bilioni 916.8, hadi kufikia Machi 2018, kiasi cha shilingi bilioni 595.6 (65%) tu ndicho kilichokuwa kimetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo katika kiasi hicho, shilingi bilioni 286.9 (48.2%) zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya Bodi ya Mikopo.
Mheshimiwa Spika, ubora wa elimu unategemea sana utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ambayo imejikita zaidi katika kuboresha sekta hiyo. Ikiwa miradi hiyo haitakelezwi ipasavyo, tusitegemee muujiza mwingine wa kupandisha viwango vya ubora wa elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, licha ya kutenga bajeti ndogo ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu; kumeibuka pia tabia ya ajabu ya kutopeleka hata senti moja kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa; na ambayo imetengewa bajeti katika sekta hii ya elimu. Kwa mfano, kati ya miradi 38 ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/18; miradi 22 haikupatiwa hata senti moja ya fedha. Kwa maneno mengine miradi hiyo ilipata asilimia sifuri (0%) ya fedha[21]
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa miradi ambayo haikupata fedha kabisa za utekelezaji licha ya kutengewa bajeti ni pamoja na mradi namba 6324 (Ukarabati wa Maktaba za Mikoa) ambao ulitengewa shilingi milioni 500; mradi namba 4305 (Kutegemeza Elimu ya Msingi) ambao ulitengewa shilingi bilioni 1.762; mradi namba 4320 (Kuimarisha Taasisi ya Elimu Tanzania) ambao ulikuwa umetengewa shilingi bilioni 40; mradi namba 6235 (Kuimarisha Uthibiti wa Ubora wa Shule) ambao ulitengewa shilingi bilioni 1; mradi namba 2228 (Kuboresha Utafiti na Maendeleo katika Elimu Sayansi na Teknolojia) ambao ulitengewa shilingi bilioni 16.338.
Mheshimiwa Spika, miradi mingine ambayo haikupatiwa fedha kabisa ni ile ya upanuzi na ukarabati wa Chuo Kikuu cha Dodoma uliokuwa umetengewa shilingi bilioni 1.7; Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa ( shilingi bilioni 1); Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu J.K.Nyerere (shilingi bilioni 3); Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (shilingi bilioni 1); Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (shilingi bilioni 5.5); Chuo Kikuu Mzumbe (shilingi bilioni 1) Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (shilingi bilioni 1); Chuo Kikuu cha Biashara Moshi (shilingi bilioni 1.3); Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (shilingi bilioni 3) na mradi wa Kujenga Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki (shilingi bilioni 1.5).
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kutotekelezwa kwa miradi hiyo; hakupandishi viwango vya ubora wa elimu hapa nchini; bali kunazidi kushusha viwango vya ubora na hatimaye kudumaza sekta nzima ya elimu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa nini bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu inapungua? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza ni kwa nini haikutekeleza bajeti ya maendeleo katika miradi iliyotajwa licha ya bajeti kwa ajili ya miradi hiyo kutengwa na kupitishwa na Bunge?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haina mgogoro na Serikali juu ya matumizi ya fedha za nje katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Ila jambo la msingi ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa angalizo ni katika kupanga miradi ipi itekelezwe na fedha za nje na miradi ipi itekelezwe na fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, ipo miradi ambayo kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa taifa, inapaswa kutekelezwa na fedha za ndani. Kwa mfano miradi ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu na huduma nyingine za jamii inapaswa kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani. Miradi ya maendeleo katika sekta nyingine ambazo hazina athari za moja kwa moja na za haraka kwa maisha na ustawi wa jamii kama vile miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inaweza kutekelezwa na fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeshtushwa sana kuona miradi mingi ya maendeleo katika sekta ya elimu – sekta ambayo ndio moyo wa maendeleo ya sekta nyingine zote; ikitengewa asilimia sifuri ya fedha za ndani na kubaki tegemezi kwa fedha za nje pekee kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, miradi zadi ya 10 ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2018/19; haijatengewa hata senti moja ya fedha za ndani kwa ajili ya utekelezaji[22]. Miradi hiyo ni pamoja na mradi namba 4312(Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo kwa ajili ya motisha – Education Programme for Results) uliotengewa shilingi bilioni 26.8; mradi namba 3280 (Huduma ya Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Shule) uliotengewa shilingi bilioni 17.033; mradi namba 4305 (Kutegemeza Elimu ya Msingi ulitotengewa shilingi bilioni 1.762); mradi namba 4312 (Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo – ujenzi wa miundombinu ya shule na ununuzi wa vifaa; uliotengewa shilingi bilioni 89.7;
Mheshimiwa Spika, miradi mingine muhimu ambayo haikutengewa fedha za ndani ni mradi wa Kuimarisha Mafunzo ya KKK ambao umetengewa shilingi bilioni 4; mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (shilingi bilioni 25); mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (shilingi bilioni 20.241); mradi wa kuboresha Utafiti na Maendeleo katika Elimu na Mafunzo (shilingi bilioni 5.240) na mradi wa Kukuza Stadi za Kazi kwa ajili ya Shughuli za Kuzalisha na Kukuza Uchumi (shilingi bilioni 29.062).
Mheshimiwa Spika, miradi iliyotajwa hapo juu imepangwa kutekelezwa kwa kutumia fedha za nje tu. Tafsiri ya Mpango huo wa bajeti ni kwamba miradi hiyo siyo ya kipaumbele kwa kuwa fedha za nje sio za kutegemea kwa asilimia mia moja. Hii ni kwa sababu uzoefu unaonyesha kwamba, fedha za nje huchelewa sana kutolewa na wakati mwingine hazitolewi kabisa.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kupanga bajeti ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu kwa kutumia fedha za nje; ni kuiweka elimu yetu rehani na kwa maneno mengine ni kuiangamiza taifa kwa kuwa mafanikio ya sekta nyingine zote yanategemea sana ukuaji na ubora wa sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeshangazwa sana kwamba hata fedha za mradi wa mafunzo ya KKK (Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu) tunategema wafadhili watusaidie?!!! Ndio maana hatushangai kuona ripoti za utafiti kama za TWAWEZA na Benki ya Dunia zikionyesha kwamba; uwezo wa kusoma na kuhesabu miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi bado uko chini ya kiwango kinachohitajika na mtaala.
Mheshimiwa Spika, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema “Kupanga ni Kuchagua” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki yoyote ya Serikali hii ya CCM kuchagua miradi muhimu kama vile Mafunzo ya KKK – ambayo ndio moyo wa Elimu Msingi itekelezwe kwa fedha za nje. Aidha, hakuna mantiki yoyote miradi ya utafiti katika elimu na kuendeleza elimu ya ualimu kutegemea fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, katika vitu ambavyo Serikali hii haitakiwi kuvifanyia majaribio ni sekta ya elimu. Madhara yanayopatikana kwa kufanya makosa katika sekta ya elimu ni ya muda mrefu na pia madhara hayo hayaishii kwenye elimu tu bali huathiri pia sekta nyingine. Mtabibu aliyepewa mafunzo kengeufu katika elimu yake; athari zake zitakwenda kuathiri sekta ya afya pia nk.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuifahamisha Serikali kwamba; zipo sekta ambazo miradi yake ya maendeleo inaweza kutekelezwa kwa kutumia fedha za nje na hata kama fedha hizo zikichelewa au zisipotolewa madhara yake yanakuwa ni ya muda mfupi na yanaweza kutatuliwa; Ila katika sekta ya elimu ni vema miradi yake ikapewa kipaumbele kwa kutengewa fedha za ndani ili hata kama nchi isipopata misaada ya kibajeti; elimu yetu isitetereke.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopelekea kupanda kwa gharama za maisha; kiasi cha ruzuku ya shilingi 10, 000/= kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na shilingi 25,000/= kwa mwanafunzi wa sekondari kilichopangwa tangu mwaka 2001 hakiwezi tena kukidhi mahitaji kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, wakati kiwango hicho kinapangwa; thamani ya dola moja ya kimarekani ilikuwa ni shilingi 1,000/= na lengo lilikuwa ni angalau kutoa dola kumi kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na dola 20 kwa mwanafunzi wa sekondari. Thamani ya dola moja kwa sasa imepanda; ambapo kwa sasa tunahitaji makadirio ya shilingi 2,200 kununua hiyo hiyo dola moja.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wa utoaji wa ruzuku kwa mwanafunzi kwa kutumia kanuni mpya, hivyo tunashauri kuwa utekelezaji huo uwe na lengo la kuongeza kiwango cha ruzuku kwa mwanafunzi ili kulinda nguvu ya manunuzi ya ruzuku hii. Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwa Serikali kutenga angalau shilingi 20,000/= kama ruzuku kwa kila mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi na shilingi 50,000/= kwa kila mwanafunzi wa sekondari wakati wa utekelezaji wa zoezi la utoaji wa ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kutumia kanuni mpya.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya juu; Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kusisitiza kwamba mikopo hii haina tofauti na ruzuku kama hiyo wanayopewa wanafunzi wa elimu msingi. Hivyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki ya fedha hizo kurejeshwa tena Serikalini. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki ya fedha za mikopo ya Elimu ya Juu kuwekwa kwenye bajeti ya maendeleo kwa kuwa matumizi yake ni ya kawaida. Waheshimiwa wabunge watakuwa mashahidi kwamba fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zinatumika na wanafunzi hao kununua chakula na kulipia gharama za malazi – matumizi ambayo ni ya kawaida (recurrent expenditure).
Mheshimiwa Spika, kitendo cha fedha ya mikopo kuwekwa kwenye bajeti ya maendeleo kunaifanya bajeti ya maendeleo kuonekana kubwa wakati fedha inayokwenda kutekeleza miradi halisi ya maendeleo katika sekta hii ni kidogo sana. Hivyo, kuna hatari ya kufikiri kwamba sekta ya elimu inaimarika kwa kuona kiasi kikubwa cha fedha kimetengwa; kumbe fedha hiyo inakwenda kutumika katika matumizi ya kawaida. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri na kupendekeza kwa Serikali kuondoa fedha ya mikopo ya elimu ya juu kwenye bajeti ya maendeleo na kuiweka kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida. Aidha, fedha hiyo itolewe kama ruzuku na wanafunzi wa elimu ya juu wasitakiwe kurudisha fedha hiyo Serikalini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikipigia kelele suala la kupanga bajeti kwa kuzingatia masuala ya jinsia (gender budgeting) na mara kadhaa tumeitaka Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi wa kike wenye umri wa hedhi taulo za kujihifadhi wakati wa hedhi ili kuhakikisha kwamba hedhi haiwi kikwazo kwa wanafunzi hao kupata elimu sawa na wenzao wa kiume.
Mheshimiwa Spika, jitihada hizo za Kambi ya Upinzani zilipelekea Mheshimiwa Upendo Peneza kuandaa hoja binafsi ya kuitaka Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kununua taulo hizo; lakini kama kawaida ya Serikali hii ya CCM ya kupuuza na kufifisha jitihada za kuwasaidia wananchi – hoja hiyo hata haikupata nafasi ya kuingia bungeni licha hoja hiyo kuwa nzito na nzuri kwa mustakabali wa watoto wetu wa kike kupata elimu bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa serikali kutenga fedha za kutosha kukidhi programu zinazochagiza kuboresha mazingira ya elimu kwa mtoto wa kike ikiwemo:-.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya mradi huu unatia hofu ikizingatiwa kuwa hata katika utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka uliopita (2016/2017) ni shilingi milioni 180 tu ndizo zilizopelekwa kwa ajili ya utekelezaji wake wakati fedha zilizoidhinshwa kwa ajili ya mradi zilikuwa shilingi milioni 600.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wasichana ndio waathirika wakuu wa mazingira na miundombinu duni ya kujifunzia katika shule za serikali, ni muhimu masuala yanayoboresha ustawi wao kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.
Mheshimiwa Spika; mwaka 2014, Serikali ilitoa Waraka wa Watumishi wa Serikali Namba 3 wa mwaka 2014 kuhusu mishahara na posho ya madaraka kwa viongozi wa Elimu Nchini. Waraka huo ulikuwa ni juu ya uamuzi wa Serikali wa kuwaingiza Wakaguzi Wakuu wa Shule wa Wilaya na Kanda katika muundo wa mshahara wa viongozi wa Serikali (LSS – E); na kulipa posho ya madaraka kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari, Wakaguzi wa ELimu Kata na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi kuwapa motisha wakaguzi wa elimu; isipokuwa ina mgogoro na mfumo wa kibaguzi wa utoaji wa motisha huo. Ukisoma waraka huo, utaona kwamba Serikali imeamua kutoa posho ya madaraka kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari, Wakaguzi wa ELimu Kata na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini na kuwaweka pembeni Wakaguzi Wakuu wa Shule wa Wilaya na Kanda.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia uzoefu mdogo tu, kati ya mratibu wa elimu wa Kata; na Mkaguzi wa Shule wa Wilaya na Kanda; ni nani mwenye majukumu makubwa ambaye angestahili kulipwa posho hiyo ya madaraka? Tukumbuke kwamba hawa wakaguzi wa shule wa Wilaya na Kanda ndio wathibiti wakuu wa ubora wa elimu katika Wilaya zote na Kanda zote Tanzania Bara. Ikiwa hawa wametengwa katika kupewa motisha; kuna hatari kubwa ya kuporomoka kwa ubora wa elimu kwa nchi nzima kwa mara moja.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni lini itawaingiza wakaguzi wakuu wa shule wa wilaya na kanda katika utaratibu wa kulipwa poho ya madaraka kama wanavyolipwa wakuu wa shule za msingi na sekondari; wakaguzi wa elimu Kata na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu? Ikiwa Serikali itaridhia kuwalipa posho hiyo; Je, itakuwa tayari kuwalipa malimbikizo ya posho hiyo tangu Julai, 2016 ilipoanza kuwalipa wakuu wa shule za msingi na sekondari, wakaguzi wa elimu Kata na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu?
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka jana nilieleza kuwa vitabu ni nyenzo muhimu sana katika utoaji wa elimu bora, hasa katika kipindi hiki chenye uhaba mkubwa wa walimu. Vitabu visipotungwa kwa ubora ni sumu mbaya sana kwa elimu hasa elimu ya shule ya msingi (awali hadi darasa la saba).
Mheshimiwa Spika, nilieleza kwamba; Taasisi ya ELimu Tanzania ilipewa mamlaka ya uchapishaji wa vitabu vya kiada nchini na imechapisha vitabu vipya kwa shule za msingi; isipokuwa vitabu hivyo vilikuwa na mapungufu makubwa ambayo yangesababisha madhara makubwa katika utoaji wa elimu, na hivyo kushusha ubora wa elimu yetu. Miongoni mwa mapungufu au matatizo ya vitabu hivyo yalikuwa ni pamoja na kutokuchapishwa Kiongozi cha Mwalimu;Kuchapisha mambo yasiyostahili kuingizwa kwenye kiongozi cha mwalimu. Aidha, kulikuwa na makosa ya Usanifu wa Vitabu hivyo kama vile picha zisizo na ubora pamoja na makosa ya lugha.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikiri kuwa vitabu hivyo vilikuwa na mapungufu; na kuchukua hatua ya kuwawajibisha waliohusika na makosa hayo pamoja na kuagiza vitabu hivyo vichapwe upya. Hata hivyo; vitabu vipya vilivyotolewa na Taasisi ya Elimu ambavyo vimesahishwa bado vina makosa mengi sana.
Mheshimiwa Spika; kwanza kuna mapengo ya vitabu. Kuna vitabu ambavyo mwanafunzi anapaswa kuwa navyo kabla ya msimu wa shule kuanza – yaani Januari. Vitabu hivyo havipo mpaka sasa. Vitabu ambavyo havipo mpaka sasa ambapo muhula wa kwanza uaelekea ukingoni ni Hesabu Darasa la Kwanza; Hesabu Darasa la Pili; Hesabu Darasa la Tatu; na Kusoma Darasa la Kwanza – Kitabu cha Mwanafuzi.
Mheshimiwa Spika, vitabu vipya vilivyotolewa bado havina Kiongozi cha Mwalimu. Kanuni ya Wizara ya ELimu inaelekeza kwamba kitabu cha kiada lazima kiwe na Kiongozi cha Mwalimu, vinginevyo kinakosa sifa ya kuwa kitabu cha kiada. Kosa hili la kukosekana kwa Kiongozi cha Mwalimu ni kosa lilokuwepo tangu Serikali ilipoagiza vitabu vya Taasisi ya ELimu vichapwe upya kutokana na makosa mbalimbali. Sasa kosa hilo limerudiwa tena!
Mheshimiwa Spika, hitilafu nyingine katika vitabu vipya ni udhaifu wa usanifu wa vitabu vyenyewe. Kwanza kuna matumizi mabaya ya kurasa za vitabu husika. Kurasa nyingi zimeachwa wazi bila kuandikwa chochote – jambo ambalo linasababisha grama kubwa za uchapishaji bila sababu na pia uwazi huo unatoa nafasi kwa watoto kuchezea kurasa hizo kwa kuzichora chora na hivyo kupelekea kuchakaa kwa vitabu mapema kabla ya muda. Aidha, hakuna mtiririko mzuri wa kuongezeka kwa kurasa kadiri madarasa yanayoongezeka. Ni jambo la ajabu kuona kitabu cha darasa la chini kina kurasa nyingi kuliko cha darasa la juu zaidi. Kwa mfano kitabu cha “Kuandika Darasa la Kwanza” kina kurasa 118 wakati kitabu wa “Kuandika Darasa la Pili” kina kurasa 42.
Mheshimiwa Spika; ukiachilia mbali udhaifu katika usanifu, bado kuna tatizo la watunzi wa vitabu hivyo kutojua saikolojia na uwezo wa watoto katika ngazi mbalimbali za kujifunza. Kwa mfano, baadhi ya vitabu vina maelekezo mengi kwa mtoto ambaye ndio kwanza anaanza kujifunza kusoma. Ni jambo la ajabu kukuta kitabu kina maswali na maelekezo mengi kwa mtoto ambaye hajaweza kusoma irabu wala silabi.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Taasisi ya Elimu kutoa vitabu vyenye makosa; na kushindwa kurekebisha makosa hayo hata pale ilipoamriwa kuchapisha upya vitabu vilivyokuwa na makosa; kunaiondolea taasisi hiyo sifa za kuendelea kuwa na mamlaka ya kuchapisha vitabu vya elimu katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuunda timu ya uchunguzi itakayofanya ukaguzi wa utendaji wa Taasisi hiyo, ili kubaini tatizo liko wapi na hatimaye kushauri hatua za kuchukua dhini ya taasisi hiyo. Aidha; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni chombo gani kinachodhibiti ubora wa vitabu kwa sasa baada ya kuvunjwa kwa Kamati ya EMAC?
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeamua kuwahamisha walimu takriban 7,000 wa ziada ziada katika masomo ya sanaa kwenye shule za sekondari wapatao kwenda shule za msingi kupunguza upungufu na kuboresha elimu hiyo ya msingi.Aidha, tayari majaribio ya mpango huo wa kuwahamishia walimu hao uameanza katika Mkoa wa Arusha na yakifanikiwa, itahusisha mikoa yote nchini hasa kwenye mahitaji. Kwa mujibu wa Katib Mkuu – Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ni kwamba; katika sekondari walimu wa sanaa (Arts) ni wengi kwa idadi hiyo ya zaidi ya 7,000 na kwamba hao wanaohamishwa wanachochea ubora wa elimu katika shule za msingi na marupurupu yao na mishahara itabaki kama ilivyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi mpango huo wa Serikali; isipokuwa ingependa kuijulisha Serikali kwamba, ualimu ni mafunzo. Kila ngazi ya kufundisha ina mafunzo yake na ina mbinu tofauti za ufundishaji na ngazi nyingine. Kwa sababu hiyo, ili uhamisho huo wa walimu wa Sekondari kwenda msingi uwe na tija, lazima walimu hao wapatiwe mafunzo ya namna ya kufundisha elimu ya msingi isije wakatumia mbinu na uzoefu ule wa sekondari na kuwachanganya watoto na zoezi zima likawa halina tija.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili; ina mpango gani wa mafunzo kwa walimu hao na imetenga bajeti kiasi gani katika mwaka wa fedha 2018/19 ili kutekeleza mpango huo.
Mheshimiwa Spika, madhara ya kuporomoka kwa elimu msingi hayaishii kwenye elimu msingi pekee bali huenda hadi elimu ya juu na athari hizo huwa mbaya zaidi katika elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali nyaraka mbalimbali zinazoonyesha kuporomoka kwa elimu nchini; mtazamo na uzoefu wa wa Profesa Casmir Rubagumya aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Humanitia na Sayansi za Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma unaonyesha kwamba hali ya elimu ya juu hapa nchini ni mbaya kuliko maelezo.
Mheshimiwa Spika, Profesa Rubagumya anathibitisha kwamba kiwango cha ubora wa elimu ya wanafunzi wanaojiunga na chuo kikuu unapungua kila mwaka; na kila mwaka wanapokea wanafunzi dhaifu kuliko mwaka uliopita. Alishangazwa kwamba; wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu hawana uwezo wa kuzungumza Kiswahili au Kiingereza fasaha. Anaeleza kwamba tatizo halikuwa tu kwenye lugha, bali pia uwezo mdogo wa kufikiri vizuri katika lugha zote mbili.
Mheshimiwa Spika, Profesa alibaini pia kwamba wanafunzi wa elimu ya juu walikuwa pia hawana uelewa wa mambo ya kawaida kuhusu Tanzania. Alishangazwa na kitendo cha mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo kikuu kushindwa kufahamu jina la Makamu wa Rais wa Tanzania; jambo ambalo hata mwanafunzi wa darasa la pili angetazamiwa kufahamu.
Mheshimiwa Spika, Profesa Rubagumya anasema matatizo ya kielimu aliyoyagundua UDOM, aliyagundua pia kwa vyuo vingine vikuu alipokuwa kama mtahini wa nje (external examiner) katika vyuo hivyo. Kwa maneno yake mwenyewe, anasema wanafunzi wa vyuo vikuu sasa hivi wanaonekana kutengeneza kizazi tofauti kisichopenda kabisa kujishughulisha na elimu.
Mheshimiwa Spika, udhaifu huu katika elimu ya Juu umezungumzwa pia na mrais wa wastaafu wa awamu ya tatu na y a nne na kutoa rai ya kufaya mjadala wa kitaifa ili kunusuru hali hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ina mkakati gani wa kunusuru elimu ya juu ambayo imeporomoka kwa kiwango kikubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu?
Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa eneo la kujenga chuo kikuu au taasisi yoyote ya elimu lazima uzingatie mazingira tulivu yatakayosaidia shughuli za kufundisha na kujifunza kuendeshwa bila usumbufu au bugudha yoyote.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kuhamishia baadhi ya ofisi za wizara katika Chuo Kikuu cha Dododma si tuo kunaodoa utulivu wa mazingira ya kusoma; bali pia kinawaathiri wanafunzi kisaikolojia kwa kuingiza shughuli nyingine ndani ya chuo ambazo ni tofauti na masomo. Athari nyingine ni hatari ya watendaji wa Serikali kujihusisha katika masuala ya mapenzi na wanafunzi wa chuo kutokana na mwingiliano uliopo na hivyo kuwaondosha wanafunzi katika malengo yao ya masomo.
Mheshimiwa Spika, jambo hili lilishazungumzwa na wabunge katika mikutano ya bunge iliyopita; na Serikali ikatoa maelezo kwamba sula hilo lilikuwa ni la muda tu kwa kuwa Serikali ilihamia Dodoma bila kuandaa ofisi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili; imetenga bajeti kiasi gani katika mwaka wa fedha 2018/19 ya kujenga ofisi za Serikali katika ene jingine ili Chuo Kikuu cha Dodoma kibaki na shughuli moja tu ya kutoa elimu kwa vijana wetu na sio kuingiza shughuli nyingine za Serikali katika eneo la Chuo?
Mheshimiwa Spika, hotuba hii imeainisha maeneo mengi yenye kasoro na mapungufu katika sekta nzima ya elimu; – mapungufu ambayo kwa ujumla wake yanapelekea kupromoka kwa ubora wa elimu hapa nchini. Aidha, hotuba hii imeeleza umuhimu wa sekta ya elimu katika ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na hivyo kupendekeza kuwekeza zadi katika elimu ili kuweza kufikia malengo ya kitaifa katika sekta nyingine hususani eneo la uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, nimetoa pia angalizo la kutofanya majaribio katika sekta ya elimu, kwa kuwa madhara ya kufanya hiyo ni makubwa na endelevu kuliko yangefanywa katika sekta nyingine. Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaendelea kusisitiza kwamba;Serikali isifanye siasa katika suala la elimu. Aidha; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kupitia kwa makini maeneo yote yenye mapungufu yaliyoainishwa ndani ya hotuba hii ya kueleza mikakati ya kuondoa mapungufu hayo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Mheshimiwa Spika, uhuru wa maoni na haki ya kupata habari nchini Tanzania vilizikwa rasmi tangu Serikali hii ya awamu ya tano iapishwe kushika madaraka ya kuliongoza taifa hili. Itakumbukwa kwamba mara tu baada ya Serikali hii kushika madaraka ndio matangazo ya Bunge Live yalifutwa; sheria kandamizi za kudhibiti mawasiliano zikatungwa (sheria ya huduma za habari nk). Aidha, ni katika kipindi cha mwanzo kabisa cha utawala wa Serikali hii ambapo taifa limeshuhudia magazeti yanayoandika habari za kiuchunguzi yakifutiwa usajali na mengine kufungiwa kwa muda usiojulikana kama adhabu ya kuandika ukweli kuhusu makosa yanayofanywa na watendaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, vilevile ni wakati huu wa utawala wa serikali ya awamu ya tano ambapo sheria ya makosa ya mtandao na sheria ya takwimu ambazo zilipingwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, wadau na Jumuiya za kimataifa zimeanza kutumika kukandamiza uhuru wa kutoa maoni na kupata habari. Ikumbukwe kuwa matumizi ya sheria hizi yalisababisha nchi kama Marekani kuondoa misaada yake kupitia mradi wa millenium challenge.
Mheshimiwa Spika; kama ilivyo desturi ya madola ya kidikteta duniani kuuwa demokrasia na kudhibiti upinzani; Serikali hii ya CCM awamu ya tano; ilianza kwa kutekeleza kaulimbiu yake ya hapa kazi tu; kwa kupiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa ya vyama vya upinzani ambayo yanaruhusiwa na katiba na sheria za nchi. Wakati huo huo CCM imeruhusiwa kufanya siasa kwa mgogo wa kukagua miradi ya maendeleo na kutathmini utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM!!! Tangu lini miradi ya maendeleo inakaguliwa na chama cha siasa? Bunge litafanya kazi gani sasa?
Mheshimiwa Spika, kazi ya Serikali hii ya CCM ya kuuwa demokrasia hapa nchini imepiga hatua nyingine, na safari hii mkakati ni kuwafutilia mbali viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kwa kuwabambikia kesi za uchochezi na ugaidi ili wafungwe gerezani; kuwadhuru miili na hata kuwauwa. Matukio ya kupigwa risasi kwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Tundu Lissu; matukio ya kuuwawa kwa viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani (Kwa mfano:- Marehemu Alfonce Mawazo – aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA –Mkoa wa Geita; Marehemu Daniel John, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA – Kata ya Hananasifu katika Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam; marehemu Godfrey Lwena, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Namawala katika Jimbo la Mlimba – Wilaya ya Kilombero huko Morogoro; na marehemu Aramu Kaigwe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi –Kata ya Nyarugusu katika Jimbo la Kasulu Vijijini mkoani Kigoma. Hawa ni wachache tu ambao wameuwawa kati ya mwezi Feburuari na Machi mwaka huu wa 2018).
Mheshimiwa Spika, kitendo cha vyombo vya dola kuendelea kukaa kimya kuhusu mauaji hayo, na kitendo pia cha Serikali kukataa vyombo vya uchunguzi kutoka nje visisaidie kufanya uchunguzi wa matukio hayo, kunathibitisha kwamba matukio hayo yana baraka za Serikali.
Mheshimiwa Spika, kazi ya Serikali hii ya awamu ya tano kuuwa demokrasia na uhuru wa maoni sasa imevuka mipaka. Baada ya kudhibiti upinzani nje ya bunge kwa kupiga marufuku mikutano ya siasa ya vyama vya upinzani nguvu sasa imeelekezwa katika kudhoofisha upinzani Bungeni. Mkakati huu umefanyika kwa njia mbili. Moja ni kwadhibiti wabunge wa Upinzani kusema bungeni kwa kuwapa adhabu kali na kuwafungia kuhudhuria vikao vya bunge kwa kuikosoa Serikali ndani ya Bunge. Aidha, wabunge wa upinzani wamekuwa wakishatakiwa mahakamani kwa mambo waliyoyasema bungeni ambayo yana kinga kwa mujibu wa katiba. Pili ni kuidhoofisha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kuiondoa Sekretarieti ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo kazi yake kubwa ni kufanya tafiti na uchambuzi wa hoja mbalimbali za Serikali zinazoletwa Bungeni na kusaidia kuandaa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja hizo ikishirikiana na Wasemaji Wakuu wa Kambi ya Upinzani kwa kila Wizara.
Mheshimiwa Spika; pamoja na kwamba Serikali inalenga kudhoofisha upinzani, lakini kwa uoni mpana ni kwamba Serikali inalidhibiti Bunge; kwa kuwa Upinzani ni sehemu ya Bunge, na upinzani mahiri unaliimarisha Bunge zima kwa jumla. Kitendo cha Serikali kulidhibiti Bunge ni kiashiria kibaya sana kwamba sasa tuna Dola kamili la kidikteta. Hii ni kwa sababu chombo pekee kinachoweza kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa katiba yetu ni Bunge; kama Bunge limeng’olewa meno na Serikali; ina maana kwamba, hakuna wa kuikemea Serikali inapofanya mambo kinyume na utaratibu. Kwa maneno mengine, ile dhana ya mgawanyo wa madaraka (separation of powers checks na balances) kwa Tanzania haipo tena.
Mheshimiwa Spika; ili kuthibitisha kwamba Serikali hii imedhamiria kabisa kuuwa demokrasia na kuzika kabisa haki na uhuru wa kupata habari na kutoa maoni; baada ya kuona kwamba inabanwa na mikataba ya kimataifa ambayo inazifunga nchi wanachama kuheshimu na kukuza haki hizo – za kupata habari na kutoa maoni; sasa imeamua kujiotoa katika mikataba hiyo.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi ziliridhia na kusaini Azimio la Kimataifa la Uwazi katika Uendeshaji wa Serikali (Open Government Partnership -OGP) mnamo mwezi Septemba, 2011. Ili kujiunga na OGP ni lazima nchi wanachama wakubali na kuapa kulinda misingi ya uhuru na haki zilizoainishwa katika Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na mikataba mingine ya Kimataifa kuhusu haki za binadamu na utawala bora; na waweke mkakati wa kukuza utamaduni wa uwazi katika uendeshaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Azimio la OGP limeridhiwa na kusainiwa na nchi 69 (lakini sasa Tanzania imejiondoa). Sehemu ya Azimio hilo inasema kama ifuatavyo; nanukuu:-
“Together, we declare our commitment to: Increase the availability of information about governmental activities.
Governments collect and hold information on behalf of people, and citizens have a right to seek information about governmental activities. We commit to promoting increased access to information and disclosure about governmental activities at every level of government. We commit to increasing our efforts to systematically collect and publish data on government spending and performance for essential public services and activities. We commit to pro-actively provide high-value information, including raw data, in a timely manner, in formats that the public can easily locate, understand and use, and in formats that facilitate reuse. We commit to providing access to effective remedies when information or the corresponding records are improperly withheld, including through effective oversight of the recourse process. We recognize the importance of open standards to promote civil society access to public data, as well as to facilitate the interoperability of government information systems. We commit to seeking feedback from the public to identify the information of greatest value to them, and pledge to take such feedback into account to the maximum extent possible”.
Mheshimiwa Spika, hilo ndilo azimio ambalo nchi yetu iliridhia na kwa kifupi kabisa lina maanisa kwamba nchi zote zilizoridhia azimio hili zinafungwa na masharti ya azimio hili kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa habari hasa kuhusu utendaji wa Serikali kwa uwazi na uhuru wa hali ya juu kabisa. Lakini sasa Serikali ya Tanzania imejiondoa rasmi katika Azimio hilo. Tafsiri ndogo ya uamuzi huo; ni kwamba Serikali ya Tanzania haiungi tena mkono tena misingi ya uhuru na haki ya kupata habari. Kwa maneno mengine; kinyume chake (yani ukandamizaji wa haki na uhuru huo) ndio kipaumbele cha Serikali.
Mheshimiwa Spika, wanazuoni wanaulezea utamaduni kama njia zote za maisha ya watu (all ways of people’s life). Namna mtu anavyofanya shughuli zake; mahusiano yake na watu wengine; mahusiano yake na mazingira; desturi yake ya kuendesha maisha yake – yote hayo yanaunda utamaduni wake.
Mheshimiwa Spika, Tunapozungumzia utamaduni na hususan katika muktadha wa Tanzania; tunakwenda mbali zaidi ya fasihi, muziki, dansi, sanaa, uchongaji, uigizaji, filamu na michezo. Kwa kundi lolote la kijamii, yote haya ni sehemu ya furaha ya pamoja ya watu hai. Lakini utamaduni ni zaidi ya sanaa. Ni kuhusu ruwaza za pamoja za utambulishi. Ni jinsi maadili ya jamii yanavyowasilishwa katika jamii husika na jinsi mtu mmojammoja anavyokuwa sehemu ya jamii. Utamaduni ni jinsi yaliyopita yanavyoingiliana na yajayo.
Mheshimiwa Spika, utamaduni wa kitanzania umejengwa katika misingi ya utu, upendo, udugu, mshikamano, uhuru na umoja. Misingi hii au sifa hizi, ndizo zilizozaa amani na utulivu katika nchi yetu; na kuifanya Tanzania iheshimike duniani kama kisiwa cha amani.
Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba amani na utulivu huo kwa sasa ni wa mashaka kutokana na kuporomoka vibaya kwa ile misingi ya utu, upendo, udugu mshikamano, uhuru na umoja. Kukithiri kwa vitendo vya kutekwa na kupotezwa kwa baadhi ya wananchi kama akina Ben Saanane na Azori Gwanda; vitendo vya mauaji ya kimya kimya ya watu wasio na hatia na miili yao kufungwa kwenye viroba na kutupwa kwenye mito na fukwe za bahari; vitendo vya kuuwawa kwa viongozi wa vyama vya siasa (mifano iko mingi); vitendo vya kutishiwa kwa bunduki na kupigwa risasi kwa viongozi – tena mchana kweupe (Kwa mfano kutishiwa na bastola kwa Mheshimiwa Nape Nauye, Adam Malima na Kupigwa risasi kwa Mheshimiwa Tundu Lissu; vitendo vya utekaji na utesaji mfano kuteswa kwa mwandishi wa habari gazeti la the guardian Finnigan Simbeye aliyeokotwa akiwa katika hali mbaya hajitambui) – vitendo vyote hivi ni viasharia vya wazi kwamba ile misingi ya utu, upendo, udugu miongoni mwa watanzania hipo tena.
Mheshimiwa Spika; katika medani za siasa, kuna mifano mingi pia ya kupotea kwa mshikamano na umoja wa kitaifa. Kwa mfano; kuongezeka kwa vitendo vya wabunge hasa wa upinzani kufungiwa kuhudhuria vikao vya bunge au kushtakiwa mahakamani kwa mambo waliyoyazungumza bungeni huku wakiwa na kinga ya kikatiba; kuongezeka kwa kesi za kubumba dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani; kuzuiwa kwa mikutano halali ya kisiasa iliyoko kikatiba na kisheria; kufanya hila ya kuwanyima watuhumiwa haki ya dhamana hata kwa makosa yanayodhaminika; na kutishia kuvifuta vyama vya upinzani vilivyoko kikatiba na kisheria ni dalili za wazi za kuvunja mshikamano na umoja wa kitaifa.
Mheshimiwa Spika, Mbali na vitendo hivyo vinavyotweza utu na heshima ya binadamu, bado kumekuwa na ongezeko la kauli za kibaguzi na hasa ubaguzi wa itikadi za kisiasa na ukanda zinazotolewa na viongozi wakubwa wa nchi ; na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Tangu kuasisiwa kwake; Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mstari wa mbele kupinga kila aina ya ubaguzi na uonevu; hata kufikia hatua ya kuzitenga baadhi ya nchi zilizokuwa zikifanya vitendo vya uonevu na ubaguzi dhidi ya raia wake na hata mataifa mengine.
Mheshimiwa Spika, utamaduni ule uliokuwepo wa kupinga vitendo vya ubaguzi na uonevu sasa umekufa. Yale mataifa yaliyotengwa kutokana na sababu za ubaguzi na uonevu dhini ya mataifa mengine kama vile Israel na Morocco; sasa ndio marafiki wakubwa .
Mheshimiwa Spika, ipo methali isemayo “ndege wa bawa moja huruka pamoja” Kwa kuwa sasa nchi yetu imekuwa rafiki na wabaguzi; dhambi ile ya ubaguzi sasa imengia nchini. Sasa hivi kumezuka kauli mbaya ya kibaguzi inayotolewa dhidi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kuwa si wazalendo; ni wapinga maendeleo; ni wachochezi; ni wafanya fujo na kwamba wanahatarisha amani ya nchi. Kauli hizo zimepelekea viongozi hao kuandamwa kila mara kwa kuharibiwa mali zao; kubambikiwa kesi za uchochezi mahakamani; kundolewa kwa stahili zao za kisheria (kwa mfano kuondolewa kwa sekretarieti ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni; na stahili nyingine kama usafiri na mafuta)
Mheshimiwa Spika, ubaguzi mwingine wa wazi ni ule wa kupendelea ukanda fulani kwa kupeleka miradi mingi ya maendeleo kuliko maeneo mengine kwa sababu tu ni ukanda anakotoka mkuu wa nchi; kufanya uteuzi wa viongozi wa Serikali kwa vigezo vya undugu na urafiki na kuacha maeneo mengine ya nchi bila kuwa na uwakilishi Serikalini; Kuwakwepesha baadhi ya watu wasiguswe na mkondo wa sheria kwa kuwa wana mahusiano na mkuu wanchi (kwa mfano sakata la bomoa bomoa – Mwanza – mkuu alisema watu wa Mwanza wasivunjiwe nyumba zao kwa kuwa walimpa kura nk).
Mheshimiwa Spika, si nia yangu kuorodhesha matukio yote; lakini hata kwa haya machache niliyotaja, yanatosha kuonesha jinsi ambavyo Taifa limesambaratika. Utamaduni wetu kama taifa wa utu, upendo, udugu, mshikamano na umoja wa kitaifa haupo tena. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilileze Bunge na wananchi kwa jumla kwamba; ni kwani tunu za taifa ambazo ndizo msingi wa utamaduni wetu vimeporomoka zaidi kwenye utawala wa awamu hii ya tano kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu?
Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 inatoa uhuru kwa kila mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake, haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila julali mipaka ya nchi na uhuru wa kutoingiliwa katika mawasiliano. Kwa miaka ya hivi karibu imeibuka mitandao mingi ya kijamii ambayo hutumiwa na wananchi waliowengi kutoa na kupokea habari.
Mheshimiwa Spika, Aidha mitandao hiyo imetumika kukosoa na kuibua mijadala ambayo pengine imekuwa ni gumzo la kuikosoa serikali iliyoko madarakani na utendaji wake. Imefikia hatua mpaka vyombo vikubwa vya habari vya radio na magazeti kutumia njia ya mitandao ya kijamii kusambaza habari kwa sababu ndiyo njia pekee kwa sasa ambapo watu wengi watafikiwa na pia vyombo hivyo hutumia mitandao kama njia nyingine ya kujipatia kipato.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano kupitia kwa Rais imeeleza wazi na si mara moja kuchukizwa na mijadala na uhuru wa watu katika mitandao ya kijamii. Ilifikia hatua Rais kutangaza kuwa angetamani malaika waje kufunga mitandao ya kijamii na hivi karibuni amenukuliwa tena akisema kuwa anatamani Tanzania iwe kama China kuhusu kuminya uhuru wa mijadala na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, Malaika ambao walikuwa katika matamanio ya Rais wameshaanza kujionyesha ambapo kupitia Gazeti la serikali namba 133 lililochapishwa tarehe 16 Machi, 2018 Gazeti namba 134 la tarehe 16 Machi, 2018 serikali imechapisha Kanuni kuhusu mitandao ya kijamii pamoja masuala ya kurusha matangazo ya radio na televisheni nchini.
Mheshimiwa Spika, Kanuni hizo zilizotolewa hivi karibuni na kusainiwa na Waziri mwenye dhamana na Wizara hii zimeweka masharti kwa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuwa na orodha ya watu wanaomiliki mitandao ya habari kama blogs and tovuti kusajiliwa na pia kulipa ada mbalimbali zilizoainishwa. Aidha internet café zote zitatakiwa kuweka kamera ambazo zitaonesha anayeingia na kutoka katika maeneo yao na pia kutumia anuani za mtandao za Tanzania (IP address).
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa si tu mitandao ya kijamii inatoa uhuru wa kuwasiliana lakini pia imekua ni chanzo cha mapato kwa wananchi waliowengi. Kwa viwango vya ada na masharti yaliyowekwa kwenye Kanuni hizo ni dhahiri Kanuni hizo zinaanza kazi ya malaika wa kuzima mitandao ya kijamii kwa sababu wananchi waliowengi hawataweza kukidhi matakwa na vigezo vya kusajiliwa.
Mheshimiwa Spika, katika hali kama hii tutegemee Taifa kuwa gizani kwa sababu litapokea taarifa za upande wa serikali peke yao na si kutoka kwa wananchi ambao wameanza kutumia mitandao ya kijamii kujipatia na kutoa habari. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa huu ni mkakati wa Serikali kupunguza kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii na kutaka kubaki na blogs au tovuti chache ambazo watakuwa na uwezo wa kuzidhibiti. Hii sio hali ya kushabikia hata kidogo, inatakiwa kupingwa na kila mpenda maendeleo.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi katika Wizara hii ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kwa Serikali, lakini Serikali haijayafanyia kazi mpaka sasa. Mambo hayo ni pamoja na haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishatoa mapendekezo mengi sana katika wizara hii; lakini ingependa kupata maelezo ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapandekezo yaliyotajwa.
Mheshimiwa Spika, “michezo ni afya, michezo ni elimu, michezo ni burudanI; michezo ni biashara na michezo ni uchumi”. Hivyo vyote ni faida zitokanazo na michezo kwa mtu mmoja au kwa jamii nzima. Mbali na kujenga afya ya mwili; michezo imethibitika kuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi pia.
Mheshimiwa Spika, hapa duniani, michezo ndilo jukwaa pekee linaloweza kuleta watu wengi kwa pamoja, kwa ridhaa yao kuliko jukwaa la aina yoyote lile. Hivyo basi, michezo kama ikitumiwa vizuri na kufanyiwa uwekezaji wenye tija ni dhahiri inaweza kuwa chanzo kikubwa cha uchumi. Hoja kubwa ni kufanya uwekezaji madhubuti katika sekta ya micheo lakini pia kuwa na taasisi imara zinazosimamia sekta ya michezo na zenye kuwajibika ipasavyo ili kuondoa mianya ya taasisi hizo kutumika kwa kwa malengo binafsi au ya kisiasa, kama ambavyo inajionesha hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kumekuwa na desturi mbaya hapa nchini kwa Serikali kutumia taasisi za michezo kwa ili kukidhi malengo ya kisiasa. Uzoefu unaonyesha kuwa Serikali inaweka viongozi inaowataka kwa vyama vya michezo ili kuwa na ushawishi katika vyama hivyo na kunufaika na rasilimali fedha za vyama vya michezo.
Mheshimiwa Spika, Shule nyingi nchini Tanzania, hususani shule za serekali, hazina miundombinu ya michezo, na hata kama miundombinu hiyo ipo, basi ipo kwenye hali mbaya sana. Shule nyingi nchini hazina viwanja vizuri vya michezo, ukiachililia mbali uhaba wa vifaa vya michezo katika shule zetu hizo. Kwa mfano, shule moja yenye wastani wa wanafunzi 600-1000 utakuta ina mpira mmoja wa netiboli na mmoja wa football na mara nyingine isiwepo kabisa.
Mheshimiwa Spika, hii imekuwa changamoto kubwa sana kwa wanafunzi ambao wengi wao wanapenda michezo, ukizingatia kwamba michezo inachangia sana katika maendeleo yao ya kiafya, kiakili, kuwajengea ubunifu na uvumbuzi, ujasiri, kushirikiana na wenzao.
Mheshimiwa Spika kwa kuwa shuleni ni kama kitalu cha kuibua na kukuza vipaji katika tasnia mbalimbali; na kwa kuwa michezo inajenga afya ya mwili na akili kwa watoto wetu; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwamba Serikali itenge bajeti maalum ya michezo shuleni ili kuweza kuibua vipaji lakini pia kupunguza utoro na hivyo kuongeza ubora wa elimu shuleni.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na Tanzania kuwa na idadi ya takriban watu milioni 56, lakini ina chuo kimoja tu cha walimu au wakufunzi wa michezo. Chuo hicho ni Malya Sports College kilichopo Mkoani Mwanza. Aidha, wanafunzi wanaohitimu masomo yao katika chuo hicho kwa mwaka hawazidi 60.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa wakufunzi wa michezo waliohitimu katika chuo hicho toka mwaka 2006 hadi mwaka 2016 (miaka kumi mfululizo) ni 158 tu. Wakati huo huo takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa idadi ya wanafunzi wa shule za msingi za Umma ni milioni 8.969 na Shule za Sekondari wanafunzi milioni 1.468 na wanafunzi katika shule binafsi za msingi ni 348,681 na sekondari ni wanafunzi 343,656. Hii ina maana kwamba idadi yote hii ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari za uma na binafsi zinategemea kufundishwa michezo na wakufunzi hawa 158 au pengine pungufu yao kwa kuwa si wote wanaohitimu ukufunzi wa michezo watapenda kuendelea na kazi hiyo; – wengine wanaweza baadaye kuamua kufanya kazi nyingine ikiwemo ujasiriamali nk.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumesema siku zote, hakuna elimu bila mwalimu; vivyo hivyo hakuna michezo bila wakufunzi wa michezo. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ina mpago mkakati gani wa kujenga vyuo vingine kwa ajili ya wakufunzi wa michezo mbalimbali ili kukuza sekta ya michezo nchini?
Mheshimiwa Spika, kwa sasa; Mkoa wa Kilimanjaro unaandaa mashindani ya mchezo wa riadha wa mbio ndefu maaarufu kama ‘Kilimajaro Marathon’ kila mwaka; na kualika washiriki toka mataifa mablimbali duniani jambo ambalo limeyafanya mashindano hao kutambulika kimataifa. Hili ni jambo zuri na kubwa la kujivunia kwani mbali ya kuibua vipaji pia linakuza shughuli za kiuchumi kama vile utalii katika mkoa huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inashauri mikoa mingine kuiga mtino huo lakini kwa namna tofauti. Badala ya kuiga moja kwa moja mchezo wa riadha; kila mkoa unaweza kuwa na mchezo wake tofauti kulingana na mazingira, mila na desturi za mkoa husika. Kwa mfano; Mkoa wa Simiyu unaweza kuwa mkoa wa kuandaa mashindano ya baiskeli na ukajulikana hivyo, Mkoa wa Kigoma ukawa ni kwa ajili ya mashindano ya Makasia, mkoa wa Tanga ukawa mashindano ya kucheza bao; Mkoa wa Mbeya ukawa na mashindano ya ngoma za asili, Mkoa wa Arusha ukawa na mashindano ya kurusha mishale au mikuki n.k
Mheshimiwa Spika, ubunifu wa aina hii ukiwa na lengo la kuifanya michezo mingi inayoshindaniwa kimataifa kuandaliwa kila mkoa kila mwaka na kuzidisha ushindani wa ndani na wa nje itasaidia kuongeza nafasi ya Tanzania katika ushiriki wa michezo kimataifa na hivyo kuzidisha ari ya ushindani na kuitangaza nchi yetu. Jambo hili litarudisha pia michezo yetu ya asili ambayo inakaribia kupotea kabisa.
Mheshimiwa Spika, hoja kubwa katika hotuba hii ni madai ya haki ya uhuru wa habari ambao Serikali hii ya awamu ya tano imewapoka wananchi kinyume na Katiba ya nchi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuifahamisha Serikali hii ya CCM kwamba; kitendo inachokifanya cha kupoka haki ya kikatiba ya uhuru wa kupata habari ni cha hatari sana kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu wananchi wana hasira kubwa kutoka na hali ya maisha kuwa ngumu zaidi hasa baada ya Serikali hii ya awamu ya tano kushika madaraka. Hasira hizi za wananchi angalau zinaweza kupungua kama wataachwa waseme madukuduku yao. Kuzidi kuwazuia watu kutoa maoni na kueleza fikra zao; ni kuchochea hasira na chuki miongoni mwao; na siku uvumilivu ukiwashinda hali itakuwa mbaya.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la msingi ni kuporomoka kwa tunu za taifa (utamaduni) na kupotea kwa thamani ya utu katika nchi yetu. Serikali hii ina wajibu wa kuliunganisha taifa kwa kujenga mazingira ya kurejesha tena ule utamaduni wa upendo, udugu, na mshikamano wa kitaifa ambao kwa sasa umeyumba sana. Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere alisema kazi ya Uongozi ni kuwaleta watu pamoja na sio kuwagawa. Ili watu wakae pamoja lazima wathaminiane, waheshimiane, wapendane, ili waweze kushirikiana kulijenga taifa lao. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa Serikali hii kukemea kwa nguvu zote vitendo vyote vya kibaguzi, vya uonevu na unyanyasaji vinavyofanywa na watendaji wake dhidi ya wananchi ili kurejesha tena zile tunu za taifa ambazo kwa sasa zimepotea.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishauri na kupendekeza kwamba; Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, hususan kitengo cha Upelelezi wa Kijeshi (Military Inteligence) kitoe msaada wa kipelelezi kwa Jeshi la Polisi ili kubaini na kukabiliana na vitendo vya kigaidi vilivyokuwa vinafanywa na “Watu wasiojulikana” dhidi ya raia wasio na hatia.
Mheshimiwa Spika, msingi wa ushauri huo ulitokana na ukweli kwamba, kulikuwa na kila dalili kwamba Polisi walikuwa wamezidiwa mbinu na nguvu ya kukabiliana na magaidi hao. Hii ni kwa sababu kwanza matukio hayo yalikwa yanawalenga Askari Polisi wenyewe; lakini pili, hawakuweza kuyadhibiti nyakati yalipotokea. Itakumbukwa kwamba takriban miaka miwili iliyopita kulikuwa na matukio ya kigaidi ya kuvamiwa kwa vituo vya Polisi na kupora silaha, kuwauwa askari Polisi na kuwapora silaha, pamoja na wananchi kuuwawa na hususan viongozi wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mheshimwa Spika, Kutokana na Jeshi la Polisi kushindwa kujihami kwa wakati ule; Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza kwamba yamkini matukio hayo yalikuwa yanafanywa na watu wenye mafunzo ya kijeshi na mbinu za kivita ndio maana waliweza kutekeleza uhalifu huo bila kukamatwa na bila kujulikana kwa majina yao, na hata walikoelekea.
Mheshimiwa Spika, matukio yenye sura ya kigaidi bado yanaendelea katika nchi yetu. Vitendo vya utekaji na kupotezwa kwa raia wasio na hatia kama vile Ben Saanane na Azori Gwanda (mwandishi wa gazeti la Mwananchi) vimeendelea kutokea. Aidha, ni katika kipindi hiki ambapo matukio mengi ya mauaji hasa ya viongozi wa vyama vya upinzani yametokea. Viongozi waliouwawa ni pamoja na Daniel John, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA – Kata ya Hananasifu katika Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam; aliyeuwawa kinyama kwa kunyongwa na kupigwa kichwani na vitu vyenye ncha kali. Kiongozi mwingine ni Godfrey Lwena, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Namawala kwa tiketi ya CHADEMA katika Jimbo la Mlimba – Wilaya ya Kilombero huko Morogoro; aliyeuwawa kikatili na watu wasiojulikana. Aidha, tunamkumbuka marehemu Aramu Kaigwe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi –Kata ya Nyarugusu katika Jimbo la Kasulu Vijijini mkoani Kigoma, aliyeuwawa kikatili kwa kukatwa katwa mapanga na watu wasiojulikana.
Mheshimiwa Spika, ni katika kipindi cha utawala huu pia ambapo taifa limeshuhudia kutapakaa kwa maiti za watu katika fukwe za bahari na nyingine zikiwa zimefungwa katika viroba kwenye mito. Ni wakati huu huu ambapo Mbunge anapagwa risasi mchana kweupe Bunge likiwa linaendelea.
Mheshimiwa Spika, wakati matukio yote haya yanatokea; vyombo vya ulinzi na usalama vipo, na vinaendelea kujisifu kwamba vipo imara na kwamba nchi iko salama. Aidha, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya uchunguzi juu ya matukio hayo. Serikali iliposhauriwa kuomba vyombo vya kimataifa kufanya uchunguzi ilikataa kwa kigezo kwamba ina uwezo wa kufanya uchunguzi. Katika mazingira hayo, usalama wa raia uko mashakani.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Jeshi la Wananchi ni mojawapo ya vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu; na kwa kuwa Jeshi la Polisi limeonyesha dhahiri kushindwa kulinda usalama wa wananchi kwa kukiri hadharani kuwa haliwafahamu watu wanaofanya uhalifu licha ya kuwa na muda mrefu usio na ukomo wa kufanya uchunguzi; na kwa kuwa matukio ya kigaidi hivi sasa yamechukua sura mpya ambapo viongozi wa kisiasa ndio walengwa; ndio maana Rais Magufuli analindwa na Makomandoo wa Jeshi wenye silaha nzito za kivita; Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutumia inteligensia ya Jeshi kupeleleza wahusika wa matukio haya kwa lengo la kuyakomesha ikiwa haitaki kutumia vyombo vya nje vya uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali jukumu la kulinda mipaka ya nchi; Jeshi ndio mbadala wa kila kitu nchi inapokuwa kwenye mkwamo (crisis). Mbadala huo hauwezi kutokea kama Jeshi halijawezeshwa kitaaluma na kubobea katika kila aina ya utaalamu katika sekta zote.
Mheshimiwa Spika, katika nchi zilizoendelea, Jeshi ni kitovu cha utafiti na ugunduzi wa teknolojia za hali ya juu. Kwa Mfano, Kwa mujibu wa Jarida la “Business Insider” la nchini Marekani lililochapishwa mwaka 2014 ni kwamba; Wizara ya Ulinzi ya Marekani inahusika na ugunduzi wa karibu vifaa vyote ki-electroniki duniani[23] Akitilia mkazo hoja hiyo, mwanauchumi wa Kiitaliano Mazzucato anaeleza kwamba; ili kufikia viwango vya juu vya teknolojia kama vile kwenda mwezini kunahitaji hali ya juu ya ujasiri, uwezo na utayari wa kuwekeza kikamilifu katika maeneo yenye hatari ambayo sekta binafsi huwa na woga wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, mchumi huyu anamalizia hoja yake kwa kusema kwamba Jeshi la Marekani lilikuwa mara nyingi linawekeza katika maeneo hatarishi (risky areas) jambo ambalo lilipelekea kuvumbuliwa kwa vifaa vya kielektroniki kama vya vya Apple nk. Matokeo ya jambo hili ni kuzalishwa kwa vifaa vinavyotumika duniani kote ambapo ni vigumu kufikiria dunia hii ingekuwaje bila vifaa hivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingangia maoni hayo; ukiachilia mbali teknolojia ya kijeshi (military technology) ambayo inatakiwa kuwepo na kuendelezwa nyakati zote ili kuimarisha uwezo wa Jeshi katika mbinu za kivita; Jeshi pia linatakiwa libobee katika teknolojia nyingine kwa maendeleo ya taifa. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kama nilivyoeleza hapo awali kwamba; Jeshi linatakiwa kufanya kila kitu nchi inapokuwa kwenye mkwamo. Ni dhahiri kwamba halitaweza kufanya kila kitu ikiwa halina utaalamu katika kila sekta.
Mheshimiwa Spika, swali la msingi hapa ni Je, Serikali imewekeza kiasi gani katika shughuli za utafiti na ugunduzi katika Jeshi letu? Je, Bajeti ya maendeleo inayotengwa inakidhi mahitaji ya kufanya tafiti katika sekta mbalimbali ili kuwezesha ugunduzi na uvumbuzi wa teknolojia mpya katika sekta hizo kwa maendeleo endelevu ya nchi?
Mheshimiwa Spika, ili kupata majibu ya maswali hayo, inabidi kufanya uchambuzi (analysis) ya bajeti ya Maendeleo katika Wizaara ya Ulinzi na JKT angalau kwa miaka mitatu iliyopita ili tuone kama kuna jitihada zozote za kulifanya Jeshi liwe kisima cha fikra.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/16, Serikali ilimeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge kwa miradi ya maendeleo katika wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na katika mafungu mengine fedha hazikutolewa kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Randama ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2015/16; Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 220. 14 (katika fungu 57 – Wizara) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2016 fedha iliyokuwa imeshatolewa na hazina ilikuwa ni shilingi bilioni 40 sawa na asilimia 18 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, miradi iliyokuwa itekelezwe, mingine ilikuwa inawagusa moja kwa moja wananchi, hivyo kitendo cha kutotekelezwa kikamilifu kiliwaathiri sana wananchi. Kwa mfano mradi mmojawapo ulikuwa ni upimaji na ulipaji wa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na jeshi. Mradi huu ulitengewa takriban shilingi bilioni 7.4, lakini fedha iliyotolewa hadi kufikia Machi, 2016 ni shilingi milioni 277.1 sawa na asilimia 3.7 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutotoa fedha ya kutosha kutekeleza mradi huu kuliendelea kuchochea migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya jeshi na wananchi ambayo ingeweza kuepukwa na hivyo kujenga uhasama kati ya Jeshi na Wananchi jambo ambalo lingeweza kuepukwa kama Serikali ingetoa fedha zote zilizoidhinishwa na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, jambo la ajabu kabisa kuwahi kutokea ni kitendo cha kutopeleka fedha yoyote kutekeleza miradi ya maendeleo katika fungu 38 (Ngome). Fungu hili lilitengewa jumla ya shilingi bilioni 8 lakini hadi kufikia Machi 2016, hakuna hata senti moja iliyotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wowote wa maendeleo uliopangwa kutekelezwa chini ya fungu hili. Hivyo Bajeti ya Maendeleo katika fungu 38 Ngome kwa mwaka 2015/16 haikutekelezwa kabisa.
Mheshimiwa Spika miradi iliyokuwa itekelezwe chini ya fungu hili ilikuwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege Tanga, utafiti na ulinzi wa anga, ujenzi wa maghala ya mlipuko, ukarabati wa zana za ulinzi wa anga na ujenzi wa gati.
Mheshimiwa Spika, katika muktadha huo huo, fungu 39 (JKT) lilitengewa shilingi bilioni 4 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa, lakini hadi kufikia Machi, 2016 hakuna hata senti moja iliyotolewa kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Spika, mazoea haya mabaya ya utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo katika wizara hii yanaonekana kuota mizizi na sasa yamekuwa ni kama desturi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, fedha ya kutekeleza miradi ya maendeleo liyoidhinishwa na bunge katika fungu 38 (Ngome) ilikuwa ni shilingi bilioni 10, lakini hadi machi 2017 ilikuwa imetolewa shilingi bilioni 1 tu sawa na asilimia 10 ya fedha iliyokuwa imeidhiniswa. Aidha, kwa upande wa fungu 39 (JKT), fedha ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge ilkuwa ni shilingi bilioni 8, lakini hadi machi, 2017 ilikuwa imetolewa shilingi bilioni moja tu, sawa naasilimia 12.5 ya fedha iliyoidhinishwa na bunge. Hii ina maana kwamba bajeti ya maendeleo katika fungu hili haikutekelezwa kwa asilimia 87.5. Mheshimiwa Spika, halikadhalika kwa upande wa wizara, fedha iliyokuwa imeidhinishwa na bunge ilikuwa shilingi bilioni 230, lakini hadi kufikia machi, 2017 ni shilingi bilioni 33.9 tu sawa na asilimia 14.7 ilikuwa imetolewa.
Mheshimiwa Spika, tafsiri nyepesi ya utekelezaji huu duni wa bajeti ya maendeleo, unairudisha nyuma wizara na unapunguza ufanisi, ubora na tija ya majeshi yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali, kwa kadri ile ile ambayo inalifu jeshi letu kuwa ni imara, lenye weledi na ufanisi mkubwa, basi sifa hizo zionekane kwenye utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ya majeshi hayo. Vinginevyo itakuwa tunajifurahisha tu kwa maneno kumbe hali halisi ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kutotekeleza bajeti ya maendeleo ya wizara hii, sio tu kunalifedhehesha Jeshi letu, lakini pia kinawaweka wananchi katika hali ya hatari kubwa. Kwa mfano wote tunafahamu jinsi matukio ya milipuko ya silaha katika maghala ya silaha za milipuko huko Mbagala na Gongo la Mboto – Dar es Salaam, yalivyosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa makazi ya wananchi. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliahidi kujenga na kukarabati maghala hayo ili kudhibiti ajali za milipuko. Lakini jambo la ajabu, ni kwamba Bunge liliidhinisha bajeti hiyo lakini Serikali haikutekeleza.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka kwa fedha 2017/18 fedha ya maendeleo iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya wizara (Fungu 57) ilikuwa ni shilingi bilioni 205 na fedha iliyotolewa hadi kufikia Aprili, 2018 ilikuwa ni shilingi bilioni 169.786 sawa na asilimia 82.82. Aidha, fedha ya maendeleo iliyokuwa imetengwa kwa fungu 38 (Ngome) ilikuwa ni shilingi bilioni 8 na fedha iliyopokelewa hadi kufikia Aprili, 2018 ilikuwa ni shilingi bilioni 6.793 sawa na asilimia 84.92. Kwa upande wa JKT (fungu 39) fedha ya maendeleo iliyokuwa imetengwa ni shilini bilioni 6 na iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 5 sawa na asiliimia 83.33
Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu hizi utaona kwamba utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ya Wizara na mafungu yake yote kwa mwaka wa fedha 2017/18 uliimarika zaidi kuliko miaka miwili iliyotangulia. Hata hivyo, ukiangalia fedha halisi iliyotolewa ni kidogo sana kuweza kufanya mambo makubwa ya tafiti na ugunduzi wa teknolojia za kisasa Jeshini na katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, kwamba jeshi ni mbadala wa kila kitu ikiwa nchi iko kwenye mkwamo. Kwa sababu hiyo jeshi linatakiwa kuwa kisima cha fikra (think tank) cha taifa ili kuliondoa taifa kwenye mkwamo ikiwa limekwama. Ili jeshi liweze kuwa na uwezo huo; lazima liwekeze sana kwenye tafiti na kubobea katika kila sekta. Kwa vyovyote vile uwekezaji huo hauwezi kuwa wa bilioni 8 au 6 ambazo tumezoea kutenga. Bajeti hiyo ni ndogo mno kuweza kujenga maabara za kisasa zenye vifaa vinavyokidhi teknolojia ya kisasa kuwezesha Jeshi kufanya tafiti katika Nyanja mbalimbali na kulisaidia taifa kusonga mbele kiuchumi. Kwa maneno mengine; pamoja na bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18 kuonekana kutekelezwa kwa kiwango kikubwa; lakini utekelezaji huo hauna tija yoyote ikiwa tunataka Jeshi liwe kisima cha fikra.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuacha tabia ya kulitumia Jeshi letu kwa shughuli ndani za kisiasa. Itakumbukwa tulilaani vikali Jeshi kutumika kufanya ulinzi wa ndani Zanzibar wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2010 na 2015 wakati hiyo ilikuwa ni kazi ya Jeshi la Polisi; na zaidi sana hakukuwa na hali ya hatari iliyotangazwa; sababu ambayo ingeweza kutumika ili Jeshi lisaidie Polisi katika masuala ya ulinzi wa ndani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na rai hiyo; tabia ya Serikali kulitumia Jeshi vibaya haijakoma. Itakumbukwa kwamba CHADEMA ilipotangaza Operesheni UKUTA, Septemba mosi na Oktoba mosi 2016; tulishuhudia ndege vita zikitanda katika anga la Dar es Salaam; na vikosi vya Jeshi vikifanya mazoezi hadharani katika maeneo ya makazi ya wananchi kwa lengo la kuwatisha wananchi wasijotekeze kwenye maandamano. Hata baada ya taarifa ya kwenye mitandao ya kijamii kwamba tarehe 26 Aprili, 2018 siku ya Muungano, kungefanyika maandamano nchi nzima; vikosi vya Jeshi vilionekana kufanya hivyo pia.
Mheshimiwa Spika, Ingawa Serikali imekuwa ikiwahadaa wananchi kwamba hayo ni mazoezi ya kawaida ya Jeshi; lakini kimsingi maana iliyofichika ni kwamba mazoezi hayo yanayofanyika kwenye maeneo ya wananchi hasa kunapokuwa na operesheni za vyama vya upinzani yana lengo la kuwatisha wananchi na hivyo siyo ya kawaida. Kama ni mazoezi ya kawaida kwanini wasiyafanye kwenye makambi yao au kwenye viwanja vya michezo?
Mheshimiwa Spika, hii sio desturi nzuri ya kutumia Jeshi kuwatisha wananchi na kuminya uhuru wa kikatiba wa wananchi kushiriki shughuli za kisiasa za nchi yao. Kitendo cha kutumia Jeshi kinatoa taswira mbaya kwamba nchi hii sio ya kidemokrasia tena na kwamba inatawaliwa kidikteta. Ni katika nchi za kidikteta tu, utakuta Jeshi likifanya shughuli za ndani za kisiasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaionya tena Serikali kuliacha Jeshi lifanye kazi yake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zao za utendaji.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 ni ya zamani sana, na kwa vyovyote vile haikidhi mahitaji ya mazingira ya sasa. Mara kadhaa Serikali imekuwa ikiahidi kuwa itaifanyia maboresho Sheria hiyo, ili iendane na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, Ilikuwa ni ahadi ya Serikali kwamba mapendekezo ya upande wa pili wa Muungano (Zanzibar) juu ya sheria hiyo yangepatikana baada ya kusuasua kwa muda mrefu lakini bado hayajapatikana pia. Tatizo hili linakwaza utendaji na maslahi ya wanajeshi kwani sheria kutofanyiwa maboresho kwa miaka 52 sasa ni jambo lisilokubalika.
Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na mgogoro wa mipaka kati ya nchi yetu na Malawi jambo ambalo limepelekea vikao vya usuluhishi katika ya nchi zote mbili kuitishwa kujadili namna ya kupata muafaka wa suala hilo. Hata hivyo, Serikali imeshindwa kutuambia ukweli wa jamb hili. Tumeteleza wapi? Ni kwa nini Malawi wanang’ang’ania wakati mpaka wa maji kimataifa unajulikana? Au Serikali kuna ukweli inaouficha juu ya mikataba ya watawala waliopita?
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na tatizo la kuondolewa kwa alama za mipaka (beacons) kati ya nchi yetu na Kenya katika maeneo ya Migori – Kenya na Tarime – Tanzania. Zoezi la kurejesha alama hizo limechukua muda mrefu sasa bila mafanikio. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri wizara husika katika nchi zote mbili ziongeze kasi ya urejeshaji wa alama hizo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni nini kimejificha nyuma ya pazia juu ya kasi ndogo ya urejeshaji wa alama za mipaka kwa usalama wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika kwa kitendo cha Serikali cha kuwanyang’anya na kuwadhulumu wananchi kwa kuchukua maeneo yao kwa ajili ya JWTZ na JKT na kukataa kuwalipa fidia. Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kulipa fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi mara kadhaa lakini haijatekeleza ahadi hizo jambo ambalo limewafanya wananchi waliochukuliwa maeneo yao kukata tama.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaelewa kwamba bajeti ya kulipa fidia huwa inatengwa lakini Serikali kwa makusudi huwa hailipi fidia hizo, jambo ambalo tunaona ni sawa na kuwakomoa wananchi. Kama kweli Serikali ina nia njema ya kulipa fidia hizo; ni kwa nini inatekeleza miradi mikubwa inayotumia fedha nyingi halafu inaacha hili la fidia ambalo fedha yake ni kidogo?
Mheshimiwa Spika, pamoja na ushiriki wetu wa Ulinzi wa Amani nje ya nchi kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua; tangu utaratibu huu uanze hadi leo hii, ni wanajeshi wangapi wamepoteza maisha na wangapo wamejeruhiwa?
Mheshimiwa Spika, sambamba na kutoa takwimu za wanajeshi waliopoteza maisha na kujeruhiwa; Kambi Rasmi ya Upinzani ingependa kujua vilevile ni kwa nini wajane wa wanajeshi waliofariki hawatunzwi inavyostahili kuendana na kustaafu kwa marehemu huyo/hao kipindi wangekuwa hai?
Mheshimiwa Spika, pamoja na utaratibu uliowekwa wa kuajiri kwa kuchukua vijana kutoka JKT na JKU; bado utaratibu wa ajira haujawekwa wazi vya kutosha. Kumekuwa na malalamiko kadhaa hususan kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya JKT lakini kupata ajira Jeshini inakuwa ni vigumu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili; kuna vigezo vya ziada vinavyohitajika kuwaajira vijana wanaohitimu JKT, au kuhitimu mafunzo ya JKT ni kigezo toshelevu cha vijana hao kupata ajira jeshini?
Mheshimiwa Spika, kwa takriban miaka saba iliyopita, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kuwekeza katika miradi ya kiuchumi ya uzalishaji ambayo hatimaye itapelekea kukuwa kwa viwanda vidogo vidogo. Tulipendekeza Serikali itumie nguvu kazi iliyopo kwenye Jeshi la Kujenga Taifa katika kujenga uchumi wa kweli nchini, na hasa kipindi hiki cha uchumi wa viwanda Jeshi la Kujenga Taifa ndio lilitakiwa litoe dira ya namna ya kuwa a uchumi wa viwanda. Tulishauri kwamba Serikali itenge mashamba makubwa ili vijana hawa wawapo mafunzoni, wafanye mafunzo kwa vitendo ya kilimo ili nchi iweze kujitegemea kwa chakula lakini zaidi sana kuzalisha ziada ambayo itatumika kwenye viwanda kama malighafi. Kwa sababu hiyo, tulipendkeza pia kwamba; Serikali iwaagize wakuu wa makambi ya JKT kutengeneza programu maalum za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda, ufundi, uvuvi nk kila mwaka na kwamba; Waziri mwenye dhamana awe anatoa taarifa ya uzalishaji uliofanywa na JKT na mapato (maduhuli) yaliyopatikana kutokana na uzalishaji huo katika kila Bunge la bajeti.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ushauri huo kwa siku nyingi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupewa mrejesho wa utekelezaji wa ushauri huo. Serikali ilieleze Bunge, JKT imekeleza miradi mingapi ya uzalishaji na imeingiza fedha kiasi gani kutokana na uzalishaji huo, na ina mpango wa kuteleza miradi mingapi kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya hapa nchini inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa rasilimali watu. Kwa mujibu wa Ripoti ya Madaktari wenza wa Afrika (Africa Cuamm); Wizara hii ilikuwa na upungufu wa watumishi kwa asilimia 49 katikamwaka wa fedha 2016/17.Hata hivyo, pamoja na kuwa serikali haijatoa tathimini ya uhitaji wa jumla wa watumishi katika sekta hii; katika taarifa ya utekelezajiwa bajeti ya Wizara(fungu 52) inaonyesha kuwa; Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilitoa nafasi za ajira 3,152. Katika nafasi hizo, ajira za madaktari bingwa zilikuwa 24,madaktari wasaidizi 45, wauguzi daraja wa pili 137 (nurses) na nafasi 2 za madaktari washauri 2(Medical Consultant na wengine walipelekwa kwenye kada mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, bado rasilimali watu katika sekta ya afya nchini ni tatizo hususani katika maeneo ya vijijini. Bado wataalamu wetu wa afya wanafanya kazi kubwa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa. Pamoja na kuwa serikali imesema imetoa ajira tukumbuke kuwa ni serikali hiyo hiyo ndio inayotaka kufanya tafiti za upungufu wa watumishi na ndio hiyo hiyo inayoamua iseme nini kwa umma kuhusiana na ajira au mapungufu ya watumishi jambo ambalo linaathiri uhalisia wa matatizo katika sekta mbalimbali. Jambo ambalo linatia mashaka katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili serikali. Tukumbuke kuwa pale ambapo taasisi au watu mbalimbali wanakuwa huru kufanya tafiti ndipo serikali inaweza kujikosoa na kufanya maboresho. Upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ni tatizo linalohitaji umakini na weledi mkubwa la kulishugulikia kwani kuna hatari ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la vifo vinavyotokana na ukosefu wa tiba kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, nimwaka jana tu, serikali ilikiri uhaba mkubwa wa madaktari. Kwa mujibu wakumbukumbu, serikali hii ya awamu ya tano iliwahi kutaka kuwapeleka madaktari 500 nchini Kenya ilhali nchi ikikabiliwa na tatizo kubwa na sugu la uhaba wa madaktari. Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Mwaka 2012 idadi ya madaktari na wauguzi kwa Tanzania ilikadiriwa kufikia 2,250 ambapo ni sawa na uwiano wa madaktari 0.5 kwa watu 10,000. Kwa mujibu wa gazeti la Guardian on Sunday mwaka 2013 nchi ilikuwa na upungufu wa madaktari 2,700[24]. Uchambuzi uliofanywa na the Citizen Tanzania mwaka 2016 unaonyesha uwiano kuwa daktari 1:25,000.kinyume na muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO)
Mheshimiwa Spika, Serikali hiyo hiyo leo inatoa ajira 24 kwa madaktari na madaktari wa daraja la pili 45 tu kwa nchi nzima bila kujali ongezeko kubwa la watu kuanzia mwaka 2012 baada ya sensa ya taifa; ambapo idadi ya watu ilikuwa milioni 44 tofauti na sasa idadi ya watu kwa nchi yetu inakadiriwa kufikia takribani milioni 52.55 mpaka mwaka 2017 kwa mujibu wa Tume ya taifa ya takwimu. Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha uwepo wa idadi ya watu takribani milioni 56 mpaka mwaka 2017 huku nchi yetu ikitajwa kati ya nchi 5 Afrika zenye watu wengi zaidi kwa mujibu wa hotuba Waziri wa Fedha na Mpango ya mwaka 2017 kuhusu hali ya uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwka 2017/2018. [25]
Mheshimiwa Spika,Pamoja na ongezeko hilo kubwa la idadi ya watu serikali imeshindwa kuzalisha ajira za wataalamu na wanataaluma watakaoweza kukabiliana na changamoto zinazoibuka kila siku ikiwemo mlipuko wa magonjwa yale ya kuambukiza na hata yasiyo ya kuambuza. Hata hivyo kwa mujibu wa The Citizen Tanzania, kuna wanafunzi wengi wanaohitimu mafunzo ya tiba na afya lakini ni wachache sana wanaopata ajira serikali kwani wengi huishiwa kuajiriwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kuajiriwa kwenye sekta za ujuzi tofauti na hata kujiajiri wenyewe. Hii imejionyesha wazi kwenye randama ya Wizara Ukurasa wa 50 ambapo idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya afya nchini walikadiriwa kuwa 47,269 huku ajira zilionekana kutolewa chache sana.
Mheshimiwa Spika, inashangaza kuona serikali ilitoa nafasi 2 tu kwa Madaktari washauri (Medical Consultant) ambapo hata hivyo serikali imekiri kushindwa kujaza nafasi hizo mbili.[26] Nchi nyingi duniani hasa zile za uchumi wa kati na zile zilizoendelea zimeweza kupiga hatua kubwa katika kuwekeza kwenye afya za wananchi wao.Viwanda haviwezi kuzalisha pasipo watu kuwa na uhakika wa tiba bora na uwezo wa kuonana na tabibu pale wanapomuhitaji. Pamoja na hilo tafiti za magonjwa, chanjo na tiba zinaweza tu kufanyika vyema hapa nchini kama serikali ikijikita kwenye uwekezaji wa afya. Mfano; kwa kupitia Bodi ya Madaktari wa California (Medical Board of California ) mwaka 2015, katika ajenda zake kuu ni kuhakikisha kunakuwepo na madaktari na wataalamu wabobezi wa afya ambao watahakikisha maendeleo ya nchi yanaakisi uimara wa afya za raia. Kwa mantiki hiyo,uwekezaji katika afya ndio unaotoa mwelekeo wa uwekezaji katika sekta nyingine.’ Naweza kusema kuwa sekta ya afya ndio uhai wetuna ndio kichocheo kikuu cha maendeleo. (Health sector is paramount of all other sectors).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia wataalamu wake mbalimbali, kuja pamoja na hata kuwa na mjadala wa kitaifa wa namna bora ya kuimarisha sekta ya afya nchini hususani kwa kuhakikisha tunawekeza katika elimu ya kuzalisha vijana ambao ni tanuru la fikra ‘think tank’ la kuokoa sekta ya tiba na utabibu nchini. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Seirikali kulieleza Bungeni hili; ni sababu zipi zilizopelekea kushindwa kuwaajiri madaktari washauri wawili ambao ilitangaza nafasi zao? Ni kwamba wamekosekana watu wenye sifa, au hakuna mtu yoyote aliyeomba nafasi hizo?.
Taasisi ya Chakula na Lishe
Mheshimiwa Spika, Randama ya Wizara fungu 52 inaonyesha kwamba; Mradi Na. 5496, (Tanzania Food and Nutrition Center) katika Taasisi ya Chakula na Lishe; haukutengewa fedha yoyote kwa mwaka wa fedha 2017/18; na pia kwa mwaka mpya wa fedha 2018/19. Katika kitabu cha taarifa za utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa kipindi cha Julai mpaka Februari 2018 kimeonyesha kuwa serikali ina azma ya kupunguza vifo vya watoto vitokananvyo na udumavu, ukosefu wa madini joto na vitamin A.
Mheshimiwa Spika, Upungufu wa vitamin na madini joto ni tatizo kubwa sana inalowaathiri watoto na wanawake walio katika umri wa kuzaa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Demographic Health Survey 2010 Takwimu zinaonyesha kwamba takribani asilimia 59 ya watoto wadogo na asilimia 41 ya kina mama wajawazito wanaathiriwa na ukosefu wa madini joto. Pamoja na kwamba kitabu cha randama ukurasa wa 70 serikali imeonyesha kuwa inatoa Vitamini A na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wadogo takribani nchi nzima lakini uhalisia wa utekelezaji wa azma hii ya serikali unatia mashaka sana.
Mheshimiwa Spika, katika kitabu cha bajeti kitengo hiki hakijatengewa fedha yoyote. Hivyo ni dhahiri kabisa utendaji kazi au utekelezaji wa shughuli za kitengo hiki ni wa kusuasua kutokana na uhaba wa fedha. Tukumbuke kuwa nchi hii ina maeneo ambayo hayafifiki kwa uraisi kule kwenye halmashauri na hivyo kupelekeza mashaka katika utekelezaji wa azma ya serikali
Mheshimiwa Spika, mwaka jana 2017, Kambi Rasmi ya Upinzani ilizungumzia kwa kina tatizo kubwa la udumavu nchini. Tatizo hili lina athari kubwa sana kwa taifa kwani kwa kadiri ongezeko la watoto wenye udumavu nchini linafumbiwa macho ndivyo hivyo taifa hili linavyozidi kuzalisha watoto wasio na uwezo wa kujifunza darasani na wasio na uwezo wa ung’amuzi wa mambo (reasoning ability) yaani ‘vilaza au mbumbumbu’. Kwa mujibu wa utafiti wa REPOA wa mwaka 2014 takribani watoto milioni 2.4 nchini walikuwa na tatizo la udumavu. Hali hii inatishasana na inazidi kukua kutokana na ukweli kwamba siku hizi watoto wengi mashuleni hawapati lishe kutokana na serikali kupiga marufuku michango mashuleni na huku ikijua wazi haina uwezo wakugawa vyakula mashuleni. Jambo hili linazidi kuhatarisha zaidi afya za watoto hususani wale wanaotoka katika kaya maskini ambapo watoto walitegemea kula mlo mmoja tu shuleni kwa kuwa familia zao wanashindwa kupata angalau milo miwili kwa siku.
Mheshimiwa Spika, tatizo hili la udumavu lina athari za muda mfupi na zile za muda mrefu. Hata kama mtoto aliathirika na udumavu utotoni athari zake zinaweza kuonekana pale anapokuwa mtu mzima. Tatizo hili huonekana pia sio katika elimu pekee bali pia katika uwezo wa kawaida wa ubunifu na ufikiri wa hali ya juu. Jambohili linajidhihirisha wazi kwani katika mkutano wa wafanyabiashara na Rais uliofanyika Ikulu Mwezi Machi 2018 mmoja wa wafanyabiashara alilalamikia uwepo wa waajiriwa wenye Shahada ya pili (Masters) lakini hawawezi kuandika barua za kitaalamu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia nukuu iliyoitoa katika hotuba yake ya Afya kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 iliyosema “Hatuwezi kupata viongozi wa serikali wenye uwezo mkubwa wa kutafuta suluhu ya matatizo yanayolikabili Taifa kama utotoni waliwahi kuugua tatizo la udumavu au hawakupata lishe bora, kamwe hatuwezi kutengeneza think tank ya taifa kama taifa limejaa watoto wenye udumavu au walioathirika na udumavu utotoni.”Udumavu hudumaza akili, husababisha ubongo wa mtoto au mtu mzima kushindwa kufanya kazi kwa haraka na kwa ufasaha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, kitendo cha wizara kushindwa kutoa fedha katika kitengo hiki cha lishe maana yake ni kuwa tutakuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaougua minyoo au walioathirika na minyoo jambo ambalo ni hatari sana kwani wapo minyoo ambao huathiri ubongo na uwezo wa kufikiri wa mtoto.
Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni nini hasa kinachosababisha kitengo hiki muhimu kushindwa kutengewa fedha hata kidogo huku serikali ikijigamba kuongeza makusanyo? Tunakumbuka katika serikali zilizopita kitengo hiki hakikuwahi kukosa fedha hata kidogo. Tafiti za magonjwa yatokanayo na lishe zinaweza vipi kufanyika endapo kitengo hiki muhimu kinakosa fedha. Je, serikali hii ya awamu ya tano ina mkakati gani wa kupunguza tatizo la idadi kubwa ya watoto walio katika hatari ya kuwa ‘vilaza’ kutokana na ukosefu wa lishe bora ikiwa kitengo muhimu kinachohusika na utatuzi wa tatizo kiko taabani kwa ukosefu wa fedha?.
MASUALA YA HAKI ZA WATOTO
Mheshimiwa Spika,sote tunatambua kwamba; mwaka 2009 serikali ilipitisha sheria ya kulinda haki za watoto (Law of the Child Act 2009). Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inalinda uhai, utu na heshima ya mtoto. Mnamo Mwezi huu wa Aprili Mwaka huu wa 2018; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliwaita kina mama wote ambao wametelekezwa na wazazi wenza katika malezi ya watoto ili ofisi yake iwapatie msaadda wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, Kitendo alichokifanya Mkuu huyo wa Mkoa kilikiuka kwa kiwango kikubwa haki za watoto. Pamoja na kwamba pengine Mkuu wa Mkoa hakuwa na utaalamu wa masuala ya haki za Watoto, lakini ilikuwa ni muhimu sana wito huo uwe na tahadhari ya kulinda haki za watoto; kwa kuhakikisha watoto hao wanalindwa dhidi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Matumizi mabaya ya picha za watoto hao kwenye mitandao yana athari mbaya za kisaikolojia kwao kwa siku za baadae. Kimsingi kitendo hicho ni kinyume kabisa na Mkataba wa kimataifa wa kilinda haki za watoto (Child rights Conventions ) na ni kinyume na Sheria za haki za watoto.
Mheshimiwa Spika,Sheria zinatambua kuwa mambo ya kifamilia hususani migogoro inayohusu watoto hutatuliwa katika njia za kisheria na njia ambazo ni faragha ili kumlinda mtoto. Vilevile katika taratibu za mila na desturi zetu tunatambua kwamba migogoro ya kifamilia inaposhindikana katika ngazi za familia basi tuna ofisi za maafisa ustawi wa jamii ambao kimsingi ndio waliokabidhiwa kushughulikia migogoro hiyo na pale inaposhindikana sheria zaidi huchukua mkondo wake.
Mheshimiwa Spika, masuala yoyote yanayohusu kulinda haki na utu wa mtoto yasichukuliwe kisiasa hata kidogo kwani madhara yake ni makubwa kwa watoto. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka viongozi wa kisiasa kufuata sheria za nchi zilizopo na sio kujiamulia mambo kwa utashi wao binafsi. Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea na itazidi kukemea tabia hizi zisizo za kistaarabu zinazoendelea kushamiri kila uchwao ambapo baadhi ya wanasiasa wanadhani wao wako juu ya sheria. Tuna wajibu wa kutengeneza taasisi Imara ndani ya nchi yetu na sio kumtengeza mtu kwani kwa kufanya hivyo tunaathiri mifumo mingi ya utoaji haki na utendaji kazi serikalini. Tuziachie taasisi zifanye kazi yake.
Mheshimiwa Spika, Mwezi huu wa AprilI, 2018 pametokea kifo cha mtoto wa miezi sita kwa jina la Halfani Lema ambaye alikuwa mkazi wa Ibanda Kata ya Nyegezi jijini Mwanza. Mtoto huyo alifariki saa chache baada ya mama yake kuachiwa kutoka kituo cha Polisi cha Igogo Nyegezi. Mtoto Halfani aliingia mahabusu na mama yake akiwa mzima na baada ya siku mbili alitoka akiwa na hali mbaya sana iliyopelekea umauti wake. Pamoja na kuwa mama huyo alitoa taarifa ya kubadilika kwa hali ya afya ya mtoto wake lakini polisi hawakujali.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kumuweka mama huyu mahabusu na mtoto mchanga, na hata alipoomba apewe ruhusu ya kumpeleka mwanaye hospitali alikataliwa mpaka hali ilipokuwa mbaya na kupelekea kifo cha mtoto huyo kutokea ni kitendo cha kinyama na kilaaniwe na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema. Uhai ni mali. Uhai wa mtoto ni maandalio ya nguvu kazi ya taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na unyama mkubwa unaofanywa na baadhi ya askari wasio waadilifu; tutakumbuka mnamo tarehe 16/02/2018 Jijini Dar es Salaam palitokea kifo cha binti mdogo Akwilina Akwilini ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) . Katika moja ya Agenda ya Mendeleo Endelevu 2030; ni kumsaidia mwanamke kufikia malengo ya 50-50 ya usawa wa kijinsia. Kupotea kwa uhai wa mwanamke mmoja au binti mmoja ni kukwamisha jitihada za kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Spika, Akwilina alikuwa ni binti mdogo aliyetarajia kupata mafanikio katika elimu yake, atoe mchango kwa nchi yake na zaidi pangine awe mama mwenye familia yake. Lakini kutokana na udhalimu na matumizi ya nguvu na ukatili unaoshamiri nchini kila uchwao hasa katika serikali hii ya awamu ya tano ndoto za mtoto Akwilina zilizimishwa kama mshumaa.
Mheshimiwa Spika, Lengo namba 5 kati ya malengo 17 ya Maendeleo Endelevu; ni kukomesha ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Kwa muktadha wa Tanzania, lengo hili limeshindwa kufikiwa kutokana na Serikali hii kuendelea kufumbia macho matendo ya kikatili na unyama dhidi ya binadamu. Kwa kuwa Akwilina alikuwa ni binti, mtoto,na mwanamke mwenye ndoto na zaidi ya yote ni msichana aliyejitahidi kujielimisha kwa kadri ya uwezo wake; basi hatuna budi kama Taifa; kuungana kupinga vitendo hivi viovu dhidi ya taifa letu ambalo lilijipambanua mbele ya mataifa mengine kama kisiwa cha amani.
Mheshimiwa Spika,Ili kukomesha matukio ya vifo kwa watoto vinavyosababishwa na uzembe au ukatili wa baadhi ya watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kulinda maisha ya watu na mali zao; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili; ni hatua gani ilizochukua dhidi ya waliohusika kusababisha vifo vya watoto; Halfan ambaye mama yake alinyimwa ruhusa na Polisi kumpeleka hospitali, Akwilina Akwilini aliyepigwa risasi na Polisi; pamoja na mtoto wa miaka 17 aliyejulikana kwa jina la Allen Mapunda aliyepigwa na polisi mpaka kufa.
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara hii; kwamiaka miwili mfululizo, imezungumzia kushamiri kwa ugonjwa wa akili nchini. Katika hotuba ya mwaka wafedha 2017/2018 tulionyesha kwamba takribani watu 150-200 huhudhuria kliniki kwenye hospitali zinazotoa huduma kwa watu wenye matatizo ya akili kwa wiki kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee. Idadi hii ni kubwa mno!!!
Mheshimiwa Spika,pamoja na kwamba jambo hili linaonekana kupuuzwa na kutotiliwa mkazo na Wizara pamoja na wadau mbalimbali nchini vikiwemo vyombo vya habari, ni muhimu serikali hii ikatambua kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya kujiua, kuuana ndani ya familia, watu kutembea wakizungumza wenyewe barabarani n.k . Hali hii pengine inaweza kuchangiwa na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku pamoja na matukio yake hali inayopeleka watu wengi kuwa na wasiwasina hofu za maisha.
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani tulikwenda mbali zaidi kueleza idadi ya madaktari ambao ni wataalamu wa magonjwa ya haya ya akili. Ambapo mpaka mwaka jana 2017; idadi ya madaktari hao walikuwa 26 tu kwa nchi nzima, huku hospitali Kuu ya Magonjwa ya akili Dodoma ikiwa na madaktari 5 tu.
Mheshimiwa Spika, hali ya hofu isiyo na kikomo huathiri zaidi uwezo wa mtu katika kufikiri na baadae huweza kuleta matatizo makubwa zaidi. Katika maadhimisho ya siku ya Afya ya Akili Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 10 ya mwezi Octoba kila mwaka, kwa mwaka 2017, kauli mbiu ilikuwa Afya ya Akili Mahali pa Kazi.
Mheshimiwa Spika, magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri au yanapeleka mabadiliko katika kufikiri,kuhisi,kutambua na kutenda mambo.Hata hivyo mabadiliko ya kitabia au mwenendo wamtu huweza kuwa wa tofauti na usioendana na mwenendo wa jamii husika, mila au kidenturi. Magonjwa ya akili huathiri ufanisi wa utendaji kazi, na hivyo husababisha migogoro, na kuathiri uhusiano wa mtu husika na kuathiri jamii nzima inayomzunguka. Ni vyema pia jamii ikatambua matatizo ya afya ya akili hayaathiri watu maskini peke yao, bali pia hata viongozi. Tatizo hili lisipotafutiwa ufumbuvulinaweza kuleta athari kubwa hasa kwa watu walio katika ngazi za maamuzi (decision making)
Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua je, kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi katika vitengo vya afya nchini, serikali ina mkakati gani mahususi wa kuongeza rasilimali watu katika hospitali na vitengo vinavyoshughulikia matatizo ya Afya ya akili?Je, serikali inampango gani kupunguza matatizo ya afya ya akili mahali pa kazi na kuielisha jamii kwa ujumla kuhusiana na matatizo ya afya ya akili ili kupunguza athari za matatizo yanayotokana na changamoto za kimaisha hususani hali ngumu ya maisha, madeni, unyapaa au kubaguliwakatika familia au jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia isiyoridhisha ndani ya Wizara ikiwemo Wizara ya Afya katika matumizi ya fedha mbalimbali zinazotengwa kwa shughuli za maendeleo ndani ya Wizara. Ushahidi wa tabia hii isiyoridhisha katika utendaji na usimamizi wa fedha za serikali umejidhihirisha katika kitabu cha Randama Fungu 52 ukurasa wa 184.
Mheshimiwa Spika, Katika ukurasa huo, unaibua maswali ya matumizi ya fedha zilizotengwa kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa Miundombinu ya vitengo vya dharura (emergency unit) katika hospitali za Rufaa za Mikoa. Lakini cha kushangaza hakuna mchanganuo ya mgawanyo kwa kila hospitali kama zilivyoanishwa. . Kwa mujibu wa Randama mikoa iliyojumuishwa katika mgao huo ni pamoja na mikoa ya Katavi, Njombe, Geita,Chato, Simiyu, Songwe na Mara
Mheshimiwa Spika,kwa uzoefu wa ni kuwa fedha nyingi hupotea serikalini kwa kukosa mchanganuo wa mgawanyo wa fedha au fedha kutumika vibaya au kwa upendeleo katika maeneo fulani. Vitabu hivi vya randama ndivyo hasa hutumiwa na Bunge lako kujua mgawanyo na matumizi ya fedha na hivyo kuwapa hoja Waheshimiwa Wabunge pale wanapozungumzia masuala mbalimbali katika majimbo yao kujua ni kiasi gani cha fedha kimetengwa katika maeneo yao. Kutenga fedha kiujumla katika miradi isiyo ya ujumla (in a blanket form) mara nyingi hakutoi fursa wa kuhoji na pia huwanyima haki wananchi kujua maeneo yao yametengewa kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa kuona Wilaya ya Chato ikiwa miongoni mwa maeneo yanayotajwa kama mkoa tena wenye hospitali za Rufaa.Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua nilini hasa serikali hii ya awamu ya tano ilitangaza au kuidhinisha Chato kuwa Mkoa. Je, tangazo la kuutangaza mkoa wa Chato ulitangazwa katika gazeti la serikali namba ngapi?
Pensheni wa wazee
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Wazee ndani ya taifa hili wamekuwa na kilio kilichoshindwa kupata suluhu katika awamu zote za utawala wa Chama cha Mapinduzi.Ni masikitiko kuona watu waliolitumikia taifa kwa nguvu zao zote wakipata manyanyaso makubwa katika nyakati ambazo nguvu zao zinakwenda zikiisha.
Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kijana wa leo ni mzee wa kesho na hivyo hatuna budi kuwajali wazee wetu na kuhakikisha wanaishi maisha ya furaha baada ya kustaafu. Pamoja na malalamiko ya muda mrefu ya Wazee yaliyotokana na sheria kandamizi mfano; sheria ile ya kikoloni iliyojulikana kama “ The Pensions Ordinance of 1954”iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 1999 na baada ya hapo ikatungwa sheria nyingine iliyojulikana kama ‘The Public Service Retirement Act ya mwaka 1999’iliyoanza kutumika kuanzi tarehe 01Julai, 1999. Pamoja na sheria hiyo ilienda sambamba na sheria ya ‘The Political Pensions Act No 3 ya mwaka 1999’ ambayo nayo iliwalenga watumishi wenye nafasi za kisiasa.
Mheshimiwa Spika, tunatambua moja ya ajenda kuu ya serikali ya awamu ya nne kwa wazee ilikuwa ni kuandaa mfumo wa pensheni kwa wazee wote yaani ‘universal pension’.Katika mijadala mbalimbali ya kitaifa iliyohusu haki za Wazee iliwagawa wazee katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni wazee waliokuwa wakifanya kazi katika mfumo rasmi na kundi la pili ni lile ambalo linajumuisha takribani asilimia 94 ya wazee wote walio katika mfumo usio rasmi. Kundi hili linahusisha asilimia kubwa ya wazee waishio vijijini wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, mafundi mchundo, wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mama lishe, n.k
Mheshimiwa Spika, pamoja na makundi hayo wazee waliokuwa katika mfumo rasmi nao wamegawanyika. Wapo wazee waliofanya kazi kwa mikataba (On contract basis) wapo wazee ambao waliajiriwa na serikali kwa muda mfupi tu (Temporary terms) na wapo wazee ambao walioajiriwa kwa masharti ya kudumu (Permanent and pensionable terms).
Mheshimiwa Spika, pamoja na ahadi hiyo ya uongozi wa awamu ya nne utawala huu wa serikali ya awamu ya tano uliwahi kuzungumzia kuleta Bungeni Sheria ya Wazee. Tutakumbuka mwaka 2016, tarehe 29 April aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya alizungumzia kuanzishwa kwa sheria ya Wazee ili kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wazee. Jambo hili pia limezungumzwa pia mara nyingi na Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuwa Kambi inaamini Wazee ni hazina ya taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika randama za Wizara ya Afya hakuna kipengele kinachozungumzia ahadi ya uwepo wa Pensheni ya wazee wote kama serikali ya chama cha mapinduzi kilivyowaahidi wazee hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua je, serikali hii ya awamu ya tano imeifuta rasmi hoja ya kuanzisha malipo ya pensheni kwa wazee wote? Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua mchakato wa kuileta Muswada wa Sheria ya Wazee Bungeni umefikia wapi ili kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili wazee zinatatuliwa. Pamoja na hayo serikali ione umuhimu wa kuanzisha chombo kitakachowaleta wazee pamoja kama chombo cha kuwasema na kutetea maslahi yao kama vilivyo vyombo vingine vilivyoanzishwa kutetea maslahi ya kada mbalimbali.
HALIYA MAAMBUKIZI VVU NA UKIMWI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mapema mwezi Machi mwaka huu wa 2018, tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) ilitoa ripoti yake kuhusu maambuzi mapya ya VVU nchini. Katika ripoti yake ilibaini kuwa takribani Watanzania 225 huambukizwa virusi vya UKIMWI kwa siku. Huku Watanzania takribani 6,750 huambukizwa kwa mwezi na kwa mwaka takribani watu 82,125 huambukizwa virusi vya Ukimwi. Katika ripoti hiyo maambukizi makubwa yalionekana kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-24 na wengi wao wakiwa ni vijana wa kike. Kwa mujibu wa tume ya taifa ya takwimu(NBS) mpaka 2017 takribani watu milioni 1.4 walikutwa na maambukizi ya Ukimwi[27]. Hii inaonyesha ongezeko la maambukizi tofauti na tafiti zilizofanyika mwaka 2010-2015 ambapo maambukizi yalipungua kwa asilimia 20 (UNAIDS 2017).[28]
Mheshimiwa Spika, hali hii inatisha sana hasa tukizingatia kuwa maambuzi kwa vijana hawa wadogo ni asilimia 40. Wengi wa vijana hawa ni wale wenye umri wa kumaliza shule ya msingi mpaka chuo kikuu. Maana yake ni kuwa nguvu kazi ya taifa inapungua kwa kasi sana na pengine tatizo hili lisipochukuliwa kwa uzito mkubwa pengine miaka kadhaa mbele tutakakosa kabisa vijana wenye afya bora wa kulijenga taifa letu.
Mheshimiwa Spika,kuna haja sasa kuwekeza nguvu zaidi katika njia za kuzuia maambukizi mapya badala ya kutenga fedha nyingi katika kutibu magonjwa nyemelezi. Kwani kinga ni bora kuliko tiba. Ni muhimu kufanya tafiti zenye tija ili kuweza kubaini sababu zinazopeleka maambuzi makubwa kwa vijana wenye umri huu mdogo tofauti na miaka ya nyuma ambapo vijana wenye umri wa kati kuanzia miaka 35-49 ndio waliobainika kuathirika zaidi.
Mheshimiwa Spika, kubadilika kwa mfumo wa maisha, hali ngumu sana ya uchumi ambapo kwa sasa vijana hutumia lugha isiyo rasmi kuwa ‘vyuma vimekaza’, kupungua kwa jitihada za kupaza sauti na elimu ya juu ya masuala ya Ukimwi, ongezeko la ngono zembe napengine changamoto za upatikaji wa dawa za kufubaza virusi zinaweza kuwa miongoni mwa sababu za maambukizi makubwa na ya kutisha kwa vijana hawa wadogo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo pameibuka wimbi kubwa la ulawiti wa watoto hasa wa kiume. Jambo hili sio la kufumbia macho hata kidogo. Serikali na wadau mbalimbali lazima tuungane kukemea vitendo hivi viovu wanavyofanyiwa watoto. Japokuwa mambo haya huchukuliwa pia kwa usiri mkubwa kutokana na mila na desturi zetu lakini hatuna budi kama taifa kuanza kukemea hadharani mambo haya. Vitendo vya ushoga navyo vimeshamiri jambo ambalo linachochea kwa kasi maambuzi mapya ya virusi vya Ukimwi[29]
Mheshimiwa Spika,vilevile pamekuwa na malalamiko kwenye jamii juu ya uwepo wa takwimu zinazotolewa zisizo za kweli kuhusu maambukizi kwa sababu za kujipatia fedha kutoka kwa wafadhili. Takwimu za maambukizi zinatumiwa kama sehemu ya ‘miradi ya upigaji’. Novemba 28, Mwaka 2017Waziri Mkuu aliitoa kauli ya kukemea matumizi mabaya ya fedha za miradi ikiwemo miradi ya UKIMWI jambo ambalo linaonyesha dhahiri fedha nyingi za serikali zinazotengwa katika kupambana na janga la UKIMWI zinatumiwa kinyume na mpango wa matumizi na hivyo kuathiri juhudi za kupambana na janga hili.
Mheshimiwa Spika,kwa mwaka huu wa fedha takribani bilioni 84.9 zimetengwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi. Fedha hizi ni nyingi sana na hivyo ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe sasa ili kupunguza tatizo hili la sivyo, bajeti kubwa ya serikali itaendelea kutumika katika kupambana na ugonjwa huu bila mafanikio. Katika hotuba ya Waziri Mkuu aliyoitoa akifungua kongamano la kitaifa la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani Jijini Dar es Salaam alitoa kauli ya maazimio ya kumaliza tatizo la Ukimwi nchini ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika,Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali iliambie Bunge lako; ina mikakati gani ya kumaliza tatizo hili mpaka mwaka 2030 iwapo kasi ya maambuki kwa vijana wadogo inaongezeka, upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi ni wa kusuasua na maeneo mengi nchini hayapati dawa kwa wakati. Serikali ituambie ni nini mkakati wake katika kukabiliana na ongezeko kubwa la vitendo vya ulawiti na ushoga nchini ambapo tafiti mbalimbali zinaonyesha maambuzi ni makubwa zaidi hasa kwa wanaume wanaoshiriki ngono za jinsia moja (MSM).
JUKUMU LA SERIKALI KATIKA KUWASAIDIA WATOTO WA KIKE MASHULENI
Mheshimiwa Spika,katika lengo namba nne la Mendeleo Endelevu (SDG’s) linasema “Achieving inclusive and equitable quality education for all”na katika lengo namba tano linasema “Achieving gender equality and empower all women and girls”.Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kuwa malengo haya mawili yanaitaka serikalikuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote kwa kuzingatia jinsia katika kupata elimu bora huku watoto wa kike wakipewa kipaumbele kutokana na changamoto kubwa za kiafya zinazo wakabili ikiwa ni pamoja na changamoto za kibaiolojia naza kimazingira.
Mheshimiwa Spika, katika harakati za kumsaidia mtoto wa kike katika kupambana na ujinga,umaskini na maradhi ni pamoja na kutatua changamoto anazokumbana nazo kila siku katika jitihada zake za kujiletea maendeleo. Ni hivi karibuni ndani ya Bunge lako Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza alileta hoja ya kuitaka serikali kuanza kugawa taulo za kike mashuleni ili kunusuru afya za watoto wengi wa kike ambazo zipo hatarini kutokana na kukosa taulo safi za kujihifadhi wakati wa hedhi.
Mheshimiwa Spika, katika tafiti mbalimbali zinaonyesha ukosefu za taulo safi za kike kwa watoto wa kike mashuleni imekuwa ni miongoni mwa sababu za watoto wa kike kushindwa kuendelea na masomo,kukosa ufaulu mzuri na hata chanzo cha matatizo mengi ya uzazi na kansa. Ni dhahiri kabisa afya za watoto wa kike hususani maeneo ya vijijini yako hatarini kutokana na mifumo mibovu na mazingira duni yanayowafanya watoto wa kike wawapo katika siku zao kushindwa kuhudhuria masomo[30]
Mheshimiwa Spika, shule nyingi nchini hazina vyoo vya kutosha na hata vilivyopo havina mazingira mazuri kwa mabinti kubadili taulo zao wakati wa hedhi.Hivyo wengi huzitupa hovyo na wengine kulazimika kukaa nazo muda mrefu jambo linaloathiri afya zao.[31]
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta alisaini sheria ya marekebisho ya sheria ya elimu ya msingi,kuweka wajibu wa kutoa taulo za usafi (pads) za kutosha na zenye ubora kwa kila mtoto msichana aliyesajiliwa na kujiandikisha katika taasis ya elimu ya msingi ya umma. Hii ni kuonyesha kuwa serikali ya Kenya imejizaatiti kwa vitendo katika kumsaidia mtoto wa kike na sio maneno matupu.
Mheshimiwa Spika, inashangaza sana kuona pamoja na jitihada mbalimbali za wadau na sekta binafsi serikali hii ya awamu ya tano imekuwa mstari wa mbele katika kukwamisha jitihada za mtoto wa kike katika kujikwamua kwenye lindi la ujinga na maradhi yanayozidi kuwatesa wanawake kila kukicha. Serikali hii ya hapa kazi tu imekuwa mzigo mzito kwa watoto wa kike kwani haki zao nyingi zimekuwa zikivunjwa bila kuangalia athari za muda mrefu (long term impact). Kwa mfano, kitendo cha kukwepa au‘kupotezea’mjadala mzito wa kugawa taulo kwa watoto wa kike maana yake ni kutaka watoto wa kike wa taifa hili wazidi kudhalilika na kuathirika kiafya na kielimu. Na sio hivyo tu, wengine hujikuta katika matatizo ya kupata ujauzito kutokana na kurubuniwa wakati wakitafuta fedha za kununulia taulo (pads )nyakati za hedhi ili kukwepa fedheha. Na hivyo watoto hawa hujikuta kwenye matatizo makubwa zaidi ikiwemo kufukuzwa masomo. Jambo hilo linazidi kuwazamisha katika lindi la umaskini,ujinga na maradhi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali hii kuacha ‘hadaa’ na ‘kuwanyanyapaa’ watoto wa kike kwa kuwa elimu na afya bora kwa mtoto wa kike ni msingi wa kuzalisha taifa bora la baadae. Mama borawa leo huleta mtoto mwenye matumaini ya kesho. Bila kuwekeza kwa mtoto wa kike hatuwezi kamwe kupata viongozi bora,madaktari,walimu,makandarasi,wanasheria n.k wenye weledi katika kujenga kesho ya taifa letu.
BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019
Mheshimiwa Spika, sote tunatambua umuhimu wa sekta ya afya katika maendeleo ya Taifa. Hakuna na wala hakutakuwepo kamwe Tanzania ya viwanda pasipo kuwa na taifa la watu wenye afya bora. Nguvu kazi ya taifa lolote duniani ni uwepo wa watu wenye afya bora ya mwili na akili. Ni jambo la kushangaza sana kuona zaidi ya asilimia 71 ya bajeti ya afya iliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2017/18; ilitegemea wahisani huku fedha za ndani ikiwa ni asilimia 19 tu. Hii maana yake ni kuwa asilimia 71 ya maisha ya Watanzania imewekwa rehani kwa wahisani.
Mheshimiwa Spika,kimsingi majigambo ya Serikali kwamba imeboresha sekta ya afya nchini ni katika kujitafutia umaarufu wa kisiasa tu. Hii ni kwa sababu bajeti ya afya kwa mwaka mpya wa fedha 2018/19 imepugua kutoka shilingi trilini 1. 07 kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia shilingi bilioni 866.233[32] kwa mwaka 2018/19 ikiwa ni punguzo la shilingi bilioni 211.468.
Mheshimiwa Spika, hili ni anguko la asilimia 19.622 la bajeti ya Wizara ya afya. Na kama ilivyo kawaida ya Serikali hii kutokeleza bajeti inayoidhinishwa na Bunge, hatuna imani pia kama fedha hii pamoja na upungufu wake kama itatolewa yote.
Mheshimiwa Spika, huu ni ushahidi wa wazi kwamba sasa afya si kiupaumbele tena cha Serikali hii ya awamu tano jambo ambalo ni hatari kwa afya za watanzania na ukuaji wa uchumi wa taifa ambao hutegemea nguvu kazi yenye afya.
Mheshimiwa Spika, upungufu huu wa bajeti ya afya hauendani kabisa na ongezeko la watu ambao pia hupelekea ongezeko la watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya. Aidha, bajeti hii haiakisi haja ya kufanya tafiti mbalimbali juu ya magonjwa mapya yanayoibuka mara kwa mara. Sekta ya Afya ina changamoto nyingi ambazo huongezeka siku hadi siku. Kitendo cha kupunguza bajeti ya afya hakuendani na kuongezeka kwa changamoto hizo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu katika Miji mikubwa nchini hasa kwa Jiji la Dar es Salaam ambapo ongezeko hilo linaenda sambamba na mahitaji makubwa ya nyumba za kuishi, ofisi za biashara mbalimbali, maduka makubwa pamoja na Hoteli. Taarifa zinaonyesha kuwa kwa nchi nzima kuna mahitaji ya nyumba 200,000.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa sekta ya nyumba hasa majengo makubwa ya biashara inapitia katika changamoto kubwa sana kutokana kuyumba kwa uchumi na biashara nyingi kufungwa, inakadiriwa kuwa kwa sasa kuna mita za mraba 300,000 ambazo ziko wazi hazina wapangaji. Wapangaji wengi wameshindwa kuhimili bei za majengo makubwa ambazo zilikuwa zinatozwa kwa dola[33].
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuporomoka na kuyumba kwa uchumi, inakadiriwa kuwa kwa sasa ni 35% hadi 45% ya majengo makubwa ya kibiashara na maduka yana wapangaji. Hii sio ishara njema kwa sekta ambayo imekua kwa mfululilo kwa miaka saba iliyopita. Tafsiri pana ya anguko hili ni kuwa serikali itakosa mapato kwa sababu biashara zinafungwa na pia kutakuwa na ongezeko la mikopo ya nyumba isiyolipika (mikopo chechefu) jambo ambalo litaathiri pia sekta ya fedha kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 sekta ya majengo ilikadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1 ambapo mpaka mwaka 2014 sekta hiyo ilikuwa mpaka dola 1.8 bilioni sawa na 3.7% ya pato la taifa ambapo ni ongezeko la 63%.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Bunge kuchukua hatua za haraka kuokoa sekta ya majengo nchini ambapo imefikia hatua waliokuwa wanaendesha biashara zao katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam wameamua kuhamishia shughuli zao katika maeneo ya makazi ambapo gharama za kupangisha ni ndogo ukilinganisha na gharama za majengo makubwa katikati ya Jiji.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa Bunge la kumi mwaka 2011 tulipendekeza na kuishauri serikali kuleta Bungeni muswada wa kuanzisha mamlaka ya kusimamia sekta ya majengo makubwa (The Real Estate Regulatory Authority Bill) ambapo leo ni miaka saba toka ushauri huo utolewe na serikali kuahidi kuleta muswada lakini bado hoja hiyo haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, katika randama ya Wizara serikali imesema kuwa muswada kwa ajili ya kuanzisha mamlaka ya majengo nchini upo katika hatua za mwisho na umekabidhiwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali jambo ambalo ni kinyume na ahadi ya serikali katika randama za Wizara kwa mwaka 2016/2017 ambapo serikali ilisema kuwa muswada huo umekamilika.
Mheshimiwa Spika, ni vema sekta ya nyumba ikasimamiwa kwa sababu pamoja na tatizo la anguko la uchumi bado sekta hiyo ilikuwa inakabiliwa na kupandisha hovyo kwa bei ya kupangisha kwenye majengo makubwa pamoja na matumizi ya dola jambo ambalo limeendelea kuathiri shilingi yetu.
Mheshimiwa Spika, tunataka kauli ya Waziri kuhusu hatua ambazo serikali itazichukua kuokoa sekta ya nyumba nchini kwa sababu kuyumba kwa sekta hii muhimu kunaenda sambamba na kuathiri sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla. Aidha, kwa sababu serikali haioni umuhimu wa kutafuta suluhisho la jambo hili ni vema Bunge likaingilia kati kwa kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi na kulishauri Bunge hatua ambazo serikali itatakiwa kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, tafiti zinaonyesha kuwa 62.5% ya wakazi wote wa mijini wanaishi kwenye makazi yasiyokuwa rasmi[34] na 37.5 % pekee ndio wanaishi kwenye makazi katika maeneo ambayo yamepimwa. Sababu kubwa ya wakazi wa mijini kuishi kwenye maeneo ambayo sio rasmi inatokana na gharama kubwa za kupanga au kujenga kwenye maeneo rasmi ambayo yamekwisha kupimwa.
Mheshimiwa Spika, Aidha kwa mujibu wa sensa ya watu kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu kutoka milioni 22 mwaka 1988 hadi milioni 52 kwa mwaka 2014. Ongezeko hili limekua kichocheo cha mahitaji na ushindani mkubwa kwenye ardhi hasa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na makazi.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa pia migogoro ya muda mrefu kati ya serikali na wananchi au kati ya wananchi na wawekezaji ambao wamepewa ardhi kwa ajili ya kuendeleza. Migogoro hii imetokana hasa na namna serikali inavyotwaa ardhi bila kulipa fidia stahiki na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, masuala yote haya sio mageni kwa serikali kwa sababu taasisi za serikali zenyewe pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yameshafanya utafiti wa kina juu ya changamoto ya makazi holela katika maeneo mbalimbali nchini. Katika jambo la kushangaza ni kuwa ni serikali ya CCM ambayo imekua ikilea mambo haya bila ya kuyafanyia kazi kwa manufaa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, mpaka Juni mwaka 2015, takwimu zilikuwa zinaonyesha kuwa ardhi ya jumla (General Land) mbayo ilikuwa imepimwa ilikuwa na jumla viwanja milioni 1.6 na mashamba ambayo yalisajiliwa kwa hati yalikuwa 23,000 pekee na pia leseni za makazi zilikuwa ni jumla ya 379,000. Kwa maana hiyo inakisiwa kuwa ni 10% pekee ya ardhi ya jumla ambayo imepimwa[35].
Mheshimiwa Spika, Kwa tafsiri ya moja kwa moja ni kuwa katika nchi yetu takribani 90% ya ardhi ya jumla haijapimwa na hivyo haijatolewa kisheria na kumilikishwa kwa wananchi. Jambo hili sio la kujivunia kwa sababu ardhi ni urithi wa wananchi na pia ikitumika vizuri ni rasilimali ambayo inaweza kuwa na tija kwa wananchi kiuchumi kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kuwa ardhi ya jumla haijapimwa kwa 90% Wizara katika randama wanaonyesha kuwa wanatekeleza mradi wa kupima ardhi ya Kijiji katika Wilaya za Ulanga na Malinyi. Ni jambo jema lakini vema serikali ikaja na mkakati wenye mashiko na wenye kasi stahiki wa kuhakikisha kuwa ardhi ya jumla inapimwa na kumilikishwa ili kuepuka majanga yanayotokana na makazi ya wananchi hasa kwenye Miji na Majiji kutokupimwa.
Mheshimiwa Spika, Jiji la Dar es Salaam limekuwa likikumbwa na mafuriko ambayo yamekuwa yakileta majanga kwa miaka mingi sasa. Aidha serikali haijaweka wazi kuhusu uwepo au kutokuwepo kwa mpango mkuu (Master Plan) wa matumizi na uendelezaji wa ardhi katika Jiji. Jambo ambalo linasababisha watu kuendelea kujenga na kuanzisha miji mingine nje ya Jiji ambayo haijapangwa wa kuratibiwa na mamlaka husika.
Mheshimiwa Spika, Aidha serikali imekuwa na maamuzi ya kisiasa zaidi kuliko kutegemea ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kupunguza msongamano pamoja na kupanga makazi ya wakazi wa Jiji. Mathalani serikali iliwahamisha kwa nguvu wakazi wa Mkwajuni na Jangwani na kwa kubomoa makazi yao lakini ni serikali hiyo hiyo ambayo imewaruhusu kampuni ya Mabasi “yanayokwenda kasi” (UDART) kujenga kituo cha maegesho Jangwani huku wakijua ile ni sehemu ambayo maji ya Bonde la Msimbazi hukusanyika pale kuelekea Baharini.
Mheshimiwa Spika, Vilevile Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga daraja kutoka Ocean Road hadi Coco Beach, ukweli ni kwamba ujenzi wa daraja hili hautagusa wananchi wengi zaidi ya upendeleo wa viongozi wa serikali ambao wengi wao huishi maeneo hayo. Badala ya kuhakikisha barabara za pembezoni ambazo zingepunguza msongamano au kufikiri kujenga daraja lingine kisasa ambalo lingeunganisha Magomeni na Fire cum Muhimbili ili kuepukana na adha ya kufunga barabara eneo la Jangwani serikali inapanga kutekeleza mradi ambao hauwagusi wananchi waliowengi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwa Bunge kupitia Kamati yake ya Miundombinu au Kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili kuhakikisha kuwa Bunge linakuwa sehemu ya kusimamia Jiji la Dar es Salaam kuepukana na majanga na kuhakikisha kunakuwa na Master Plan ya Jiji ambayo haiwaumizi wananchi na kuhakikisha tunaepukana na majanga ya mafuriko ya mara kwa mara. Tunapendekeza hili kwa sababu inaonekana serikali imeona ni kawaida majanga kujirudia katika Jiji la Dar es Salaam ambapo mara nyingi vifo vimeripotiwa.
Mheshimiwa Spika, Ni vema Bunge likaingilia kati jambo hili kwa sababu serikali pamoja na kushindwa kutafuta suluhisho la kudumu, imeamua kuziua mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzinyang’anya vyanzo vya mapato ambavyo wangevitumia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya mipango ya ardhi nchini. Kwa kuwa serikali kwa makusudi wameamua kuziua halmashauri nchini na kwa kuwa Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi ni vema likachukua hatua ya kuchunguza na kuja na taarifa ambayo serikali italazimika kuitekeleza kuhusu namna ya kuhakikisha tunaepukana na majanga ya mafuriko katika Jiji la Dar es salaam.
Mheshimiwa Spika, Waziri atoe maelezo hapa Bungeni kuhusu mamlaka na maafisa waliohusika kutoa kibali kwa kampuni ya UDART kuruhusiwa kujenga kituo cha maegesho katika eneo la Jangwani huku wananchi wakihamishwa kwa madai kuwa ni eneo hatari kwa makazi. Wananchi wameshuhudia hivi karibuni jinsi eneo hilo la maegesho lilivyokuwa limejaa maji kama Bwawa na serikali kuonekana kutochukua hatua yoyote kuhusu jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali ya ufanisi katika ugawaji wa viwanja nchini ya Machi, 2018 (CAG PERFORMANCE AUDIT REPORT ON THE MANAGEMENT OF PLOTS ALLOCATION) imedhihirisha kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Mamlaka za serikali za Mitaa zimeshindwa kusimamia na kutatua changamoto za umilikishaji wa ardhi kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, changamoto kadhaa zimewekwa bayana ikiwemo uwepo wa uhitaji mkubwa wa viwanja/ardhi kwa wananchi hasa katika mamlaka za Miji kuliko uwezo wa Wizara au Halmashauri kuwa na idadi ya viwanja vinavyotosheleza mahitaji ya wananchi. Vilevile ilidhihirika kuwa Halmashauri hazikuwa na uwezo wa kusimamia vizuri ugawaji wa viwanja ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwa na viwanja ambavyo vinawavutia watu kwa kupimwa kwenye maeneo ambayo huduma za kijamii zimeshapelekwa.
Mheshimiwa Spika, CAG ameeleza pia kuwa bei za maeneo ambayo yalitangazwa kuuzwa zilikuwa kubwa kiasi cha watu wengi kushindwa kugharamia na kukidhi vigezo ili wamilikishwe viwanja. Ni dhahiri kuwa bei za viwanja kwa mita mraba katika maeneo mbalimbali ambayo miradi hiyo inatangazwa ni kuanzia Tshs. 5000 na kuendelea, kulingana na bei hizo sio watu wote watakaokuwa na uwezo wa kumiliki viwanja na wengi wao huamua kutafuta maeneo ya mashamba au yale ambayo sio rasmi na kuamua kujenga makazi.
Mheshimiwa Spika, mathalani kwa Jiji la Dar es Salaam maeneo ya Manzese, Tandale, Mwananyamala, Kigogo, Mburahati, Mabibo, Buguruni n.k ni maeneo ambayo sehemu yake kubwa sio rasmi na wananchi wengi hupenda kuishi huko kutokana na urahisi wa kufika mjini kwenye shughuli zao, masoko ya bidhaa mbalimbali za kuchuuza pamoja na uhusiano wa kijamii. Kambi Rasmi ya Upinzani ingetegemea kuwa Serikali ambayo inaona mbali ingeanza kupima miji ya pembezoni mwa Jiji (Peri-urban) ili kuepuka changamoto za makazi holela za maeneo hayo na kuhakikisha kuwa Miji ya pembezoni inayochipukia inapimwa na kuwekewa miundombinu pamoja na huduma mbalimbali za kijamii. Kwa kuwa ulipaji kodi wa viwanja ambavyo humilikishwa huwa ni jambo linalochukua muda mrefu, jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani haioni sababu ya ulipaji malipo ya awali kuwa makubwa
Mheshimiwa Spika, hilo limeshindikana kwa serikali hii ya CCM na hasa wakati huu wa awamu inayojiita ya “hapa kazi tu” huku changamoto zilezile za makazi holela zikiendelea katika miji mipya ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Miradi mingi ya ugawaji wa viwanja ilikumbwa pia na changamoto ya kukamilika kwa wakati kutokana na kukosekana kwa wataalam pamoja na serikali au mamlaka za serikali za mitaa kushindwa kulipa fidia maeneo ambayo yametwaliwa kwa ajili ya kupimwa. Hali hii pia ilishawahi kujitokeza katika Halmashauri ya Liwale ambapo mwaka 2004 Halmashauri ilitwaa maeneo ya wananchi kwa lengo la kuyapima na kuyarasimisha lakini mradi huo umekuwa kilio kwa wananchi wa pande zote kwa maana ya walioonyesha nia ya kununua ardhi na wale ambao ardhi yao imetwaliwa kwa ajili ya kurasimishwa.
Mheshimiwa Spika, miradi kuchukua muda mrefu bila kukamilika na wananchi kulipwa fidia inajitokeza changamoto ya kutokulipwa fidia shahiki kwa sababu mradi ukikaa muda mrefu thamani ya shilingi nayo inakua chini kwa hiyo inawaathiri wananchi kimaendeleo kwa sababu wanashindwa kujipangia mipango yao kulingana na thamani ya shilingi. Huko Liwale ilifikia hatua hata wale waliokuwa wamelipa fedha kwa ajili ya kupata ardhi walielekezwa waongeze fedha mara tatu zaidi ya ile ambayo ilielekezwa ili kuendana na thamani ya shilingi.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya CAG inaonyesha pia kuwa Wizara imeshindwa kusimamia na kutoa maelekezo kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yenyewe au Halmashauri jambo ambalo linaifanya Wizara kutotoa maelekezo kwa wakati mpaka ifike hatua ya migogoro na wananchi. Tofauti na jinsi ilivyokuwa inategemewa Wizara imejikita kukusanya kodi ya pango la ardhi pekee kuliko kusimamia ugawaji na umilikaji wa ardhi kwa ufanisi ili pia kodi wanayoipigia kelele iweze kukusanywa na kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ambazo zimekuwa zikitekeleza miradi imeonekana kuwa hazina vifaa vya kitaalamu kufanya kazi hiyo. Hii inatokana gharama za vifaa hivyo kuwa kubwa huku bajeti ya kutekeleza kazi hizo ikiwa kidogo na au hata kile kidogo kimekuwa hakitolewi kwa wakati. CAG aligundua kuwa ili uwe na vifaa vizuri kwa ajili ya kupima ardhi gharama zake sio chini ya milioni 50, jambo ambalo Halmashauri nyingi nchini hazina vifaa hivyo na hivyo kushindwa kuwa na ufanisi katika kupima ardhi kwa ajili kumilikisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuu kuchukua jukumu hili la kuhakikisha inatoa ruzuku kwa Halmashauri kwa ajili ya kununua vifaa hivi, pendekezo hili angalau litasaidia ahadi ya CCM ambayo ya kutoa milioni 50 kila Kijiji ambayo imekuwa ahadi hewa hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, Wizara pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI wameonekana kushindwa kuwa na vigezo vya matokeo ya utendaji yanayotegemewa pamoja na mfumo wa kupata taarifa kutoka katika Halmashauri kuhusiana na masuala ya ardhi. Jambo hili pia limesababishwa na kutokuwa na mahusiano ya moja kwa moja na au kuwa utofauti wa taarifa kwa jambo moja. Hali hii inaonyesha udhaifu wa kiutendaji wa serikali pamoja na kuendelea kuchochea migogoro katika sekta ya ardhi. Kama jambo limeamuliwa na mamlaka ya serikali za mitaa alafu Wizara haina taarifa, Wizara nayo inaweza kuja na maamuzi mengine kwa jambo lile lile. Kutokana na hali kuwa hivi ni wazi kuwa migogoro ya ardhi bado itaendelea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri kuhakikisha kuwa inasimamia na kutekeleza ushauri na mapendekezo ya CAG kuhusu changamoto za ugawaji na usimamizi wa ardhi nchi la sivyo ataendelea kuwa Waziri wa kutatua migogoro ya ardhi kila wakati kuliko kuendelea na kazi zingine za Wizara.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imekua ikieleza na kuwasilisha migogoro ya ardhi nchini ambapo inaweza kuwekwa katika makundi kulingana na jinsi inavyoshabihiana na kutokana na pande zinazohusika katika mgogoro au sababu zinazochochea migogoro hiyo.
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni imeibuka migogoro katika ya wananchi na mamlaka za hifadhi ambapo inasemekana wananchi wamevamia hifadhi au hifadhi zimeongeza mipaka yake tofauti na jinsi ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Spika, zipo sababu kadhaa zinazochangia migogoro kati ya mamlaka za hifadhi na wananchi na mojawapo ni Vijiji ambavyo vipo katika hifadhi lakini wakati huo vimesajiliwa na kupewa hati na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inaonyesha kuwa kati ya Vijiji 228 ambavyo vimebainika kuwa vipo katika maeneo ya hifadhi ni Vijiji 157 ambavyo ni takribani 68% vimepewa hati ya usajili.
Mheshimiwa Spika, Hifadhi zetu zinasimamiwa na serikali na TAMISEMI ni serikali na inaongozwa na Rais wa nchi. Kama serikali ni moja, iweje kuwe na utofauti wa kiutendaji kati ya mamlaka mbili za serikali ambazo zinaongozwa na Chama kile kile? Huu ni udhaifu mkubwa wa kiutendaji wa Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Spika, imebainika pia kwamba hakuna mipango endelevu ya matumizi ya ardhi ya Vijiji jambo linasababisha ardhi yenye rutuba na maeneo ya ufugaji kupungua na kuanza kutokea kwa migogoro ya ardhi. Aidha wananchi wengi wamekuwa na tabia ya kufuga mifugo mingi jambo linalopelekea ardhi kushindwa kuhimili wingi huo.
Mheshimiwa Spika, Vilevile mamlaka nyingi za hifadhi zimeshindwa kuwa na tafsiri ya mipaka yao jambo linalopelekea kushindwa kuwa na alama za kudumu. Hali hii imepelekea baadhi ya hifadhi kuongeza mipaka na kuingilia makazi ya wananchi. Pamoja na Waziri Mkuu kuagiza mipaka yote ya hifadhi iwekewe vigingi (beacons) jambo hilo mpaka sasa halijafanikiwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge kuingilia kati ili kuja na suluhisho la kudumu kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wananchi na mamlaka za hifadhi. Hali imekuwa mbaya zaidi ambapo taarifa zinaonyesha kuwa Askari wa hifadhi wamekuwa wakitumia silaha za moto kuua mifugo ya wananchi inayoingia katika hifadhi jambo ambalo linachochea chuki na uhasama na kuwa sababu ya tabia za kujichukulia sheria mkononi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tulieleza kwa undani jinsi ambavyo zoezi la bomoa bomoa katika Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Kimara mpaka TAMCO Kibaha Mkoani Pwani lilivyokiuka sheria na serikali kushindwa kuheshimu amri ya Mahakama Kuu kusitisha zoezi kabla shauri la msingi lililokuwa Mahakamani kusikilizwa.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza tarehe 30 Oktoba,2017 akiwa Jijini Mwanza Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa wananchi zaidi ya 3000 waliotakiwa kubomoa makazi yao karibu na uwanja wa Ndege wa Mwanza wasibomoe kwa sababu walimpa kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hii maana yake ni kuwa wananchi wa Jimbo la Kibamba na maeneo mengine wameadhibiwa kwa sababu ya kutumia haki yao ya kidemokrasia. Huu ni ubaguzi, dhana na tabia mbaya ambayo inatakiwa kukemewa na kila mmoja wetu kwa sababu serikali inawabagua wananchi kwa itikadi zao kisiasa.
Mheshimiwa Spika, kauli hiyo hiyo ya Rais ameirudia Mjini Kahama kuwa wananchi wasibolewe makazi yao kwa sababu walimpa kura mwaka 2015. Ikumbukwe kuwa Katiba ya nchi yetu ibara ya 13(4) inaweka marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza mamlaka yake katika utekelezaji wa shughuli yoyote ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kwa kauli na maelekezo ya Rais kuhusu bomoa bomoa ni dhahiri kuwa serikali imekiuka misingi ya Katiba ya nchi yetu kwa sababu ya kuonyesha ubaguzi wa wazi kwa wananchi. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri kulieleza Bunge lako tukufu kama maelekezo ya Rais ndio msimamo wa Serikali na kama ndivyo kwa nini bado anaendelea na wadhfa huo ilihali akijua anatekeleza majukumu au maagizo ambayo yanakiuka Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya CAG ya Mwezi Juni 2017, ilizitaja baadhi ya Taasis za Serikali zisizokuwa na haki miliki ya Ardhi kinyume na maelekezo yaliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya tarehe 7,Septemba 2016.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Taasis hizo ni Wakala wa Maabara ya Mifugo,Shirika la Maabara ya Mifugo,Wakala wa Utafiti wa Miamba, Wakala wa Hifadhi ya Chakula,Taasis ya Uhasibu,Wakala wa Ugavi na Huduma za Manunuzi,Bonde la Maji la Mto Ruvu,Mamlaka ya Maji safi na maji taka Handeni,Bonde la Maji Pwani ya Kusini Ruvuma na Bonde la Maji Rufiji, ardhi za majengo mbalimbali ikiwemo majengo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto, Wizara ya Fedha na Mipango,Ofizi ya Makamu wa Rais, Balozi mbalimbali ukiwemo Ubalozi wa New Delhi,Rome na Kampala Uganda
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa ni aibu kwa Mamlaka za Serikali kukosa hati miliki ya ardhi, lakini pia ni muhimu Mamlaka na taasisi hizi zikatambua masuala yote yanayohusu ardhi ni masuala nyeti. Usalama wa ardhi siku zote upo kwa mwenye hati ya umiliki. Ardhi ni ulinzi. Hivyo kuendelea kuwa na maeneo ya serikali ambayo hayana hati maana yake ni kuanza kukaribisha uvamizi au migogoro baina ya serikali na wananchi hususani katika maeneo yenye vyanzo vya maji na vinavyotegemewa kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Spika, kukosa hati za umiliki wa ardhi kunaweza kuisababisha serikali ikaingia katika hasara kubwa endapo patajitokeza watu ambao nao watadai kuwa wamiliki wa ardhi ya maeneo hayo kisheria. Vilevile, serikali itashindwa kujua thamani ya ardhi inayomilikiwa na taasisi au Wakala husika na hivyo kukosa ufanisi katika kufuatilia na kusimamia mali zake
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jambo hili limewahi kusemwa na Waziri mwenye dhamana pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara na pia ofisi ya CAG bila kufanyiwa kazi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuanza kuzichukulia hatua mara moja taasisi na Mamlaka zote za serikali ambazo hazijatimiza wajibu huu mkubwa wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa miaka mitatu mfululizo imepinga uamuzi wa serikali kupoka Halmashauri chanzo cha mapato kinachotokana na kodi ya majengo. Tulieleza kwa kirefu kuhusu nia ovu ya serikali kupoka chanzo hicho kuwa ni mkakati wa kuziua Halmashauri nyingi za Mijini ambazo huongozwa na Vyama vya Wapinzani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote limeibuka sakata lingine la utaratibu mbovu wa kufanya tathmini za nyumba za wananchi kwa kuongeza thamani ya nyumba ili waweze kulipa kodi kubwa ya majengo. Jambo hili linalalamikiwa sana na wananchi kwa sababu Halmashauri nyingi ambazo zimefanya kinachoitwa tathmini ya nyumba hawajawashirikisha wananchi ambao ndio wamiliki wa majengo hayo.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Mipango alilihakikishia Bunge kuwa nyumba yoyote ambayo haijafanyiwa tathmini mmiliki atalazimika kulipia shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na shilingi 50,000 kwa jengo la ghorofa.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini ya mwaka 2016 kifungu cha 55 kinampa Mthamini ardhi mamlaka kuingia eneo au nyumba ya mtu kwa ajili ya uthamini isipokuwa atatakiwa kutoa taarifa kwa mmiliki au mkazi wa nyumba au eneo hilo. Aidha, kifungu cha 51 kinaweka utaratibu wa njia zitakozotumiwa na Mthamini kufanya tathimini ambapo Mthamini atatakiwa kueleza sababu za njia alizotumia.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 7(1)(a) cha Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini inatoa mamlaka kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kufuta tathmini yoyote ambayo anaona kuwa utaratibu haukufuatwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya Waziri wa Ardhi ya sababu zinazopelekea serikali kufumbia macho utaratibu wa hovyo wa kufanya tathimini ya nyumba za wananchi bila kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria ambao umefanywa kwa kuwavizia wananchi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali imwelekeze Mthamini Mkuu kufuta tathmini zilizofanywa katika Halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Manispaa ya Bukoba Mjini ambapo tathmini ilifanyika bila kuzingatia taratibu.
Mheshimiwa Spika, zipo baadhi ya hoja ambazo ziliibuliwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambazo serikali imeshindwa kuzitekeleza kwa ujumla wake; hoja hizo ni kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, masuala haya pamoja na mengine mengi bado ni changamoto ambazo serikali haijazifanyia kazi kwa ukamilifu wake. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kulieleza Bunge lako tukufu ni kwa nini mpaka sasa haijafanyia kazi hoja hizi ambazo zilitolewa na baadhi yake serikali kukubali kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Wizara ilitengewa jumla ya shilingi 61,873,949,000.00 kati ya fedha hizo, miradi ya maendeleo ilitengewa shilingi 20,000,000,000.00 ambazo shilingi 10,000,000,000.00 zikiwa fedha za ndani na shilingi 10,000,000,000.00 Fedha za matumizi mengineyo zilizotengwa ni shilingi 25,531,158,000.00
Mheshimiwa Spika, takwimu za wizara zinaonesha kuwa hadi mwezi februari, 2017, fedha za matumizi mengineyo (OC) zilizopokelewa ni shilingi 9,994,249,148.00 sawa na asilimia 39.2 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Aidha kwa miradi ya maendeleo fedha zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi 7,626,219,314.00 sawa na asilimia 38, lakini katika hizo fedha za maendeleo kuna shilingi 3,301,058,684.65.00 kwa ajili ya kulipia deni la Mkandarasi aliyeandaa Mipango Kabambe ya Majiji ya Arusha na Mwanza.
Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo ni kwamba fedha halisi zilizopokelewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha bajeti ya mwaka 2016/17 ni shilingi 4,325,160,629.4 pekee ambapo ni sawa na asilimia 21.62 tu.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2017/18 Wizara iliomba na kuidhinishiwa jumla ya shilingi 68,030,880,526/- kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali. Kati ya fedha hizo shilingi 21,470,166,074.00 ni matumizi mengineyo, ikiwa ni pungufu ya shilingi 4,060,991,926.00 kwa kulinganisha na maombi ya mwaka 2016/2017 kwa matumizi mengineyo. Fedha za maendeleo zilizokuwa zimeombwa ni jumla ya shilingi 25,400,000,000/- ambapo shilingi 16,400,000,000.00 ni fedha za ndani na shilingi 9,000,000,000.00 ni fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Wizara ya Ardhi bado inao uwezo wa kukusanya mapato mengi zaidi ya ndani, lakini imeshindwa kufanya hivyo kutokana na serikali hii kushindwa kuwekeza katika kurasimisha Makazi na ardhi kwa ujumla. Hii inaonekana wazi kwa kuangalia kiasi kilichotengwa mwaka 2016/2017 na kiasi kilichotolewa. Kambi Rasmi ya Upinzani ilishauri kuwa fedha za maendeleo ziongezwe ili upimaji wa ardhi na umilikishwaji ufanyike kwa haraka ili kodi ya ardhi ikusanywe kwa sababu haiwezani serikali ikataka kuvuna pasipo kuwa na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Februari, 2018 Wizara ilipokea fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha shilingi 5,830,000,000.00 ambazo ni fedha za ndani sawa na 35% na shilingi 6,998,186,360.00 ni fedha za nje sawa na 77.7%. Kwa takwimu hizi za Wizara ambayo fedha za ndani zinatolewa kwa 35% kwa ajili ya miradi ya maendeleo na wahisani kutoa 77.7% ni ishara kuwa serikali haina umakini na wala haina nia ya kutatua changamoto katika sekta ya ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa fedha za matumizi mengineyo fedha zilizopokelewa ni kiasi cha shilingi 12,265,022,342.92 sawa na 49.3% ya bajeti iliyokuwa imetengwa. Katika hali ya kushangaza serikali ilikuwa imepanga na kutenga kiasi cha shilingi 10,000,000,000.00 kwa ajili ya kuziwezesha Halmashauri nchini kusimamia sekta ya ardhi, hadi kufikia Februari mwaka, 2018 Wizara haikuwa imepokea chochote kwa ajili ya kuziwezesha Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ni wadau muhimu katika kusimamia na kuweka mipango ya ardhi nchini lakini serikali imeona isipeleke chochote kuziwezesha Halmashauri kufanya jukumu hilo. Ni dhahiri kuwa changamoto zilizoelezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za serikali zitaendelea kuwepo kwa sababu serikali haina nia ya kupeleka fedha kuziwezesha Halmashauri kwa ajili ya miradi ya kuendeleza ardhi.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara inaomba bajeti ya jumla ya shilingi 65,989,347,638.00 ambapo fedha maendeleo ni kiasi cha shilingi 30,537,602,000.00 sawa na ongezeko la shilingi 5,137,602,000.00 ambapo fedha za ndani ni 20,000,000,000.00 na za nje ni shilingi 10,537,602,000.00. Kwa upande wa matumizi mengineyo kiasi cha shilingi 35,451,745,638.00 pungufu ya 7,803,337,288.00 ambapo kwa mwaka uliopita matumizi mengineyo yalikuwa 43,255,082,926.00.
Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasimali muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, ardhi ni sehemu kubwa ya maendeleo ya wananchi. Kuporomoka kwa sekta ya miliki ya nyumba (Real Estate), udhaifu katika kusimamia ugawaji na upangaji wa ardhi, migogoro ya ardhi kati mamlaka za hifadhi na wananchi ni changamoto ambazo zinarudisha nyuma wananchi katika maendeleo yao.
Mheshimiwa Spika, aidha serikali kushindwa kutoa fedha za maendeleo za ndani kwa ukamilifu na pia kushindwa kabisa kupeleka fedha za kuzisaidia Halmashauri ni ishara kuwa serikali haioni umuhimu wa kuendeleza ardhi nchini. Hali hii inapelekea wananchi waliowengi kuishi maeneo ambayo sio rasmi na hivyo kupelekea kukosa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuipa kipaumbele sekta ya ardhi nchini kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Urekebishaji wa Mifumo Ili kuwa na taasisi Imara za kusimamia Kilimo
Mheshimiwa Spika, Msingi mkuu wa maendeleo ni dola iliyo na katiba thabiti inayoweka urari katika maslahi ya raia wake wote na ambayo inatenganisha madaraka ya mahakama, bunge na serikali. Hii ndiyo huleta mfumo ambamo sekta binafsi inaweza kujenga ukuaji wa uchumi ambao, kama haukupatikana, basi maisha ya watu masikini hayawezi kuboreshwa.
Mheshimiwa Spika, katika muktadha huo, sekta ya kilimo ili kuwa na tija kwa watanzania inatakiwa kuwa na mfumo imara (taasisi imara) zinazoongoza sekta badala ya taasisi zinazohusika na kilimo kuongozwa kwa matamko, jambo ambalo linasababisha sekta binafsi kushindwa kuwekeza katika kilimo, sambamba na hilo taasisi za fedha zinasita kutoa mikopo ya muda mrefu katika shughuli za kilimo kutokana na kukosekana kwa taasisi imara zinazoongoza sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kuna methali moja inasema “Kutojua ni vibaya, lakini Kutotaka kujua ni vibaya zaidi”, hivyo kuchukua maamuzi bila kuwahusisha wahusika wakuu wa sekta hiyo ni kosa kubwa ambalo kwa njia moja au nyingine maamuzi yanachangia kuendelea kuleta umasikini kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika, Kuhusishwa kwa wananchi katika mipango ya kunagalia fursa na vikwazo katika kilimo limekuwa ni changamoto kubwa, Utaratibu wa Serikali wa kushusha maamuzi yake ngazi za chini ili yatekelezwe bila kujali kuwa kunaleta tija au la. Jambo hili ni chanzo cha matumizi ya fedha nyingi kwa miradi ambayo sio kipaumbele kwa wananchi katika maeneo mengi. Hivyo ni muhimu ili kilimo kiwe na tija uhusishwaji wa wadau (wakulima, wafanyabiashara wa kilimo na taasisi zinazotoa fedha kwa wakulima) katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, Kilimo ni eneo ambao lilibainishwa kama eneo la kipaumbele katika mkakati wa kukuza na kuondoa umasikini (MKUKUTA 1, MKUKUTA 11 na Mpango wa maendeleo wa miaka 5 (FYDP). Mkakati wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo (ASDS) ulizinduliwa rasmi 2001 ili kuwezesha kufikiwa kwa dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025 (TDV 2025) na ikiwa ni katika kufanikisha kwa malengo ya kisera ya MKUKUTA.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21, sekta ya kilimo inaajiri karibia asilimia 70 ya watu, ikichangia asilimia 28 ya Pato la Taifa (GDP), robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nchi za nje na asilimia 65 ya pembejeo za sekta ya viwanda. Aidha, sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye kipindi chenye mvua za kutosha.Hadi Juni 2014, ukuaji wa kilimo ulikuwa asilimia 3.4 mbali kabisa na lengo lililowekwa katika MKUKUTA II na FYDP I ambayo ilikuwa asilimia 6 kwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali inayotengwa kwa kilimo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hivi sasa imefikia zaidi ya asilimia 7 lakini fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na hazina zimekuwa zikipungua kila mwaka. Kiasi cha asilimia 34 ya wananchi wanaishi katika hali ya umaskini uliokithiri na hivyo, hulazimika kuendelea kutegemea moja kwa moja rasilimali ardhi kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Spika, eneo la miliki ya Tanzania ni jumla ya hekta 94,508,700, kati ya hizo hekta milioni 89 ni eneo la nchi kavu, na linalobakia ni eneo la maji. Inakadiriwa kuwa jumla ya hekta milioni 44 ni eneo linalofaa kwa kilimo ambapo asilimia 24 zinatumika kwa shughuli za kilimo. Ardhi inayotumika kwa mashamba makubwa na ya kati ni hekta milioni 1.5, wakati hekta milioni 8.6 hutumika na wakulima wadogo.
Mheshimiwa Spika, inaonesha kuwa Serikali katika kuhakikisha kwamba inajaribu kila mbinu na kwa gharama yoyote katika kuinua uchumi, lakini mara zote imeshindwa au imesahau kuelewa kwamba madhara ya kutofikiria umuhimu wa ardhi kwa wananchi wake ni makubwa sana, kwani imekuwa ikivutia wawekezaji wenye mitaji mikubwa kwenye ardhi kama vile Mashamba makubwa, madini, utalii n.k Ni muhimu sana kufikiria katika kuvutia uwekezaji kufikiria na kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya watanzania waishia vijijini ambao zaidi ya asilimia 70 ya mahitaji yao yanategemea ardhi kwa ajili ya kilimo na mifugo[36].
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2009 Serikali imekuwa na miradi kadhaa iliyozinduliwa ili kufanya Mapinduzi katika kilimo kwa kuhimiza uwekezaji binafsi katika kilimo program kadhaa zilinduliwa ambazo ni; programu ya SAGCOT mwaka 2010; Jukwaa la Kilimo Afrika (Grow Africa Forum) mwaka 2011; Mpango wa Uwekezaji wa Kilimo na Usalama wa Chakula Tanzania (TAFSIP), Mpango wa Taifa wa Uwekezaji Tanzania chini ya CAADP mwaka 2011; Matokeo Mkubwa Sasa’ (BRN) mwaka 2013, kuanza kwa utekelezaji wa Mfuko wa Kuchochea Kilimo wa SAGCOT mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, Randama fungu 43 ya mwaka 2018/19 inaonesha kuwa kwenye SAGCOT wawekezaji wakubwa binafsi wameweza kuunganishwa na wakulima ili kuleta tija, kuongeza kipato kwa wakulima, na kuongeza chakula na lishe kwenye kaya za wakulima wa mazao mbalimbali. Hadi sasa jumla ya Dola Milioni 500 zimewekezwa katika kilimokwenye ukanda wa SAGCOT kati ya Dola Bilioni 3.5 zilizopangwa kuwekezwa ifikapo mwaka 2030. Kati ya uwekezaji huo Dola bilioni 2.4 zitatokana na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumeeleza hapo awali mipango hiyo yote ya Serikali ya kuleta mapinduzi ya kilimo bado haimuangalii mkulima mdogo anayelima hekari moja hadi tano na badala yake inawaangalia wawekezaji wakubwa tu. Jambo hili haliwezi kuondoa umasikini kwa mkulima mdogo badala yake litamfanya mkulima mdogo kutoka kwenye kumiliki ardhi na kuwa kibarua/ manamba katika mashamba makubwa.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kwamba rasilimali ardhi haiongezeki lakini watumiaji wake wanaongezeka kila siku, hivyo mpango imara na uliofanyiwa upembuzi yakinifu ambao umejielekeza kwa mkulima mdogo na mkubwa wa matumizi ya ardhi unahitajika. Hivyo basi, ni muhimu sana kuwa na takwimu za uhakika zinazoelezea vikwazo vya uendelezaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali, sambamba na hilo kuwa na mwongozo unaonesha vipaumbele katika matumizi ya hiyo raslimali finyu tuliyonayo.
Mheshimiwa Spika, kuwekeza katika kilimo si tu inatatua changamoto ya ukosefu wa chakula na lishe bali pia kupunguza umaskini, maji na utumiaji wa nishati, mabadiliko ya tabia ya nchi na uzalishaji na utumiaji usiyoendelevu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na uchambuzi wa shirika la kilimo Duniani (FAO) Ukuaji kwenye sekta ya kilimo ni mara 11 zaidi kama njia bora ya kupunguza umasiki kuliko sekta zingine kwenye ukanda wa nchi za Afrika zilizo kwenye jangwa la Sahara.
Kufikia malengo ya kikanda na kitaifa katika sekta ya kilimo inahitajika nguvu za dhati kama watalaamu wanavyosema kwamba kuongeza usalama wa chakula katika nchi za Ukanda wa Afrika wa Jangwa la Sahara inahitaji kutafuta majibu sahihi kwa maswala ya kitaalamu, mifumo na sera. Pia, maswala ya ardhi, pembejeo (mbegu, mbolea na viuatilifu), huduma za ugani, mikopo, miundo mbinu vijijini, masoko, ajira na sera za biashara.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa kilimo kinaendeshwa kwa kupatiwa mikopo ya muda mfupi na mrefu japokuwa mikopo ya muda mrefu bado ni tatizo, kuna taasisi ambazo zimekuwa zikijishughulisha kwa kadri inavyowezekana kutoa mikopo na ushauri unaohusu biashara za kilimo (Agri Business), nazo ni;
BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilianzishwa mnamo Septemba 2011 chini ya Sheria ya Makampuni, 2002. Kazi kuu ya Benki ni uhamasishaji utoaji wa huduma za fedha na huduma zisizo za kifedha kwa sekta ya kilimo Tanzania ikiwa ni pamoja na:
Mheshimiwa Spika, Mnamo Septemba 2014, Serikali ilitoa mtaji wa Shilingi bilioni 60 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, lakini taarifa za ukaguzi zinaonesha kuwa; benki hiyo badala ya kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo shughuli kuu, Benki imekuwa ikiwekeza sehemu kubwa ya fedha zake katika amana za kudumu. Kufikia tarehe 31 Desemba 2016, jumla ya Shilingi bilioni 54.70 zilikuwa zimewekezwa kwenye amana za kudumu, ambayo ni karibu asilimia 91 ya mtaji. Aidha ilibainika kuwa, kati ya Shilingi bilioni 3.95 bilioni jumla ya mikopo iliyotolewa, Shilingi bilioni 1.71 ni mikopo kwa watumishi na Shilingi bilioni 2.23 tu ndio zimetolewa mikopo kwenye sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mpango uk 100 aya ya 5.5.2 unasema kuwa kwamba Serikali imeji-commit kuiongezea mtaji benki hiyo hadi kufikia shilingi trilioni 3 kwa kipindi cha miaka mitano cha uhai wa mpango wa pili wa maendeleo, Kambi Rasmi ya upinzani inapenda kufahamu hadi sasa Benki hiyo imeongezewa fedha kiasi gani kati ya hizo shilingi trilioni 3 zilizoahidiwa na Serikali?
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba maboresho mbalimbali yaliyofanywa na ambayo yanaendelea kufanywa katika Sera, Sheria na Kanuni yamelenga kumuwezesha Mtanzania kiuchumi na kuongeza ushiriki wake katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uwekezaji mkubwa wa ndani, uwekezaji mkubwa kutoka nje pamoja na miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Msukumo unaowekwa katika kufungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani na faida ya shughuli za kilimo na kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda unaonekana kutokwenda kama inavyotakiwa kutokana na uwekezaji kuwa mdogo na pia uzalishaji huo mdogo uliopo wa mazao ya kilimo kukosa soko la ndani lenye uhakika, jambo linalowakatisha tamaa wakulima.
MATUMIZI YA PEMBEJE0
Mheshimiwa Spika, Pembejeo ni eneo muhimu sana katika kuchangia uzalishaji wa mkulima. Nidhahiri kwamba; mbegu bora pekee huchangia takribani asilimia 40 ya mavuno ya zao husika,
baadhi ya changamoto zinazoonekana kuwa kikwazo kwa mkulima ni kama vile:
Mheshimiwa Spika, kwa changamoto hizo ni dhahiri kuwa kufikia Tanzania ya viwanda bado tunahitaji miaka 20 ijayo kama hatutowkeza vya kutosha ili kukabiliana na changamoto tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 61 ya ardhi ya Tanzania imeharibika hususan, katika maeneo kame katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Geita na Kilimanjaro. Uharibifu wa ardhi unaosababishwa na chumvichumvi ni takribani hekta milioni 1.7 na tatizo hili linaonekana zaidi katika mikoa ya Dodoma, Singida, Kilimanjaro na Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, Uharibifu wa ardhi pia unahusishwa na uchafuzi wa udongo unaotokana na matumizi mabaya ya madawa na mbolea za kilimo. Mfano mmojawapo wa uharibifu huu ni uwepo wa tindikali katika udongo unaosababishwa na matumizi makubwa ya mbolea zenye asili ya naitrojeni (hususan, katika mashamba ya mahindi) katika mikoa ya Ruvuma na Iringa. Mfano mwingine ni uwepo wa vumbi la madawa ya kilimo ya salfa kwenye maeneo yanayolimwa korosho, hasa katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Rejea taarifa ya hali ya Mazingira 2014
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona matumizi ya mbolea za chumvi chumvi kwa sasa zinashika kasi bila ya kuangalia madhara ya udongo kwa maeneo mengi hapa nchini. Ni mpango gani wa makusudi wa kutumia mbolea zisizo za chumvi chumvi ili kuwa kama tiba ya udongo kwa maeneo ambayo udongo wake tayari umeathirika?
Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa sasa yako chini, huku takribani asilimia 17 ya kaya zinazolima wakitumia mbegu zilizothibitishwa (hasa mahindi) na wastani wa kilo 5.5 za mbolea ya kiwandani kwa hekta. Matumizi ya mbolea za kiwandani yameongezeka kwa haraka tangu mwaka 2009 ikiambatana na kuanzishwa kwa Mfumo wa Kitaifa wa Vocha za Pembejeo za Kilimo, ambao ulitoa ruzuku katika gharama za mbegu bora (pamoja na mbegu chotara) na mbolea za kiwandani. Wakulima katika utafiti wetu walibainisha ukosefu wa masoko (68%) na uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyama waharibifu (58%) kwamba ndio changamoto yao kubwa ya kilimo; pia walieleza bei za juu za mbolea (51%), upatikanaji wa ardhi (47%) na bei za mbegu (44%) zilikuwa muhimu
USAMBAZAJI WA MBOLEA
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na kutolewa katika hali ya mazingira hapa nchini, kna baadha ya maeneo hasa the big four hawawezi kulima na kuvuna bila ya matumizi ya mbolea. Mkoa wa Mbeya ni moja ya maeneo hayo, Busokelo-Rungwe, Mkoa wa Mbeya, kwa sasa bei ya mbolea ya UREA na DAP ni shilingi 46,000/- na shilingi 56,500/-, wakati bei elekezi iliyokuwa imetolewa na Serikali ilikuwa ni shilingi 43,500 na 53,500/-.
Mheshimiwa Spika, Lakini ili wafanyabiashara wapate faida ni lazima gharama za kusafirisha ziwekwe na hivyo kilo moja ya UREA inauzwa kwa shilingi 1,200 na DAP shilingi 1,500/- Mahesabu haya yanaufanya mfuko wa UREA kuuzwa kati ya shilingi 60,000 hadi 75,000 kwa mfuko wa kilo 50. Gharama za kusafirisha Tani moja ya Mbolea kutoka Bandarini hadi mkoani inapohitajika mbolea ni kati ya shilingi 90,000/- hadi shilingi 100,000/- Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na ANSAF na taarifa yake kutolewa tarehe 22 March, 2018, Ukumbi wa St. Gaspar Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, mfumo wa BULK PROCUREMENT kwenye mbolea umesaidia au unaongeza ukiritimba kwenye biashara ya mbolea? Na tukumbuke kwamba ukiritimba ni njia inayotumika sana kutengeneza mazingira ya RUSHWA kubwa na ndogo.
HUJUMA KATIKA ZAO LA KOROSHO
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha mwenendo wa uzalishaji wa zao la korosho kwa miaka mitatu kuanzia msimu wa mwaka 2015/16 hadi msimu wa 2018/19 umekuwa unapanda tani 155,416 (2015/16); 265,238(2016/17); 311899(2017/18) na matarajio ya tani 350,000 kwa mwaka 2018/19.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinaashiria kwamba, wakulima wa Korosho kama watapatiwa pembejeo kwa muda unaostahili na zikiwa na ubora unaotakiwa uwezekano wa kuzalisha zaidi ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la pembejeo kwenye zao la korosho ni kwa wahusika kushindwa kufuata Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 pale wanapotoa zabuni kwa makampuni ya wazabuni wa pembejeo za korosho kupatikana kwa halali na sio kwa kutumia njia za panya na mwisho wa siku ni kuleta dawa yenye viwango duni, kultokuletwa kwa wakati na muda mwingine kuletwa kidogo hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wakulima wote.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG inaonesha kwamba; Ugawaji wa zabuni za kuingiza dawa ya korosho (sulphur powder) kwa kampuni isiyo na vigezo kukasababisha ishindwe kufikisha pembejeo kwa walengwa kwa wakati na kwa kukidhi mahitaji.
Wizara husika inapaswa ichukue hatua za kinidhamu kwa watumishi wote walioshiriki kuipa zabuni Kampuni ambayo haikuwa na vigezo na Kampuni kwa kushindwa kutimiza masharti ya makubaliano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa hii Kampuni ina mahusiano ya karibu na watendaji wakuu wa Wizara husika. Hivyo tunataka kufahamu ni hatua gani zinachukuliwa kwa wahusika kusababisha hasara kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, mbali na hilo pia, CDTIF waliingia kwenye mkataba na M/s Hammers Incorporation Ltd kwa ajili ya usambazaji wa tano 3000 za sulphur. Hata hivyo, wakati wa ukaguzi ilibainika kuwa msambazaji alisambaza tani 2307 huku tani 693 zikiachwa. Nikagundua zaidi uzito wa baadhi ya mifuko iliyosambazwa ni pungufu kiasi cha kupelekea upungufu wa zaidi ya tani 144. Udanganyifu huo uliogundulika umesababisha hasara ya tani 837 zenye thamani ya Shilingi milioni 803.52. Hivyo, naishauri Menejimenti ya mfuko, wakishirikiana na Serikali, kuwachukulia hatua kali watumishi ambao kwa namna moja au nyingine, walishiriki kwenye udanganyifu huo; pia hatua kali zichukuliwe dhidi ya kampuni/ Msambazaji.
UZALISHAJI TUMBAKU
Mheshimiwa Spika, zao la tumbaku ni zao linalolimwa kwa wingi na Wakulima wadogo wadogo kutoka sehemu tofauti zinazolima tumbaku kwa wingi hapa nchini ikiwemo Sikonge, Urambo, Kahama, Manyoni, Iringa, Lupa, Kigoma, Songea na Mara na takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wake kwa miaka miwili unapanda na kushuka.
Mheshimiwa Spika, takwimu za uzalishaji kwa msimu za tani (58,639) 2016/17 na (63,800) 2017/18 ni takwimu zinazotia mashaka makubwa kwani ukweli ni kwamba wakulima wamebakia na tumbaku nyingi sana bila kuiuza kutokana na masharti ya wanunuzi kununua tumbaku kidogo.
Mheshimiwa Spika, Jambo hili ambalo wakulima wanazalisha sana lakini kunawekwa masharti na mnunuzi, hiyo ni hujuma kubwa sana kwa mkulima na jambo hili Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo ni kwanini Tumbaku yote haikununuliwa kwa msimu uliomalizika. Hata kama itauzwa kwa sasa ni ukweli kuwa ubora wa hiyo tumbaku umekwisha pungua sana na hivyo itauzwa kwa bei ya hasara sana kwa kulinganisha na gharama za uzalishaji wa Tumbaku hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la Serikali la undumilakuwili la Serikali kuhusiana na kilimo cha Tumbaku hapa nchini,huku wizara ya afya ikitoa tamko kuwa Serikali imekubali kuachana na Kilimo cha Tumbaku kutokana na madhara yake kwa afya za watanzania. Kwa upande mwingine Serikali inasema kuwa inafanya juhudi kutafuta soko la Tumbaku hivyo wakulima wasikate tamaa na kulima Tumbaku.
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa kimataifa wa kudhibiti Tumbaku wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WFCTC) ambao Tanzania iliridhia Mkataba huu Aprili 2007 miaka 11 iliyopita, hivyo ina wajibu wa kuutekeleza,ili kulinda watu wake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kama Serikali ingekuwa makini ingeongea na Shirika la Afya la Dunia (WHO) kugharamia kilimo cha zao mbadala na Tumbaku ili kuwalinda waliokuwa wakulima wa Tumbaku.
HUDUMA ZA UGANI
Mheshimiwa Spika, sera ya kilimo ya mwaka 2013 na mwongozo vinaeleza bayana kwamba kila kijiji kinahitajika kuwa na afisa ugani mmoja. Aidha, uwiano unaohitajika kati ya afisa ugani na idadi ya wakulima ni 1:600; Utafiti uliyofanyika katika maeneo ya Singida na Chamwino unaonyesha kwamba afisa ugani mmoja uhudumia vijiji zaidi ya kimoja au kata.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Raslimali watu inayotakiwa kwa sekta ya kilimo, watumishi wenye sifa mbalimbali katika kilimo wanaohitajika ni 19,228 lakini waliopo ni 8,756 sawa na 45.4%. Hii ni kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na Jukwaa la Wadau wa Kilimo wasio wa Kiserikali (Agricultural Non – State Actors Forum – ANSAF). Utafiti huo unaonyesha kwamba; watumishi wenye taaluma kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea mahitaji halisi ni 2,746 lakini waliopo ni 1,530 ambao ni sawa na 55.7%. Wakati wenye taaluma ngazi ya Cheti na Diploma mahitaji ni 16,542 lakini waliopo ni 7,226 sawa na 43.7%
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maafisa ugani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2013 waliokuwepo ni 7,974 wakati Tanzania ina vijiji vilivyo sajiliwa 15,082. Wakati kuna upungufu huo; Muongozowa Serikali maafisa ugani ni kila kijiji kimoja kuwa na afisa ugani mmoja.
Mheshimiwa Spika, Changamoto zilizopo mbali ya uchache/upungufu huo zinazokabili huduma ya ugani ni pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu, mfano: ukosefu wa vitendea kazi (mfano; pikipiki, vifaa vya kupimia udongo na mafunzo ili kukabiliana na mabadiliko ya tecknolojia.
Mheshimiwa Spika, maafisa ugani kupangiwa majukumu ambayo ni nje na ueledi wao, mfano kuwa watendaji wa vijiji/kata.
Hata hivyo, utafiti unaonyesha kwamba maafisa ugani hawatimizi wajibu na majukumu yao vizuri, Muda mwingi wanafanya kazi ofisini au shughuli binafsi. Hali hii husababisha njia zisizo bora kwenye kilimo na kuchangia kushuka kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini
UPOTEVU WA MAZAO BAADA YA MAVUNO (POST HARVEST LOSSES)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama fungu 43 uk. 28 aya 6.1.3 kuhusu kuimarisha usimamizi wa mazao kabla na baada ya mavuno na kuongeza thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko kwa mazao yote ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba wakulima wengi wanapata hasara sana kutokana na kutokuwa na njia bora za uhifadhi wa mazao yao baada ya mavuno,inakadiriwa kwamba kati ya asilimia 30-40 ya jumla ya mazao hupotea kila mwaka. Upotevu mkubwa kutoka kwenye matunda, mboga, mihogo, karoti na vitunguu nk. Tanzania hutumia Zaidi ya dola milioni 200 sawa na bilioni 400 (Mutungi and Affognon 2013) kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Wakulima wadogo wadogo wanalazimika kuuza mazao yao kwa bei ya chini kwa sababu ya uwezo mdogo kwenye usimamizi wa mazao baada ya mavuno. Katika Afrika Mashariki, ni asilimia 5 huwekezwa kwenye usimamizi wa mazao baada ya mavuno ambayo asilimia 95 hutumika katika uzalishaji. Inakadiriwa
kwamba kila mwaka hasara inayotokana na kuharibika kwa mazao ya nafaka barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, inafikia dola za Kimarekani bilioni 4 na hii ni sawa na asilimia 15 ya thamani ya mavuno hayo.
Mheshimiwa Spika, hakuna kumbukumbu zinazotaja sera inayohusu suala la kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba kwa mwaka 12 Tanzania ina maghala 1,260. Idadi hii ni ndogo mno ukiilinganisha na mahitaji halisi ya takribani vijiji 11,000 vilivyokuwepo, sasa hivi Tanzania ina vijiji vipatavyo 13,000. Hii ni kwa mujibu wa Tanzania Market Plan chini ya utafiti uliofanywa na taasisi zifuatazo[37]
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha licha ya ongezeko la uzalishaji wa nafaka kitaifa (uzalishaji ukifikia takriban tani 9,388,772 kwa mwaka) teknolojia zinazotumiwa wakati wa kuvuna na kusindika ni duni sana. Hali hii husababisha upotevu wa mavuno unaokisiwa kuwa tani 1,877,754.4 kila mwaka. Tafsiri ya takwimu hizi ni upotevu wa takribani asilimia 20 baada ya mavuno. Na tukichukuliwa kwa uzalishaji jumla wa mazao yote ya chakula, matunda na mboga jumla ni tani 22,476,504 upotevu wa asilimia 20 ni sawa na tani 4,495,300.8
Mheshimiwa Spika, upotevu huu unachangiwa na matatizo mbalimbali kama vile; maghala mengi hayawafai wakulima kwa sababu ya kuwa mbali, baadhi ya maghala ni mabovu kwa kuachwa kwa muda mrefu bila kukarabatiwa, maghala mengine ama yamekodishwa kwa wafanya-biashara binafsi, au yanatumiwa kwa shughuli nyingine tofauti na kuhifadhi mazao.
Maghala mengi kutokutumika
Mheshimiwa Spika, Maghala mengi katika mkoa wa Songwe haya fanyikazi kutokana na kujengwa kwa maelekezo au uamuzi wa watendaji wizarani,au wakala za Serikali na wanasiasa bila ushirikishwaji wa wadau na mwisho wa siku yamekuwa ni “white elephants”.
Mheshimiwa Spika, Jambo hili la kutoshirikisha wadau linaleta ugumu kwa watendaji wa Serikali za mitaa katika kutekeleza sera za nchi kwani wanakutana na ugumu toka kwa wadau mbalimbali kutokuona umuhimu wa kile kinachotakiwa kutekelezwa na Serikali kwa wakati huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge, idadi halisi ya Maghala iliyopo kwa sasa kulingana na hongezeko la vijiji pamoja na ongezeko la uzalishaji hasa kwa mazao ya nafaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali haisemi jinsi ya kukabiliana na tatizo hili ambalo linawakabili wakulima wengi hasa wadogo na badala yake inatoa suluhu ya uongezaji thamani kwa mazao jambo ambalo ni hatua inayofuata baada ya uhifadhi katika ngazi za familia. Tukumbuke wakulima inawalazimu kuuza mazao yao kwa bei ya chini kutokana na kutokuwa na sehemu muafaka za kuhifadhia mazao yao.
MFUKO WA TAIFA WA PEMBEJEO ZA KILIMO(Agricultural Inputs Trust Fund-AGITF)
Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu yake mengine lakini lengo kuu ni kutoa mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo na mifugo. Randama uk. 25 na 26 inaonesha kwamba hadi kufika mwezi Februari 2018, mfuko ulikuwa umetumia jumla ya shilingi 3,090,330,825.19 japokuwa kwenye Jedwali Na. 7 zinasomeka jumla ni shilingi 2,260,246,400.00
Mheshimiwa Spika, maelezo yanasomeka kuwa lilikopesha trekta dogo moja aina ya “power tiller” kwa shilingi 39,000,000/-. Hapa tunaona kuna jambo halijakaa sawa, kwani kwa bei iliyowekwa na idadi ya matrekta ni dhahiri, maelezo ya Mheshimiwa Waziri yanatakiwa ili kuweka hesabu hizi ziendane na uhalisia wa bei ya power tiller.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo yaliyomo kwenye Jedwali Na.7 inaonesha kuwa mfuko huo umetoa maelezo ya kijumla mno kiasi ambacho kinatia mashaka, miundombinu ya kilimo na uvuvi 6 kwa shilingi 323,550,000/- au Pembejeo za Kilimo na Mifugo 10 kati ya 80 kwa shilingi 593,343,200/- Hii ni taarifa inayotia mashaka ni muhimu kupatiwa maelezo ya kutosha katika matumizi ya Mfuko huu wa Pembejeo za Kilimo.
CAADP /AUC NEPAD – Mpango Kabambe wa Kuendeleza Kilimo Africa
Mheshimiwa Spika, mwaka 2003, wakuu wa nchi za Afrika walikutana Maputo, nchini Msumbiji na kuazimia kuhusu kuendeleza kilimo barani Afrika. Maazimio hayo yalirudiwa pia mwaka 2014 kule Malabo,Guinea Biassau kwa kuweka maazimio juu ya nguzo saba.
Moja ya nguzo hizo ni kuhakikisha kuwa kila nchi inatenga asilimia 10 ya bajeti ya taifa kwa ajili ya sekta ya kilimo ili kuchochea ukuaji wa asilimia 6. Hadi sasa, Tanzania inatenga chini ya asilimia 5 (mfano asilimia 4.7 kwa mwaka 2017/18).
Mheshimiwa Spika, Tathimini iliyofanyika inaonyesha kwamba kati ya nchi 47 za Africa, ni nchi 20 tu zimeonekana zinaelekea kufikia malengo hayo ifikapo 2025. Tanzania imekuwa ya mwisho katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kupata alama 3.1 kati ya 10, ambapo Rwanda imepata 6.1, Kenya 4.8, Burundi 4.7, na Uganda 4.4 6. Pamoja na kuwa sekta ya kilimo kuwa muhimu kwa usalama wa chakula na lishe; kuajiri zaidi ya nguvu kazi kwa asilimia 65, kuchangia pato la taifa kupitia uuzaji mazao nje; kutoa mali ghafi kwa ajili ya viwanda, n.k. sekta haijapewa kipaumbele cha kutosha. Ni muda wa kujifanyia tathmini sasa kabla tunakokwenda hakujakuwa kubaya zaidi.
UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana kwamba hakuna uwekezaji wa maana uliofanywa katika sekta ya Kilimo hapa nchini. Nasema hivi kwa sababu kwa mujibu wa tamko la Maputo “Maputo Declaration on Agriculture and Food Security in Africa” kuhusu Kilimo na usalama wa Chakula kila nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) inatakiwa kutenga angalau asilimia10 ya bajeti ya Taifa, na kuilekeza kwenye sekta ya Kilimo ili kusaidia ukuaji wa sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, Tanzania toka kusaini tamko hilo mwaka 2003, haijawahi kutenga bajeti kwa sekta hiyo zaidi ya 6% ya bajeti ya Taifa. Kwa mfano mwaka wa fedha 2016/17 fedha za maendeleo zilizotolewa zilikuwa ni chini ya asilimia 3 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge ya Tshs bilioni 101.5 Kwani hadi Kambi Rasmi inawasilisha Maoni yake zilikuwa zimetolewa shilingi bilioni 2.25 sawa na asilimia 2.22 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya maendeleo katika sekta ya kilimo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili; ni muujiza gani utatendeka ili kilimo kiweze kusukuma uchumi wa viwanda ikiwa haitengi fedha za kutosha katika sekta hiyo?
Mheshimiwa Spika, ili kuonyesha msisitizo wa wa umuhimu wa sekta ya kilimo Umoja wa Afrika ulikutana tena Malabo, Equatorial Guinea tarehe 26-27 Juni, 2014 na kuweka vigezo vya upimaji wa ukuaji wa Sekta ya Kilimo katika nchi wanachama. Moja ya azimio la Malabo ni kilimo kuchangia au kukua kwa angalu 6% kwenye pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na azimio hilo, Tanzania bado imeshindwa kutekeleza. Takwimu zinaonyesha kwamba; kwa miaka miwili 2015 na 2016 ukuaji wa kilimo nchini Tanzania ulikuwa ni 2.3% na 1.7% kwa mfuatano.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 – 2016/2017 Kilimo na Ushirika (Fungu 43) imepata wastani wa TZS 250 bilioni ambayo ni sawa na 1.8% tu ya bajeti ya taifa. Kati ya wastani huo, bajeti ya maendeleo ilipata wastani wa TZS 80.3bilioni ambayo ni sawa na 32% tu ya bajeti ya kilimo na ushirika na 1.6% ya bajeti ya maendeleo taifa.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Wizara ya Kilimo kupitia fungu 43 kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilitengewa jumla ya Shilingi 206,816,421,000/-. Kati ya fedha hizo, Shilingi 174,103,348,000/- zilikuwa ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi 32,713,073,000/- ni fedha za maendeleo. Hadi mwaka huo wa fedha unamalizika Wizara ilipokea shilingi 2,663,428,542/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikiwa ni fedha za ndani na shilingi 5,035,062,321/- zikiwa ni fedha za nje, na hivyo kufanya jumla ya fedha za maendeleo kwa fungu 43 zilizopokelewa kwa mwaka 2015/16 kuwa shilingi 7,698,490,863/- sawa na asilimia 23.53 ya fedha za maendeleo zilizopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 43 lilitengewa jumla ya Shilingi 210,359,133,000 ziliombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 100,527,497,000 zilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Fedha za ndani zilikuwa shilingi 23,000,000,000/- na fedha za nje shilingi 78,527,497,000/- Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 fedha zilizokuwa zimetolewa na shilingi 2,251,881,250/- sawa na asilimia 2.22 tu na kati ya fedha hizo fedha za ndani zilikuwa shilingi 1,382,191,924/- na fedha za nje shilingi 349,081,000/-
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/18 wizara fungu 43 imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 214,815,759,000/- kati ya fedha hizo shilingi 150,253,000,000/- ni fedha za maendeleo, lakini hadi mwezi Machi 2, 2018; shilingi 16,520,540,444/- zimetolewa ambazo ni sawa na asilimia 11 ya fedha zilizoidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 wizara fungu 43 linaombewa jumla ya shilingi 162,224,814,000/- kati ya fedha hizo shilingi 64,105,298,000/- ni fedha za miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/17, sehemu ya Kilimo kifungu cha 3.2.3.3 kinaonesha kuwa; “Lengo ni kuhakikisha uwepo wa chakula cha kutosha na upatikanaji wa uhakika wa malighafi za uzalishaji katika viwanda vya mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, ufinyu wa bajeti ya maendeleo inayoenda kwenye kilimo fungu 43 ni dhahiri kwamba dhamira ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano kama ilivyonukuliwa hapa juu haiwezi kufikiwa hata kwa robo yake. Hii ni kutokana na mwenendo wa utoaji wa fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi ya kilimo kulingana na bajeti zinazokuwa zimeidhinishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwa Serikali kuheshimu ahadi yake ya kutenga walau asilimia 10 ya bajeti yake kwa sekta ya kilimo kama inavyoonekana katika Azimio la Maputo. Kwa mgawo huu wa sasa ambapo chini ya asilimia 10 ya fedha za serikali zinatengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo tuna wasiwasi kwamba malengo yaliyopangwa hayatafikiwa.
Mheshimiwa Spika,kwa bahati mbaya sana sekta ya kilimo imekuwa haipewi umuhimu kama ule ilionao katika uchumi wa nchi. Ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha Ukomo wa Bajeti ya mwaka 2018/19 na kutoa mrejesho wa matumizi kwa bajeti ya mwaka 2017/18; alisema yafuatayo:-
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgao wa bajeti ni pamoja na: kulipa deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma; kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia elimu-msingi bila ada; utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa tiba”.
Mheshimiwa Spika, kwa nukuu hiyo; Kilimo sio kipaumbele kwa Serikali. Vipaumbele ni kulipa madeni (kwa kifupi bajeti ya mwaka huu tunaweza kuiita ni bajeti ya madeni). Si vibaya kulipa madeni lakini lazima pia kuzingatia uwekezaji katika sekta muhimu za uzalishaji kama kilimo ili sekta hizo ziweze kuzalisha fedha ambazo zitatumika kulipa hayo madeni. Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa na Serikali hii kujinasibu kuwa inajenga uchumi wa viwanda wakati sekta ya kilimo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa malighafi za viwandani si kipaumbele chake.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji. Tofauti na nchi nyingi majirani, nchi ya Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha za maji safi – mito, maziwa, maji ya kwenye miamba, na ardhioevu – za kutosheleza mahitaji yake yote ya sasa ya maji.
Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Tanzania wa Kusaidia Rasilimali za Maji wa Mwaka 2006 unatambua umuhimu wa kipekee wa maji katika utendaji kazi wa sekta muhimu za kiuchumi na ustawi wa Watanzania. Mkakati huu unabainisha athari za uwekezaji duni katika: (a) usambazaji wa maji na huduma za usafi kama hitaji la msingi kwa maisha zalishi (b) uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa umeme wa maji kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula na nishati ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, Mkakati huu unabainisha namna utendaji kazi wa sekta kuu za uchumi (nishati, kilimo, viwanda, mifugo, uchimbaji madini, utalii, na uvuvi) zinavyoathirika kutokana na ukame, mafuriko, na usimamizi duni wa rasilimali za maji. Pia, unasisitizia haja ya kufanya juhudi za haraka za kupanua uwekezaji katika uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji, udhibiti mzuri wa rasilimali za maji, na ulinzi na uhifadhi wa vyanzo muhimu vya maji – mito, maziwa, maji ya kwenye miamba, na ardhioevu.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, ushahidi huo ni ukweli kabisa kuwa Maendeleo ya kijamii na kiuchumi yana uhusiano wa moja kwa moja katika upatikanaji wa rasilimali ya maji na utunzaji wa mazingira. Maji ni rasilimali inayomalizika kama haikutunzwa ili kuwa endelevu, hivyo maendeleo ya kilimo, mifugo, viwanda vyote vinatagemea upatikanaji wa uhakika wa rasilimali ya maji.
Mheshimiwa Spika,ni ukweli pia kuwa mahitaji ya matumizi ya maji yanazidi kuongezeka, japokuwa upatikanaji wa maji unazidi kupungua na mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka kutokana na ukweli kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka, kutokuwa na mifumo mizuri ya kuhifadhi maji ya mvua (Inadequate rain-water storage), mabadiliko ya tabianchi pamoja na shughuli za kiuchumi ambazo hazizingatii utunzaji wa mazingira ambayo ndicho chanzo kikuu cha maji mengi ya mito yetu. Hivyo ni lazima kuwa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha maji yaliyopo yanatumiwa kwa uagalifu na uendelevu.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la maji na kuifanya rasilimali hii kutumika kwa uangalifu na kwa uendelevu baina ya makundi yote ya kijamii, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwa ni lazima mahitaji kwa kila kundi katika mfumo mzima wa uzalishaji(kilimo,mifugo,viwandani na majumbani) lijulikane mahitaji yake (water demand) kwa siku ni lita ngapi, hapo ndipo tunapoweza kupanga mgawanyo wa uendelevu.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwa sasa hakuna huduma yoyote ya kijamii inayotolewa bure na Serikali, Hiyo elimumsingi ambayo wanasema elimu bila ada, maana yake yake kama tunaona elimu ni ghali tujaribu ujinga na hilo ndilo linaenda kuizamisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere, kwani sasa ni bora elimu na sio elimu bora.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa “huduma ya maji” hakuna eneo lolote katika Tanzania ambalo wanapata maji ya bomba bila ya malipo ya aina yoyote. Hivyo huduma hii ya maji, iwe ni kwa matumizi ya majumbani, matumizi ya mifugo, matumizi ya viwandani au kwa matumizi ya kilimo, hiyo yote ni sehemu ya biashara kama biashara zingine.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya Wizara inaonesha kuwa mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ili ukamilike unahitaji kiasi cha dola za Kimarekani milioni 215, na Serikali imeshindwa kukubaliana na wawekezaji kwani fedha hizo zitaongeza deni la Taifa kwani zitakopwa kwa masharti ya Kibiashara.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumetangulia kusema, kuwa hakuna huduma ya bure na hivyo ukiangalia mwongozo wa biashara kwa mradi huo ni dhahiri inajulikana wanufaikaji ni wangapi na kwa muda gani uwekezaji huo utakuwa umerejesha fedha hizo. Kwa mantiki hiyo basi kushindwa kumalizia mradi huo ambao kwa sasa umeishachukua takriban miaka zaidi yam inane (8) na wakati huo huo thamani ya shilingi yetu dhidi ya dolla inazidi kuporomoka.
Mheshimiwa Spika, mtazamo huo wa Serikali maana yake ni kwamba miradi mingi ya huduma za jamii hazitakuja kukamilika kwa miaka ya karibuni hadi watu wenye muono wa kibiashara watakapo kuwa kwenye madaraka.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika randama uk. Wa 44 hadi uk. Wa 49 kuna miradi ya maji inayofanyiwa usanifu na mingine inayoendelea au mingine iliyokamilika (Mradi wa Same -wanga-Korogwe,Maji mkoa wa Kigoma, mradi wa maji wa Ntomoko, Maradi wa Chiwambo, mradi wa Ukarabati na ujenzi wa Mabwawa, Mradi wa Maji wa Lukululu n.k) lakini mingi haifanyi kazi na imetumia fedha nyingi na mingine inailazimu Wizara itoe maelekezo kuwa miradi mingine isitekelezwe na Halmashauri kutokana na sababu zao na hivyo mamlaka za maji za mikoa zihusishwe katika utekelezaji wake. Lakini hoja ya msingi ni je ikishatekelezwa ni mamlaka ipi itakuwa inaiendesha miradi hiyo? Hapa ndipo kutupia mpira kunapoanzia, kwani waendeshaji watasema haikujengwa kwa kiwango kinachohitaji na visingizo vingine kama hivyo.
Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa miradi mikubwa Serikali inaweza kuingia katika ubia na Sekta binafsi na miradi kutekelezwa kwa utaratibu wa Kujenga mradi na kuuendesha na baadae kuurudisha Serikali (Build Operate and Transfer-BOT). Utaratibu huu kwa mazingira yetu ambayo Serikali imeshindwa kupata mikopo ya masharti nafuu-(concessional/soft loans) ndio utaratibu utakaokuwa suluhisho katika miradi ya maendeleo. Na katika hili mjenzi wa mradi kwa njia ya ubia naye ndiye atakauwa muendeshaji hadi fedha zao zilizowekwa kwa mujibu wa mkataba zitakaporudi na faida ndipo mradi utaendeshwa na mbia mwenza (Halmashauri).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa hili inasisitiza mikataba kuwa wazi na yenye tija baina ya wabia watakao husika katika utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.
MFUKO WA MAJI
Mheshimiwa Spika, mfuko wa maji unachangiwakwa makato ya watumiaji wa mafuta ili kutuna, lakini makato hayo hayawezi kuwa ya milele bila kuwepo kwa ukomo kuwa mfuko unaweza kujiendesha wenyewe, kama ni hivyo huo sio mfuko bali ni kitu kingine. Mfuko kwa maana ya mfuko unatakiwa ukishafikia muda Fulani ni lazima uweze kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, kwa dhana hiyo ya mfuko, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia mfuko huo kuingia katika ubia na Sekta binafsi kuendesha miradi mikubwa ya maji kama vile miradi ya umwagiliaji, miradi ya marambo kwa ajili ya ufugaji na miradi ya maji kwa ajili ya katumizi ya majumbani. Kwa njia hii ni dhahiri mfuko utazidi kuwa endelevu na hivyo kupunguza kilio cha kila siku kuwa Serikali haina fedha.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza uhusishwaji wa Sekta binafsi katika hatua zote za utoaji wa huduma za msingi hasa miradi ya maji, kwa kutokana na historia ya matumizi ya Serikali inaonesha kuwa sekta ya maji imetumia fedha nyingi sana lakini upatikanaji wa maji hauakisi thamani halisi ya fedha zilizowekezwa.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama uk. Wa 50 Serikali kwa kushauriwa na shirikia la Maendeleo la kimataifa la Uingereza(DFID) wamebuni mpango wa kuimarisha uendelevu wa Huduma ya maji vijiji-mfumo wa malipo kwa matokeo. Hii ni kutokana na miradi mingi kutokuwa endelevu na hivyo kuwa changamoto kubwa sana kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo hili kwa kiasi kikubwa ni kutohusisha sekta binafsi na hivyo kukosekana kwa dhana nzima ya umiliki wa miradi hiyo, fedha za mikopo au ufadhili zinaonekana kutokuwa na mwenyewe (Kasumba ya Mali ya umma haina mwenyewe) kwa kuanzia na hatua za mwanzo kabisa za usanifu na utekelezaji wa miradi na inapofikia hatua ya uendeshaji ndipo balaa la ufujaji wa fedha linapogundulika. Tunatakiwa kuondoa kwanza kasumba hiyo kwa watendaji kwa kupitia umiliki na uendeshaji wa Sekta binafsi kwa miradi ya maji.
Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa vyombo vya watumiaji maji (COWSOs) kuhusu uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa suala hili halitoweza kutoa suluhisho la tatizo lililopo katika miradi hiyo, kwani watumiaji hawana umiliki wowote kwa maana ya uchangiaji wakati mradi unaanza na kutekelezwa.
UTAFUTAJI WA FEDHA ZA MIRADI YA MAJI
Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 53 wa Randama unaonesha kuwa mbali na kupatikana na ahadi za dola za Kimarekani bilioni 1.93 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Pili ya maendeleo ya Sekta ya Maji, pia Serikali ina kamilisha majadiliano kwa ajili ya mikopo ya masharti nafuu yenye jumla dola za Kimarekani milioni 829.7.
Mheshimiwa Spika, Programu ya pili ya Sekta ya Maendeleo ya Maji (WSDP-II) inatakiwa kutekelezwa kwa gharama ya dolla za kimarekani bilioni 3.3, lakini kuna kitu kinachoitwa Joint Supervision Missions, nadhani hii pia ni njia ya kupunguza fedha na kuzirudisha kule zinapotoka wakati ni mkopo unaotakiwa kulipwa. Hapa wameishabaini kuwa tatizo kubwa la miradi ya maji hapa Tanzania ni uendeshaji wa miradi hiyo na hivyo wameamua kuja na ujanja huo.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa tangu mwaka 2006- WSDP-I ilipoanza, jumla ya miradi 1810 ilipangwa kutekelezwa, lakini hadi sasa ni miradi 1493 ndiyo imekamilika na miradi 366 inaendelea kujengwa. Aidha, vituo vya kuchotea maji 123,888 vilijengwa lakini vinavyofanya kazi ni vituo 85,286 na vituo 38,602 havifanyikazi kabisa.
Mheshimiwa Spika, katika miradi hiyo yote ni kuwa fedha zilikwishatolewa lakini matokeo yake wananchi wanaendelea kukosa maji. Kambi Rasmi ya Upinzani inaelewa kuwa hata hiyo miradi ambayo Serikali inasema kuwa imekamilika kwa ajili ya matumizi ya wananchi,uwezekano mkubwa ni kuwa iko pale lakini wananchi hawanufaiki nayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kwamba richa ya jitihada hizo za kutafuta mikopo lakini bado tunatatizo la uendelevu wa miradi, kama tulivyo shauri ni muda mwafaka sasa PPP itakayohusisha BOT ndilo litakalokuwa suluhisho la uendelevu wa miradi ya maji (kwa kilimo, matumizi ya nyumbani, mifugo na viwandani).
Uwekezaji Mdogo na Usioaminika katika miundombinu kwa ajili ya Sekta nyingine Zinazotumia Maji.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ina kiwango cha juu kabisa cha uwezo wa kuhifadhi maji asilia barani Afrika, lakini bado nchi hii inategemea kilimo cha maji ya mvua. Kilimo kinachotegemea maji ya mvua kinasaidia maisha ya watu takriban asilimia 80 lakini kinaathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi. Chini ya asilimia 20 ya eneo linaloweza kumwagiliwa ndilo linalomwagiliwa kwa sasa, na kuna hifadhi ndogo sana ya maji ya mvua yatakayotumika kwenye kilimo kwa ajili ya kujihami na vipindi ambapo maji ya mito hupungua sana.
Mheshimiwa Spika, mbali na uwekezaji mdogo katika kilimo cha umwagiliaji mahitaji ya maji kulingana na ongezeko na kupanuka kwa makazi ya watu yanazidi kuwa makubwa lakini rasilimali watu na fedha ni kidogo mno kukabiliana na mahitaji. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona itakuwa ni vyema kuwekeza vya kutosha katika kuhakikisha miradi yote ambayo imeishaanza inamalizika kabla ya kuanzisha miradi mipya ambayo haina uhakika wa fedha za utekelezaji.
Kiwango kidogo cha Uratibu wa Kisekta na Uwezo wa Kitaasisi.
Mheshimiwa Spika,Sekta hii bado inakabiliwa na tatizo la uratibu duni wa mipango na maendeleo miongoni na baina ya sekta. Utengano huu unasababisha kushughulikia kwa mtazamo finyu maji kama suala la kisekta (yaani, usambazaji wa huduma ya maji, usafi, na utupaji wa maji taka) badala ya kushughulikia maji kama kipaumbele kikubwa na kugharimia maendeleo na usimamizi wake kama kitovu cha mafanikio kwa sekta kadhaa kuu za uchumi. Jambo hili ni muhimu katika kufanikisha nguzo za ukuaji wa uchumi za Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini Tanzania (MKUKUTA) kukuza kipato binafsi, ubora wa maisha, na utawala bora.
MAPITIO YA BAJETI KWA MIRADI MAENDELEO YA MAJI
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 Wizara ya Maji na Umwagiliaji Fungu 49 na Fungu 05 iliidhinishiwa jumla ya shilingi 565,862,426,195. Fungu 49, liliidhinishiwa jumla ya shilingi 512,235,736,000 kati ya fedha hizo shilingi 26,966,326,000 ni fedha za matumizi ya kawaida (fedha hizi zinajumuisha mishahara shilingi 17,960,716,000 na matumizi mengineyo shilingi 9,005,610,000). Na kiasi cha shilingi 485,269,410,000 zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2016, fungu 49 lilikuwa limepokea fedha za maendeleo shilingi 136,900,281,752 tu kati ya shilingi 485,269,410,000 zilizotengwa ambazo nisawa na asilimia 28 ya bajeti yote ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Fungu 05 iliidhinishiwa jumla ya shilingi 53,626,690,195. Kati ya fedha hizo shilingi 232,116,195 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 53,394,574,000 ni fedha kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Hadi kufikia tarehe 31, Machi, 2016 fedha za matumizi ya kawaida kiasi cha shilingi 96,884,227 zilitolewa ambayo ni sawa na asilimia 42 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge. Fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 5,131,032,985 zilitolewa ambazo ni sawa na asilimia 10 ya fedha zilizoidhinishwa. (Fedha hizo ni fedha za nje tu na hakuna fedha za ndani zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo).
Aidha, Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliidhinishiwa kiasi cha shilingi 53, 394, 574,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati mahitaji halisi yanakadiriwa kufikia shilingi 400,000,000,000. Uwiano huu hauonyeshi dhamira ya dhati ya Serikali ya kutambua na kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na kilimo cha umwagiliaji.Rejea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo ya mwaka 2016/17
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 49 na Fungu 05 yaliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,001,658,553,800. Fungu 49 likiidhinishiwa jumla ya shilingi 938,246,195,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 913,836,029,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Aidha,Fungu 05 lilitengewa jumla ya shilingi 63,412,358,800. Kati ya fedha hizo, shilingi 58,905,747,200 zilikuwa ni kwa ajili ya kutekelezamiradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, lakini hadi mwaka huo wa 2016 /17 una malizika wizara fungu 49 ilipokea fedha za maendeleo jumla ya shilingi 230,997,934,672. tu sawa na asilimia 25.7 ya bajeti yote ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 fungu 49 liliidhinishiwa na Bunge fedha za maendeleo jumla ya shilingi 623,606,748,000. Lakini hadi mwezi Machi 2018 fedha za maendeleo zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi 135,191,256,566 tu, sawa na asilimia 22 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji-fungu 49.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 bunge linaombwa kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo yenye jumla ya shilingi 673,214,033,677 jambo ambalo litafanyika. Lakini kwa kuangalia miaka mitatu ya nyuma ambavyo Bunge limekuwa likipitisha fedha za maji kwa bajeti inayoletwa na Wizara na fedha halisi zinazotolewa zikipungua kila mwaka ni dhahiri kuwa Maji sio kipaumbele kwa Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi ambayo imekosa fedha na iliyopatiwa fedha ni dhahiri kwamba tunachokipanga na kukipitisha hapa Bungeni, kinakuwa sio kinachopatiwa fedha; mfano mradi wa maji toka ziwa viktoria kwenda Kahama-Shinyanga-Tabora ulitengewa shilingi bilioni 1 lakini hadi Mwezi Machi 2018 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa. Mradi wa Masasi-Nachingwea hakuna fedha yoyote iliyotolewa, Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda zilitengwa shilingi bilioni 10 lakini hakuna fedha iliyotolewa. Mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji katika miji ya Same na Mwanga shilingi bilioni 12 lakini hadi Machi hakuna fedha iliyotolewa na Hazina. Mradi wa kupanua na kukarabati miradi ya maji vijijini ambayo inaendelea ya shilingi bilioni 20.7 hakuna fedha zilizotolewa hadi Machi 2018, (rejea Jedwali na.5 uk.14 hadi 16 wa Randama, fungu 49)
Mheshimiwa Spika, hapa kuna miradi ambayo toka imeanza kuandikwa kwenye vitabu vya bajeti ni zaidi ya miaka 7 sasa nab ado haioneshi kama inamalizika, kama mradi wa bwawa la kidunda na Mpera na Kimbiji. Madhara yake ni kwamba gharama zinazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na ukweli kwamba thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Kimarekani inazidi kuporomoka. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni muda mwafaka sasa kwa Serikali kabla ya kuanzisha miradi mipya tumalize miradi iliyopo tayari, kinyume cha hapo ni kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi. (Matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi)
Mheshimiwa Spika,Mradi wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 6.66 Kuchelewa Ukamilishaji, Tarehe 25 Mei 2015 MWAUWASA iliingia mkataba na kampuni ya M/s Jassie& Company Limited wa Ujenzi wa Miundombinu ya Maji Safi na Majitaka katika Mji wa Geita wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.66. Mradi huu ulipangwa kuanza mwezi Juni 2015 na kumalizika ndani ya siku 360. Hata hivyo, hadi mwezi Novemba 2017, mradi ulikuwa haujakamilika na mkandarasi ameshaondoka eneo la kazi. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa hizi ni fedha za walipa kodi na matumizi kama haya yanapofanyika wahusika wanahamishwa toka eneo moja kwenda eneo lingine. Katibu Mkuu wa wakurugenzi wa wizara wapo ofisini wanazunguka kwenye viti vyao tu.
UHIFADHA WA VYANZO VYA MAJI
Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa vyanzo vya maji nchini unafuata taratibu za mipango shirikishi ya usimamizi wa rasilimali za maji kwenye Bodi za Maji za mabonde tisa yaliyopo nchini, ambapo saba katika hayo yanahusisha majishirikishi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa iliyopo kwenye usimamizi wa rasilimali za maji ni kupungua na kuharibika kwa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji na katika misitu ya hifadhi ya maji (catchments forests and wetlands). Hifadhi hizi zinawezesha upatikanaji wa maji juu na chini ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, Takwimu za kitaifa za rasilimali za maji zilizopo zinaonesha kuwa kiasi cha maji kwa sasa kwa kila mtanzania ni wastani wa mita za ujazo 1,952 kwa mwaka. Endapo hatua madhubuti za utunzaji wa vyanzo vya maji hazitachukuliwa mapema, kiasi hicho kinatarajiwa kupungua hadi kufikia mita za ujazo 883 mwaka 2035. Kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa ni mita za ujazo 1,700
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri hapa kama hatutachukua hatua stahiki si muda mrefu Tanzania inaweza kuwa kwenye tatizo kubwa la maji kama ambavyo ilivyo sasa katika Mji wa Cape Town-Afrika ya Kusini ambapo ukosefu wa maji linakuwa janga kubwa na hivyo kupelekea rasilimali hiyo kuwekewa utaratibu wa jinsi gani ya kugawanywa kwa kila familia, mifugo na kwa matumizi ya viwandani.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa mabonde, Kambi Rasmi ya Upinzani itaonesha umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya bonde la Rufiji ambalo chanzo chake ni mabonde ya Kilombero na Ruaha.
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe hapa kwamba, Mto Rufiji hupata maji yake mengi kutoka mito miwili mikuu—Kilombero na Ruaha Mkuu—na hasa Mto Kilombero, ambao huchangia theluthi mbili ya maji ya Mto Rufiji kabla hayajafika Stiegler’s Gorge. Hivyo ustawi wa Mto Rufiji unategemea ustawi wa Mto Rufiji; ambao nao pia unategemea (kwa asilimia 60) ustawi wa Mto Kilombero; hususan Bonde la Mto Kilombero.
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri, kwamba uwezekano wa Watanzania kupata umeme wa maji wa bei nafuu kutoka Stiegler’s Gorge, ni ndoto inayokaribia kuwa ya kweli endapo Serikali itashindwa lichukua hatua za kuhifadhi (conservation measures) Bonde la Mto Kilombero, kwani ustawi wa bonde hilo hivi sasa unasambaratishwa na shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, Wataalamu wanakubaliana kwamba, uharibifu wa mazingira ukiongeza na tatizo la sasa linaloikumba dunia nzima—mabadiliko ya tabianchi (climate change), vinaashiria kuwa muda si mrefu Bonde la Kilombero linaweza kupoteza sifa yake ya kuwa bonde adhimu la maji baridi ambalo ni kubwa kuliko yote duniani, lililokuwa linajaa maji misimu yote.
Mheshimiwa Spika, kitu pekee ambacho wataalamu hao wanatofautiana, ni muda uliobakia kabla Bonde hilo halijasambaratika kabisa. Ni muhimu Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge kuhusu hali halisi ya Bwawa la Ngapemba lililopo katika Kata ya Utengule na lile la Kibasila ambayo ni makubwa na yamekuwepo kwa miaka mingi likiwa ni chanzo kikuu cha shughuli za kiuchumi kwa wanavijiji wanaozunguka Bonde la Kilombero. Bwawa hilo Ngapemba lililokuwa na ukubwa wa eka za mraba 1,000 na lililokuwa na hekaheka nyingi za uvuvi, sasa limenyauka na kusinyaa na kubakia eka chache sana za mraba.,
Mheshimiwa Spika, Utafiti uliofanywa na JET kuhusu hali ya mito kati ya Kihansi na Ifakara, unaonyesha zamani kuwa kulikuwapo na mito 29, lakini sasa imebaki mito mitano tu, huku mito tisa ikiwa na maji yaliyotuama. Miongoni mwa mito hiyo mitano ambayo inatiririsha maji, ni Luipa, Mpanga na Mnyera ndio bado ina maji ya kutosha mwaka mzima.
Kwa hiyo, hali ya mito katika Bonde la Kilombero ni mbaya, na chanzo kikubwa cha hali hiyo ni uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo ni kwa vipi uzalishaji wa umeme wa maji kwa mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa endelevu?
HUDUMA YA MAJI TAKA
Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma ya uondoaji wa majitaka mijini bado ni tatizo kubwa sana, hii ni kutokana na uwekezaji mdogo katika utoaji wa huduma hii. Takwimu zinaonesha kuwa ni miji 11 tu ndiyo yenye mifumo ya uondoaji wa maji taka, na ni asilimia 20 tu ya wakazi wa mijini ndio waliounganishwa na mtandao wa majitaka.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tunashauri kwamba ni muda mwafaka haya maji taka yasafishwe na kuingizwa upya kwenye mfumo wa matumizi (recycling). Na tulitoa mfano wa Singapore kama nchi inayotumia vizuri rasilamli ya maji.
Mheshimiwa Spika, hoja hiyo inapata nguvu kutokana na ukweli kuwa kwa mwaka 1962 wastani wa matumizi ya maji kwa mtu yalikuwa ni mita za ujazo 7,862 kwa mwaka na mwaka 2002 zikashuka hadi 2,700 na kwa mwaka 2017 zikashuka hadi 1,800 na tunaambiwa ifikapo mwaka 2015 kiwango hicho kitashuka hadi 1,500. Wastani unaohitajika ni mita za ujazo 1,700, chini ya hapo ni balaa na nchi inawekwa kwenye kundi lenye uhaba mkubwa wa maji Duniani, (Randama uk.1).
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuanza kufikiria au kukaribisha wawekezaji wa kuweza ku-recyclemajitaka ili hapo baada tuweze kuwa salama kwani viashiria vya upungufu wa maji viko wazi kabisa na jambo hilo halihitaji kubishaniwa au kufanyiwa tafiti.
Mheshimiwa Spika, kuna watu wanajiaminisha kuwa tuna maziwa makubwa hapa kwetu na hivyo maji sio tatizo, lakini wafahamu kwamba uwekezaji wa kuyatoa maji hayo kwenye hayo maziwa na kuyaleta kwenye miji mingi na gharama ya kufunga mitambo ya kusafisha maji hayo ni vitu viwili ambavyo uwezi kulinganisha.
UJENZI WA MAOFISI
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama uk.51 kigungu cha 3.4.2.4 ukarabati na ujenzi wa majengo ya Wizara. Hili kwa kweli linatusumbua kwani, ujenzi wa maji house Dar es Dar es salaam jingo lenye ghorofa 13 na pale pale kuna ujenzi wa Makao Makuu ya Wizara. Hizi zote ni fedha ambazo zingetakiwa ziingie katika utoaji wa huduma. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa majengo bado ni mengi kwa watendaji kufanyia kazi na sio jambo la haraka kiasi cha kupelekea miradi ya maji kukosa fedha za kumalizia miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi utendaji katika Serikali unaunganishwa katika mtandao mkuu wa Utumishi, na pia malipo yote kwa huduma zinazotolewa na Serikali zinakuwa kwenye mfumo wa e-payment uliopo Hazina au TRA. Kwa muktadha huo inakuwaje taasisi za kutoa huduma kwa wananchi zinaweza kutumia Mamilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi badala ya fedha hizo kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi? Mfano Mzuri ni MWAUASA ambao wametumia takriban Bilioni 1 kwa ujenzi wa Ofisi wakati wakazi wa Mji wa Mwanza wanapata shida ya maji, na wakati huo maji yamejaa ziwa viktoria. Rejea taarifa ya CAG
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano ilikuja na zuio la mikutano ya hadhara ambalo kila mmoja anajua linakiuka sheria ya Vyama vya Siasa ambavyo vina haki kikatiba na kisheria ya kufanya kazi za siasa ikiwa ni pamoja na mikutano na maandamano.
Mheshimiwa Spika, Demokrasia ni msingi wa haki na amani wa nchi yetu. Hata hivyo Jeshi la Polisi limeendelea kuzuia kazi za siasa nchini hususani mikutano ya hadhara pamoja na kazi za ndani za Vyama.
Mheshimiwa Spika, Hatua hii inatazamwa kama ni kukisaidia Chama Tawala kwa macho ya wale wenye fikra za kipumbavu. Lakini mwanzo wa fikra hii unatazamwa kama ushindi kwa Chama cha Mapinduzi lakini ni hatari kwa ustawi na usalama wa nchi, kwani ni dhahiri kwamba watu wakaposhindwa kujieleza kwa kutumia mifumo rasmi ya kisheria bila shaka taifa letu litaingia kwenye majanga makubwa na huenda ukatokea mgogoro mkubwa katika jamii.
Mheshimiwa Spika, Demokrasia ya haki ni msingi wa amani ambapo wanaopishana katika fikra wanashindana kwa hoja, kufanikiwa kuondoa demokrasia ni kuwatafutia wanaopishana kwa hoja kutafuta njia nyingine ya kupigania uhuru na haki zao. Serikali makini itakuwa na wajibu wa kuimarisha demokrasia ya haki na sio kudidimiza kama ambavyo inafanyika sasa. Kwa bahati mbaya viongozi waandamizi wa serikali wanaitazama demokrasia kama mtu binafsi na sio moja misingi ya tunu ya amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika utawala huu wa serikali ya awamu ya tano, tumeshuhudia vyama vya Upinzani wakipitia katika majaribu makubwa ya demokrasia. Vyama kama CHADEMA, CUF na ACT Wazalendo wamekuwa wahanga wakubwa wa manyanyaso kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo. Wengi wa wafuasi na viongozi wa Vyama hivi wako magerezani na au wanatakiwa kuhudhuria Mahakamani katika kesi mbalimbali zenye sura ya kisiasa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, mathalani Mkoani Mwanza Kamanda wa Jeshi la Polisi Ahmed Msangi amefikia hatua ya kuwakataza wafuasi na wanachama wa CHADEMA kushiriki misiba wakiwa na sare za Chama au bendera. Aidha, hawaruhusiwi hata kufanya vikao vyao vya kikatiba vya ndani, huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na serikali inamfumbia macho mpaka leo.
Mheshimiwa Spika, tarehe 17 Aprili, 2018 baadhi ya Viongozi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA walikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro usiku wa manane wakiwa wamepumzika na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa bila kuelezwa kosa lao wala sababu za wao kuvamiwa na kusweka rumande.
Mheshimiwa Spika, baada ya Jeshi la Polisi kukaa na viongozi hao kwa muda zaidi ya masaa kumi waliaachia bila masharti yoyote kwa maelekezo kuwa wakiwahitaji watawapigia simu. Huu ni udhalilishaji mkubwa ambao unafanyika katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa na ziara yake Pemba, wanachama na wapenzi wa demokrasia walizuiwa kumpokea katika Uwanja wa Ndege, aidha amezuiwa mara kadhaa kutembelea Mikoa ya Lindi na Tanga ambapo Chama hicho kina viongozi wa kuchaguliwa na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Haya yote yakifanyika dhidi ya CHADEMA, CUF na Vyama vingine vya Upinzani Katibu wa CCM wa Itikadi na Uenezi amekuwa akifanya mikutano ya hadhara kwa kivuli cha ufuatiliaji wa utekelezaji wa ilani ya CCM na huku Mwenyekiti wake Rais Magufuli akitumia mikutano ya kiserikali kufanya shughuli za kisiasa kama vile kupokea Madiwani ambao wamesaliti utumishi kwa wananchi wao kwa njia ambazo zinatiliwa mashaka makubwa na kila raia wa Tanzania. Mathalani Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alifanya tukio la kisiasa kwenye hafla ya Kijeshi Jijini Arusha jambo ambalo ni hatari sana kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu, kwani ni hatua ambayo inatafsiri kwamba Jeshi nalo ni sehemu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa ni kosa kutumia majukwaa ya serikali kufanya shughuli za kisiasa au kutumia mali na pia Vyombo vya Dola kukandamiza Vyama vingine vya Siasa. Haya yote yanafanyika wazi bila kificho na Serikali inaonekana kuyabariki yaendelee huku wakijua mambo hayo yanajenga chuki miongoni mwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Tunayo nafasi finyu katika hotuba hii ya kueleza matukio ya ukatili wa Polisi dhidi ya raia wa nchi hii.Tunasisitiza kuwaKatiba yetu inaruhusu mfumo wa Vyama vingi vya Siasa na sheria zetu zinatoa haki na wajibu kwa Vyama hivyo katika kuendesha shughuli zao za kisiasa nchini. Haki ya Kujumuika na haki ya kujiunga na Chama chochote au taasisi nyingine yoyote zinajumuishwa na kuitwa haki za kiraia hivyo kuwapa mateso mpaka vifo watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusiana na Vyama vya Siasa vya Upinzani sio tu kumkosea Mwenyezi Mungu bali ni kukiuka haki ambazo sisi wenyewe tumezikubali kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 17 Februari, 2018 ulifanyika uchaguzi wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha na baadhi ya Kata nchini. Ikumbukwe kuwa uchaguzi wowote unatoa wajibu na haki kwa Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, moja ya haki za Vyama na Wagombea wanaoshiriki uchaguzi ni pamoja na haki ya kuwa na Mawakala katika kila kituo cha uchaguzi na pia wakala wa ziada kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi. Katika hali ya kushangaza mpaka kufikia tarehe 16 Februari, 2018 majira ya jioni Mawakala wa CHADEMA walikuwa hawajapewa viapo vyao vya Uwakala pamoja na kuwa ni takwa la kisheria viapo hivyo kutolewa siku saba kabla ya uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi kupitia kwa Mkurugenzi wake waliahidi kutoa viapo hivyo kabla ya siku ya uchaguzi jambo ambalo halikutekelezwa. Ulikuwa ni uamuzi wa busara wa mtu yeyote au kiongozi kuhakikisha kuwa Mawakala wake wanakuwa na viapo pamoja na barua za utambulisho wa kuwaruhusu kuingia vituoni.
Mheshimiwa Spika, Kwa kauli za Jeshi la Polisi ni kuwa maandamano ni kosa la jinai na hata kusema neno maandamano kwa sasa inaonekana ni kosa la jinai huku wakijua ni haki ya kikatiba na kisheria. Viongozi wa Chama waliondoka pamoja na wanachama ambao ni Mawakala kwenda kudai viapo na barua za utambulisho kwa ajili ya usimamizi wa kura, ilikuwa ni lazima kulingana na muda pamoja na uhitaji kwani wasingefanya hivyo vituo vyote vingekosa Mawakala.
Mheshimiwa Spika, baada ya Viongozi wa CHADEMA kuondoka na Mawakala kufuata viapo na barua zao za utambulisho, Jeshi la Polisi waliamua kuwatanya kwa mabomu bila hata kutoa onyo na pia walitumia risasi za moto ambazo mojawapo ilimpata Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) AkwIlina AkwIlin.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam kupitia Kamanda wake wa Polisi Lazaro Mambosasa alitoa taarifa kuwa walikuwa wanawashikilia Askari sita ambao walituhumiwa kuhusika na kifo cha Akwelina.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Masauni Masauni alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa wanao ushahidi wa kifo cha AkwIlina ambao utaishangaza dunia.
Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi walinukuliwa wakisema kuwa uchunguzi ufanyike na hatua stahiki zichukuliwe. Katika hali ya kushangaza inaelekea Polisi wameamua kuwatetea Askari hao sita ambao waliwakamata awali na kuamua kuwaachia bila kuchukua hatua yoyote na tunaona jambo hili la kuwaachia Askari lilisababishwa na Maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Mtanzania Mange Kimambi anayeishi nchini Marekani ili kutowavunja moyo Askari ambao waliandaliwa kuzuia maandamano hayo.
Mheshimiwa Spika, Ukistaajabu ya Mussa utaona ya Firauni, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ametangaza rasmi kuwa wamefunga shauri la uchunguzi wa kifo cha Akwelina jambo ambalo linaashiria kuwa Serikali imeamua kuwalinda askari ambao wamehusika kufyatua risasi na kumuua Akwelina.
Mheshimiwa Spika, hatua hii imekuja baada ya dola kujaribu kutumia kila njia kuwabambika kesi ya mauaji ya Akwelina viongozi waandamizi wa CHADEMA jambo ambalo jitihada ovu bado zinaendelea. Kauli ya Mkururgenzi wa Mashtaka (DPP) inaonekana wazi kuwa mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola yanafumbiwa na serikali.
Mheshimiwa Spika,Jeshi la Polisi linatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria ya Jeshi la Polisi na Watoa huduma Wasaidizi wa Polisi ikiwa ni pamoja na Kanuni za Kudumu za Polisi. Aidha kwa upande mwingine wa kusimamia na kuratibu masuala ya uhalifu nchini, Jeshi la Polisi linatumia na linatakiwa kuongozwa na sheria ya Kanuni za Adhabu pamoja na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Mheshimiwa Spika, Ni kwa msingi huo ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapiga marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. Pamoja na msingi na takwa hili la kikatiba vituo vingi vya Polisi nchini vimegeuka sehemu za kutweza utu na kutesa raia badala ya lengo la msingi la ulinzi na usalama wa raia wa Jeshi hilo.
Mheshimiwa Spika, ni hivi majuzi tu Mkoani Mbeya ambapo kijana Allen Mapunda (20) mkazi wa Iyela alifariki muda mfupi baada ya kuachiwa na Jeshi la Polisi, pamoja na Polisi Mkoa wa Mbeya kukanusha kuhusika na kifo hicho lakini mtu yeyote anaweza kuhoji ushahidi wa kimazingira baada ya kijana huyo kuachiwa na jeshi la Polisi kuwa huenda akawa amepigwa na kutweza jambo lililopelekea kifo chake na ndiyo maana Polisi baada ya kuona udhaifu wa mtuhumiwa wakaamua kumwachia huru kukwepa lawama.
Mheshimiwa Spika, huko Sirari Wilayani Tarime Jeshi la Polisi limefanikiwa kumuua Suguta Chacha Kijana mdogo wa miaka 26, hii ni baada ya kaka yake ambaye ni Mheshimiwa John Heche (Mb) ambaye anaendelea kuandamwa na mipango ya kumbambikia kesi ya kudhuru mwili, jitihada ambazo zinaendelea chini ya viongozi waandamizi vya vyombo vya usalama nchini.
Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Machi, 2018 Kituo cha Polisi cha Mwandoya Wilayani Meatu kilichomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kupewa taarifa kuwa mmoja wa mwananchi mwenzao aliuwawa katika kituo hicho akiwa mikononi mwa Polisi.
Mheshimiwa Spika, katika hali kama hii ambayo wananchi wanajikulia sheria mkononi baada ya kukosa imani na vyombo vilivyopewa mamlaka ya kusimamia na kutekeleza sheria kuwa sehemu ya kukiuka sheria husika, hakika mustakabali wa amani na utulivu wa nchi yetu utakuwa mashakani. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Jeshi la Polisi na Polisi wote kwa ujumla kuwa hata kama mfumo wa ndani ya nchi unawalinda kwa ukiukwaji wa Katiba na haki za binadamu bado kuna jumuiya za kimataifa ambapo Tanzania imeridhia mikataba yake ambazo zinaweza kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, matukio kama haya ya watu kuumizwa, kupigwa risasi, kuteswa, kutwezwa na kuuawa ni mengi na hatuwezi kuyaweka yote hapa lakini ripoti zote hizi zinapatikana kwenye taasisi za haki za binadamu na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 23 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinamtaka askari au mtu yeyote anayemkamata mtuhumiwa kumjulisha makosa yake, sio lazima iwe katika lugha ya kitaalam lakini ni haki ya mtuhumiwa kujulishwa makosa yake hata kwa lugha ya kawaida ili ajue sababu za yeye kukamatwa.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu ambao umeanza kuzoeleka katika utendaji wa Jeshi la Polisi ambapo watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa bila kujulishwa makosa yao jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria. Mawakili au ndugu wa watuhumiwa wanapojaribu kuhoji ni kwa nini watuhumiwa wanashikiliwa bila kuelezwa makosa yao wanajibiwa kuwa wanasubiri maelekezo kutoka juu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kupata kauli ya serikali kuwa huko juu ni wapi? Hayo mamlaka mengine ya “amri kutoka juu” ambayo hayajatajwa na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ni yapi? Kwa nini Jeshi la Polisi limerekebisha sheria bila kuletwa Bungeni kwa kutengeneza mamlaka zingine ambazo sio kwa mujibu wa sheria?
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 32 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kinatoa masharti na utaratibu kwa Jeshi la Polisi kumfikisha Mahakamani Mtuhumiwa yeyote ndani ya masaa 24 isipokuwa kwa makosa ambayo adhabu yake ni kifo. Masharti haya yamekuwa kiini macho katika vituo vingi vya Polisi nchi ambapo Jeshi la Polisi limekuwa likiwashikilia Watuhumiwa zaidi ya masaa ambayo yanatakiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kawaida kwa wanachama na viongozi wa Vyama vya Upinzani kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kupelekwa Mahakamani. Jeshi la Polisi linapotakiwa kutoa maelezo kwa nini hawawapeleki Watuhumiwa Mahakamani wanarudia kauli ile ile ya “tunasubiri maelekezo kutoka juu”.
Mheshimiwa Spika, adha ya ukiukwaji huu wa sheria sio tu kwa wanasiasa wa Vyama vya Upinzani tu bali imeenda hata kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo ni majuzi tu ambapo Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul Nondo alikaa kwenye mahabusu za Polisi Iringa na Dar es Salaam kwa zaidi ya siku 15 bila kupelekwa Mahakamani kinyume na utaratibu wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya watu ambao wameshikiliwa kwenye vituo vya Polisi mbalimbali kwa zaidi ya miezi miwili bila kupelekwa Mahakamani, aidha wapo makumi na mamia ya wananchi ambao wamekuwa wakiteseka kwenye vituo mbalimbali vya Polisi kwa muda mrefu kinyume na utaratibu wa sheria kwa tuhuma za makosa ya kimtandao. Kasi ya wananchi kukamatwa kwa makosa yanayodaiwa ni ya mtandao imekuwa kubwa katika serikali hii ya awamu ya tano ambayo ni ishara ya kuminywa kwa uhuru wa mawazo na uhuru kupokea na kutoa habari.
Mheshimiwa Spika, Katika randama ya Wizara fungu 28 ukurasa 5 inaonyesha kuwa jumla ya makosa 2,571 ya mtandao yaliripotiwa kufikia Februari, 2018. Pamoja na takwimu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuhoji kuwa pamoja ubovu wa Sheria ya Makosa ya mtandao ambayo kimsingi inatakiwa kufutwa kabisa, hakuna kifungu chochote cha sheria hiyo ambacho kinawapa Jeshi la Polisi mamlaka ya kuwashikilia watuhumiwa wa makosa hayo kwa muda mrefu bila kuwapeleka Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, imefikia hatua Mawakili na ndugu wa watuhumiwa wa makosa ya mtandao kutoruhusiwa hata kuwapelekea chakula wakiwa mikononi mwa Jeshi hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya serikali hapa Bungeni kama makosa ya Mtandao sasa yametengenezewa utaratibu mpya ambao umekuwa unawatweza na kuwatesa kinyume cha Katiba na sheria za nchi yetu. Taifa linaelekea kuwa la dola la kipolisi kwa sababu ambazo serikali inazijua. Tukiendelea hivi ilivyo, majuto ni mjukuu huja baadae.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasema kuwa; watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kusisitiza msingi huo wa Katiba kwa sababu kumeibuka vikundi vya watu ambao hufanya matukio ya utekaji, utesaji, kuua na kushambulia watu mbalimbali; na mara zote Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama imekuwa ikiwaita watu hao kuwa ni watu wasiojulikana.
Mheshimiwa Spika, Aidha Katiba yetu inaweka msingi na haki katika ibara ya 14 kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria!. Kwa utaratibu ulivyo sasa haki ya kuishi inaweza kuondolewa kwa utaratibu wa Mahakama; ambapo Tanzania bado inatekeleza adhabu ya kunyonga kwa baadhi ya makosa ya jinai.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 4 (2) Katiba inaweka masharti pamoja na mambo mengine kuwa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama vyombo vya utoaji haki nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarejea masharti haya ya Katiba kwa matukio ya utekaji, utesaji, kushambuliwa kwa risasi na kupotea kwa watu nchini inaelekea zipo mamlaka zingine (Kangaroo Courts) ambazo zinahusika na kukamata watu na kuwapa adhabu nje ya mfumo wetu wa utoaji haki.
Mheshimiwa Spika, tarehe 07 Septemba, 2017 hapa Dodoma Mheshimiwa Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi takribani 38 na matundu hayo ya risasi yakionekana kwenye gari lake pamoja na risasi 16 zilizompata kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake, tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Area D hapa Dodoma na watu wale wale “wasiofahamika” walitajwa kuhusika. Mpaka sasa hakuna uchunguzi uliofanywa na wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Jeshi la Polisi zaidi ya kumshuhudia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma akihukumu watu kwenye vyombo vya habari.
Mheshimiwa Spika, Aidha, kumekuwa na mauaji mengi ya raia na askari Wilayani Kibiti ambapo imefikia hatua Mwandishi wa habari wa gezeti la Mwananchi Azory Gwanda na viongozi wa Vyama vya Siasa wengine hawajulikani walipo mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza zipo taarifa kuwa watu hao wasiojulikana wanaowavamia wananchi huwaeleza kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na hivi karibuni Maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Katika muktadha huo huo aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Kata ya Hananasif Marehemu Daniel John alichukuliwa na hatimaye kuuawa na watu waliokuja na gari aina ya Land Cruiser wakijitambulisha kama maafisa wa Jeshi la Polisi. Mpaka sasa Polisi hawajatoa taarifa ya uchunguzi wa kifo hicho.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya uchunguzi ya kuonyesha sababu za kifo (Post-mortem report) inaonesha kuwa Marehemu Daniel alipigwa na kitu kama shoka kichwani, kufungwa kamba kwenye miguu na mikono na hatimaye kunyongwa kwa kutumia waya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kulieleza Bunge lako tukufu kama Jeshi la Polisi lipo likizo kwa kuruhusu mamlaka zingine haramu kuwatesa, kuwatweza, kuwashambulia na kuwaua watu.
Mheshimiwa Spika, tukio lingine la hivi karibuni ni kuuawa kwa Diwani wa Kata ya Namawala Godfrey Lwena ambaye alikatwa mapanga na watu wasiojulikana. Jambo la kushangaza baadae Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro walieleza tukio hilo kuwa lilitokana na ugomvi binafsi. Jambo la kuhoji ni kuwa kama ni ugomvi binafsi, Je huyo aliyekuwa amegombana na Marehemu wanamfahamu? Na kama wanamfahamu kwa nini mpaka leo hakuna taarifa ya kukamatwa kwake? Kauli hii ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro inadhihirisha kwamba huenda wao wanaelewa kila kitu kuhusu kifo cha Diwani huo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo mnamo mwezi Julai, 2017 aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma Bwana Simon Kanguye alipotea katiaka mazingira ya kutatanisha na mpaka leo hajapatikana. Kuongezeka kwa matukio ya kupotea na kutekwa kwa waandishi wa habari nchini pamoja na kutekwa kwa wanachama 6 wa CUF kisiwani Zanzibar yanaonyesha dhahiri tusipoungana kama wananchi wa taifa moja bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kiimani na kikanda hakika tutapoteza tunu yetu ya umoja, amani na mashikamano kama taifa moja.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haioni hatia kukumbusha kushambuliwa na kuuawa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo, kupotea kwa Ben Saanane ambaye alikuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Mheshimiwa Spika, ni wiki chache zilizopita tangu vijana sita watekwe huko Pemba ambapo watatu wamepatikana lakini watatu hawajapatikana mpaka sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji kama Taifa tutaendelea kushuhudia mambo haya yanayojenga chuki mpaka lini? Kama vyombo vya Serikali au watu wengine wanaona kuna haki zinakiukwa na baadhi ya watu nchini kwa nini wasiwapeleke watu hao Mahakamani?
Mheshimiwa Spika, Kwa matukio haya, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa haki ya usawa na haki ya kuishi nchini vipo hatarini kupotea na Taifa letu litaanza kuona matukio ambayo tulikuwa tunayasikia na kuyaona kutoka mataifa mengine na sio Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza mjadala mpana wa kitaifa ili kulitoa taifa kwenye mtanziko wa kusinyaa kwa misingi ya haki kama tulivyoeleza. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani ya Upinzani inapendekeza kuwa tiba ya haya yote ni kuwa na Katiba mpya iliyoridhiwa na wananchi pamoja na kujenga taasisi zilizo huru kusimamia misingi ya haki.
Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 13(6)(b) inatoa katazo na marufuku kwa mtu anayeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. Aidha ibara ya 13(6)(e) inatoa marufuku kwa mtu yeyote kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza na kumdhalilisha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na masharti na makatazo hayo ya Katiba kumekuwa na tatizo ambalo linaanza kuwa sugu la kuwachukulia watuhumiwa wakiwa mikononi mwa Polisi na wengine Mahakamani kama vile wameshahukumiwa kuwa wakosaji. Dhamana ya Polisi imekuwa kama ni zawadi kutoka kwa dola kwa sababu ambazo hata hazina mantiki yoyote; wala misingi ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, mwanzoni mwaka Mkutano huu wa Bunge Waziri wa Mambo ya Ndani aliulizwa swali na Mheshimiwa Dr Suleiman Yusuph (Mb) kuwa ni kwa nini Jeshi la Polisi lilimshikilia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini Bw. Abdul Nondo kwa zaidi ya siku 15 bila kumpeleka Mahakamani. Maelezo ya Waziri yalionyesha kuhalalisha vituo vya Polisi kuwashikilia Watuhumiwa zaidi ya masaa 24 kama Sheria inavyohitaji kwa muda mrefu kwa kigezo cha upelelezi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani amefanya marekebisho Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai peke yake kinyume na utaratibu wa marekebisho ya Sheria
Mheshimiwa Spika, Mawakili wakiwawakilisha wateja wao mbalimbali wamechukua hatua za kuwasilisha maombi Mahakama Kuu (Habeas Corpus) ili kumtaka Inspekta Jenerali wa Polisi kuja mbele ya Mahakama kueleza sababu za kuwashikilia watuhumiwa muda mrefu kinyume cha Sheria. Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya Mahakama Kuu kutoa hati ya wito kwa Jeshi la Polisi, siku ya kusikiliza maombi hayo au kabla watuhumiwa wamekuwa wakipelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, uharaka wa Jeshi la Polisi kuwapeleka Mahakamani Watuhumiwa baada ya kupata wito wa Mahakama Kuu ni ishara kuwa Polisi hawana sababu wala nia njema ya kuwashikilia Watuhumiwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa huu ni ukiukwaji wa haki wa wazi unaofanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi. Utaratibu huu ambao ni kinyume cha Katiba na Sheria wa Jeshi la Polisi umekuwa ukijirudia mara kwa mara na kuonekana kama mazoea na jambo ambalo ni halali mbele yao.
Mheshimiwa Spika, dhamana ya Jeshi la Polisi sio zawadi ni haki ya msingi kabla Mtuhumiwa hajahukumiwa na Mahakama. Jambo hili lisipoangaliwa vizuri na Serikali linalifanya Jeshi la Polisi kuwa maeneo ya utesaji na unyanyasaji kwa raia kuliko kuwa chombo cha ulinzi na usalama wao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulitaka Jeshi la Polisi kutokamata watuhumiwa mpaka pale uchunguzi au upelelezi wao unapokamilika, hii ni kwa sababu kumekuwa na sababu za mara kwa mara zinazotolewa na Mahakamani kuwa upelelezi wa shauri flani la jinai haujakamilika jambo linalopelekea Watuhumiwa wengi kuendelea kusota Magerezani kwa sababu za kutokamilika kwa upelelezi.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imeanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pamoja mambo mengine; inatakiwa kutekeleza mamlaka yake kwa kuzingatia misingi ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.
Mheshimiwa Spika, inaelekea msingi wa kutenda haki na kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki umekuwa msamiati mchungu wa ofisi ya DPP, kwa sababu badala ya kuzuia matumizi mabaya ya utoaji haki, ofisi hiyo ndiyo imekua kinara wa kukiuka taratibu hizo wakishirikiana na Jeshi la Polisi. Jambo hili limepelekea watuhumiwa wengi wa makosa ya jinai kuendelea kusota Magerezani bila mashauri yao kuendelea kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika au kwa sababu nyingine.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itatolea mfano shauri la Wakili Median Mwale ambaye alikamatwa tarehe 02 Agosti, 2011 na tarehe 09 Agosti, 2011 alishtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha na masuala ya udanganyifu kwa shauri la jinai namba 330/ 2011 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 20 Septemba, 2013 DPP aliwasilisha hoja kuwa ofisi yake haina nia ya kuendelea na shauri hilo, ambapo hoja yake ilikubaliwa na kupelekea shauri hilo kuondolewa Mahakamani. Pamoja na hatua hiyo ya DPP baada tu ya Wakili Mwale kuachiwa na Mahakama, alikamatwa tena na Jeshi la Polisi na kurudishwa rumande hadi mwaka 2015 ambapo DPP alifungua tena shauri namba 1/2015 ambapo Mwale alishtakiwa na wenzake watatu.
Mheshimiwa Spika, ilivyofika mwezi Desemba 2015 DPP aliwasilisha tena maombi Mahakama Kuu ya kutoendelea na shauri hilo; na maombi hayo yalikubaliwa lakini Mwale na wenzake walikamatwa tena na kurudishwa rumande.
Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba 2015 kwa mara nyingine tena Mwale na wenzake walishtakiwa tena kwa kesi ya jinai namba 61/2015 ambapo ilipangwa kuanza kusikizwa tarehe 30 Novemba, 2017 ambapo kwa mara nyingine tena DPP aliwasilisha nia ya kutoendelea na shauri hilo, maombi hayo yalikubaliwa kwa kuwa DPP aliahidi kuwa Mwale na wenzake wasingekamatwa tena. Jambo linalostaajabisha ni kuwa, mara baada ya uamuzi wa Mahakama Mwale na wenzake walikamatwa na Jeshi la Polisi ndani ya vyumba vya Mahakama Kuu na kupelekwa tena rumande.
Mheshimiwa Spika, baada ya jambo hilo kutokea, Mwale na wenzake walishtakiwa tena kwa shauri namba 77/2017 ambapo mashtaka ni yaleyale kwenye mashauri namba 330/2011, 01/2015 na 61/2015. Leo ni mwaka wa 8 toka Mwale na wenzake wakamatwe na bado shauri hilo ambalo linaonekana jipya halijapangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Mheshimiwa Spika, sakata lingine ni la kukamatwa kwa Masheikh wa Uamsho ambao mpaka leo mashauri yao yanapigwa danadana huku kukiwa na tuhuma lukuki dhidi ya Jeshi la Polisi kuwatesa na kuwatesa Masheikh hao kinyume na Katiba na Sheria za nchi yetu. Hata wakati walipoomba kupatiwa matibabu Masheikh hao walikataliwa jambo ambalo linaonyesha nia ovu ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, Vilevile wapo Masheikh na waumini wa dini ya Kiislam zaidi ya 60 waliopo katika Gereza Kuu Arusha ambao wanashikiliwa kwa zaidi ya miaka minne bila mashauri kukamilika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa wapo zaidi ya viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu zaidi ya 300 katika Magereza mbalimbali nchini ambao wameshikiliwa kwa muda mrefu bila mashauri kuendelea, hali iliyowalazimu Masheikh wa Arusha kuvua nguo hadharani kama ishara ya kuonesha kuchoka na kupinga uonevu unaofanywa dhidi yao.
Mheshimiwa Spika, hiyo ni mifano michache tu ya baadhi ya watuhumiwa walioko magerezani ambao mashauri yao yana miaka mingi bila kuendelea na hawajui hatma yao.
Mheshimiwa Spika, lengo la Kambi Rasmi ya Upinzani kutumia mifano hiyo sio kuweka msimamo au kulishawishi Bunge kuwa watuhumiwa hao wana hatia au hawana hatia. Lengo ni kuonesha jinsi utendaji wa ofisi ya DPP na Jeshi la Polisi unavyoathiri msingi wa utoaji haki kinyume kabisa na misingi ya uanzishwaji wa ofisi hiyo kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa mwito kwa vyombo vya dola kuhakikisha kuwa hakuna kumkamata mtuhumiwa kama bado hawajafanya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kwa sababu kwenye Mahakama zetu zipo hoja ambazo zinajirudia mara kwa mara kuwa uchunguzi bado unaendelea au jalada liko kwa DPP kwa ajili ya uamuzi au jalada lipo kwa Mkemia Mkuu jambo ambalo linasababisha kuchelewesha haki za watuhumiwa.
Mheshimiwa Spika, katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka (1977), Ibara ya 13 (6) (c )(d) inazungumzia kwa kina kuhusu haki za raia wote bila ubaguzi wowote . Katika Ibara ndogo ya sita inatoa marufuku kwa mtu yoyote kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chochote ambacho alikitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwepo wakati kosa linalohusika lilipotendwa. Ibara hii pia inazungumzia haki na usawa wa binadamu ambapo heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote za upelelezi ambapo mtu huyo atakuwa chini ya ulinzi bila uhuru.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mahabusu na magereza zetu nchini. Tatizo kubwa sio kwa waliopewa dhamana za kuwasimamia wafungwa magerezani bali kwa sababu ya mfumo kandamizi wa vyombo vya utoaji haki nchini vinavyopokea maelekezo nje ya mfumo wa Magereza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa magereza zetu nchini zina msongamano mkubwa sana wa wafungwa jambo ambalo ni hatari kubwa kwa afya za wafungwa. Lakini pia ndani ya magereza kuna wafungwa wengi ambao wamefungwa muda mrefu kwa makosa madogo madogo na hivyo kusababisha msongamano huo pasipo ulazima wowote. Mfano, zipo kesi za wafungwa waliokutwa wakiiba chakula, waliogombana na kupigana mitaani, waliokutwa wamelewa, wanaotuhumiwa kuwakosoa viongozi wa nchi mitandaoni au kwenye mikutano ya hadhara n.k
Mheshimiwa Spika, katika Ibara 13 (6) Katiba yetu inakataza kutolewa kwa adhabu kubwa kuliko adhabu iliyokuwepo wakati kosa linalohusika lilipotendwa. Jambo la kushangaza ni kuwa makosa haya madogo madogo yamekuwa yakiwaweka watu wengi mahabusu kwa muda mrefu jambo ambalo ni kinyume kabisa na matakwa ya kikatiba. Yapo makosa mengi yanayofanywa katika jamii ambayo yanaweza kabisa kurekebishika bila watuhumiwa kufikishwa mahabusu au magerezani lakini kutokana na mifumo mibovu ya utoaji haki vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa wameishia magerezani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo katika mfumo wa utendaji kazi ndani ya jeshi la polisi pameibuka tabia inayozidi kushamiri nchini kwa sasa ambapo yapo mambo yanayotajwa na polisi kama makosa ya kisheria ila kwa uhalisia sio makosa ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, wapo vijana wengi wamewekwa mahabusu kwa kueleza fikra zao na kutoa maoni dhidi ya mwenendo wa viongozi waliowapa dhamana ya kuongoza serikali. Jambo la kushangaza ni kuwa haki hiyo ya kutoa maoni inavishwa taswira ya uchochezi au ukosoaji. Vijana wengi wamejikuta mikononi mwa vyombo vya dola wengi wao wakitupwa mahabusu au magerezani kwa kutumia haki yao ya kueleza fikra zao ambayo ipo kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Jambo hili sio tu kwamba linazidisha msongamano usio wa lazima katika magezera bali pia ni hatari kwani linatengeneza tabia za usugu hususani kwa vijana wadogo walio kwenye magereza hizo.
Mheshimiwa Spika, Mwanasaikolojia Christian Jarrett katika kitabu chake cha “on the dark underbelly” anaeleza kwa kina madhara yanayoweza kutokea endapo mrekebishaji wa tabia atatumia njia isiyo sahihi katika kurekebisha tabia fulani ya mwanadamu. Kitendo cha kuendelea kuwaweka mahabusu watuhumiwa wenye makosa madogo madogo kunazalisha matatizo makubwa sio tu kwa mtuhumiwa bali kwa jamii kwa ujumla na kufanya Magereza na Polisi kuonekana kama sehemu za kawaida na hivyo kuhamasisha wahalifu wengine katika Nyanja zingine kujenga dhana kuwa Magereza ni sehemu za kawaida za kuishi.
Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inapunguza msongamano kwenye mahabusu na magerezani kwa kutumia adhabu mbadala ya vifungo vya nje au kazi za kijamii . Pia, serikali hii ya awamu ya tano iache mara moja kuendelea kuwashikilia vijana mahabusu au kwenye magereza eti kwa makosa ya kuzungumza fikra zao au kutoa maoni dhidi ya mienendo ya viongozi wa serikali. Ni lazima serikali itambue kuwa haki hii ipo kikatiba na ni lazima serikali iheshimu na kulinda katiba ya nchi kwa kuwa hakuna mtu yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye mamlaka yoyote juu ya katiba ya nchi.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa Muswada wa Fedha wa mwaka 2017 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tulihoji kuhusu namna Polisi wa Usalama Barabarani walivyogeuka kuwa mamlaka ya kutoza mapato badala ya kusimamia usalama kwa watumiaji na wamiliki wa vyombo vya moto.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na msisitizo kuwekwa kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanatakiwa kutoa elimu na kuonya kuhusu makosa madogomadogo barabarani, hali ni tofauti kwa sababu wananchi wengi wanalalamika kutozwa fedha za faini ya makosa ya barabarani ambayo hayahitaji kupigwa faini zaidi ya kupewa elimu ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, Aidha imefikia hatua Askari kupewa idadi ya makosa ambayo wanatakiwa kutoza faini kwa siku, jambo ambalo linaweza kujengewa hoja kuwa kwa sasa faini za barabarani ni chanzo kimojawapo cha mapato.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiungi mkono uvunjwaji wa sheria za usalama barabarani na wala haijengi hoja ya wakosaji kutoadhibiwa kwa mujibu wa sheria hizo, lakini cha kushangaza ni pale Askari wa Usalama barabarani wanapotoza faini hata kwa makosa ambayo hayapo kwa mujibu wa sheria. Mathalani kuweka mizigo kwenye siti ya abiria kwa gari binafsi jambo ambalo halipo kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani.
Mheshimiwa Spika, Faini za Usalama barabarani zinaweza kuleta chuki katika jamii kwa sababu ya hisia zinazojengeka kuwa wamiliki wa magari ni watu wenye fedha kwa hiyo ni haki yao kutozwa faini kwa jinsi mtu yeyote anavyojisikia. Kambi rasmi ya Upinzani inaona kuwa hili sio jambo la kufumbia macho kwa sababu linaweza kuhatarisha amani na utulivu katika taifa.
Mheshimiwa Spika, kama kuna kada inayoteseka kwa sasa basi ni kada ya wafanyabiashara na wawekezaji. Mifumo ya usimamizi ya taasisi za serikali imekuwa na urasimu mkubwa na ni kero kubwa sana kwa wafanyabiashara. Pamoja na mambo mengine kama nchi tunakabiliwa na athari zinazotokana na kuzorota kwa biashara ambazo zinasababisha ukosefu wa ajira. Kila mwaka takribani vijana zaidi laki 7 hawawezi kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kimsingi ukuaji mzuri wa biashara ungeweza kuwahakikishia hawa ajira ambazo hazihitaji utaalam wa hali ya juu.
Mheshimiwa Spika, unapokuwa na Taifa ambalo wawekezaji wanakimbia na kuhamisha mitaji, biashara za kati na za juu zinafungwa ni wazi kwamba kutakuwa na tatizo kubwa la ajira na njaa katika Taifa jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi hasa kwa kundi la vijana ambalo ni bomu linalosubiri wakati.
Mheshimiwa Spika, Hivyo tunapenda kuweka wazi kuwa tishio lingine la usalama wa nchi Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa urasimu na manyanyaso yake dhidi ya wafanyabiashara nchini ambapo kushindwa kulipa kodi kumegeuka kuwa kesi ya jinai ya kutakatisha fedha.
Mheshimiwa Spika, naomba kuweka wazi kuwa kwa hali ilivyo sasa ni wazi kuwa hali ya nchi yetu sio salama. Kuminywa kwa demokrasia ya haki, matumizi mabaya ya mamlaka ya Jeshi la Polisi na Ofisi ya DPP na sasa uwepo wa viashiria vya kuingilia uhuru wa Mahakama havitaliacha Taifa hili salama.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mko wengi, sisi wengine tumeshapitia majaribu na mateso mengi, tumeona mengi na tumejifunza mengi. Tumieni wingi wenu kulinda Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ilitengeneza sera ya sekta ya ujenzi (the Construction Industry Policy (CIP) mwaka 2003 na kanuni zake za utekelezaji zilitolewa rasmi mwaka 2006. Kwa mujibu wa wadau ni kuwa mi sehemu ndogo sana ya sera ndiyo ilikuwa inaweza kutumika kwa kulingana na mazingira halisi ya sekta yenyewe.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 sera hiyo ili uhishwa na kupelekwa kwa wadau ili waweze kutoa maoni yao kabla ya sera hiyo kukamilika na kuanza kutumika rasmi. Lakini hadi hivi sasa tunapotoa maoni haya Sera ya tasnia ya Ujenzi bado hajatoka rasmi. Kambi Rasmi inataka kufahamu ni lini hasa sera hiyo itatolewa ili iweze kuwa mwongozo kwa tasnia hiyo ambayo kwa sasa tunaweza kusema kuwa inakabiliwa na changamoto kadhaa.
Mheshimiwa Spika, sera hii inaonesha kuwa sehemu kubwa ya shughuli za kikandarasi inafanyika katika sekta isiyo rasmi, na takriban ya asilimia 80 ya watanzania wanaishi maeneo ya vijijini. Majengo na miundombinu midogo midogo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo yanajengwa na sekta isiyo rasmi pia.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba sekta ya ujenzi isiyo rasmi inahusisha kwa kiasi kikubwa wananchi ambao hawana kinga mnyororo mzima wa uchumi; kama vile vibarua, vifaa vya ujenzi na mara zote sekta hii inafanyakazi kulingana na matakwa ya mteja[38].
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa pili wa miaka mitano uk.53 na 54 unaonesha kuwa sekta ya ujenzi hadi mwaka 2020 imewekewa lengo la kukua kwa kiwango cha asilimia 9.6, mchango wa sekta kwenye pato la taifa uwe ni 11.8% na sekta iweze kuchangia asilimia 3.7 ya ajira zote. Aidha makampuni ya ndani katika kupata kazi za ujenzi iwe ni asilimia 60 ya thamani ya jumla ya kazi ujenzi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua katika malengo hayo tuliyojiwekea hadi sasa tumeyatekeleza kwa kiwango gani?
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa ni kuwa, tulikuwa tunaingia katika uchumi wa gesi na tumeaminishwa hivyo na Serikali yetu na hadi kupelekea ujenzi wa Bomba la gesi kati ya Mtwara hadi Dar. Kwa mujibu wa wataalam wanasema bomba hilo linatumika kwa asilimia 6 tu ya uwezo wake. Jambo la ajabu ni kuwa mradi huo umepigwa chini na sasa tunakimbizana na Ujenzi wa Stiegler’s Gorge. Kambi Rasmi ya Upinzani inapata mashaka sana na umakini wetu katika kuhakikisha tunafikia uchumi wa kati.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na TACECA (TANZANIA CIVIL ENGINEERING CONTRACTORS ASSOCIATION) unaonesha kuwa masuala na mikakati mingi inayohitajika kwenye tasnia ya ujenzi na kuelezewa kwenye sera haiwezi kutekelezeka kama rasilimali za hazikuwekewa mpango maalum wa upatikanaji.
Mheshimiwa Spika, maeno ya msingi katika sera ambayo yalikuwa yanahitajika kutekelezwa kwa haraka ili tasnia iweze kubeba dhamana ya kuwa kiungo cha kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi viwanda na kipato cha kati ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuna madhaifu kama ambavyo yalibainishwa na TACECA ni kwamba; hakuna sheria au kanuni za kusimamia utekelezaji wa SERA; Uwezo hafifu (fedha na Ujuzi) miongoni mwa taasisi za utekelezaji wa Sera ya ujenzi; Kutokuwepo kwa idara maalum ndani ya wizara kwa minajiri ya sera ya ujenzi (CIP).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge ni kwa vipi mapungufu hayo ya kisera kama ambavyo yanajionesha yamefanyiwa kazi ili Tasnia ya Ujenzi iweze kukidhi malengo yake ya kisera?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ilivyotolewa Januari 2018 zinaonesha kuwa Sekta ya Miundombinu ambayo inahusisha, ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imekuwa ikikua. Shughuli za ujenzi zilikua kwa asilimia 13.0 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 16.8 mwaka 2015. Kasi ya ukuaji ilipungua sambamba na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa za kukuza mitaji kutokana na kukamilika kwa miradi mikubwa ya ujenzi wa kiwanda cha saruji, mitambo ya kufua umeme na bomba la gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam.Habari na mawasiliano ilikua kwa (asilimia 13.0); usafirishaji na uhifadhi mizigo ilikua kwa (asilimia 11.8);
Mheshimiwa Spika, sekta ya miundombinu kwa mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18 ndiyo sekta iliyokuwa na miradi ya kipaumbele katika mgawanyo wa bajeti ya maendeleo na hivyo ndiyo sekta iliyopewa sehemu kubwa ya fedha za walipa kodi. mwaka wa fedha 2016/17, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano – Idara ya Ujenzi fungu 98 iliidhinishiwa shilingi 2,176,204,557,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Idara ya uchukuzi fungu 62 ambayo iliidhinishiwa shilingi 2,495,814,130,000.00, na mawasiliano fungu 68 zilitengwa jumla ya Shilingi 92,730,110,000.00 na hivyo kuifanya sekta nzima ya miundombinu kutengewa fedha za maendeleo jumla ya shilingi 4,764,748,797,000.00
Aidha kwa mwaka 2017/18 Sekta ya Ujenzi fungu 98 imetengewa jumla ya shilingi 1,895,582,432,000.00 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ni ya kimkakati na isiyo ya kimkakati. Uchukuzi fungu 62, fedha za miradi ya maendeleo zilitengwa Shilingi 2,477,931,183,000.00 na fungu 68, mawasiliano zilitengwa jumla yaShilingi 14,000,000,000 na hivyo kufanya bajeti nzima ya maendeleo kwa sekta hii ya miundombinu kuwa shilingi 4,387,513,615,000.
Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu hizo ni rahisi sana kuona kuwa kwa kipindi cha miaka miwili sekta ya miundombinu imetengewa jumla ya shilingi 9,152,262,422,000. Vyanzo vikuu vya fedha hizo vilikuwa ni mikopo ya masharti ya kibiashara na misaada ya kibajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 FUNGU 98 Ujenzi kwa miradi ya maendeleo imetengewa jumla ya shilingi 1,822,093,269,360.00 zikiwa ni pungufu ya shilingi 78,489,162,640.00 kwa kulinganisha na fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa fungu hilo.
Mheshimiwa Spika, uchukuzi fungu 62 kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa jumla ya shilingi 2,300,739,000,000.00 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Ukilinganisha na fedha za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka 2017/18 kuna upungufu wa shilingi 177,192,183,000.00.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani sio kama inapingana na uwekezaji katika miundombinu ya uchumi ambayo inachukua mabilioni ya fedha, bali hoja yetu ya msingi imekuwa ni jinsi gani fedha za uwekezaji katika miundombinu hiyo zinavyopatikana.
Mheshimiwa Spika,Japokuwa uwekezaji mkubwa huo umefanywa lakini miradi husika bado inahitaji kiasi kingine kikubwa cha fedha zaidi ya hicho kilichowekezwa ili iweze kukamilika. Uwekezaji huu kulingana na hali halisi ya nchi yetu ni kwamba miundombinu hii inafanywa kwa gharama ya huduma za msingi kama vile Elimu na Afya mambo ambayo kwa muda mrefu kimeendelea kuwa kilio cha watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya rejea ya bunge la Kumi, kamati ya Bajeti ilikuwa imeiangiza Serikali kuhakiki madeni ya wakandarasi ambayo ilikuwa inadaiwa Serikali, na Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati huo aliunda kikosi kazi kuhakiki madeni hayo. Kwa mtindo huo Kambi rasmi ya Upinzani ingependa kufahamu kati ya fedha za miradi ya maendeleo ya fedha zilizoombwa kupitishwa na Bunge ni kiasi gani cha fedha ambazo zinatakiwa kulipa madeni kwa kazi ambayo tayari imefanyika? Kwani katika Randama FUNGU 98 inaonesha fedha zinazotengwa ni sehemu ya kulipia madai ya washauri waelekezi au wakandarasi kwa miradi kadhaa ya ujenzi na hivyo kukosa ufahamu wa jumla zinazokwenda ni kiasi gani. Mfano Ujenzi wa madaraja makubwa shilingi bilioni 46.96 ikiwa sehemu ni kulipia madai ya washauri na wakandarasi wa madaraja ya Kilombero na Kavuu(Katavi). Lakini kazi mpya ni madaraja takriban 13. Hapa ni kiasi gani kimetengwa kwa kila daraja ikiwa ni kazi mpya?
Mheshimiwa Spika, hoja inayoshabihiana na hiyo ya kuweka fedha pamoja ni uendelezaji/ujenzi wa viwanja vya ndege kwa mikoa shilingi bilioni 62.447. Katika maelezo ni kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege kwa mikoa ya Geita, Iringa,Ruvuma,Lindi,Tanga, Mara na Kiwanja kipya cha Simiyu, Kiwanja cha Lake Manyara. Pia Ukarabati wa jingo la abiria pamoja na kumalizia ulipaji wa fidia kwenye kiwanja cha ndege cha Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka bajeti zinazopangwa ziwe na uhalisi kulingana na kazi zinazotakiwa kutekelezwa, Mikoa mingine bajeti zao zimetajwa wazi. Hivyo tunaitaka Serikali itoe mchanganuo wa fedha hizo kwa viwanja vya ndege vilivyoorodheshwa kwenye Randama kifungu kidogo namba 4226 ukurasa wa 26, kwa kila mkoa na kazi inayotarajiwa kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa IMF Country Report No. 18/11 iliyotolewa January 2018 (UNITED REPUBLIC OF TANZANIA- SEVENTH REVIEW UNDER THE POLICY SUPPORT INSTRUMENTPRESS RELEASE; STAFF REPORT)inaonesha kuwa matumizi makubwa kwenye miradi mikubwa pasipo kuwepo na uhakika wa vyanzo vya fedha vya kuimalizia miradi hiyo kunaleta madhara kwa kukua kwa shughuli za kiuchumi, kwani fedha nyingi zinaingia na zinafungiwa huko bila kuwapo kwa mzunguko wa fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa maneno mengine ni kwamba matumizi makubwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo kuna zuia fursa mpya za uwekezaji kwa sekta zingine.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaonesha kuwa bajeti iliyokuwa imepangwa kwa ajili ya miradi hiyo ya maendeleo ilikuwa itumie sawa na 10% ya Pato la Taifa hadi imalizike, lakini kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa fedha za miradi hiyo imelazimu kuwepo na upungufu wa fedha sawa na 1.2% ya Pato la Taifa, na hivyo kusubiri hadi mwaka huu wa fedha wa 2018/19.
Mheshimiwa Spika, kwa uchambuzi wa taarifa hizo za Serikali pamoja na IMF na kwa kuangalia bajeti ya Maendeleo iliyotengwa kwa sekta ya Miundombinu ambayo ni pungufu ukilinganisha na ile iliyotengwa kwa miaka miwili iliyopita ni dhahiri kuwa lengo la uwekezaji katika kuinua uchumi haliwezi kufikiwa kwani fedha nyingi zimefungiwa na hivyo haziwezi kuchochea maendeleo katika sekta zingine za uchumi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kama ambavyo imekuwa inashauri, nafasi ya Sekta binafsi katika kuwekeza imechukuliwa na Serikali. Jambo hili linapelekea Serikali kushindwa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake, mf. Ubora wa elimu unazidi kufifia kutokana na uwekezaji uliotakiwa kufanyika kuelekezwa kwenye sekta za miundombinu na huko lengo linashindwa kutimilika.
ZABUNI ZA UJENZI KUBWA KUTOLEWA BILA KUFUATA ZABUNI
Mheshimiwa Spika, sifa kubwa ya utawala bora ni kufuatwa kwa sheria na kanuni, kinyume na hapo ni kuwapo kwa dhana ya rushwa na upendeleo jambo ambalo hatuwezi kulikataa.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Tanzania tunafuata sheria na kanuni tulizojiwekea katika sekta ya manunuzi, kwa mujibu wa taarifa ya PPRA ya mwaka 2016/17 kazi za ujenzi zilikuwa na idadi ya mikataba 3,638 yenye thamani ya shilingi bilioni 4,743.6 sawa na asilimia 75.2 ya jumla ya tuzo nzima ya mikataba.
Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu kama utaratibu wa kisheria ulifuatwa katika utoaji wa kandarasi kwenye majukwaa ya kisiasa, kuwa kazi hii au ile wapewe TBA au kandarasi za kujenga barabara na hii au ile na kiwanja hiki cha cha ndege au kile ni kampuni Fulani.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Kambi imesema kuwa sera katika sekta ya ujenzi ndiyo inayoelekeza hivyo basi taasisi husika zinatakiwa kuwa imara katika kusimamia sekta hiyo, kwani kama inavyoonekana kwa takwimu za PPRA kwamba matumizi ya Serikali kwa zaidi ya 75% ni kwenye kandarasi za ujenzi, na hivyo rushwa kubwa ziko kwenye kandarasi za ujenzi.
UJENZI NA UKARABATI WA NYUMBA ZA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa maendeleo kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 17.45 kwa lengo la ujenzi na ukarabati wa nyumba kwa ajili ya makazi ya Viongozi na watumishi wa Serikali pamoja na majengo ya Serikali. Ikiwa na vipaumbele ujenzi wa nyumba za viongozi Dodoma na Mikoani pamoja na ujenzi wa nyumba za Majaji.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa mtazamo wa Kambi kwa jambo hili, naomba kurejea hoja yangu niliyoitoa hapa Bungeni tarehe 17 Mei,2016 kuhusuiana na suala zima la nyumba za Serikali zilizouzwa;
“Mheshimiwa Spika, wakala huyu wa majengo ndiye mhusika mkuu katika kuhakikisha nyumba za Serikali zinakuwa katika hali nzuri kwa watumishi wa serikali kuishi. Katika muktadha huo kambi Rasmi ya Upinzani inalikumbusha Bunge kwamba, kati ya mwaka 2002 mpaka 2004 Serikali iliuza nyumba zipatazo 7,921 na mpaka mwaka 2008 Serikali ilikuwa imejenga nyumba 650 tu.
Mheshimiwa Spika, katika biashara hiyo kwa kuuza zilizokuwa mali ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ilipata Sh.252,603,000/- sasa inahitaji kusaka nyumba zaidi ya mara dufu ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia. Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya uuzaji wa nyumba za serikali kinyume cha taratibu, serikali itatumia Sh.677,606,000/- kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe kwa Tamisemi, Rejea taarifa ya Serikali Bungeni tarehe 25 April 2008.
Mheshimiwa Spika, Kwa vile hata wale waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kati yao wapo walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo, KRUB inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.
Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonesha kwamba Serikali ilitoa taarifa ndani ya Bunge hili kuwa, kuna Kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya Nyumba ya Serikali na Kamati hiyo ilitegemewa kumaliza kazi mwezi Februari, 2007, lakini hadi Bunge la tisa na Bunge la Kumi linamaliza uhai wake hakuna taarifa iliyotolewa na Serikali. KRUB, inaitaka serikali ya awamu ya tano irejeshe nyumba hizo”.
Mheshimiwa Spika, mbali na Serikali kushindwa kutekeleza azimio la Bunge la kurejeshwa nyumba hizo na pia Waheshimiwa mbalimbali wameishatoa hisia zao kuhusiana na kurejeshwa kwa nyumba hizo. Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia tena kuitaka Serikali ya awamu ya Tano kuzirejesha nyumba za Serikali ambazo kwa kiasi kikubwa zilitolewa kwa watu ambao hawakustahili na zoezi zima liligubikwa na rushwa na upendeleo mkubwa wa kiundugu na uchafu mwingine wa aina hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni serikali ya kunyosha nchi itakuwa vyema kunyoosha pale ambapo zoezi la uuzwaji nyumba za Serikali na wahusika walioendesha zoezi hilo kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria. KRUB inauliza ni lini TAKUKURU itachukua nafasi yake katika hili?
SEKTA YA UCHUKUZI
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imeoneshwa hapo juu, Sekta hii imetengewa fedha za maendeleo shilingi 2,300,739,000,000.00 ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, fedha hizo zote zilizotengwa ni fedha za ndani na zinatakiwa kuhudumia miradi tisa mikubwa na sio ya kumalizika leo au kesho katika sekta ya uchukuzi. Huu ni uwekezaji mkubwa ambao kama haukukamilika kama ilivyokuwa imepangwa maana yake tutaendelea kufunga mikanda kwa miaka kadhaa ijayo. Jambo hilo litawanyika watanzania haki yao ya kupatiwa huduma za msingi za kijamii. Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na kuwekeza katika sekta hizo, lakini sio kwa kutumia fedha za ndani katika kujenga miundombinu mikubwa namna hiyo, huu ndio unaitwa upangaji mbaya wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, kiasi hicho cha fedha kimeelekezwa katika miradi mbalimbali na mchanganuo wake umetolewa. Moja wapo ya maeneo zinazopoelekezwa ni kwenye mfuko wa Reli, kiasi cha shilingi bilioni 252.639. Kwa mwaka 2017/18 Fedha za ndani zilizotolewa kwa ajili ya mfuko wa reli zilikuwa ni Shilingi 111,669,711,654. Huu mfuko unatakiwa uwe umetuna na una uwezo wa kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, Kwa maana ya mfuko ni kuwa fedha hizi zinawekwa kwa muda Fulani na baadae mfuko huo uweze kujiendesha wenyewe. Sasa kwa matumizi ya fedha hizo kama inavyooneshwa katika Randama ni dhahiri kuwa fedha hizo sio za kujizungusha na kuweza kutunisha mfuko huo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge, Kambi Rasmi ya Upinzani wakati inawasilisha Maoni yake kuhusu Bajeti Kuu ya mwaka 2013/14 ilisema yafuatayo kuhusiana na fedha za kuendeleza Reli, nanukuu;
“Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa kodi maalumu (Special Railways development levy) ya manunuzi na mauzo ya bidhaa nje. Tunapendekeza tozo ya asilimia moja (1 %) ya bei ya bidhaa zinazoagizwa toka nje na asilimia 0.5 (0.5%) ya thamani ya bidhaa kwa zile zinazouzwa nje. Mapato ya tozo hii maalumu yote yatumike kujenga miundombinu ya Reli hapa nchini”.
Mheshimiwa Spika, pendekezo hili lilichukuliwa na Serikali kwa kuanzisha kodi ya maendeleo ya Reli, lakini fedha zinapatikana kwa mtindo tofauti na tulivyo shauri na madhara ya hilo ni fedha hizo zinatengwa kwa “expense” ya huduma zingine za jamii. Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani bado tunashauri fedha za kuendeleza reli zitokane mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ujenzi wa Reli ya kati kwa Standard Gauge, kwa maombi ya kuanzia bajeti ya mwaka 2016/17 hadi 2017/19 jumla zilitengwa shilingi trilioni 1 na milioni 900(1,000,900,000,000). Kwa maana kuwa mwaka wa bajeti 2016/17 zilitengwa shilingi trilioni 1 na 2017/18 zilitengwa shilingi 900,000,000.00
Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba ya Waziri wa fedha ni kuwa hadi sasa fedha ambazo zimeishalipwa kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa Standard Gauge jumla yake ni shilingi Trilioni 1 na bilioni 221. Ambazo ni zaidi ya zile zilizokuwa zimeomba na Wizara na zilizoidhinishwa na Bunge kwa shilingi 220.1 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.02.
Mheshimiwa Spika, hili ni eneo moja tu la matumizi ambayo yanafanyika bila kupitishwa na Bunge, lakini tukiangalia katika wizara zote ni dhahiri jambo kama hili litajitokeza sana.
Mheshimiwa Spika, jambo hili linaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani kuamini kuwa Serikali ina fedha nyingi ambazo hazipitishwi na Bunge lakini zinaingia katika matumizi ya miradi ya maendeleo na zingine katika shughuli ambazo ni vigumu kuhoji.
Mheshimiwa Spika, katika Randama za Wizara hatuoni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo tayari mikataba ya ujenzi na Serikali ya Chini ilikwisha sainiwa. Hapa kuna kitu gani ambacho hakiendi sawa?
SHIRIKA LA NDEGE LA TANZANIA -ATCL
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujadili naomba kunukuu hotuba ya Waziri Mbarawa aliyoitoa hapa Bunge mwaka jana;
“Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kampuni ya Ndege (ATCL) imetengewa shilingi milioni 500,000 kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege 3 ambapo ndege mbili (2) ni za aina ya CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja na ndege kubwa moja (1) ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262”.
Mheshimiwa Spika, ukisoma mwongozo wa Mpango uliotolewa mwezi March,2018 na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mpango uk.10, kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa 2017/18 anasema, nanukuu; “
“Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: shilingi bilioni 7.85 zimetolewa kutekeleza mkataba wa ununuzi wa ndege, ambapo ndege mbili za aina ya Bombadier CS 300 zimelipiwa kwa asilimia 30 na ndege moja kubwa ya masafa marefu, Boeing 787, kwa asilimia 52”;
Mheshimiwa Spika, katika Randama ya mwaka huu 2018/19 kumetengwa jumla ya shilingi bilioni 495.6 kwa ajili ya kununua ndege mbili (2) moja aina ya Q 400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege kubwa moja ya masafa narefu aina ya Boeing 787-8(Dreamliner).
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kuwa tulikwisha nunua ndege tatu za Q400 na tayari zimefika, sasa hizi hela za ndege zinazotengwa ni kwa ndege nyingine ili kufikisha Q400 kuwa nne (4)?
Mheshimiwa Spika, Takwimu hizi za fedha na ndege zinatia wasiwasi, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge ni kiasi gani hasa kimelipwa na kwa ndege ngapi na kiasi gani kinadaiwa hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, kutofautiana kwa takwimu ni ishara kuwa kuna tatizo kubwa katika kadhia nzima ya ATCL,hapo bado katika uendeshaji wake. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri mambo ya Kitaalam waachiwe wataalam na Serikali ikusanye kile kilichochake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Kama tulivyotangulia kusema huko nyuma kuwa haiwezekani Serikali kujiingiza katika biashara na bado tunaendelea kusisitiza hivyo kwani itapelekea Taifa kuingia katika hasara kubwa jambo ambalo tungeweza kuliepuka sasa hivi na kuiacha taasisi hii ijitegemee ili ijiendeshe kwa faida na kuifanya sekta hii iwe endelevu na sio kuendelea kutegemea ruzuku toka Serikalini.
Mheshimiwa Spika, Tunayasema haya leo kwa manufaa ya Taifa na kuepuka yaliyowatokeya wenzetu ambao walikuwa na nia njema tu kama ilivyo leo lakini kwa kukataa ushauri kama inavyotokea kwetu leo matokeo yake wanaka kujinasua lakini ni ngumu kutokana na ushindani wa biashara hii ya ndege. .
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kabla ya shirika la Air Tanzania kufa mara ya pili walijitokeza wawekezaji kuliokoa shirika letu ambao walikuwa ni British Airways, Emirates na South Africa Airways. British Airways walionesha ni jinsi gani wangeijengea uwezo katika eneo letu la Afirica Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla, lakini pia Emirates walitaka kulichukuwa shirika letu kufanya kazi pamoja na kuahidi kuwa wange vifanyia marekebisho viwanja vyote vya ndani lakini kutokana na watu wenye tamaa na ulafi wakatanguliza maslahi binafsi ndio makubaliano yafanyike kwa masikitiko watu makini kama Emirates wakaona hawawezi kufanyakazi na watu wasio na maadili kama sisi na kwa bahati mbaya South Africa Airways walikubali njia za panya na hivyo wakapewa shirika wakalirudisha Marehemu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kushindwa Tanzania, Emirates walikwenda kuzungumza na Sir-Lanka Airline wakakubaliana na kufanya nao kazi na waliwajengea uwanja wa ndege wa kisasa kwa shape ile ile ya Dubai International Airport.
Mheshimiwa Spika, katika biashara hii ya Usafiri wa anga ni muhimu sana tuwe na Sera inayofuatwa na isiwe utashi wa Yule aliyepo madarakani kwa wakati huo na hiyo ndiyo itakuwa siri ya mafanikio ya taifa lolote. Kwa muktadha huo ndio maana Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kusema kuwa atafutwe mtaalamu wa biashara ya ndege atuanzishie shirika na haya mambo yanatakiwa yawe tayari kwenye sera yetu.
Mheshimiwa Spika, kujitathmini ndiyo njia sahihi ya kwenda mbele wenzetu Kenya wameweza na Kq ni mwaka juzi wamebadilisha Management na ku-reform shirika lao na wameagiza ndege mpya 42 kwa awamu na ni mwaka huu tu wamepata “route” ya New York- Marekani na kuanzia October mwaka huu wataruka moja kwa moja kutoka Nairobi kwenda New York. Tayari imezinduliwa rasmi January mwaka huu kupitia vyombo vya habari vya Marekani ikiwa ni miezi kumi kabla ya safari kuanza.
Mheshimiwa Spika, leo hii Tanzania Ndege zetu CS 300 na Boeing 787 zinakaribia kufika lakini hakuna taarifa zozote za kwamba zitakuwa na routes za wapi na kuanza kuzitangaza. Tukumbuke kuwa hakuna njia ambayo haina shirika kubwa la ndege,Leo Emirates ana mashirika matatu yote yanakuja Tanzania Emirates, Fly Dubai na Etihad. Ethiopia analeta Dream liner 787-8 2 kwa siku moja inakuja Dar na ya pili inakwenda Zanziba kupitia Kilimanjaro. Hapo bado hatujazungumzia safari za Qatar, Oman Air, Kenya Airways n.k
Mheshimiwa Spika, hii ni kuonesha kuwa kuna ushindani kiasi gani katika biashara ya ndege na ili kuifanya biashara hii kwa faida inabitubidi tuachie wataalam na sio kwa matamko ya kutoka juu. Tuna kazi kubwa kujenga uaminifu kwa abiria ni nani leo anakwenda kutuamini katika hali hii ya uendeshaji wa shirika na ununuzi wa ndege ambao haukufuata taratibu na sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, suala la maadili bado linatusumbua sana kama nchi, sasa hivi tukiuliza ni tender namba ngapi na ilitangazwa katika media zipi kuhusu ununuzi wa ndege ambazo zimenunuliwa na fedha taslimu, hatufahamu kama Waziri atakuwa na uwezo wa kutoa majibu hayo.
Mheshimiwa Spika, masuala kama hayo ambayo yanapindisha sheria na kanuni hata kama yalikuwa na nia njema, lakini yanatia mashaka makubwa kama kweli maslahi binafsi hayakuingia na kuchukua mkondo wake.
Mheshimiwa Spika, suala la maadili litaendelea kusumbua sana kama hatutakuwa na taasisi imara za utawala bora na badala yake taasisi zote za utawala bora ziko chini ya taasisi moja tu ya Ikulu, haya ni mapungufu makubwa ya Kikatiba.
Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ni kwamba tunahitaji kuwa na katiba mpya na mchakato wa Rasmu ya Pili ya Katiba uanze upya ili tuweze kupiga hatua vinginevyo tutazidi kujenga Rais au Kiongozi Imara badala ya kujenga taasisi imara na madhara yake hatutakuwa na taasisi yoyote ya kuhoji yanayofanyika kwa fedha za walipa kodi.
Mheshimiwa Spika,Umeme kama kichocheo cha maendeleo ya kukua kwa uchumi na vile vile kuongezeka kwa kipato cha wananchi kwa kuweza kumiliki na kuzitumia vyema rasilimali zinazowazunguka, hivyo basi hata rasilimali zingine kama madini haziwezi kuwa na thamani kama hakutakuwa na umeme wa kuwezesha kuzitoa huko ziliko na kuzipatia thamani inayostahili.
Mheshimiwa Spika, nishati umeme inatokana na vyanzo mbalimbali, na kwa bahati nzuri hapa Tanzania tumebahatika kuwa na vyanzo vingi vya uzalishaji wa umeme, miongoni mwake ni chanzo cha maji, chanzo cha gesi asilia, chanzo cha upepo na chanzo cha jua.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha watanzania wanapata nishati umeme kama sera zinavyosema, imekuwa ikiingia mikataba na makampuni kadhaa; lakini katika uingiaji wa mikataba hiyo kumekuwapo na utapeli au hujuma katika mikataba husika na mwishowe manufaa makubwa ya kimkataba yanabakia kwa washirika wenza wa mikataba inayoingiwa.
Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa CAG ni kuwa Serikali iliingia mkataba wa kukopa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na kampuni ya Songas Limited. Mkataba ulielekeza kuwa gharama za mradi zilikuwa Euro milioni 392. Kwa mujibu wa mkataba, Serikali ilitakiwa kukopa Euro milioni 235.1 na kuwekeza katika mradi; pia kutoa kiasi cha Euro milioni 0.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato. Pia, Serikali ilichukua mkopo wa Euro milioni 50 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na kuikopesha Songas. Uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mradi ni Euro milioni 285.7 ambayo ni asilimia 73 ya gharama za mradi ingawa hakuna sehemu katika mkataba inayoonyesha stahiki ya Serikali katika mradi husika.
Fidia ya Ucheleweshaji wa Malipo ya Kampuni ya Pan African
Energy yenye Thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 10.43
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Usambazaji wa Gesi (Gas Supply Agreement) baina ya TANESCO na Kampuni ya Uzalishaji Gesi ya Pan African (PAET), unaeleza kuwa endapo kutatokea mgogoro wa kiasi chochote cha malipo, kiasi hicho kinatakiwa kuwekwa kwenye Akaunti ya Pamoja (Escrow Account) hadi pale mgogoro utakapotatuliwa.
Mheshimiwa Spika, Kinyume na hapo, fidia ya ucheleweshaji wa malipo itatozwa. Kutoka mwaka 2011 hadi 2016 TANESCO imekuwa na mgogoro dhidi ya baadhi ya malipo ya usambazaji wa gesi ya PAET yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 6.48. Hadi tarehe 30 Juni 2016, TANESCO ilikuwa inadaiwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 71.38 na PAET; Kuchelewa kulipa deni hilo kwa wakati kutapelekea TANESCO kulipa fidia ya ucheleweshaji kwa PAET yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 10.43.
SHIRIKA LA UMEME TANZANIA – TANESCO
Mheshimiwa Spika, Mwenendo Usioridhisha wa Hali ya Kifedha
Kwa miaka kadhaa, TANESCO imekuwa na mwenendo usioridhisha kwa kupata hasara mfululizo. Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 hasara iliyopatikana ilikuwa Shilingi bilioni 346.40; na kwa hesabu za miezi 18 hadi mwaka wa fedha ulioishia Juni 2015, hasara ilikuwa Shilingi bilioni 124.46. Mwenendo wa hasara umekuwa ukichangiwa na hali isiyoridhisha ya maji ya kuzalisha nguvu ya umeme pamoja na ongezeko la gharama za uzalishaji. Mfululizo wa hasara hizo una athari kubwa kwenye Mtaji wa Shirika, hivyo kulifanya kutokopesheka ili kukidhi mahitaji yake ya kifedha.
Pia, kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2016, madai ameongezeka kwa asilimia 23, hadi Shilingi bilioni 958 kutoka Shilingi bilioni 738 zilizoripotiwa kwenye hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2015. Kwa upande mwingine, thamani ya wadaiwa ilipungua hadi Shilingi bilioni 330.55 kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2016, kutoka Shilingi bilioni 440.66 zilizoripotiwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2015.
Usimamizi wa kampuni Binafsi za uzalishaji umeme na gharama za kuiuzia TANESCO
Mheshimiwa Spika, Shirika la umeme Tanzania, TANESCO katika jitihada za kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, shirika liliingia mikataba na makampuni binafsi yanayozalisha umeme kwa lengo la kuiuzia TANESCO. Aidha taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, TANESCO inanunua umeme kwa bei ya wastani wa shilingi 544.65 kwa kila “unit” na kuuza kwa shilingi 279.35 na hivyo kulifanya shirika kupata hasara ya shilingi 265.3 kwa kila unit.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kusitishwa kwa mkataba na kampuni ya Symbion, TANESCO ilikuwa inalipa jumla ya dola za Marekani milioni 16.36 kama capacity charge kwa makampuni yanayozalisha umeme wa dharura. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inazo zinaonesha kwamba Kwa sasa, Shirika linatumia Dola za Marekani milioni 9.75 kwa mwezi kununua umeme kutoka Aggreko, Songas na IPTL na gharama za umeme zinazolipwa na TANESCO kwa mwezi ni Dola za Marekani milioni 9.75.
Mheshimiwa Spika, Bei za nishati ya umeme inayotozwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinadhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kila robo mwaka baada ya mapitio ya gharama halisi za uzalishaji. Aidha kwa mujibu wa tarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kuwa mapitio ya kila robo mwaka ya bei ya nishati ya umeme hayahusishi madeni yaliyojitokeza kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu wa mapitio ya bei ya umeme ya robo mwaka. Hivyo,utaratibu huu Mheshimiwa Spika, hauiwezeshi TANESCO kulipa madeni yote inayodaiwa.
Mheshimiwa Spika, bei ya umeme inayopitishwa na EWURA haionyeshi gharama halisi zilizotumiwa na TANESCO jambo linaloathiri uwezo wa TANESCO katika kulipa madeni yanayolikabili Shirika. Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inaishauri Serikali kupitia EWURA kuzipitia kwa umakini gharama za umeme ili kuhakikisha kuwa gharama zote za uzalishaji wa umeme zinahusishwa, ili hatimaye, kusaidia upatikanaji wa faida baada ya uwekezaji wenye lengo la kuboresha huduma na kuongeza matokeo chanya kwa TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Kwenye Kampuni ya Umeme Tanzania (TANESCO) CAG alibaini kuwa, eneo la Ubungo Complex lilipewa Songas mwaka 2004 wakati Songas ilipoanza shughuli zake nchini Tanzania. TANESCO ilipatiwa hisa 10,000 katika kampuni ya Songas kama malipo kwa ajili ya Ubungo Complex; pia, Songas ilichukua yaliyokuwa madeni ya TANESCO yaliyotokana na ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi pamoja na mitambo husika iliyopo Ubungo Complex. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonesha kuwa Ubungo Complex pamoja na mali nyingine ilizopewa Songas Limited zilithaminishwa kabla uhamishaji haujafanyika.
Deni tarajiwa baina ya SCBHK na TANESCO lenye Thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 148.4
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Septemba 2010, TANESCO ilishtakiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCBHK) kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 258.7 kilichotokana na madai ya malipo ya uzalishaji wa umeme pamoja na fidia ya kutolipa madai ya uzalishaji umeme na uharibifu uliosababishwa na TANESCO kutoilipa IPTL kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, maamuzi ya mwisho yaliyotolewa tarehe 12 Septemba, 2016 yaliitaka TANESCO kuilipa SCBHK, ikijumuisha fidia ya kiasi cha Dola za Kimarekani 148.4, baada ya hukumu hiyo, TANESCO ilipinga maamuzi hayo kwa kukata rufaa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kisha kuwasilisha utetezi wake tarehe 21 Agosti 2017, ambapo baadaye SCBHK iliwasilisha pingamizi juu ya utetezi huo wa TANESCO.
Mheshimiwa Spika, tangu kipindi hicho, TANESCO imekuwa ikitumia gharama kubwa za uendeshaji wa kesi hiyo, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 7.58 zimetumika ikiwa ni jumla ya Shilingi bilioni 3.65 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 na Shilingi bilioni 3.93 kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Hata hivyo, suala hili litarejeshwa kwa mamlaka za kisheria za ndani ambapo utekelezaji wake kisheria utazingatia uwezo wa kulipa wa TANESCO.
Licha ya kiasi kikubwa cha fedha zinazotumika kwenye kesi hiyo, hakuna uhakika wa kushinda.
WAKALA WA NISHATI VIJIJINI- (REA)
Mheshimiwa Spika, lengo la uanzishwaji wa REA lilikiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado Serikali haijaonesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze kuimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili, kwa mfano mwaka 2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni 20.00 lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 12.06 sawa na 60%. Mwaka 2009/2010, fedha zilizopitishwa ni shilingi bilioni 39.55 na kiwango cha fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 22.14 sawa na 56%. Mwaka 2010/2011 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 58.883 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 14.652 sawa na 25%, mwaka 2011/2012 kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 71.044 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 56.748 sawa na 80%, mwaka 2012/2013 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 53.158 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 6.757 sawa na 13%.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 wakala alitengewa jumla ya shilingi 420,492,701,200/-kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Lakini kwa mujibu wa taarifa ya utendaji ya Wakala ni kwamba hadi Desemba 2015 zilikuwa zimepokelewa jumla ya shilingi 141,163,133,226/- tu ambazo ni sawa na asilimia 34.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 wakala ulipitishiwa fedha za maendeleo jumla ya shilingi 382,840,122,792/-
Mheshimiwa Spika, taarifa ya wakala iliyotolewa Januari, 2017 takwimu zake zinaonyesha kuwa jumla ya miradi 13 inayoendelea kutekelezwa yenye thamani ya shilingi 1,210,050,878,902 kama mikataba yake ilivyosainiwa, hadi sasa fedha zilizotolewa na Serikali ni shilingi 1,019,957,110,048.20 na kiasi kilicho baki ni shilingi 190,093,768,854. Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha, na ni miradi iliyoingiwa mikataba tu, lakini REA ina miradi mingi kwa kulingana na bajeti zilizopitishwa na Bunge pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 hadi kufikia February 2018 jumla ya shilingi bilioni 249.33 zilikuwa zimepokelewa sawa na asilimia 49.9 ya shilingi 499,090,426,000/- ambazo kati ya hizo shilingi 469,090,426,000/- zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi 30,000,000,000/- fedha za nje kama zilivyopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika kwa mwaka 2018/19 Bunge linaomba kupitisha jumla ya shilingi 412,083,000,000/- kwa wakala zikiwa fedha za Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ambao umegwanywa katika vipengele vinne(4) ambavyo ni sehemu ya REA III, inaonesha kuwa Miradi ya Usambazaji Umeme kwenye maeneo ambayo yameshafikiwa na Miundombinu ya Umeme (DENSIFICATION) unakadiriwa kuwa utatumia jumla ya shilingi bilioni 2,000/- na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 ya fedha. Na vijiji vitakavyonufaika ni 4,395
Mheshimiwa Spika, hizi densification zimegawanywa katika awamu II kulingana na idadi ya vijiji vinavyohitajika kupatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa REA inatumia fedha nyingi sana katika kutekeleza wajibu wake. Kwa kuwa kila mradi ili utekelezeke ni lazima kuwepo na andiko la kuonesha “costs benefits analysis”. Kwa kuwa fedha za walipa kodi wa ndani na wengine ambao wanasaidia katika kutekeleza miradi hii fedha zinatumika, kwa mahesaba ya haraka haraka kwa kuanzia mwaka wa fedha 2008/09 hadi 2018/19 takriban zimekwisha tengwa jumla ya shilingi 2,199,772,249,992/- ambazo ni fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, ni jambo ambalo haliwezi kubishaniwa kuwa REA inafanyakazi yake vizuri, matatizo ya hapa na pale kuhusiana na makandarasi kutokutimiza wajibu wao ni mambo ambayo hayawezi kukosa kutokana na wingi wa miradi inayotekelezwa nchi nzima. Na pia malalamiko ya upendeleo katika baadhi ya maeneo ni mambo ya kawaida ambayo kuyatolea ushahidi ni lazima CAG afanye ukaguzi wake.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba kwa sasa kila kitu ni biashara na hakuna kitu kinaitwa huduma tena katika nchi yetu na ndio maana hata mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu inawekwa kwenye bajeti ya maendeleo kwa maana kuwa ni lazima izalishe faida kutoka kwa wahusika. Hivyo basi hata uwekezaji kwenye umeme vijijini ni biashara na hivyo basi inatakiwa walipa kodi waelewe baada ya muda gani uwekezaji unaofanywa na REA utaanza kurudisha mtaji uliowekezwa huko.
MheshimiwaSpika, imetulazimu kuhoja hii “ return on Investiment” kwenye REA kutokana na tabia ambayo tunaona inataka kuota mizizi katika nchi hii, kwani kama tunaweza kuwekeza kwenye ATC wakati hakuna mchanganuo wa biashara wa ATC na jambo hili nimatumizi mabaya ya fedha za walipa kodi. Hili tuanze kuwa makini na fedha zetu ni muda mwafaka kuhoji suala hili.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa REA (Final Report- Mid-term Review of the Capacity Development Project of the Rural Energy Agency, Tanzania) iliyotolewa na Swedish International DevelopmentCooperation Agency (Sida) inaonesha kuwa kati ya miradi yote inayotekelezwa na REA , miradi 234 sawa na asilimia (72.9%) inatekelezwa na TANESCO ikiwa na gharama ya shilingi bilioni 289 na miradi 87 sawa na 27.1% ilitekelezwa na wakandarasi wengine. Kati ya fedha hizo Tanesco ilipatiwa asilimia 89 na wakandarasi wengine walipatiwa 2% ya kile walichotakiwa kupatiwa. Hii inaonesha kuwa fedha nyingi zinazotengwa na REA zinapelekwa kutekelezwa miradi inayotekelezwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi mingi ya REA inayotekelezwa na TANESCO ni ile ya “grid electrification” ya kutekeleza Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini (Turnkey Operation Projects).Miradi mingine ya inayohusu nishati ya umeme inayotokana na Jua, Upepo, maji katika maporomoko madogo madogo na n.k (solar, wind, biogas, hydro etc) bado miradi hiyo upatikanaji fedha kutoka REA unasuasua sana.
Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba miradi hiyo ya nishati Jadidifu (renewable energy) ndio inaweza kuwa mkombozi kwa mazingira yetu halisia badala ya kutegemea umeme unaozalishwa na kusambazwa na Tanesco.Hivyo basi ni Rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa REA kuhakikisha kipaumbele wanapewa wakandarasi ambao wanahusika na uzalishaji umeme kutokana na nishati Jadidifu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa hiyo ni kwamba REA ndiyo inaiendesha TANESCO, fedha zote zinazokatwa kwenye mafuta na gharama za kununua umeme ili zipelekwe REA kwa lengo la kusambaza umeme vijijini ambapo TANESCO haijafika, kwa mlango wa nyuma fedha hizo zinarudishwa TANESCO kupitia njia ya kuwapatia kandarasi TANESCO ili watimize wajibu wao wa kuwapatia wananchi umeme. Na pia fedha hizo ndizo inawezekana zinalipa deni la ESCROW zilizochotwa na watu wanaojulikana lakini hatua hazichukuliwi.
Mheshimiwa Spika, kwa ukweli huo ni vyema REA ikafanyiwa tathmini upya na kuangalia inatakiwa ishughulikie miradi ya aina gani katika kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
SEKTA YA GESI- NCHINI:
SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA-TPDC
Mheshimiwa Spika, Shirika hili la mafuta ndilo lililo na jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa raslimali ya mafuta na gesi iliyo hapa nchini inajulikana ilipo na inajulikana kiasi cha hazina kilichopo na inavunwa na nani na watanzania watanufaika vipi na raslimali hizo. Katika kutekeleza hayo yote shirika kwa mwaka wa fedha 2015/16 liliomba kiasi cha shilingi bilioni 12 kama fedha za maendeleo, lakini hadi kamati za Bunge zinakutana hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa na hazina kama fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha TPDC imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.5 fedha za maendeleo zikiwa ni fedha za ndani, kati ya fedha hizo shilingi milioni 700 ni ujenzi mtandao wa kusambaza gesi asili kwa mikoa ya Mtwara na Lindi na shilingi milioni 800 ni mradi wa kuchakata gesi asili na kuwa kimiminika kwa ajili ya kuisafirisha nje na ndani ya nchi ikiwa imesindikwa, na shilingi bilioni 9.2 fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imeeleza hapo awali kwamba kazi ya kusimamia kwa kuelewa rasilimali ya mafuta na gesi ilipo na ni kiasi gani kilichopo ni kazi inayohitaji rasilimali. Kitendo cha kukosa fedha kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo ni dhahiri kwamba makampuni yanayojihusisha na biashara hiyo, ambayo kwayo ni lazima yawe na fedha za kutosha ni rahisi kuiweka TPDC mfukoni mwake na mwisho wa siku watanzania wakakosa kunufaika na rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa fedha unaolikumba shirika hili ndio unaopelekea mapato ya gesi kutokukusanywa kwa kadri mikataba na sheria zinavyosema. Kwa mujibu wa taarifa ya TPDC inaonesha kuwa hadi Machi, 2018 SONGAS inadaiwa jumla ya shilingi 47,903,599,519.70 na Pan African Energy inadaiwa jumla ya shilingi 74,337,788,773.26, TANESCO inadaiwa jumla ya shilingi 286,826,407,174.26, KILIMAJARO OIL shingi 1,289,342,805.39. Na hivyo kufanya kampuni zote hizo zinadaiwa na TPDC jumla ya shilingi bilioni 410.36 Je, kwa mwendo huu gesi hii inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi, Kama madeni yanashindwa kudaiwa kwa kusimamia mikataba iliyopo?
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 TPDC ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 92 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi Machi, 2018 zilikuwa zimetengwa kutumika ni shilingi bilioni 69, lakini zilizokuwa zimetumika ni shilingi milioni 204 ambazo ni sawa na asilimia 0.29 au (0.3%), Hapa kweli tunaweze kupata matokeo chanya katika uwekezaji wa namna hii?
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 sekta ya mafuta na gesi, fedha za maendeleo imetengewa jumla ya shilingi 101,870,000,000/- kati ya fedha hizo za ndani ni shilingi 74,400,000,000/- na za nje ni shilingi 27,470,000,000/-
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa gesi ya kupikia (LPG), jumla ya tani 65,522 ziliingizwa nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani, mwaka 2014,na kwa mwaka wa fedha 2015 ziliagizwa tani 70,063 sawa na ongezeko la asilimia 7 kwa kulinganisha na uagizaji wa mwaka 2014, na mwaka 2016 ziliagizwa tani 90,296 sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa kulinganisha na uagizaji wa mwaka 2015[39].
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba sasa hivi wafanyabiashara wanazidi kuwekeza mitaji katika biashara hii ya gasi ya LPG ili kuhakikisha kuwa wanakwenda kuktosheleza soko ambalo bado ni kubwa sana hapa nchini. Kwa hili Kambi Rasmi ya Upinzani inaona lingekuwa jambo la msingi kama mitaji ya hawa wafanyabiashara ingekuwa-mobilized pamoja na zile Serikali na kuweza kufanya uwekezaji katika kujenga mtambo wa kuchakata gesi asilia kuwa katika hali ya kusafirishwa tayari kwa matumizi nchi nzima, na kuuzwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, inaonesha kuwa matumizi ya LPG kwa nchi yetu ni kidogo san asana kwa kulinganisha ma majirani zetu wa Kenya, ambao matumizi ni mara nne ya matumizi yetu. Matumizi ya gesi kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ni wastani wa of 2.3Kg kwa mwaka, kwa mujibu wa taarifa ya of World LPG Association (WLPGA),kwa kulinganisha na wastani wa matumizi ya 55Kg kwa mwaka kwa nchi za Africa ya Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, wakati wastani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahala ni matumizi ni 2.3kg kwa mwaka, Tanzania matumizi ni wastani wa 1.4kg kwa mwaka, wastani ambao ni chini na nchi ambazo tuko nazo kundi moja.
Mheshimiwa Spika,mfano mzuri ni ulinganisho wa gunia moja la mkaa linalouzwa kwa shilingi 40,000/- hadi 60,000/- na mtungi wa gesi wa kilo 15 unaouzwa kati ya shilingi 45,000/- hadi 55,000/- kulingana na eneo. Hivyo basi kama tukiwa na mkakati mzuri wa kuhamasisha matumzi ya gesi, ikiwemo kuwa na bei elekezi ni dhahiri tutaokoa misitu yetu.
Mheshimiwa Spika, tumeweka takwimu hizo kuonesha ni jinsi gani matumizi ya nishati Kuni ilivyo kubwa kwa nchi yetu na wakati huo hakuna mkakati wote wote wa kuhamasisha matumizi ya nishati gesi kwa matumizi ya nyumbani ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika, Wataalamu wawili wa Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) wakati wakiwasilisha mada kwenye semina ya wahariri iliyofanyika Bagamoyo na kutoa “Tathmini za kitaalamu na uzoefu wa masuala ya uziduaji na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi, yanaonesha pasipo shaka kuwa nchi za Afrika mapato yake hayawezi kuwa zaidi ya asilimia 25 ya pato la Taifa na hivyo ni makosa kufikiri kuwa nchi itaenda mbele sana kwa kutegemea gesi na mafuta pekee, ila kwa kuchechemua sekta nyingine za uchumi. Hivyo, kwa ujumla wake zitabainisha na kugeuza mwelekeo wa sekta hizo kwa kuzipa kipaumbele kwa mitaji na hivyo kusisimua uchumi wa nchi husika na uchumi wake kudorora,” walisema wataalamu hao wawili katika nyakati tofauti.
Mheshimiwa Spika, Wakiwasilisha mada mbili ya ‘Mapitio ya Sekta Rasilimali Gesi Asilia Historia yake, Hali ya Sasa na Mipango ya Baadaye’ iliyotolewa na Mhandisi Shaidu Nuru Mwanajeolojia na Mratibu wa Mchango wa Nchi (Local Content) wa TPDC na ya ‘Mapitio ya Matumizi, na Mkondo wa Chini wa Gesi Asilia’ iliyotolewa na Aristides Kato ambaye ni Ofisa Mtafiti wa TPDC, wameonesha wazi tatizo kubwa limezuka nchini la ‘kutawala matarajio yaliyokithiri’.
Mheshimiwa Spika, Wataalamu hao wanasema kulifanyika makosa kutoa kauli zilizokithiri wakati mambo bado yako mbali na hali ya uchumi hairuhusu kirahisi kuwekeza kutokana na mdororo wa uchumi duniani kufuatia sababu hasi lukuki zinazoendelea kudumaza mahitaji ya mafuta duniani, ikiwemo kuongezeka uzalishaji mafuta Marekani na kuanza kuuza mafuta yake katika soko la dunia na hivyo kupunguza mahitaji katika soko la dunia kwa asilimia 25.
Mheshimiwa Spika, Sababu nyingine ni kwamba, wakati huu dunia imeshuhudia matumizi makubwa ya teknolojia kule Marekani na Canada kufanya mabanzi ya mchanga (shale) kutengeneza mafuta, hivyo kuleta tafrani na utata kwa wawekezaji na kudhuru maendeleo ya miradi ghali ya gesi kama hiyo ya Tanzania ambayo gesi yake nyingi iko ndani baharini tcf 47.08 kilomita 120 toka nchi kavu kwenye kina cha mita 4000 na ile ilyoko nchi kavu ni tcf 8.04 na hivyo uendelezaji wake ni tatizo.
Mheshimiwa Spika, wataalam walifafanua kuwa mafuta ndio yanayofanyika kibiashara duniani kote, huku gesi asilia bado ikifanyika kieneo kidogo na hivyo bei ya mafuta ndio inayoamua uwekezaji katika sekta ya nishati, aidha, kuanguka kutoka zaidi ya dola 100 miaka miwili iliyopita na kuwa chini ya dola 40 mwaka huu. Hivyo kuuathiri uwekezaji wa Lindi kwani Msumbiji nayo imegundua gesi nyingi ya kiasi cha zaidi ya tcf 200 ukifananisha na tcf 57.2 ya Tanzania na hivyo kuwa mshindani mkubwa kwenye uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, kuongeza kuwa ushindani wa kupata mitaji umeimarika na kuvutia wawekezaji katika bara la Afrika, ni jambo gumu linalohitaji ushawishi mkubwa na hivyo kufanya watawala kuwa na wakati mgumu kufanya maamuzi sahihi kwa kuvutwa na kushawishiwa na matumizi ya mbinu mbalimbali kuweza kushawishi (lobby) na kuondokana na hali ya mkwamo mbele ya wananchi wao. Hoja hapa ni mwekezaji gani atakuja Tanzania kwa kauli zinazoendelea za kuwaita wawekezaji ni mabeberu na ni wezi wa Rasilimali zetu?
Mheshimiwa Spika,Statoil na mshirika wake ExxonMobil walifanya ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika visima vya Zafarani, Lavani, Tangawizi, Piri, Giligilani na Mronge katika Kitalu namba 2, chenye eneo la takriban kilometa za mraba 5,500, ambalo lipo umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka ufukweni katika kina cha maji kati ya meta 1,500 hadi 3,000.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Tanzania imeishagundua akiba ya gesi yenye futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 imegundulika.
Mheshimiwa Spika, Huwezi kusafirisha gesi katika hali yake ya kawaida, ni lazima kuisindika kwa kuibadili kuwa katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG), hivyo mtambo wa LNG una umuhimu mkubwa kwa biashara ya gesi kwa kusafirisha kwenye soko la kimataifa pamoja na matumizi ya ndani. Ni ukweli kwamba, katika ujenzi wa mtambo wa LNG, gharama zote zitalipwa na wawekezaji wakati serikali jukumu lake ni kutoa ardhi mahali mtambo huo utakapojengwa inaonekana jambo hilo kwa mwaka huu 2018/19, Serikali imetenga jumla ya shilingi 6,500,000,000/- ikiwa ni fedha za kulipa fidia kwa waathirika wa makazi katika eneo la mradi na pia zikiwa ni fedha za kufanya tafiti ili kusaidia timu ya Majadiliano(GNT). Hoja ya msingi hasa ni je wawekezaji ambao fedha za majadiliano tayari zimetengwa wapo tayari?
Mheshimiwa Spika, tulikwisha oneshwa manufaa faida katika kutumia gesi asilia katika kuendeshea magari badala ya kutumia mafuta ya petrol, kwamba Unafuu katika bei ya kununulia nishati hii ni rahisi zaidi ya asilimia 45 kulinganisha na bei ya mafuta ya petroli. Ulinganifu wa gesi asilia na petrol. Kilo 1 ya gesi asilia iliyoshindiliwa ni sawa na lita 1.54 ya petrol, bei ya kilo moja ya gesi asilia ni ndogo kuliko lita moja ya Petrol. Pia, gharama za ukarabati (service) wa magari zinapungua endapo utatumia gesi asilia badala ya mafuta ya petroli. Hii ni kwa sababu gesi asilia ni safi, muwako wake hauna masizi (carbon) kulinganisha na mafuta, hivyo itachukua muda mrefu kufanya ukarabati wa gari linalotumia gesi asilia (kilomita 5000) ukilinganisha na gari linalotumia mafuta (kilomita 3000).
Mheshimiwa Spika, TPDC walikwisha leta magari yanayotumia gesi asilia badala la Petrol au Dizeli na tukapewa matumaini kuwa kituo cha kujazia gesi kwenye magari kitajengwa Ubungo. Lakini hadi sasa Bunge halifahamu chcochote kuhusu mradi huo mkubwa wa matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya usafiri. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa Mradi huo ambao ulikuwa ni mkombozi kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 2 Desemba, 2013, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Prof. Sospeter Muhongo na ujumbe wake nchini Algeria, alisema kuwa makubaliano yamefikiwa baina ya Tanzania na Algeria ya kuanzisha kampuni ya Ubia itakayohusika na ujenziwa miundombinu ya kusambaza umeme na Kampuni ya Ubia ya kujenga mtambo wa kusindika gesi ya “Liquefied Natural Gas” (LNG) na kuiuza gesi kwa wananchi kwa kutumia mitungi.
Mheshimiwa Spika, Katika hatua nyingine, tuliambiwa kuwa Mawaziri hao waaliziagiza kampuni za mafuta na gesi likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za mafuta na gesi za Algeria za NAFTAL na SONATRAC kukamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya ubia ya kujenga mtambo wa LPG na kuuza gesi hiyo kwa wananchi kwa kutumia mitungi, ambapo kampuni zote za ubia zimetakiwa kuanza kazi ifikapo Januari, 2015[40].
Mheshimiwa Spika, ni muda mwafaka sasa Bunge hili kupewa mrejesho wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi zetu hizi yamefikiwa hatua gani ya utekelezaji?
Mheshimiwa Spika, wakati huohuo Waziri wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo alizindua ofisi za “Liquefied Natural Gas” LNG – Tanzania jijini Dar es Salaam. LNG ni muunganiko wa makampuni matano ya BG Group, Statoil, ExxonMobil, Ophir na Pavilion kwa ajili ya kufanikisha mipango itakayopelekea ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi. Makampuni hayo yanayounda LNG yatashirikiana na serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, hizo hadithi kwa kiasi kikubwa zimepelekea kuaminisha wananchi kuwa tunakwenda kwenye uchumi wa Viwanda na wimbo huo unaendelea kuimbwa na Serikali iliyopo madarakani wakati uhalisia wa jambo hilo haupo.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha 2018/19 ndio zimetengwa jumla ya shilingi 6,500,000,000/- kama fedha za ulipaji wa fidia kwa waathirika wa makazi katika eneo la mradi wa Kusindika gesi alisia kwenye hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG)
MATUMIZI YA GESI ASILIA KWENYE MAGARI
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo ni kwamba upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuweka mtandao wa mabomba ya kusambaza gesi na vituo vya kujazia gesi magari ulifanyika toka mwaka 2006/2007 na kuhusisha magari 8,000 na makazi yapatayo 30,000. Ujenzi wa mradi huo ulitarajiwa kuanza Julai 2015 ambapo zoezi la kumtafuta Mkandarasi pamoja na fedha za ujenzi takribani Dola za Marekani milioni 76 zilikuwa zikihitajika.
Mheshimiwa Spika, randama uk. 27 inaonesha kuwa kwa mwaka 2017/18 TPDC imeedelea na juhudi za kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya viwandani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambazia gesi hiyo kwa wateja. Usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga ulitengewa shilingi 6,274,252,000/- lakini hadi mwezi Machi,2018 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa.
Mheshimiwa Spika, aidha, bomba hilo linalosambaza gesi limehusisha uunganishaji wa nyumba 70 katika mtandao wa gesi asilia. Kwa mwaka huu wa bajeti 2018/19 jumla ya nyumba 60 zitaunganishwa katika maeneo ya Mikocheni na Mwenge, na imetengwa jumla ya shilingi 1,500,000,000/-.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupatiwa ufafanuzi kuhusu uwekezaji wa shilingi bilioni 1.5 katika usambazaji wa gesi kwa nyumba 60 tu kwa mwaka. Kwa kuwa kuona ni kuamini katika hili la kusambaza miundombinu ya matumizi ya gesi asilia majumbani, mikoa ya Mtwara na Lindi ambako gesi asilia inaanzia, baadae ifuatie mikoa mingine?
Malipo Yasiyostahili kwa Kampuni ya Maurel & Prom ya Dola za Kimarekani Milioni 27.18
Mheshimiwa Spika,Maurel & Prom (operator, 48.06% interest) ni kampuni inayoendesha visima viwili vya gesi vilivyopo Mnazi Bay vinavyo peleka gesi pale kituo cha Madimba Mtwara (processing centre -operated by GASCO, a subsidiary of TPDC) linapoanzia Bomba la Gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es Salaam.
.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 15.1 cha Makubaliano ya Mauziano ya Gesi (GSA) uliosainiwa Sept. 12, 2014, kati ya TPDC na Maurel & Prom (M&P) kinataka TPDC kuweka dhamana ya fedha kwa kuweka kiasi cha fedha kwenye akaunti ya pamoja (Escrow) au kwa Barua ya Mkopo kutoka Benki (letter of credit) au kwa mkataba wa dhamana ya malipo (payment guarantee agreement).
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ukaguzi wa CAG umebaini kuwa, TPDC ilitoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 27.18 (sawa na Shilingi bilioni 56.70) kwa kulipa akaunti ya M & P kinyume na masharti tajwa hapo juu huku ikichukulia fedha hizo kama malipo ya awali (prepayment). Pia, ilibainika kuwa fedha zilizolipwa kwa M&P zilikopwa kutoka Benki ya Maendeleo ya TIB.
Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa makubaliano rasmi juu ya namna fedha za dhamana zinavyotakiwa kuhifadhiwa unaiweka TPDC kwenye nafasi mbaya endapo kutatokea mgogoro wowote. Pia, kukopa fedha kwa lengo la kuweka dhamana kunaongeza gharama kwa taasisi kwa sababu ya riba. Mtindo huu wa kuendesha taasisi zetu ndio umekuwa ukisababisha taasisi zetu kutokupiga hatua za kwenda mbele. Kambi Rasmi ya Upinzani inaadharisha uwepo mwingine wa IPTL kutokana na mkataba huo kuingiwa kihuni baina ya Serikali na Kampuni hiyo ya Kifaransa.
Bomba la Gesi kutoka Mtwara – Dar es Salaam – Tanga-Mwanza-Kagera- Uganda
Mheshimiwa Spika, Bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lilijengwa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Company (CPTDC) kwa gharama ya takriban Dola za Kimarekani takriban bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China. Marejesho ya mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara.
Mheshimwa Spika, kwa sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo mteja mkuu wa gesi asilia; ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku, sawa na asilimia sita (6%) tu ya ujazo wa bomba; ambapo, kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba. Matumizi haya ni tofauti na makubaliano ya awali ambayo ilikua TANESCO liweze kutumia takribani futi za ujazo milioni 80 kwa siku kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya mkataba wa mauziano ya gesi asilia (GA).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inapenda kupata ufafanuzi kutoka Serikali kuhusu jitihada ambazo Serikali imechukua ili kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya TPDC na TANESCO uko wazi kwamba TANESCO itatumia gesi asilia kwenye mitambo yake sita (6) ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II, Tegeta na Symbion kwa kima cha chini cha matumizi cha futi za ujazo milioni 80 kwa siku na futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku kama kiwango cha juu. Hata hivyo, hadi sasa mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I ndio pekee unaotumia gesi asilia kuzalisha umeme; na unatumia kiwango asilimia thelathini na nne (34%) ya kiasi cha gesi yote iliyolengwa kutumiwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Mitambo mingine mitano iliyokuwa imekadiriwa kutumia kiasi cha (66%) bado haijaanza kutumika; na haijulikani ni lini mitambo hiyo itaanza kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kwamba gharama za ujenzi wa Bomba hilo toka Mtwara hadi Dar ulikuwa ni mkopo toka Exim Bank ya China na mkopo huo unatakiwa kulipwa, hoja ya msingi ni kwamba matumizi ya gesi hiyo bado ni kidogo kulinganisha na mahitaji yake.
Mheshimiwa Spika, ukianangalia Randama uk 68 inaonesha kuwa mradi huu unahusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda kupitia Tanga, bomba hilo linatakiwa kutumia mkuza uliopo wa Bomba la mafuta ghafi kutok Uganda hadi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa maana rahisi ni kuwa Bomba jipya linalojengwa ni kutoka Dar hadi Tanga, na gesi asilia iliyopo ni kwamba matumizi yake hapa kwetu yameishatosheleza na zaida ndiyo inatakiwa ipelekwe Uganda.
Mheshimiwa Spika, katika mradi huo zimetengwa jumla ya shilingi 1,500,000,000/- kwa ajili ya upembuzi yakinifu utakaoonesha gharama halisi za mradi na namna bora ya kutekeleza mradi huo.
BOMBA LA MAFUTA TOKA HOIMA-CHONGOLEANI
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi ni Mradi wa Sekta binafsi unatekelezwa katika nchi mbili (Uganda na Tanzania). Mradi huo uliokadiriwa kugharimu Dola za Marekani 3.55 bilioni na kuleta ajira za kati ya watu 6,000 na 10,000 ndani ya miaka mitatu (3). Mafuta Ghafi ya Hoima (ya aina yake), yatasafirishwa kutoka Uganda kwenda sokoni nchi za nje,kupitia Tanzania. Mradi wa Bomba umbali wake ni kilometa 1,445 ambapo kilometa 298 zitakuwa nchini Uganda, na kilometa 1,147 zitakuwa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, taarifa zinasema kuwa katika mchakato huo wa mradi ni dhahiri kuwa shughuli kadhaa za uchumi katika sehemu litakapoptia Bomba hilo na mwisho wake zitaimarika zaidi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba kilometa za urefu za bomba hilo zipo nchini Tanzani, na kati ya fedha Dola za Kimarekani 3.55 zilizotarajiwa kutumika ili kukamilisha mradi huo,
Kwa kuwa sekta binafsi inatarajiwa kushiriki kikamilifu, sekta hiyo itaunganishwa na TPSF. Kambi Rasmi ya Upinzania inauliza, Serikali inachangia kiasi gani katika fedha tajwa hapo juu na Sekta binafsi inatakiwa kuchangia kiasi gani? Kwani kwa mujibu wa Randama inaonesha kuwa mwaka huu wa fedha zimetengwa jumla ya shilingi 54,200,000,000/- kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la mafuta toka Uganda hadi Tanga.
STIEGLERS’ GORGE
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilikuwa inakadiria kuwepo na nakisi ya 4% ya Pato la Taifa katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo, kwa mwanzani ilikadiriwa kwamba matumizi kwa miradi ya maendeleo ingekuwa sawa na 10% ya pato la taifa, kutokana na makusanyo ya mapato kutokuwa mazuri ilikubalika kucheleweshwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo yenye thamani ya 1.2% ya pato la taifa hadi mapema mwaka 2018. Taarifa inaonesha kuwa bado kuna upungufu wa 1.6% ya pato la taifa katika lengo la bajeti ya maendeleo, kwa muktadha huo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mahitaji muhimu ya huduma za kijamii hauuwezi kufanikiwa[41].
Mheshimiwa Spika,miradi kipaumbele kwa mwaka huu 2018/19 ya uwekezaji ni mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha “standard gauge railway-SGR” kati ya Dar es Salaam na Mwanza, uzalishaji wa umeme wa 2100 MW Stiegler’s Gorge , ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda- Hoima hadi Tanga. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la fedha la Kimataifa ni kwamba miradi hiyo yote haina muda maalum wa utekelezaji ambao unaoneshwa na mpango madhubuti wa jinsi ya upatikanaji wa fedha utakavyokuwa.
Mheshimiwa Spika, nimeanza kwa kutoa maelezo hapo awali kuhusiana na nakisi katika bajeti ya miradi ya maendeleo kama ilivyokuwa imepangwa kwenye bajeti ya 2017/18 na matarajio ya nakisi hiyo kuwa kubwa zaidi. Hii ni ishala kwamba miradi hii mikubwa ambayo imekuwa kipaumbele ni dhahiri kwamba inahitaji fedha nyingi za utekelezaji wake lakini hakuna fedha za utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, jambo hili linapewa nguvu kutokana na taarifa ya tarehe 12/5/2018 iliyowasilishwa kwenye kamati ya nishati na madini na Serikali kuhusu uendelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu za maji Rufiji- (RUFIJI HYDROPOWER PROJECT RHPP) –Haionesha popote kuwa mradi huo utakamilishwa kwa fedha kiasi gani na kila mwaka zitakuwa zinatengwa kiasi gani na chanzo cha fedha hizo ni kipi.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi au muda wa utekelezaji wa mradi unakuwa –“determined” na “budgetary component” bila kuwepo na uhakika wa fedha mradi wa miaka mitatu au mitano unaweza kutumia hata miaka 15 bila ya kukamilika na kuna uwezekano kabisa mradi kuishia katikati bila kumalizika na kuanza uzalishaji. Hivyo basi, itakuwa ni vyema Serikali ioneshe “financing plan” ya mradi huo, kinyume na hapo ni kuzamisha fedha za walipa kodi bila sababu yoyote.
VYANZO VINGINE VYA UMEME WA MAJI
Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanyika miaka hiyo ya 80 inaonesha kuwa mbali ya Stiegler’s Gorge RUBADA inavyanzo vingine vya kuzalisha umeme wa maji, ambavyo ni;
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kuelezwa toka upembuzi huo ufanyike ni hatua gani tena imeishafanyika kuona vyanzo hivyo vinatumika kuzalisha umeme kwa matumizi ya maendeleo?
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Aldwych International Ltd ya Uingereza ndiyo iliyokuwa inashughulika na kuendeleza mradi wa umeme wa Ruhudji toka mwishoni mwa mwaka 2006.
Mradi wa Ruhudji wa uzalishaji 360 MW, kwa mujibu wa Power system Master Plan (PSMP) mwanzoni ulipangwa kumalizika 2014. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo na Kampuni tanzu ya Aldwych International Ltd ambayo itaingia ubia na Tanzania iitwayo Ruhudji Power Development Company Limited, (RPDC) umefikia kiwango gani?
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI ZA WIZARA
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara ya Nishati na Madini iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,122,583,517,000/- na kati fedha hizo, shilingi 1,056,354,669,000/- zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Aidha hadi mwaka wa fedha unamalizika kiasi kilichotolewa na hazina kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kilikuwa shilingi 698,612,973,035/- sawa na 66.1 % ya fedha zote za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara ya Nishati na Madini ilikadiria kutumia jumla ya shilingi 998,337,759,500 ikilinganishwa na shilingi 1,122,583,517,000 zilizoidhinishwa na Bunge mwaka 2016/2017, sawa na upungufu wa 11%. Sababu zinazotolewa na Serikali za kupungua kwa Bajeti ni kupungua kwa makadirio ya fedha za nje kutoka shilingi 331,513,169,000 mwaka 2016/ 2017 hadi shilingi 175,327,327,000
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ilitenga kiasi cha shilingi 938,632,006,000 ikilinganishwa na shilingi 1,056,354,669,000 zilizotengwa mwaka 2016/17, sawa na upungufu wa 11.1%.
Mheshimiwa Spika, uchambuzi huo wa bajeti kwa miaka hiyo miwili ilikuwa ni kwa wizara ya nishati na madini kabla ya wizara hiyo kutenganishwa na kuwa wizara mbili.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 wizara ya nishati ikiwa peke yake imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,665,141,000,000/- kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni shilingi 1,489,741,000,000/- na fedha za nje ni shilingi 175,400,000,000/-
Mheshimiwa Spika, katika fedha zote za maendeleo zilizotengwa, Mradi wa Rufiji-Hydro Power Project(Stieglers’ Gorge) umetengewa shilingi 700,000,000,000/- sawa na asilimia 42 ya fedha zote za maendeleo. Fedha zingine nyingi ni fedha za REA shilingi 412,083,000,000/- ambazo ni sawa na asilimia 24.7 ya bajeti nzima ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyoonesha hapo awali kuwa fedha hizi zote za REA takribani asilimia 85 zunarudishwa TANESCO, kwani miradi inayooneshwa hapo kwa ni ya REA inatekelezwa na TANESCO (Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Pili nay a Tatu- Turnkey Phase II na Phase III), na ukiangalia miradi hiyo kwa maana halisi ni jukumu la TANESCO. Kama kweli Miradi hiyo ni ya REA basi pasipo shaka kuwa TANESCO haina kazi ya kufanya na ipo tu kwa kuongeza gharama kwa walipa kodi, kwani fedha za REA kwa mlango wa nyuma ndizo zinaendesha TANESCO na fedha za TANESCO zinazotokana na mauzo ya umeme zinatumika kulipa “Capacity Charges” kwa wazalishaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya uvuvi hapa nchini inaongozwa na sera ya Taifa ya uvuvi ya mwaka 2015 ambayo inatoa mwelekeo wa sekta katika kukuza na kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa kuweka Dira na Dhamira ya sekta.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi mojawapo yenye fursa nyingi kwenye shughuli za mazao ya uvuvi. Fursa kubwa zinazopatikana katika sekta ya uvuvi nchini Tanzania zipo katika maeneo kama;, usindikaji wa samaki, uongezaji wa thamani ya samaki na bidhaa nyingine za samaki, utengenezaji wa vifaa vya uvuvi, ujenzi wa bandari za uvuvi na bandari kavu. Eneo jingine muhimu la uwekezaji kwa wajasiriamali kwenye upande wa uvuvi ni ufugaji wa samaki,kaa, lulu, ukulima wa mwani, na uzalishaji wa vyakula, mbegu na vifaranga vya samaki.
Mheshimiwa Spika,jukumu la kusimamia rasilimali za uvuvi nchini lipo chini ya Wizara ya mifugo na Uvuvi, aidha Wizara inashirikiana na Taasisi za Serikali ikijumuisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI,pamoja na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uvuvi wa Samaki ya mwaka 2016 inaonesha kuwa kiwango cha Raslimali kinachoweza kuvuliwa bila kuleta madhara ya upatikanaji wa ralimali hiyoni tani 750,000; na wastani wa uvunaji wa samaki kwa mwaka ni tani 350,000.Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa tani hizo zinavuliwa na wavuvi wapatao 203,529 ambao hutumia vyombovya uvuvi vipatavyo 59,338.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inaukanda wa bahari upatao kilometa 1,424 kwa mikoa ya (Tanga,Pwani, Dar, Lindi na Tanga), kwa takwimu za mwaka 2015 ni kuwa samaki wanaovuliwa kwa ukanda wa pwani ni tani 51,912 sawa na 14% tu ya samaki wote wanaovuliwa hapa nchini na maziwa yote kwa pamoja yenye ukubwa wa kilometa za mraba64,500(Kagera,Mwanza,Geita,Simiyu,Mara,Kigoma,Sumbawanga,Ruvuma, Mbeya na Njombe), samaki wanaovuliwa ni tani 314,062 sawa na 85%.
Mheshimiwa Spika, hali ya uvunaji na uzalishaji wa rasilimali katika maji ya nchi yetu imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka kutokana na sababu ambazo Wizara wanaona ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wavuvi kutoka 102,329 mwaka 2000 hadi 203,529 mwaka 2017; kuongezeka kwa vyombo vya uvuvi kutoka 30,171 mwaka 2000 hadi vyombo 59,338 mwaka 2017;
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa sababu hizi ni za ujumla mno, kwani kwa hali halisi ni kuwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vyombo na wavuvi ni dhahiri hata samaki wanaovuliwa wanatakiwa waongezeke, kwani kama baharini au ziwani hakuna kinachopatikana ni kwanini watu wazidi kufanyakazi huko badala ya kutafuta shughuli zingine?
Mheshimiwa Spika,katika maeneo yote yenye shughuli za uvuvi, Halmashauri husika zinapata mapato yake ya ndani kwa kutegemea sekta hii. Ni masikitiko ya Kambi ya upinzani kuwa, wavuvi ambao ni wachangiajiwakubwa wa mapato katika Halmashauri hizi wamekuwa wakipata madhira makubwa sana ambayo yanawafanya badala ya kuondoa umasikini yanawaongezea umasikini na hivyo mapato ya halmashauri yanapotea kutokana na kukosa taasisi imara za kusimamia sekta hii.
Operation Sangara na Jodari Ukanda wa Ziwa Viktoria na Pwani
MheshimiwaSpika, Operation Sangara inayoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Ziwa Viktoria ya kukamata wavuvi ambao wanatumia nyavu ambazo kikosi kazi cha Operation hiyo kinahisi sio mwafaka imeleta kilio kikubwa sana kwa wavuvi na kuwaletea umasikini wa ghafla. Operation hii imeleta maafa makubwa ya kiuchumi kwa wavuvi kutoka Kanda ya Ziwa. Zaidi ya watu milioni 5 ambao ni wavuvi na watu wanaoendesha shughuli zao kwa kutegemea uvuvi kwasasa hawana ajira. Taratibu zilizofanyika ni za kushangaza sana kwani zana za uvuvi kama mitumbwi, nyavu zimechomwa motowakati wa operesheni hii. Zaidi ya kuharibiwa dhana zao za uvuvi, wavuvi hawa na hata wamepigwa faini kubwa sana. Mfano, hata basi la abiria likikutwana mzigo wa mazao ya uvuvi wamekuwa wakipigwa faini; gunia moja la dagaa linapigwa faini zaidi ya shilingi milioni tatu.
Mheshimiwa Spika, Operation hii pia imeshusha kwa kiasi kikubwa biashara hasa mafuta ya petrol kwani sehemu kubwa za biashara hufanyika na wavuvi. Wavuvi hutumia kiasi cha lita zaidi ya milioni mbili kwa siku na kwasasa hiyo haipo.Kwasasa shughuli za uvuvi zimesimama kabisa baada ya nyavu zinazohitajika kukosekana madukani. Jitihada ya wafanyabiashara wa nyavu hizo zinazohitajika zimekwama kuingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Kenya baada ya nyavu hizo kuzuiwa kuingia katika kituo cha forodha Sirari zikisubiri kibali kutoka Wizara yaUvuvi na Kilimo.
Mheshimiwa Spika, sheria inasema nyavu zitakazotumika kuvulia ziwani ni lazima ziwe na matundu yenye inchi 6 na kuendelea, lakini katikaZiwa Viktoria kuna samaki wadogo chini ya inchi 6. Mfano; Furu, Gogogo (ngore) na Ningu. Hawa ni samaki maarufu sana katika Ziwa hili. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hawa wanavuliwa na Nyavu za inchi ngapi? Kambi rasmi inauliza pia inakuwaje wafanyabiashara wamekuwa wakiachiliwa kuingiza nyavu hizi huku wakiwa wanalipia kodi zote stahiki na kuwauzia wavuvi? Operesheni hii imekuwa ikienda kinyume na Sheria ya uvuvi namba 22 ambayo inaruhusu nyavu za uvuvi za inchi 6 na 7.
Mheshimiwa Spika,ukweli ni kuwa zaidi ya 60% ya wavuvi wa dagaa wameshindwa kuendelea na shughuli zao kwa sababu nyavu zilizopo hazina ubora wa kuweza kuhimili kazi za kila siku. Jambo hilo linazidi kupunguza mapato kwa halmashauri zetu, na kuzorotesha uchumi wa mfumo mzimaa wa uvuvi huu wa dagaa.Mfano, katikaHalmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, operesheni hii imeteketeza zana haramu za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya Tsh 900,000,000.
Mheshimiwa Spika, kutokuwepo au kupatikana kwa nyavu zinazokubalika kisheria kwa ajili ya uvuaji wa dagaa imekuwa ni usumbufu mkubwa sana na hivyo kutoa mwanya kwa watendaji kudai rushwa na kuwabambikizia kesi wavuvi.Mfano dhahiri ni walioendesha operesheni katika visiwa vya Irugwa-Ukerewe kudai fedha nyingi kuliko thamani halisi ya mali walizonazo wavuvi na wakishindwa wanakamatwa na kufunguliwa kesi za uvuvi haramu.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Wizara inasema kuwa katika Operation Sangara iliyoendeshwa kuanzia tarehe 01/01/ 2018 na kumalizika tarehe 11/02/2018 ikiwa imetumia siku 40 ilihusisha watendaji 252 kutoka wizara ya mifugo na uvuvi,Jeshi la Polisi, Baraza la usimamizi wa mazingira, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Idara ya Usalama wa Taifa navikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama hayo ambapo wahusika ni vyombo vyote vya dola, waathirika watapeleka wapi malalamiko yao ya kutokutendewa haki? Ni muda mwafaka wa kutafakari jinsi hizi Operation zinavyoendeshwa, tukumbuke hapo awali ilipoendeshwa operation tokomeza jinsi gani wafugaji walivyopata madhira na mifugo yao, na bila Bunge kuingilia kati mambo mengi yasinge fahamika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona hapa ni muda mwafaka kwa Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kuchukua nafasi yake katika kuangalia haki inatendeka kwa wavuvi na watu wote ambao hawakutendewa haki katika uendeshwaji wa zoezi hilo la Operation Sangara.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wavuvi wa Ukanda wa Pwani, nao wanapata madhila makubwa sana kutokana na makatazo ambayo hayaangalii hali halisi ya ukuaji wa sekta hii na hivyo kuongeza mapato kwa Halmashauri zilizo katika ukanda wa Bahari. Wavuvi wengi wadogo wanatumia uvuvi wa Mtanda “ring net” na ni lazima uzame ukiwa na mtungi wa gesi ya Oxygen.
Mheshimiwa Spika,operesheni Jodari nayo pia imeleta madhara makubwa kwa wavuvi upande wa pwani (baharini). Nguvu kubwa imekuwa ikitumika na watu wa operesheni hadi kufikia baadhi ya wavuvi kuuawa ama kujeruhiwa na silaha za moto na watendaji hao. Kambi rasmj yaupinzani bungeni ina kemea jambo hili kwa vikali kwani ni uvunjifu wa sheria zeth na kukandamiza haki za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya watendaji wasiofahamu uvuvi unafanyikaje wanashindwa hata kukaa na wahusika ili wajifunze, matokeo yake ni kuwafanya wavuvi kuwa masikini kwa kuteketeza mitungi na kupora engine za boti na wavuvi kukamatwa. Kwa upande wa Nyavu wanasema nyavu zenye ukubwa wa mm 38 au Inchi 2 ndizo zinazotakiwa. Sasa dagaa watavuliwa na nyavu zenye matundu ya ukubwa huo?
Mapato ya Uvuvi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za mapato kama yalivyotolewa na “kundi la Fungamano la vyama na vikundi vya sekta ya uvuvi”katika soko la samaki Magogoni/Ferry na maeneo mengine, ni kwamba wastani wa mapato yanayochangiwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa Taifa kwa soko la samaki Magogoni/Feri kwa mwaka mmoja niShilingi 8,663,294,000/- hizi ni stahiki za Serikali peke yake bado mzunguko wa biashara kwa wananchi. Aidha, vyombo vikubwa vinavyotumika katika mwambao wa Dares Salaam na Pwani ni 3,000 na vyombo vidogo 650, lakini wamiliki wanashindwa kufanyakazi kutokana na mazingira magumu wanayowekewa na watendaji na hivyo kupelekea Halmashauri zetu na Serikali kukosa stahiki za mapato kwa maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuiangalia vizuri sekta hii ya uvuvi hususan wavuvi wadogo ili wasiendelee kukandamizwa ili waweze kuzalisha ka kuwekea mazingira rafiki na kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni husika.
Tanzania Fisheries Research Institute- TAFIRI
Mheshimiwa Spika, sekta ya uvuvi hasa ile inayofanyika katika maji baridi inakabiliwa na changamoto nyingi, moja wapo ni kutokuwepo kwa uwekezaji katika rasilimali yenyewe na kwa wadau wanaohusika na uvunaji wa rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Spika, maendeleo ya sekta ya uvuvi yatafanikiwa kama uwekezaji hasa kwenye utafiti wa rasilimali iliyopo ili iwe endelevu na kwa rasilimali watu ili itumie rasilimali iliyopo kwa uendelevu. Ni ukweli kuwa tuna Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), katika randama yaa Wizara inaonesha kazi zilizopangwa kufanywa na taasisi hii kwa mwaka wa fedha 2018/19 zina gharimu jumla ya shilingi 662,492,693katika fedha hizo fedha zinazokwenda kwenye utafiti ni shilingi 177,446,000 sawa na asilimia 26.78 tu.
Mheshimiwa Spika, hakuna utafiti wowote unaofanywa wa kimaabara, ambao tunaamini ndio njia pekee ambayo inaweza kutusaidia katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwezesha samaki kufugwa(aquaculture)katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa uhakika zaidi tofauti na ufugaji samaki wa sasa ambao ni wa kubahatisha zaidi.
Mheshimiwa Spika,katika randama ukurasa wa 59 kifungu 9002; Idara ya ukuzaji viumbe kwenye maji zimetengwa jumla ya shilingi 259,137,000 kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza vituo 5 vya ufugaji samaki wa maji baridi kwa ajili ya kuzalisha vifaranga milioni 10. Aidha zimetengwa shilingi 64,950,000 kwa ajili ya kuendeleza vituo viwili vya ufugaji samaki wa maji ya bahari kwa ajili ya kuzalisha vifaranga milioni 3.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza sana kuwa TAFIRI iwezeshwe vya kutosha ili kabla ya kuanza kuzalisha vifaranga vya samaki ni muhimu kufahamu mazingira halisi ya wafugaji wetu na kama vifaranga hivyo vitaweza kuishi na kukua na kufikia uzito unahitajika sokoni kwa muda tarajiwa katika mazingira halisi ya wafugaji.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kuwa samaki hao wazazi ni wale wanaochukuliwa ziwani au baharini na kufugwa bila ya kufanyiwa utafiti wowote wa kimaabara (genetic modification), kama ambavyo sekta ya mifugo wameweza na kupata kuku wa nyama au wa mayai. Kambi Rasmi inasisitiza kuwa, kinyume na hapa ni ufugaji wa samaki utakuwa ni wa kubahatisha tu na katika kufanya hivyo tunazidi kuwafukarisha watanzania badala ya kuwatajirisha.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara, na kuwatengea fedha za kutosha TAFIRI ili utafiti ufanyike kwa ajili ya kuondokana na uwekezaji wa kubahatisha katika sekta hii kubwa ya kiuchumi.
Kupungua kwa Viwanda vya Kuchakata Samaki
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 1992 vilizinduliwa viwanda vya samaki ukanda wa ziwa Viktoria. Kwa upande wa Tanzania viwanda vipatavyo 13 vilifunguliwa kwa nyakati tofauti, lakini kwa sababu tofauti viwanda vimekuwa vikipungua na hivi sasa vimebakia viwanda 8 tu ambavyo vinafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, viwanda hivyo 13 vya awali vilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,065 kwa siku na kutoa ajira 4,088; kwa sasa uzalishaji unaofanyika kwa viwanda 8 umeshuka hadi tani 171 kwa siku sawa na asilimia 16 ya uzalishaji unaotakiwa. Viwanda hivyo 8 vinatoa ajira ya watu 2,179 ikiwa ni punguzo la ajira kwa asilimia 53.3
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kwamba samaki katika Ziwa ili kuwa endelevu inatakiwa wavuvi nao waelimishwe njia bora za uvuvi kwa kufanya uvuvi wa mzunguko kama ambavyo wafugaji wanavyofanya kwa kuhama hama ili kuacha samaki wazaliane na wakue. Ni ukweli kazi hiyo inafanyika na kuwa yenye tija kama taasisi zinazohusika zitatoa elimu ya kutosha badala ya kutumia Operations za mida mifupi na ambazo si enedelevu zinazowajeruhi wavuvi badala ya kutibu majeraha yao.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio kikubwa sana kutoka kwa wavuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika kuhusiana na uhamasishaji wa Serikali ili kuwekeza viwanda kwenye Ziwa Tanganyika, Kambi Rasmi inataka kufahamu hadi sasa kuna mpango gani wa kujenga viwanda katika ukanda huo au tayari viwanda vimeshajengwa?
Biashara ya Mabondo
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na kilio kikubwa cha wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na biashara ya mabondo. Mabondo ni mifuko ya hewa ya samaki “air bugs” hasa samaki aina ya sangara na kitoga au mboju, hivyo samaki wanapo pasuliwa mifuko hiyo inatolewa na kukusanywa.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikali wakati wanafanya semina kwa wabunge tarehe29 April 2018 inaonesha kuwa biashara hii ilianza toka mwaka 1990 kwa kusafirisha mabondo mabichi kwenda nchi za Asia, lakini taarifa hiyo hiyo inasema viwanda vya samaki katika ukanda wa Ziwa Viktoria vilianza rasmi mwaka 1992. Hapa tunaona kuna kitu ambacho sio sahihi kulingana na ukweli wa biashara hii ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mheshimiwa Spika, biashara hiyo inafanywa na watu ambao walikuwa ni wapaa samaki lakini kwa kujiongeza au kwa ujasiriamali wao wametafuta masoko kwa bidhaa hiyo na sasa hivi kimekuwa nacho ni chanzo kikuu cha mapato cha Serikali. Hayo mabondo hayawezi kupatikana kama Serikali haitotengeneza mazingira mazuri kwa wavuvi.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwa mtindo huu wa Serikali, mifupa inayobakia baada ya kutoa minofu (fish fillets) au kwa jina maarufu“mapanki” nayo yataanza kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa Serikali na wahusika wataanza kusakwa kama “digi digi”. Hoja ya msingi ni kufanya uwekezaji katika sekta ya uvuvi kwa kuanza kwanza kwa kuziimarisha taasisi zetu za utafiti ziwe imara zaidi kwa zinashirikiana pia na wadau katika kuendeleza raslimali zetu badala ya hali ilivyo ya kuwaongezea umasikini watanzania ambao tayari walikuwa wameishavuka msitari wa umasikini.
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Mpango pamoja na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18, katika Fungu 64 la Wizara; uvuvi ilitengewa kiasi cha shilingi 2,000,000,000/-zikiwa ni fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi,2018 hakuna fedha yoyote ya maendeleo iliyokuwa imetolewa na Hazina ,Kwa mwaka huu wa fedha 2018/19;imetengewa jumla ya shilingi 7,126,680,000/- zikiwa ni fedha za maendeleo na kati ya fedha hizo fedha za ndani ni shilingi 3,000,000,000/- na fedha za nje ni shilingi 4,127,680,000/-.
Mheshimiwa Spika, kwa kurejea Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge toka mwaka 2007 hadi 2016 Kambi Rasmi imekuwa ikisisitiza ujenzi wa bandari ya Uvuvi katika mwambao wa Bahari ya Hindi. Sambamba na hilo katika taarifa ya kamati iliyoundwa na Mhe Anne Makinda (Spika Mstaafu) na Kuongozwa na Mhe Andrew Chenge, taarifa hiyo maarufu kama Chenge 1 kuna maelezo ya kina kuhusu jinsi gani Tanzania inaweza kunufaika na uvuvi wa Bahari Kuu kwa kuwa na bandari ya Uvuvi.
Mheshimiwa Spika, miradi inayotekelezwa ni mradi mkuu wa “South West Indian Ocean Fisheries Governance and Shared Growth Project (SWIOfish)”, moja ya kazi zitakazo tekelezwa chini ya mradi huu ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kubwa ya Uvuvi nchini (kasma 4701 (CO1DO1)ambao umetengewa jumla ya shilingi 500,000,000/-. Kambi rasmi inamatumaini kuwa jambo hili litapewa kipaumbele kwa kuzingatia umuhimu uliopo katika sekta ya uvuvi wa Bahari Kuu katika kuinua uchumiwa nchi kwakuwa sekta hii ina uwezo wa kuwa chanzo kikuu cha uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa uchumi wa nchi na uchumi wa wa wananchi wa ukanda wa Pwani jambo hili lilitakiwa lipewe kipaumbele zaidi kuliko uwekezaji uliofanywa kwenye manunuzi ya ndege za Bombadier wakati shirika halikuwa na mkakati wa kibiashara (business plan) kwa ajili ya uendeshaji wa ndege hizo. Kwa maana nyingine uwekezaji huo kwenye Bombadier ni kupoteza fedha za walipa kodi au uwekezaji usiokuwa na malengo kwa kuangalia wanufaikaji ni wangapi na fedha zitarejeshwa baada ya muda gani.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia taarifa iliyowasilishwa katika semina iliyotolewa kwa wabunge tarehe 29/4/2018 inaonesha kuwa mapato ya uvuvi katika bahari kuu kati ya mwaka 2009/10 – 2018 ni jumla ya dola za Kimarekani 12,981,164.50 tu na hizi fedha zote ni fedha za ada ya leseni za meli zilizovua kwenye ukanda wa EEZ, na hakuna fedha zozote zilizokusanywa kutokana na mrahaba wa samaki waliovuliwa.Vilevile, hakuna taarifazozote za samaki ambao hawakutakiwa kuvuliwa (by-catch) wameuzwa, na kama wameuzwa haijulikani ni kiasi gani kimepatikana. Samaki hawa piawalitakiwa kuingizwa kwenye soko letu la ndani, lakini haijulikani kama hili nalo linatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kuna mradi mwingine katika kasma 4701 (CO1DO3) wa kufufua shirika la Uvuvi (TAFICO) kwa kuinunulia Meli 2 za Uvuvi na hivyo kutengewa jumla ya shilingi 243,500,000/-. Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na jambo hili bali ina wasiwasi mkubwa kutokana na ukweli kwamba hapo awali kilikwisha nunuliwa kivuko cha Bagamoyo- Dar es Salaam na kilitumia fedha nyingi lakini imekuwa bahati mbaya sana hakikukidhi matarajiwa ya walipa kodi. Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa tahadhari tusije tukanunua meli ambazo hazitoweza kukidha matarajio ya watanzania /wadau walio wengi kwenye sekta hii.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni muhimu tukafahamishwa kwa kina je sababu za shirika hilo kufa ilikuwa ni kukosekana kwa meli tu au kulikuwa na sababu zingine? je hizo sababu zingine ambazo tunaamini bado zipo zimepatiwa ufumbuzi wa kutosha?
Uagizwaji wa Samaki kutoka Nje
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi inataka kujua ni kwanini nchi yetu inaagiza samaki kutoka nje ilhali ina rasilimali kubwa ya maji yenye hazina kubwa tu za viumbe wanaoweza kuibeba sekta ya uvuvi. Sekta hii pia ina rasilimali watu (wavuvi) wa kutosha wa kuwezaa kuiendesha sekta hii. Kwasasa nchi ina zalisha tani 350,000 tu badala ya tani 700,000 ambazo zinahitajika.
Makusudio ya Bajeti kwa Mwaka 2018/19
Mheshimiwa Spika,Kwa mwaka huu wa fedha 2018/19; Wizara imetengewa jumla ya shilingi 7,126,680,000/- zikiwa ni fedha za maendeleo na kati ya fedha hizo fedha za ndani ni shilingi 3,000,000,000/- na fedha za nje ni shilingi 4,127,680,000/-.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi imeona dhahiri kuwa Serikali hii haijatambua bado umuhimu wa Sekta ya uvuvi katika kuukuza uchumi wake na kuwagusa moja kwa moja wavuvi.
1.0 HATMA YA SEKTA YA MADINI NCHINI
Mheshimiwa Spika, Sekta ya madini imekuwa haifanyi vizuri tofauti na matarajio ya walio wengi nchini. Utajiri mkubwa wa madini yaliyoko nchini ,hauendani kabisa na hali ya umaskini mkubwa wa wananchi . Mpaka sasa 45% tu ya mauzo ya nje ya nchi yanategemea madini huku nchi yetu ikiwa ni ya 4 barani Afrika kwa uzalishaji wa madini hususani ya dhahabu. Ni wazi kuwa bado wananchi walio wengi hawanufaiki na sekta hii na taifa halipati mapato stahiki kutokana na madini.
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini nchini imeshindwa kutoa mchango wenye manufaa katika bajeti ya serikali. Kwa mujibu wa hotuba ya Naibu Waziri aliyeitoa tarehe 15,Januri 2018 akizungumza na Wakuu wa Idara na tengo wa Wizara ya Madini Ofisi Kuu Dodoma alisema mpaka sasa sekta ya madini huchangia 3.5% tu katika pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, ni fedheha kwa nchi yetu iliyozungukwa na madini na miamba ya aina mbalimbali kushindwa kukusanya kodi na maduhuli kiasi cha kutosheleza angalau mahitaji ya bajeti ya wizara nne.Mfano, kwa mujibu wa ripoti ya Jiolojia ya Mwaka 2007 kuhusu aina za madini na kiwango cha madini nchini inasema nchi yetu ina aina 5 kuu za madini yakiwemo madini ya metali inayojumuisha madini ya dhahabu takribani tani 2,222, chuma (iron ore takribani tani milioni 103,nikeli takribani tani milioni 209, kobalti na fedha. Aina ya pili ya madini ni yale ya vito inayojumuisha madini ya almasi ambapo nchi yetu ina takribani karati milioni 50.9, tanzanite takribani tani 12.60, yakuti, garnets na lulu. Aina ya tatu ni madini ya viwandani kama vile chokaa, magadi soda takribani tani mil 109 (soda ash), jasi (gypsum) ambapo tuna takribani tani mil 3, chumvi na fosfet(phosphet) takribani tani mil 577.4 Aina ya nne ni madini yanayozalisha nishati kama vile makaa ya mawe takribani tani mil 911, na pamoja na uranium. Aina ya tano ni madini ya ujenzi kama vile kokoto, mchanga na madini kwa ajili ya terazo.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa katika soko la dunia mathalani soko la dhahabu kwa wastani once 1 huuzwa kati ya dola 1,296, na kilo moja ya dhahabu huuzwa mpaka dola 41,696 sawa na shilingi milioni 92,565,120 kwa exchange rate yashilingi 2,220. Pamoja na gharama nyingine nyingi kuanzia kwenye uchimbaji mpaka kwenda sokoni bado nchi yetu ina uwezo wa kukusanya fedha nyingi kupitia sekta ya madini ambayo kwa sasa imekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi kwa kuwa wengi wao hawanufaiki.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo sekta hii imeshindwa kuwa kipaumbele cha kutoa ajira kama ambavyo kwa nchi nyingine imekuwa ikichangia kiasi kikubwa ch ajira hususani kwa vijana. Mfano, katika nchi ya Afrika ya Kusini, sekta hii inatoa ajira takribani 30,000 kwa mwaka ikilinganishwa na hapa nchini. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ya Mwaka 2015 inaonyesha kuwa sekta rasmi ya uchimbaji madini ilitoa ajira 7,355 ambazo ni za moja kwa moja na takribani ajira 3,000 za wakandarasi tu. Pamoja na hilo madhalani, kwa mwaka 2015,sekta hii ya madini ilipunguza wafanyakazi kutoka 7,335 hadi kufikia 6,205 wenye ajira za moja kwa moja kwa kipindi cha mwaka 2015 pekee.
Mheshimiwa Spika, hii ni sawa na punguzo la takribani 15% ya punguzo la ajira katika sekta ya madini. Mwaka 2017, takribani ajira za wafanyakazi wapatao 2,000 walipunguzwa kutoka kampuni ya Acacia pekee. Kati yao wafanyakazi 1,200,kutoka mgodi wa Bulyanhulu na wakandarasi wapatao 800 kutoka kwenye kampuni zenye zabuni kwenye mgodi.[42] Hili ni punguzo kubwa la ajira nchini kwa kampuni moja kusimamisha idadi kubwa ya wafanyakazi kiasi hicho. Maana yake ni kuwa familia zilizokuwa zikitegemea kupata riziki kupitia mgodi huo zimeachwa katika lindi kubwa la umaskini. Vilevile, serikali kupitia mifuko ya hifadhi nayo imekosa kodi na hivyo kupunguza pato la serikali. Hizo ni baadhi tu ya athari ambazo zimejitokeza kutokana na kuporomoka kwa sekta hii ya madini.
2.0 MWENENDO WA BAJETI KATIKA SEKTA YA MADINI
(1) Fedha zinazotolewa kwenye Miradi ya maendeleo ni fedheha kwa serikali
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2017/2018, serikali ilitenga kiasi cha shilingi 21,783,000,000 (21.783 bil) kwa ajili ya miradi ya maendeleo mpaka kufikia Mwezi Februari Mwaka huu (2018) fedha iliyotolewa ni shilingi 834,976,618 (mil 834.976) tu sawa 3.83% ya bajeti yote ya Miradi ya Maendeleo zilizopokelewa. Hata hivyo katika fedha hizo hakuna fedha yoyote iliyotoka katika fedha za ndani..
Mheshimiwa Spika, katika mchanganuo wa fedha zilizotengwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani ni pamoja na mradi wa usimamizi endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) ambao ulitengewa shilingi 8,900,000,000 (bil 8.9), Mradi wa Regional Mining Development (Ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara) kiasi cha shilingi 1,500,000,000 (bil 1.5) na mradi wa Kiwira Coal Mines and 200 MW Power Plant ulitengewa kiasi cha shilingi 10,000,000,000 (10 bil) lakini jambo la kushangaza hakuna kiasi chochote kilichotolewa mpaka kufikia Mwezi Februari 2018.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika Mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara imetengewa kiasi cha shilingi 19,620,964,000 ikiwa ni bajeti ya Miradi ya Maendeleo ikilinganishwa na shilingi 21,783,000,000 zilizotengwa Mwaka 2017/2018.Hii ikiwa ni sawa na pungufu ya asilimia 9.93%. Hii ikionyesha wazi hali kutokuwa kwa uchumi wetu sio katika sekta ya madini pekee bali katika sekta nyingine zikiwemo kilimo, maji, afya n.k
(ii) Upelekaji wa fedha TEITE na harufu ya Ufisadi
Mheshimiwa Spika, fedha iliyopokelewa kwa ajili ya za utekelezaji wa kazi za Taasis ya Uhamasishaji Uwazi katika Rasilimali za Madini , Mafuta na Gesi Asilia (TEITE),fedha iliyotolewa kwa robo tatu ya Mwaka 2017/2018 ni shilingi 29,412,207.87zikiwa ni fedha za ndani na kiasi cha shilingi 834,976,618 zikiwa ni fedha za nje kutoka Serikali ya Canada. Fedha iliyokuwa imetengwa kwa Mwaka 2017/2018 ni kiasi cha shilingi 1,490,959,600 ambapo fedha za ndani zilikuwa ni shilingi 107,959,600 ikiwa fedha iliyotolewa ni sawa na 27% tu ya fedha za ndani zilizotengwa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo Mwaka 2013, Serikali ilisaini mkataba na serikali ya Canada kupitia Idara ya Global Affairs Canada(GAC. Mkataba huo ulilenga kuipatia serikali kiasi cha Dola za Canada milioni 2.5 kwa awamu tano. Katika awamu ya nne Dola za Canada 500,000 zilitolewa Mwezi April 2016 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa TEITE kwa Mwaka 2016/2017. Hizi ni sawa na shilingi 878,655,861.36 (mil 878.655) kwa exchange rate ya shilingi 1,757.31Tsh. Mpaka sasa fedha hizo hazikuwahi kutolewa na HAZINA licha ya jitihada nyingi kufanyika. Kwa kuwa fedha hizi zilikuwa zimeshaingizwa kwenye utekelezaji wa Mpango Kazi, kazi nyingi zimeshindwa kufanyika na hivyo kupeleka fedha zilizotolewa 2017/2018 kutumika kulipa wataalamu elekezi waliokamilisha kazi zilizopangwa kwa Mwaka 2016/2017. Hivyo bajeti ya 2017/2018 nayo ikaathirika kutokana na upungufu wa fedha hiyo iliyotumika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inataka kujua kiasi cha Dola za Canada 500,000 hazijatolewa na HAZINA kwenda TEITE kwa kazi iliyokusudiwa mpaka leo? Fedha hizo zinafanya nini HAZINA?
(iii) Upelekaji wa fedha –Chuo cha Madini Dodoma (Serikali na Mkakati wa kukiua Chuo cha Madini Dodoma).
Mheshimiwa Spika, hali ya fedha katika Chuo cha madini Dodoma imeendelea kuwa mbaya tofauti na miaka ya nyuma 2013-2015 ambapo fedha ilikuwa ikitolewa angalau kwa utoshelevu. Chuo hiki ndicho kinachotegemewa kuzalisha wataalamu wa Jiolojia nchini. Pamoja na ukosefu mkubwa wa fedha chuoni hapo bado chuo kinalazimika kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 529 kwa Mwaka wa Masomo 2016/17 mpaka wanafunzi 542 kwa Mwaka 2017/18.
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2013/14 bajeti iliyoidhinishwa ni shilingi bil 3.609 na iliyotolewa ni shilingi bil 3.055 sawa na 84.64% , fedha iliyoidhinishwa kwa Mwaka 2014/15 ilikuwa shilingi bil 4.609 na fedha iliyotolewa ni shilingi bil 3.020 sawa na 65.52%. Kuanzia Mwaka wa fedha 2015-2018 hali ya fedha imezidi kuwa mbaya chuoni hapo kwani fedha iliyoidhinishwa kwa Mwaka 2015/16 ni shilingi bil 5.714 na iliyotolewa ni shilingi bil 1.540 sawa 26.96% tu, kwa Mwaka 2016/2017 fedha iliyoidhinishwa ni shilingi bil 1.319 na iliyotolewa ni shilingi mil 549.8 sawa na 41.67% , kwa Mwaka 2017/18 fedha iliyoidhinishwa ni shilingi bil 1.238 na iliyotolewa ni mil 337.3 sawa na 27.25%
Mheshimiwa Spika, upelekaji wa fedha katika chuo hiki unaonyesha wazi kuwa serikali inafanya mzaha na sekta ya madini hususani kwenye kuzalisha wataalamu. Wakati serikali ikiwa haina wataalamu wa miamba na madini wa kutosha , huku ikiwa na ndoto ya kujenga kiwanda cha uchenjuaji madini hapa nchini, haipeleki fedha ili kuwekeza katika taaluma. Hii inaonyesha wazi kuwa serikali ya CCM imepoteza dira ya Maendeleo ya Taifa hili. Kamwe hatuwezi kufikia Malengo Endelevu 2030 kwa hali hii serikali inavyoipeleka taifa letu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuacha mzaha na sekta ya madini ambayo ndio tegemeo kubwa la rasilimali ya kukutoa kwenye umaskini. Uwekezaji wenye tija katika elimu na vifaa vya kisasa na technolojia inayoendana na wakati ndio suluhu pekee la kutukoa katika hali hii mbaya katika sekta ya madini. Hivyo, Kambi Rasmi linaitaka Bunge lako bila kujali itikadi za vyama kusimamia kwa sauti moja upelekaji wa fedha katika Chuo cha Madini Dodoma ili tuweze kuzalisha wataalamu wa kulisaidia taifa.
(iv) Upelekaji wa fedha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kugeuka mzigo kwa serikali na walipa kodi
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, STAMICO ilipanga kukusanya shilingi 20,951,569,301. Kati ya fedha hizo fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ni shilingi 13,248,988,251, na shilingi 4,061,271,600 kama matumizi mengineyo (OC) na shilingi 3,641,309,450 kama fedha za mishahara.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kuanzia Julai, 2017 mpaka kufikia Februari 2018, STAMICO ilipokea shilingi 2,183,541,383,00 sawa na 10% ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Fedha hizi zilitumika zaidi kwenye matumizi mengineyo, OC, na mishahara. Katika miradi ya maendeleo Shirika lilipaswa kuwezeshwa mtaji wa shilingi bil 50 ili kuweza kujiendesha kibiashara kwani mpaka sasa STAMICO inajiendesha kwa hasara. Hata hivyo, katikamiradi ya maendeleo kiasi kwa Mwaka 2015/2016 serikali ilitenga shilingi bil 2, kwa Mwaka 2016/2017 ilitenga bil 2 na Mwaka 2017/2018 ilitenga shilingi bil 10.Hata hivyo, kwa miaka yote hiyo Shirika halikuwahi kupokea fedha yoyote ya maendeleo au mtaji ijapokuwa kila fedha inayokusanywa ya maduhuli na kodi hurudhishwa serikalini.
Mheshimiwa Spika, katika mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo kwa Mwaka 2017/18 serikali ilipanga kukusanya shilingi bil 2.100 kutoka kwenye huduma za uchorongaji na ushauri wa kitaalamu ila kufikia februari 2018 ilikusanya shilingi mil 40.384 sawa na 6% tu ya makadirio. Katika mradi wa dhahabu wa Buhembailikadiria kukusanya shilingi mil 60 hata hivyompaka februari 2018 haikukusanya fedha yotote. Kupitia mradi wa Tanzanite One ilikadiria kukusanya shilingi bil 1 ila mpaka februari 2018 ilikusanya shilingi mil 116.798, sawa na 11.7% . Katika mradi wa STAMIGOLD ulikadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi mil 529,012,749 ila mpaka Februari 2018 hakuna fedha yoyote iliyokusanywa, Gawio kutoka TML ilikadiriwa kukusanywa mil 60 mpaka februari 2018 hakuna fedha yoyote iliyokusanywa. Hii ni baadhi tu ya miradi ambayo inaonyesha wazi hali ya sekta ya madini bado ina changamoto kubwa. Kambi Rasmi inahoji ni nini hasa kiLichosababisha miradi hiyo kushindwa kukusanya fedha mpaka Mwezi Februari Mwaka huu 2018. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kulieleza Bunge hili Je, mpango wa Serikali ni kuiua STAMICO au kuna mpango gani wa kuweza kulinusuru Shirika hili lenye majukumu mengi na makubwa huku likijiendesha kwa hasar?
3.0MADINI YA VITO NCHINI NA FUNGAMANISHO KATIKA KUKUZA AJIRA
Mheshimiwa Spika, Tanzania imebahatika kuwa mzalishaji wa madini ya vito ya aina mbalimbali, ambayo ni kama ifuatavyo; amethyst, aquamarine, cordierite, emerald, garnet, ruby, sapphire, spinel, tanzanite, and tourmaline.
Mheshimiwa Spika, Maeneo ambayo yamebahatika kuwa na madini ya vito ni pamoja na yafuatayo; Winza wilaya ya Mpwapwa Dodoma na Milima ya Uluguru yamejaliwa kuwa na ruby na sapphire ambapo uchimbaji unafanyika maeneo ya Matombo, Ngongolo, Mwaraze, na Kibuko.Wilaya ya Mahenge ni maarufu kwa madini ya spinel na ruby Tunduru maeneo ya Muhuwesi, Lumesule, na mto Ruvuma hadi maeneo ya juu ya Ngapa na Kitowelo, ni maarufu kwa uchimbaji wa blue, yellow, green, pink, and purple sapphires, na rubby. Wilaya ya Kilindi eneo la Loolera ni maarufu kwa uchimbaji wa ruby.
Mheshimiwa Spika, Faida moja wapo kubwa ya Madini ya Vito ni kwamba mara baada ya kuchimbwa yanaweza kuuzwa moja kwa moja (direct to the market like harvested crops). Madini haya hayahitaji hatua nyingine kama dhahabu inayohitaji uchakataji na uchomaji ili kupata zao la mwisho kwa ajili ya kuuza. Endapo dhahabu isipopitia hatua hiyo hujulikana kama ‘ghafi’ ambapo hata bei yake sokoni inabidi ipungue.
Mheshimiwa Spika, Kwa mantiki hii, uwekezaji katika shughuli ya biashara ya Madini ya vito si wa gharama kubwa ikilinganishwa na Madini ya metali. Mbali ya faida hiyo, Madini ya vito huuzwa bei kubwa zaidi ya Madini ya metali. Kwa ujumla, uwekezaji katika Madini ya vito ni njia mahususi katika kuondoa umaskini kwa wananchi na kuongeza mapato kwa serikali. Aidha suala la uharibifu wa mazingira hasa vyanzo vya maji, ni mdogo kwa sababu madini ya vito hayahitaji kemikali maana hayahitaji uchakatajii kama madini ya metali.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu zilizotolewa na Kamati ya Jaji Bomani inaonesha kwamba Tanzania ina hazina ya Almasi karati milioni 50.9, Tanzanite tani 12.60. na madini mengine ya vito ambayo tumeyaonesha hapo juu bado hatujafahamu tuna hazina kiasi gani. Lakini tunaamini hazina ni kubwa pia.
Mheshimiwa Spika, Ni muhimu pia kufahamu kuwa Serikali ilishaweka katazo la kusafirisha nje ya nchi madini ya vito ghafi kwa lengo la kuongeza faida kwa wazawa katika biashara nzima ya madini ya vito.
(i) Mchakato mzima wa mnyororo wa kuongeza thamani ( Beneficiation)
Mheshimiwa Spika, huu ni mchakato mzima wa mnyororo wa uongezaji wa thamani wa madini ya vito unaohusu ukataji na uchongaji wa madini kwa sura (shape) na ukubwa (size) kwa kusafisha na kung’arisha madini kulingana na mahitaji ya soko, hapa kunahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu na vifaa. Kwa njia hiyo ni dhahiri fungamanisho la madini ya vito na utoaji wa ajira vitaenda sambamba na hivyo sekta hii ndogo inaweza kuwa ni moja wapo ya vivutio vya watalii wengi kutembelea eneo letu la Tanzania. Hivyo ni muhimu kuwa na eneo maalum nchini kwa “Beneficiation of gemstones”
(ii) Kitengo cha Uchambuzi na Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito (Tansort )
Mheshimiwa Spika, TANSORT ni Kitengo cha Uchambuzi na Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Madini ambapo uthamini unalenga ukokotoaji sahihi wa mrabaha wa Serikali kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010,Kitengo hiki kilichoanzishwa mwaka 1966 kina ofisi tano sehemu tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na Antwerp nchini Ubeljiji, Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam),Kanda ya Kati-Magharibi (Shinyanga) Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Kusini (Songea).
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana ni kuwa TANSORT haina Ofisi nchini India au Thailand nchi ambazo ndizo zinasifika kwa biashara ya madini ya vito duniani. Aidha, TANSORT haioneshi kuwa na mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kufanya ‘Beneficiation’ kwa madini ya vito yanayopatikana hapa Tanzania.
(iii) Uzoefu wa nchi ya Thailand kuhusu madini ya vito
Mheshimiwa Spika, Thailand ni nchi iliyoendelea ikilinganishwa na nchi nyingine zinazoizunguka. Serikali ya Thailand ilitunga sheria; shughuli zote za uchimbaji na biashara ya madini vito itakuwa chini ya wazawa na kupiga marufuku usafirishaji wa madini vito ghafi nje ya Thailand bali ina ruhusu uingizwaji wa madini ghafi ya aina yoyote ndani ya Thailand bila kibali.Hatua iliyofuata ni kutengwa kwa mji wa CHANTHABURI kama kitovu cha biashara ya madini hususan madini ya Vito.Serikali ya Thailand kwa kushirikiana na taasisi za elimu walianzisha mafunzo ya utengenezaji na uvumbuzi wa mashine za bei nafuu zitakazotumika kukata, kuchonga na kung’arisha madini vito ili kuyaongeza thamani.
Mheshimiwa Spika, Zoezi hili lilianza kwa kuwatumia Wahunzi wa Jadi. Kwa kuwatumia hao, ilikuwa rahisi kuweza kutengeneza mashine kwa kutumia tekinolojia ya ndani. Zoezi hilo lilipata mwitikio mkubwa na mashine mbalimbali na ujuzi tofauti wa kukata madini ya vito vilivumbuliwa zaidi. Nchi ya India pia ilifuata mfano huu kwa kuwachukua baadhi ya Wahunzi wa mashine za kutengeneza nguo na kuwapeleka nchini Thailand kujifunza namna ya kutengeneza mashine za kuchonga na kung’arisha madini ya vito ikiwa ni pamoja na kujifunza kukata.
Mheshimiwa Spika, Baada ya mafunzo husika walirudi na serikali ya India ikatenga mji wa Jaipur kuwa eneo la kuanzia shughuli husika.Ndani ya muda mfupi Jaipur ukawa mji maarufu kwa uuzaji na ukataji wa madini ya vito. Itakumbukwa madini ya Tanzanite hukatwa kwa wingi na kuuzwa katika mji huu sababu kuu ikiwa ni hizo zilizotajwa – Manguli wa Kukata,kuchonga na kung’arisha Madini ya Vito kwa ustadi wa hali ya juu pamoja na Gharama nafuu.
Thailand imeendelea kuboresha biashara ya madini ya vito kwa kuanzisha huduma fungamano; vyuo vinavyotoa elimu ya Madini ya vito, viwanda vinavyotengeneza bidhaa (mapambo) zinazotumia madini ya vito, uanzishwaji wa maeneo rasmi ya uuzaji na ununuzi wa madini (Minerals Bourses), maonesho ya biashara ya madini ya vito mwaka mzima katika vipindi tofauti.
Mheshimiwa Spika, Katika nchi zote zinazo jishughulisha na madini ya vito, ‘Bourses’ imekuwa ndiyo suluhisho la makusanyo badala ya ‘Individual Broker and Dealers’’.
Masharti yamewekwa ya kuongeza kodi zaidi kwa ‘Individual Broker and Dealers’ na kuondoa au kupunguza kodi kwa wafanyabiashara katika ‘Bourses’.Bourses ni eneo linalotengwa na kujengwa na serikali na kuandaa meza ambazo wafanyabiashara huruhusiwa kufanya mauzo na manunuzi ya madini na watumishi wa serikali kutoza kodi na kutoa vibali vyote katika eneo hilo.
4.0 AHADI HEWA KATIKA SAKATA LA MAKINIKIA NA FUNZO KWA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Machi 2, 2017, Wizara ya Nishati na Madini iliandika barua kwa umma kuwajulisha wafanyabiashara na makampuni yanayojishuhulisha na shughuli za uvunaji wa madini kuacha mara moja shughuli za usafirishaji wa makinikia (concentrates) na mawe yenye madini ya metaliki kama vile dhahabu, shaba, nikeli na fedha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na katazo hili Rais aliunda kamati mbili za uchunguzi wa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Pamoja na mambo mengine ripoti zote zilizungumzia hasara kubwa tunayoipata kama taifa kutokana na sheria mbovu za madini na mikataba mibovu iliyoingiwa baina ya serikali ya ccm na wawekezaji. Ripoti zote mbili zilijikita zaidi katika kubaini viwango vya madini vilivyopo katika makinikia na mikataba ya uchenjuaji ambayo haikuwa wazi.
Mheshimiwa Spika, sakata la makinikia lilikuwa ni sakata la kisiasa lililojawa na ahadi nyingi hewa ambapo mpaka sasa linaigharimu serikali kutokana na maamuzi hayo ya kukurupuka. Kwa takribani miaka zaidi ya 20 Wabunge kutoka vyama vya upinzani walikuwa wakidai uwepo wa uwazi katika mikataba ya madini na ubovu wa mikataba mingi ikiwemo mkataba wa Buzwagi, Resolute, Bulyanhulu n.k. Katika awamu tofauti za serikali Mawaziri ambao ndio watendaji wakuu wa serikali walikuwa walilifumbia macho pamoja na kupigiwa sana kelele.
Mheshimiwa Spika, katika tume ya Jaji Bomani, iliainisha mapungufu makubwa katika mikataba ya madini ambayo iliruhusu upenyo wa ukwepaji kodi na ikiwemo ukwepaji wa mrabaha, usiri katika uendeshaji wa biashara ya madini nchini na rushwa. Japokuwa Sheria zilikuwepo, tatizo kubwa lilikuwa katika mikataba ambayo serikali iliingia na makampuni ya madini. Mfano Mwaka 1997 mpaka 2009 hakuna kampuni hata moja iliyolipa kodi ya mapato. Madhalani kampuni ya Resolute iliyokuwa inachimba dhahabu katika mgodi wa Lusu iliyochimba dhahabu kwa takribani miaka 14 ililipa kodi kwa kipindi cha miaka 2 tu kabla ya kufunga mgodi. Pamoja na hilo katika ripoti ya Makinikia ya mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagwi unaonyesha kuwa kampuni ya Acacia ambayo ndiyo mmiliki wa migodi hiyo ilikuwa ilkidaiwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kiasi cha dola za Marekani 190 bilioni sawa na zaidi ya trilioni 424 ambayo ni kodi iliyokuwa ikikwepwa pamoja na riba
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kiasi hiki cha fedha kiliwafanya watanzania kuwa na matumaini makubwa wengi wao wakiamini kila Mtanzania ataweza kumiliki gari aina ya Naoh na wengine wakiamini huduma za kijamii zitapatikana bure. Katika sakata zima la makinikia lililoihusisha kampuni ya Acacia serikali imeendelea kuyafanya yale yale ambayo iliifanya Mwaka 2007. Hii ni kutokana na kwamba Acacia waliikana taarifa iliyotolewa na serikali kuwa haijawahi kukwepa kodi na huilipa serikali 4% ya mirahaba ya dhahabu, shaba na fedha kwenye makinikia kama ilivyo kwenye makubalino baina ya serikali na Acacia.
Mheshimiwa Spika, tutakumbuka Mwaka 2007, kampuni hii ilituhumiwa kukwepa kodi na hivyo kuzua mtafaruku mkubwa na serikali wakati huo. Katika makubaliano Barrick iliilipa serikali kiasi cha dola milioni 700 kama kishika uchumba wakati mazungumzo zaidi yakiendelea ili kuona ni namna gani nchi itanufaika. Kuanzia kipindi kile matatizo na lawama za ukwepa kodi zimeendelea. Katika sakati hili la makinikia serikali imefanya yale yale kwani imepokea kiasi cha dola milioni 300 tenakama kishika uchumba. Hii ni pungufu ya mil 400 iliyopatikana mwaka 2007.Kwa maana hiyo timu ya makubaliano (negotiation team) imeshindwa hata kufikia kiwango cha milioni 700 kilichotolewa takribani miaka 10 iliyopita. Madhaifu haya ya kufanya majadiliano ya dili za kibiashara yanashindwa kutoa majibu chanya kutokana na kwamba watu waliolitengeneza tatizo hao hao ndio wanaotumwa kwenda kutafuta suluhu ya tatizo.
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika ripoti ya makinikia ilianisha takribani aina 11 za madini yaliyopo katika makinikia , serikali ilikubalina na Acacia kulipa asilimia 4 ya mrabaha tu bila kuangalia aina nyingine za madini yaliyo katika makinikia. Hii yote ni kutokana na mikataba mibovu na utendaji kazi uliokosa ufanisi katika taasis mbalimbali za serikali zinazojishughulisha na madini. Mpaka sasa serikali inazungumzia madini ya dhahabu, fedha na shaba pekee. Kamati ya makinikia ilianisha aina nyingine za madini kutoka kwenye nyaraka za usafirishaji wa makontena yaliyokamatwa bandari ikiwa ni pamoja na Sulfur, Chuma na madini mkakati (strategic metals) yaani iridium,rhodium,ytterbium,beryllium,tantalum na lithium)
Mheshimiwa Spika, kabla ya serikali kutoa zuio la kusafirisha makinikia nje ya nchi, kulikuwa na mazungumzo yanayoendela baina ya kampuni ya Acacia na kampuni ya Endeavour Mining kutoka nchini Canada. Mazungumzo hayo yaliyoanza mwezi January 2017, yalikuwa kuhusu kuuza kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara. Katika hatua za awali za majadiliano hayo kampuni ya Endeavour ilitaka kuinunua Acacia kwatakribani paundi bil 3, sawa na dola bil 4.4.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na mauziano hayo (Transfer of shares) Tanzania ingeweza kupata capital gain tax. Kutokana na zuio lililowekwa na serikali ya Tanzania dhidi ya kampuni ya Acacia iliilazimu kampuni ya Endeavour kusitisha majadiliano. Hivyo nchi ilipoteza takribani dola 880 mil sawa na shiling trilioni 1.8 ambayo ni 20% ya mauziano kama mpango huo wa mauziano ungefanikiwa. Hivyo kauli za kisiasa na maamuzi yasiyopimwa yamelisababishia taifa kukosa 1.8 trilioni ambayo ni zaidi ya bajeti ya kilimo ya mwaka 2018/2019.
(ii) Mfumo mpya wa uchenjuaji mbale
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, baada ya kutolewa kwa ripoti ya makinikia tarehe 22/09/2017 kampuni ya Acacia ilitoa tangazo kuhusu kubadilisha mfumo wa uchenjuaji mbale, .Hii ni kutokana na utafiti uliofanywa na Wakala wa Jiolojia (GST) katika mgodi wa Buzwagi ili kuhakiki ufanisi wa mfumo huo mpya (mbale) wa kuchenjua dhahabu ili kubaini kama serikali inapata faida au hasara.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa GST 2018, wakati mgodi wa Buzwagi ukiwa unazalisha makinikia mgodi huo ulikuwa unazaisha dhahabu kilo 28, fedha kilo 5 na shaba tani 18.9 kwa siku. Baada ya kubadili mfumo wa uchenjuaji kwa sasa unazalisha dhahabu kilo 23.5,fedha kilo 0.24 na shaba kilo 1.6 pekee kwa siku. Baada ya kutumia mfumo huu mpya uzalishaji wa dhahabu umepungua kutoka asilimia 97 mpaka asilimia 87 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu mpya wa uchenjuaji unasababisha kupotea kwa madini ya fedha na shaba . Hivyo kwa mfumo huu serikali inapata hasara kubwa tofauti hapo awali. Mauzo ya dhahabu hapo awali ilikuwa ni 95% ya mapato ya jumla,na 70% ni kutoka kwenye mauzo ya tofali za dhahabu, na 25% hutoka kwenye dhahabu iliyomo ndani ya makinikia. Iliyobaki 5% ya mapato ni kutokana na shaba iliyomo katika makinikia na kiasi kidogo tu cha fedha. Kwa maana hiyo kwa sasa kampuni inapoteza 30% ya jumla ya mapato. Na karibia 50% ya mapato ya pamoja ya Bulyanhulu na Buzwagi.Kwa katazo la kusafirisha makinikia tunapoteza mapato ya zaidi dola mil 1 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, kwa mfumo huu mpya wa uchenjuaji unasababisha pia mabaki ya fedha na shaba kuchanganywa na mabaki ya zamani ambayo hayakuwa yanasafirishwa kwa kuwa hayakuwa na madini yoyote au kiwango kidogo sana cha madini. Mchanganyiko huo (dilution) unasababisha serikali kupata hasara kwa kuwa mali iliyopo katika makinikia inapotea.
(iii) Mchakato wa kujenga kiwanda cha uchenjuaji (smelting)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Bunge lilipitisha Sheria mpya ya Mamlaka ya Nchi kuhusu umiliki wa Maliasili (The natural Wealth and Resources –Permanent Sovereignity 2017), iliyoletwa kwa hati ya dharura ndani ya Bunge na kujadiliwa kwa dharura katika kifungu cha 9 (1) kimeweka masharti kuwa shughuli zote za uzinduaji, uchimbaji na upatikanaji au utumiaji wa rasilimali utahakikisha kuwa hakuna rasilimali ghafi itakayosafirishwa nje ya Tanzania. Maana yake ni kuwa hata makinikia yasisafirishwe nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, maana yake ni kuwa nchi inapaswa kuwa na uwezo wa kufanya uchenjuaji hapa hapa nchini. Kuanzia mwaka 2011 serikali kupitia TMAA ilifanya upembuzi yakinifu(visibility study) ya uwezekano wa kujenga kinu cha uchenjuaji (smelting) hapa nchini. Baada ya upembuzi huo serikali ilitoa ripoti kuwa kujenga kinu cha uchenjuaji hakina faida ya kibiashara kwa nchi. Mwaka jana (2017) Waziri Mkuu alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mbeya, alitembelea mgodi wa Sunshine Group uliopo Chunya. Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji ili kuona namna ya kujenga mitambo ya kuchenjulia makinikia.
Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza ni kuwa,kama serikali ilifanya tathimini Mwaka 2011 na ikaja na majibu kuwa makinikia hayana faida hivyo hakukuwa na sababu ya kujenga kiwanda hapa nchini na kwa sasa tunaona serikali inaweza kupata faida kupitia makinikia, Je, serikali imechukua hatua gani ya kuwawajibisha wataalamu wale waliolisababishia hasara Mwaka 2011 kwa kuishauri serikali vibaya? Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama serikali imefanya tena upembevu yakinifu juu ya kujenga kiwanda cha uchenjuaji nchini na ripoti ya upembuzi huo inasemaje. Pamoja na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua mazungumzo baina ya serikali na Kampuni ya Sunshine Group yamefikia wapi?
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 60,000 za makinikia. Kwa kawaida viwanda vya uchenjuaji (refinery) huhitaji takribani tani 150,000 za makinikia. Hivyo, mpaka sasa bado hatujawa na utoshelevu wa malighafi ya makinikia kama ambavyo wataalamu mbalimbali wameainisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni aina gani mbadala ya teknolojia mbayo serikali itaitumia ili kuweza kufanya uchenjuaji wa kiwango hicho ambacho kinazalishwa nchini. Vilevile, ni muhimu kutambua kwamba uchenjuaji hufanyika kutokana na aina ya miamba.Kila aina ya miamba hutegemea aina fulani ya uchenjuaji.mfano, uchenjuaji unaofanyika mkoani Mara na maeneo ya Geita hatua zote huweza kufanyika mgodini na kuzalisha matofali ya dhahabu hii ni tofauti na Buzwagi na Bulyanhulu ambapo dhahebu yenyewe ndio bidhaa muhimu.
Mheshimiwa Spika,vilevile, ili kuweza kuendesha mitambo ya uchenjuaji ni lazima nchi iwe na umeme wa uhakika. Mpaka sasa tuna takribani megawati 1,500 ambazo hazitoshelezi mahitaji hususani mahitaji ya viwandani. Mpaka sasa serikali haijachukua mbinu mbadala katika uzalishaji wa umeme. Umeme unaotegemewa zaidi nchini unatokana na maji (hydro power). Hivyo serikali ni lazima ifanye uwekezaji wa kutosha katika vyanzo vingine vya umeme ikiwemo umeme wa upepo. Mpaka sasa upepo unaoweza kuvunwa katika maeneo ya Same, Singida na Makambako tuna uwezo wa kuzalisha takribani megawati 5,000 ambao utaweza kutusaidia katika viwanda kwa kuanzia. Hata hivyo, ni muhimu zaidi kuwekeza katika umeme wa jua (solar power) ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo vyanzo vingi vya maji vinakauka kutokana na kukata miti na kuongezeka kwa hewa ya ukaa.
5.0 MRADI WA MADINI YA BATI (KYERWA TIN COMPANY LIMITED)
Mheshimiwa Spika, kwa takribani miaka minne sasa kampuni tanzu ya Kyerwa Tin Company Limited (KTCL) ambayo hisa zake zinamilikiwa na STAMICO kwa 99% ya 1% inamilikiwa na Msajili wa hazina imekuwa ikishindwa kununua madini hayo kutoka kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kutoka Mwaka 2014 mpaka 2017 kampuni iliweza kununua jumla ya tani ya 106.267 tu kwa gharama ya shilingi 1,570,996,000. Mpaka sasa STAMICO wameshindwa kuendelea na shughuli za kununua kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wamewekeza fedha nyingi katika kuchimba madini haya na sasa serikali inashindwa kununua na hakuna soko jingine , ni kwa nini serikali isitafute wadau wengine wenye uwezo wa kuyanunua madini hayo?Mpaka sasa wananchi wengi wa maeneo hayo wamekopa fedha ili kuwekeza katika uchimbaji huo. Hivyo hawana fedha za kurudisha mikopo kitendo kinachowapelekea wengi kuishi maisha magumu na wengine hata kujitoa uhai kutokana na hofu ya kudhalilika kwa wingi wa madeni.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa baadhi ya walanguzi wameanza kujipenyeza baada ya kuona serikali haina uwezo wa kufanya manunuzi ma hivyo kununua madini hayo kwa fedha ndogo na kuyapeleka nchini Rwanda kwa bei rahisi ambapo serikali inakosa mapato. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua hatua ambazo serikali inachukua ili kuwanusuru wananchi hawa na madeni na hali ngumu ya kiuchumi. Serikali ieleze Bunge lako ni lini hasa serikali itaanza ununuzi wa madini hayo ya bati.
6.0 MRADI WA DHAHABU BUHEMBA UWEKEZAJI WENYE SHAKA
Mheshimiwa Spika, mgodi wa Buhemba ni moja ya mgodi ulioacha historia mbaya kwa wananchi wanaoishi Musoma Vijijini. Mradi huu uliachwa na kampuni ya Meremeta ambayo ilifunga uzalishaji katika mgodi huu na kuacha mashimo makubwa na uharibifu mkubwa wa mazingira. Karika ripoti ya ukaguzi wa mazingira iliyofanywa na TMAA 2007-2009 iliyowasilishwa kwenye kamati ya Bunge ya Nishati na Madini 2010, iliainisha uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo kuitaarifu serikali kuwa inahitaji takribani Dola mil 1.1 ili kufukia mashimo yaliyoachwa wazi na Kampuni ya Meremeta iliyofunga shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wa Buhemba.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, mapema Mwaka huu (2018) serikali ilitangaza kuufungua tena mgodi huu ili kuanza kuangalia kiwango cha mashapo ya dhahabu (mabaki) yaliyosalia baada ya Kampuni ya Meremeta kufunga mgodi. Hivyo, STAMICO ilitangaza zabuni ya kumpata mbia wa kushirikiana nae katika kuendesha mradi huo kwa njia ya ushindani ili kujiridhisha na uwepo wa mashapo hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Spika, mradi huo unakadiriwa kutoa takribani wakia 600,000 za dhahabu japo jambo hilo halijadhibitishwa kwa kuwa tathimini bado inaendelea. Mabaki hayo yaliachwa tangu wakati wa ukoloni, na vilevile unahusisha uchimbaji wa dhahabu katika miamba migumu (hard rocks mining)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 8.6 kwa ajili ya mradi. Pamoja na serikali kutenga fedha hii ni dhahiri kabisa mradi huu hauwezi kufanya vizuri kutokana na madeni makubwa yanayoukabili mradi huu yaliyoachwa kipindi cha nyuma. Wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi katika mgodi huu mpaka leo wanadai fedha zao. Wananchi waliohamishwa kupisha shughuli za mgodi hawakulipwa fedha zao ambapo takribani nyumba 100 zilivunjwa, zahanati na shule, Kambi ya Jeshi JKT iliyoitwa Buhemba nayo ilivunjwa.
Mheshimiwa Spika, Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa mashimo yaliyoachwa baada ya kampuni ya Meremeta kuondoka yanajaa maji jambo ambalo ni hatari kwa mazingira, na hata wachimbaji wadogo ambao wameendelea na shughuli za kujipatia riziki ndogo ndogo kutoka kwenye mabaki hayo. Mgodi huo ulikuwa sababu kubwa ya kupungua kwa maji katika Bwawa la Kiarano na kwa sasa maeneo hayo yanakabiliwa na shida kubwa ya maji hasa wakati wa ukame. Pamoja na kuwepo kwa malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi dhidi ya Kampuni ya Meremeta iliyokuwa inaedesha mgodi bado kampuni hii ilikuwa ni moja ya makamuni yaliyotajwa kukwepa kodi .
Mheshimiwa Spika, Sheria za kimataifa za migodi na miamba inatambua kuwa kabla kampuni yoyote haijafunga mgodi ni lazima ifanye miradi ya utunzaji wa mazingira angalau miaka miwili kabla ya kufunga mgodi ikiwa ni pamoja na kufukia mashimo, kuvunja mabanda, kuondoa mitambo na kupanda miti. Endapo kampuni itashindwa kufanya hivyo basi serikali ina uwezo wa kuinyang’anya mitambo ya uchimbaji au kufungua kesi ya madai.
Mheshimiwa Spika,hivyo basi, Kambi Rasmi inataka kujua ni kwa nini kampuni ya Meremeta iliacha mashimo hatari wazi huku sheria na matakwa ya leseni yakiwa wazi?Je, endapo kazi ya kufukia mashimo haikufanywa na Meremeta lakini serikali ikachukua jukumu, je, ni kiasi gani cha fedha kilicholipwa kwa serikali kutoka kampuni ya Meremeta katika shughuli ya kufukia mashimo? Je,endapo fedha hizo zilitolewa zilikwenda wapi au kufanyia shughuli gani? Mpaka sasa serikali ituambie je, iliwahi kufungua kesi yoyote kwa kampuni ya Meremeta kushindwa kufukia mashimo na kuchukua hatua za kulinda mazingira? Pamoja na hilo, serikali ilieleze Bunge ni mbia gani aliyeshinda tenda ya kushirikiana na STAMICO katika kuendesha mradi huu wa kutafuta mabaki ya dhahabu?
7.0 TANZANITEONE : MRADI UNAOFANYA VIBAYA
Mheshimiwa Spika, mgodi wa TanzaniteOne unamilikiwa na ubia baina STAMICO na Kampuni ya TanzaniteOne kwa usawa wa 50/50.Mpaka sasa shughuli za uzalishaji katika mgodi huu zimesimama tangu Mwezi Desemba. Hii ni kutokana na mapendekezo ya kamati maalum ya Spika katika kuchunguza mwenendo wa Biashara. Hata hivyo mgodi huu unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa wataalamu wa kuthaminisha madini, mitobozano, na madeni makubwa yanayotokana na madai ya wafanyakazi. Mpaka sasa ni takribani miezi sita wafanyakazi wa kampuni ya TanzaniteOne hawajalipwa mishahara yao takribani shilingi 3,094,756,320.
Mheshimiwa Spika, Mwezi Desemba 2017, kampuni iliuza madini ya vito yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.8 huku serikali ikipokea mrahaba wa shilingi milioni 126. Kiasi kingine cha takribani kilo 159.34 kimehifadhiwa kwenye maghala ya mgodi. Bado wafanyakazi wanasota kwa kukosa mishahara, familia zao zinateseka lakini hatuoni hatua stahiki zikichukuliwa na serikali kuhakikisha wafanyakazi hao wanapata fedha zao.
8.0 MAONI YA RIPOTI ZA KAMATI ZILIZOUNDWA KATIKA SEKTA YA MADINI NCHINI
Mheshimiwa Spika, kutokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu sekta hii ya utalii kuwa hainufaishi wananchi ipasavyo, serikali iliamua kwa nyakati tofauti kuunda kamati mbalimbali ili kuwa sehemu ya ufumbuzi wa changamoto katika sekta ya madini nchini.
Mheshimiwa Spika, zilizoundwa ni pamoja na kamati ya Mboma ya Mwaka 2002, iliyoundwa kuchunguza chanzo cha migogoro baina ya Kampuni ya AFGEM na wachimbaji wadogo katika eneo la Mererani mkoani Manyara, kamati nyingine iliundwa mwaka 2004, ilijulikana kama kamati ya Dkt Kipoloma iliyokuwa na jukumu la kudurusu sera ya Uwekezaji katika Sekta ya Madini, ilifuatiwa na kamati ya Masha mwaka 2006 iliyokuwa na jukumu la kupitia Mikataba ya Madini na kuchambua mfumo wa kodi katika Sekta ya Madini, kisha ilifuatiwa na kamati ya Bukuku,iliyokuwa na jukumu la kufanya majadiliano baina ya serikali, Chemba ya Madini ya Tanzania na Kampuni binafsi za Madini ili kufungua meza ya majadiliano kuhusu kufanya marekebisho ya baadhi ya vipengele katika mikataba ya madini nchini ili serikali nayo iweze kunufaika na wekezaji ano waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa ya nne aliunda kamati chini ya Jaji Bomani aliyotaka itoe mapendekezo kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini nchini. Mpaka Mwaka 2017, ambapo Rais wa awamu ya tano nae aliunda kamati chini ya Profesa Mruma ili kuchunguza sakata la usafirishaji wa mchanga wa Madini (Makinikia) pamoja na kamati ya wachumi na wanasheria iliyoundwa ili kuchunguza kinachojiri katika mchanga wa madini chini ya Profesa Osoro.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa kamati ya Spika ili kuchunguza madini ya Almasi na Tanzanite japo ripoti ile haikuwasilishwa ndani ya Ukumbi ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu wa Wizara wakiwemo mawaziri , kuvunjwa kwa bodi ya TMAA na baadhi ya watendaji kubadilishiwa kazi,Kambi Rasmi ya Upinzani inaona jambo hilo halitoshi hata kidogo kwani bado kuna mambo mengi hayajafanyiwa kazi, na serikali haionyeshi dalili za kuchukua hatua za kimkakati na za kisayansi za kuinusuru sekta hii. Maana yake ni kuwa bado mambo katika sekta hii ya madini yanafanyika kwa mtindo ule ule, walioliletea taifa hasara kubwa bado wengine wanaendelea na majukumu yao kama kawaida na hivyo kufanya zoezi zima kuwa la kisiasa na lenye kukosa tija.
(a). Kiasi cha madini ya Almasi
Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya Almasi, kamati ilibaini kuwa serikali haina takwimu sahihi kuhusu kiwango cha madini kilichopo katika migodi mbalimbali hapa nchini kwa sasa. Hili linajihidhirisha kwa kuwa katika ripoti ya Wakala wa Jiolojia (GST) ya Mwaka 2007 ilionyesha kuwa Tanzania ina hazina ya madini ya Almasi takribani karati milioni 50, katika taarifa ya Wakala wa Jiolojia Tanzania Mwaka 2009 ilionyesha Tanzania ina hazina ya almasi takribani karati milioni 40.4, na kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa serikali walitoa takwimu waliifahamisha kamati kuwa nchi inahazina ya almasi takribani karati milioni 38.0
Mheshimiwa Spika, mkanganyiko huu wa takwimu hautokei kwa bahati mbaya. Kukosekana kwa takwimu sahihi katika hazina ya madini maana yake ni kuruhusu mwanya wa kuibiwa na serikali kushindwa kudhibiti mwenendo wa rasilimali madini pamoja na mapato. Jambo la kusikitisha ni kuwa takwimu zilizopo zimetolewa kutoka upande wa mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, Jambo hili linashtua sana. Wakala wa Jiolojia nchini kamwe hataweza kufanya kazi zake za utafiti vizuri ikiwa serikali haiwekezi ipasavyo katika tafiti na vifaa vya kisasa na vya kisayansi vya kufanyia tafiti. Kwa kuwa katika utekelezaji wa mpango kazi wa GST fedha zinazotengwa ni fedha za matumizi (OC) na fedha za mishahara (PE) pekee. Hivyo utendaji kazi unakosa ufanisi kutokana na uhaba wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Mathalani fedha iliyotengwa (GST) kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 ni kiasi cha shilingi 5,225,916,900 (bil 5.225) kwa ajili ya fedha za mishahara na matumizi mengineyo. Hii ikiwa na maana kwamba uwekezaji katika tafiti ikiwa ni pamoja na upimaji wa kiasi cha madini,aina za madini, uratibu wa majanga mbalimbali ikiwemo milipuko na matetemeko ya ardhi ambayo kwa sasa yameanza kutokea mara kwa mara hususani mkoani Dodoma na Kagera, masuala ya kutengeneza ramani za jiosayansi ili kuanisha aina mbalimbali za madini na miamba itakuwa haifanyiki ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuangalia namna bora ya kuiwezesha GST ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Ni muhimu sana madini yote nchini yakafanyiwa utafiti upya ili kujua kiwango cha hazina ya madini iliyopo ardhini badala ya kuwaachia wawekezaji kufanya kazi za namna hiyo.
(b) Mapato yatokanayo na Almasi
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mkanganyiko mkubwa wa takwimu za uzalishaji wa madini nchini hususani almasi. Takwimu hizi zinaenda sambamba na takwimu za mauzo ya almasi nje ya nchi. Katika rejea ya mwenendo wa uzalishaji wa almasi nchini kabla ya kupitishwa kwa Sheria mpya ya madini 2017 na kusainiwa kwa kanuni mwezi Januari 2018,katika kitabu cha hali ya Uchumi nchini, 2016 kilionyesha kuwa uzalishaji wa Almasi ulikuwa kama ifuatavyo;
Mwaka | 2012 | 2013 | 2014 | 2015 | 2016 |
Karati | 127,174 | 179,633 | 253,875 | 216,491 | 237,685 |
Mheshimiwa Spika, hivyo basi katika kipindi cha miaka hiyo mitano uzalishaji wa almasi haukuwahi kufikiwa kiasi cha karati 300,000. Katika kitabu cha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti Julai 2017 mpaka 2018, Februari uzalishaji wa almasi umefikia kiasi cha karati 3,047,784.56 ( milioni 3.047) hii ikiwa ni uzalishaji wa takribani zaidi ya asilimia 1,282. Pamoja na hayo katika mlolongo (trend) ya takwimu za uuzaji wa almasi nje ya nchi Wizara haikuweza kuchanganua ni kiasi gani cha fedha kinachopatikana kwa kuuza almasi ghafi (rough) iliyokatwa au construct goods.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua usahihi wa takwimu hizi. Vilevile, Kambi ya Upinzani inahitaji kujua mpaka sasa nchi inaingiza kiasi gani cha fedha kutokana na kuuza almasi ghafi, Iliyokatwa na construct goods. Hii ni kutokana na historia iliyopo katika machimbo ya almasi nchini ambapo madini ya almasi yamekuwa hayainufaishi kabisa serikali kwa kipindi cha miaka mingi japokuwa madini haya huuzwa fedha nyingi katika soko la kimataifa.
Mheshimiwa Spika,tatizo la takwimu za uzalishaji madini hususani almasi na mapato halisi yatokanayo na almasi nchini lilizungumzwa pia katika ripoti ya kamati ya almasi ambapo uchambuzi wa Kamati ulibaini kuwa kiasi cha madini ya Almasi yaliyozaishwa kuwa kati ya mwaka 2007 hadi 2016 Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Madini (kabla ya kutenganishwa)ni jumla ya karati 1,484,471.17 . Huku takwimu za TMAA zinaonyesha katika kipindi hicho kulizalishwa jumla ya karati 1,513,200.00 za Madini ya Almasi. Kwa msingi huo takwimu za wizara zilikuwa chini kwa kiasi cha karati 28,728.83 za Madini ya Almasi sawa na asilimia1.9. Katika mapato yatokanayo na kuuza almasi nje ya nchi takwimu za Wizara zilionyesha kutoka mwaka 2007 mpaka 2016, ni Dola za Marekani 362,106,540.43 wakati taarifa za TMAA zinaonesha thamani ya Madini ya Almasi ilikuwa Dola za Marekani374,600,000.00. Hivyo takwimu za Wizara kuwa chini kwa kiwango cha Dola za Marekani 12,493,459.57 sawa na asilimia 3.4. Kwa upande wa mrabaha uliolipwa kati ya mwaka 2007 hadi 2016 ni kiasi cha Dola Marekani 18,105,327.01 kwa mujibu wa takwimu za Wizara, na kwa takwimu za TMAA mrabaha uliolipwa ni Dola za Marekani 15,000,000.00 hivyo taarifa za wizara kuripoti kiasi cha ziada cha Dola za Marekani 3,105,327.01 sawa na asilimia 17.1
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya utekelezaji wa Bajeti Julai, 2017 mpaka Feb,2018 bado haijaonyesha ni kwa namna gani biashara ya madini inayofanyika katika soko la ndani ya nchi inavyoinufaisha serikali. Mpaka sasa serikali haijajenga sehemu mahususi ya kibiashara yenye huduma na vifaa vya kisasa kama sehemu ya soko la ndani la madini nchini. Mara nyingi madini yanayovunwa nchini huuzwa katika masoko ya nje. Pamoja na kufanyika moboresho ya Sheria ya Madini na kubadilishwa kwa Watendaji wa Wizara ,Kambi Rasmi ya Upinzani inatazamia kuona maboresho ya soko la ndani la madini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi ya kibiashara kwani soko la ndani linawalenga Watanzania walio wengi hususani wachimbaji wadogo.
(c ) Kigogo aliyepewa zawadi ya Almasi
Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya kamati ilibaini kuwa kuna kigogo mmoja aliyepewa zawadi ya almasi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 200 kutoka kampuni ya Williamson Diamond Ltd. Pamoja na hilo kamai haikutaja jina la Kigogo huyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala la kupokea zawadi katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali au la namna yoyote ya kutengeneza mazingira ya kupewa zawadi ni kosa la kimaadili na vilevile ni kosa kama yalivyo makosa ya rushwa tunategema serikali ituambie Kigogo huyo alikuwa ni nani na hatua gani zimechukuliwa dhidi yake mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Rais amekuwa akisema mara nyingi kuwa yeye anachukia mafisadi na wala rushwa tunamtaka katika jambo hili achukue hatua stahiki na kigogo huyo ajulikane kwa umma . Endapo Mawaziri walijiuzulu nafasi zao kwa uzembe katika utendaji kazi ni kwa nini pia viongozi wengine akiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna wa madini, Msajili wa hazina na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa nini hawakuwajibishwa?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzania inaitaka serikali kuchukua hatua za kinidhamu ili kuhakikisha kuwa maadili ya umma yanaheshimiwa, na sekta hii ya madini inapunguza viongozi wasio waadilifu.
Ripoti ya Tanzanite
Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya kamati ilionyesha kuwa kuna hasara kubwa iliyosababishwa na vigogo wa serikali hususani katika mchakato wa upatikanaji wa leseni ya ubia. Leseni namba ML 490/2013 ilitolewa mnamo tarehe 20 Julai, 2013 kwa ubia kati ya STAMICO na TML kukiwa na dosari za utekelezaji wa sheria na dosari ikiwa ni pamoja kosa la kutokubadilisha leseni lililofanywa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambapohakubadilisha leseni namba SML 8/92 ya uchimbaji wa madini kwa kipindi cha miaka miwili na kusababisha leseni hiyo kuendelea kumilikiwa na kampuni ya kigeni TML kinyume na Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Hii iliisababishia serikali kukosa takribani shilingi 37,004,666,631.225 tangu mwaka 2010 sheria ilipopitishwa hadi mwaka 2013 Mkataba wa ubia uliposainiwa kwa kuwa kwa wakati wote leseni ya uchimbaji katika Kitalu hicho ilikuwa inaendeshwa na kampuni ya kigeni.
Mheshiwa Spika, vilevile, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Mb alitoa leseni Na. ML 490/2013 ya Uchimbaji wa Madini kwa Ubia kati ya STAMICO na TML bila kushauriana na Bodi ya Ushauri wa Madini kinyume na Kifungu cha 8(4) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Leseni hiyo ilitolewa ikiwa na mchanganyiko wa madini ya viwandani na madini ya vitoikiwa ni kwa ajili ya utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji, uuzaji na matumizi ya madini ya graphite, marble, tanzanite pamoja na madini mengine yanayohusiana na hayo yaliyopo katika eneo la leseni. Mchanganyiko huo wa makundi ya madini ya vito pamoja na madini ya viwandani ni kinyume na masharti ya kifungu cha 49(2)(a) kikisomwa pamoja na kifungu cha 28(1)(c) na 34(1)(g)(iii) vya Sheria ya Madini vinavyotaka leseni moja itolewe kwa kundi moja la madini.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kuchanganya madini ya vito na madini ya viwandani katika leseni moja, leseni Na. ML 490/2013 imetolewa kwa eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 7.60 kwa namna ambayo pia ni kinyume na kanuni ya 5(1) (f) ya Kanuni za Madini za mwaka 2010. Kanuni hiyo imeweka sharti kwamba leseni za madini ya vito hazitatolewa kwa eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilometa 1 ya mraba.
Mheshimiwa Spika, vilevile, TML ilipewa leseni mpya ya uchimbaji licha ya kwamba kampuni hiyo ilikuwa na madeni ya kodi na mrabaha ya leseni ya awali (SML 8/92). Kwa mujibu wa TRA kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2013 TML ilikuwa inadaiwa kodi ya mapato ambayo ni shilingi 16,446,518,361/= na kodi nyingine kiasi cha shilingi 1,591,458,995/=ambazo jumla yake ni shilingi 18,037,977,356/=. Aidha, kampuni ya TML ilikuwa deni la mrabaha kuanzia mwaka 2004 hadi 2012 ambalo nidola za Kimarekani 1,507,000/=. Kwa utaratibu uliowekwa na TRA kampuni ya TML ilipaswa kulipa madeni haya kabla ya kupewa leseni mpya.
Mheshimiwa Spika, katika sakata ya makinikia viongozi hawa ambao walikuwa ni Mawaziri waliwajibishwa kwa kusimamishwa nafasi zao. Pamoja na uzembe huu mkubwa na wizi wa aina yake bado viongozi hawa wapo uraiani tofauti na watendaji ambao walifikishwa mahakamani. Tutakumbuka Ndugu Ngeleja alirejesha TRA kiasi cha shilingi mil 40.4 zizlizokuwa zimechotwa kwenye akaunti ya Escrow fedha zilizokuwa sehemu ya shilingi bil 306. Kambi Rasmi inataka kujua ni kwa nini Ndugu Ngeleja alirudisha fedha wakati wa sakati hili la makinikia na sio wakati wa EPA ? Je, kitendo cha kurudisha fedha za wizi kimemfutia makosa haya makubwa aliyoyafanya ya kuingizia serikali hasara hiyo kubwa? Je, ni kwa nini viongozi wengine waliburuzwa mahakamani na wengine kesi zao zimeisha kimya kimya
9.0 MADINI NA UKIKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya Tume za Haki za Binadamu (LHRC),Mnamo Mwaka 2017,inasema kuwa hali ya watetezi wa haki za binadamu wanaofanya kazi katika sekta ya uchimbaji wa madini ni mbaya sana katika maeneo ya vijiji wanaozunguka migodi hususani Wilayani Tarime ambako watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakiteswa,kutishiwa,kushtakiwa kinyume cha sheria kwa sababu ya kazi zao za utetezi wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi karibu na migodi wamekuwa wakipata mateso sana kwani kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za kinadamu yakiwemo mauaji na wengine kupata ulemavu, uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji, kuongezeka kwa vumbi ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu na mifugo, na zaidi ya yote serikali imeanza kuweka vigingi ndani ya miji ya watu.
Mheshimiwa Spika, kuanzia Mwaka 2009-2012 jumla ya vifo 35 viliripotiwa kutokea katika mgodi wa North Mara, na kuanzia mwaka 2013 mpaka sasa takribani vifo 74 vimeripotiwa kutokea vingi vikiwa ni vifo vya vijana waliouawa kwa risasi na walinzi wanaolinda mgodi na hivyo kuongeza idadi ya watoto waliochwa yatima. Vilevile, familia nyingi zimekumbwa na wagonjwa wanaopata matatizo ya mfumo wa upumuaji ikiwemo kifuu kikuu (TB) na kansa za ngozi kutokana na vumbi jingi. Mfano katika kijiji cha Mjini kati,Nyangoto, barabara ya Gokona-Nyabirama imejaa vumbi jingi sana .Vilevile, nyumba nyingi zimepasuka kutokana na milipuko inayotoka migodini hususani katika vitongoji vya Kegonga,Masangora,Kwinyinyi n.k Haya ni baadhi ya tu maeneo yaliyoathirika Wilayani Tarime. Aidha, ardhi za mashamba na visima vya maji vimechafuka kutokana na maji ya machafu na ya sumu yanayotoka migodini (telling waste damp Nyabirama pit) yanayoathiri afya za binadamu na mifugo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Simanjiro ambapo kuna mgodi wa madini ya Tanzanite –Mererani kuna umaskini wa kutupwa kwani bado kuna nyumba nyingi za tope na nyasi huku wananchi wakipata huduma duni za afya, elimu na maji.
Mheshimiwa Spika, Katika eneo la Buzwagi na Bunyanhulu hali ni ile ile kwani maeneo hayo kuna kaya nyingi maskini na zisizonufaika na mgodi japo wao ndio wamekuwa walinzi wakuu wa migodi. Tutakumbuka Mwaka 2007, tarehe 31, Julai katika kijiji cha Nyamalembo mkoani Geita, polisi waliwavamia wananchi katika kijiji hicho saa tisa usiku na kuanza kurusha risasi za moto, kuchoma nyumba za wananchi, kuharibu mashamba kwa magreda na kuumiza vibaya wananchi.Pamoja na unyama huo mkubwa serikali iliwasomba wananchi hao na kuwaweka katika jumba moja chakavu lililokuwa jengo la mahakama wakati wa ukoloni ,na wengine wakikosa hata mahema ya kujihifadhi.Mpaka leo wengi wao hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, hali ya umaskini imekuwepo katika maeneo mengi yenye migodi nchini.Hayo ni baadhi tu ya maeneo ambayo wananchi wamekumbwa na maumivu makubwa na umaskini wa kutisha wakati wamezungukwa na rasilimali muhimu na ya thamani kubwa duniani. Yaani ni utajiri mkubwa katikati ya dimwi la umaskini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu wanaofanya kazi katika sekta ya madini wamekuwa wahanga wakubwa wa mashambulizi, vitisho, kukamatwa na mashtaka ya kutengenezewa ya uchochezi. Utafiti wa haki za binadamu katika maeneo ya hifadhi umekuwa na vikwazo vingi ili kufifisha jitihada za wanaharakati kuwasemea wananchi wanaonyanyaswa na baadhi ya watendaji wa serikali.
Mheshimiwa Spika, endapo wapiga kura wa nchi hii wangeijua thamani ya kura zao, pengine maumivu wanayoyapata, yaliyosababishwa na watawala wa nchi hii basi yangeyaepuka. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuheshimu utu wa kila Mtanzania, kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo bila ubaguzi wowote, kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kulinda haki za binadamu na mifugo inayoishi kando kando ya migodi.Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka wadau wote wenye mapenzi mema na nchi hii kuungana katika kupinga mifumo yote inayodhalilisha utu wa binadamu kama ilivyofanyika nchini Zimbabwe ambapo wanaharakati walipaza sauti kwa umoja wao mpaka Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu (Human Right Watch) mwaka 2013 lilipolazimika kuingilia suala la ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe .
Mheshimiwa Spika, bado wachimbaji wadogo wa madini wanapata shida kubwa katika nchi hii. Nchi yetu ina takribani wachimbaji wadogo wapatao 3,000,000. Pamoja na idadi hii kubwa ya wachimbaji ambao hutegemea kupata kipato kupitia uchimbaji mdogo bado wachimbaji hawa wanakabiliwa na matatizo yanayokwamisha juhudi zao za kujikwamua na uamskini.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo hukumbana na tatizo kubwa kujaa maji katika migodi (mashafo au shafts ) huku wengi wakiwa hawana pampu za kutolea maji nje ya migodi wakati uchimbaji ukiwa unaendelea. Jambo hili limesababisha vifo vya wachimbaji wengi ndani ya migodi.
Mheshimiwa Spika, tatizo jingine ni kutokana na miamba migumu ambayo inakwamisha shughuli za uchimbaji. Kutokana na ukosefu wa mashine za kisasa za kupasulia miamba migumu ambazo zinahitaji mashine za za jack hammers na compressors) ambavyo navyo vinahitaji uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wanashindwa kupata faida kutokana na kwamba wengi hulazimika kutumia nguvu kubwa kutokana na uduni wa vitendea kazi. Wachimbaji hawa husomba udongo kwa ndoo ambapo hulazimika kutumia muda mrefu. Hivyo uwepo wa mashine za cranes ambazo hubeba mizigo angalau kuanzia tani ingeweza kupunguza nguvu kubwa na muda mrefu wanaoutumia katika kubeba udongo.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi ya wachimbaji wadogo hakuna sehemu za huduma za dharura na vifaa vya wokozi. Hali hiyo imepelekea wachimbaji wengi kupoteza maisha kutokana na kufukiwa na vifusi au kukosa hewa wakiwa ndani ya migodi. Pamoja na hilowachimbaji wadogo wamekutwa na madhila na wengine kuoigwa risasi na askari wanaolinda migodi mikubwa kutokana na tabia ya kufuata mabaki ya dhahabu maarufu kama magwangara. Hii yote ni kutokana na serikali kutokuweka mfumo mzuri wa uchimbaji na soko la ndani la madini kwa wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuona umuhimu wa kuwekeza kwa wachimbaji wadogi ambao ndio hasa walinzi wa rasilimali madini yanayotuzunguka, kuweka mfumo mzuri wa uchimbaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikani wa vifaa vya huduma ya kwanza katika maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi. Katika ripoti ya Tanzania Chambers of Mining (2018) iliyowasilishwa kwenye kamati ya Bunge ya nishati na madini ilieleza baadhi ya changamoto katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na usalama duni wa leseni za utafiti wa madini (hii ikiwa na maana kwamba bado kuna uvamizi mkubwa katika maeneo ya uchimbaji),urasimu katika kufanya maamuzi ya msingi,mkanganyiko katika uelewa wa jinsi sekta ya madini unavyoendeshwa duniani,mabadiliko ya mara kwa mara ya sera,sheria na kanuni katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya madini.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2017, Bunge lilipitisha Mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika Mwaka 2017 ambayo yameleta changamoto kubwa katika sekta ya madini hususani kwa wawekezaji, wachimbaji na watafiti.Hii ni kutokana na baadhi ya vifungu kutokupata tafsiri (vinaleta mkanganyiko) , baadhi ya vifungu havina afya kwa wawekezaji na haviwezi kuwa na tija kwenye maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 5(3) cha Sheria kinatamka kwamba serikali itakuwa na haki ya umiliki wa madini yote yatakayovunwa. Kifungu hiki kimezua mkanganyiko katika utekelezaji. Hii ni changamoto kubwa hususani kwa wawekezaji kutokana na masharti ya taasis nyingi za fedha hususani pale wanapotafuta mikopo ya kuendeleza uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 9 (1) cha Sheria kimeweka masharti kuwa shughuli zote za uzinduaji, uchimbaji na upatikanaji au utumiaji wa rasilimali utahakikisha kuwa hakuna rasilimali ghafi itakayosafirishwa nje ya Tanzania. Kifungu hiki kimezua mkanganyiko kutokana na kutoeleza wazi ni aina gani ya rasilimali ambazo hazitasafirishwa nje ya nchi zikiwa ghafi (Raw minerals/rough minerals). Baadhi ya rasilimali ambazo zimetajwa katika rasilimali asili haziwezi kuchakatwa na pengine uchakataji wake unaweza kuwa na athari kwa mazingira, afya za watuamiaji na hata kuharibu thamani ya bidhaa husika. Mfano, Madini kama Uranium ambayo yana athari za moja kwa moja za kimazingira na pia ni hatari kwa viumbe hai watakaozunguka jirani na maeneo hayo ya uchimbaji, baadhi ya maliasili ambazo ni viumbe vidogo vidogo (micro-organisms),viumbe wa baharini nk. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza maana halisi ya rasilimali ghafi (raw resources).
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 10 (1) na (2) ni muhimu vifungu hivi vikawa na maelezo ya ziada. Kifungu cha 10 (1) kinapaswa kueleza bayana ni asilimia ngapi ya mapato inapaswa kubaki katika benki zetu au taasisi za fedha. Vilevile, kifungu cha 10 (2) kinalenga kukataza uhamishaji wa mapato yatokanayo na mauzo ya rasilimali na kwa kusema kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria. Pamoja na hiyo Sheria hii inakinzana na baadhi ya vipengele katika Sheria ya fedha (Finance Act 2016) kuhusu utaratibu wa Ring fencing ambayo inaleta changamoto katika sekta ya madini japo inailetea serikali mapato, pia vifungu 56(1) kuhusu ‘Change in Control’. Kifungu hiki kina changamoto kwa kampuni zinazofanya tafiti.
Mheshimiwa Spika, katika maoni ya wadau kupitia Chemba ya Madini , wamebaini kuwa katika kanuni zilizosainiwa hakuna sehemu inayozungumzia namna ya kuendesha maghala ya kuhifadhia madini ghafi. Kanuni hazizungumzii ni nani namna ya uendeshaji wa maghala hayo wala bima endapo jambo lolote litatokea.
Mheshimiwa Spika, katika maoni ya wadau katika sekta ya madini yaliyo katika ripoti ta Tanzania Chamber of Mines , wanahitaji Chemba ya Madini ambayo wanachama wake wanachangia 95% ya makusanyo wa kodi na mrahaba iingizwe katika Kamisheni ya Madini. Pamoja na hilo ni wakati muafaka sasa wa serikali kushiriki katika makongamano mbalimbali ya kimataifa kuhusu madini kama vile Mining Indaba. Hivyo basi Kambi rasmi inaitaka serikali kutoa ufafanuzi katika maeneo yote yanayoleta mkanganyiko katika Sheria.
Mheshimiwa Spika, Dira ya Sekta ya Mifugo kama ilivyokubaliwa na Serikali pamoja na wadau wa Sekta mwezi Aprili 2001 inatamka kuwa; “Kuwe na Sekta ya Mifugo ambayo ifikapo mwaka 2025 kwa sehemu kubwa, itakuwa na ufugaji wa kisasa na endelevu, yenye mifugo bora, yenye uzalishaji mzuri, inayoendeshwa kibiashara na yenye kuboresha lishe ya Mtanzania, kuinua kipato cha mfugaji na Taifa na kuhifadhi mazingira”.
Mheshimiwa Spika, Sera ya mifugo ya mwaka 2006 inasisitiza dira tajwa hapo awali kwamba; “Malengo ya muda mrefu ni kuwa na uhakika wa chakula, kupunguza umaskini, kuchangia katika uchumi wa nchi na hivyo kuongeza mchango wa Sekta ya Mifugo katika pato la Taifa. Ili madhumuni ya Sera hii yafanikiwe, Wizara itaandaa
mikakati na mipango ya utekelezaji wake”.
Mheshimiwa Spika, hali halisi ya ufugaji wetu ambao kwa asilimia kubwa ni ufugali wa kiasili kwani zaidi ya asilimia 90 ya mifugo wetu ni wa asili na wanafugwa kienyeji, Serikali inakwenda kinyume kabisa na mtazamo na malengo ya Dira yake kama ambavyo ilikubaliana na wadau wa sekta. Kitendo cha Serikali kunyanyasa wafugaji kwa njia yoyote iwe ya halali au ya haramu ni hatua kumi nyuma ya kufikia malengo yaliyowekwa na Sera ya mifugo, na jambo hili liko wazi kabisa kwa mujibu wa hali halisi ya mifugo na wafugaji kwa kuporwa mifugo au kuuliwa wafugaji na vyombo vya dola.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina rasilimali kubwa ya maliasili ikiwemo ardhi, malisho na idadi kubwa ya mifugo. Kati ya jumla ya hekta milioni 94 za rasilimali ya ardhi, hekta milioni 60 ni nyanda za malisho zinazofaa kwa ufugaji. Hii ni kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mifugo ya mwaka 2006,lakini kwa ukubwa wa eneo haubadiliki bali kinachobadilika ni matumizi ya eneo hilo, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona itakuwa ni busara kwa Waziri Mwenye dhamana kuwaeleza wafugaji kwa sasa eneo linalofaa na kutumiwa kwa mifugo ni hekta ngapi na ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, takwimu za NBS zilizotolewa katika taarifa ya “Environment Statistics in Tanzania Mainland, 2014“ zinaonesha kuwa eneo linalofaa kwa uchungaji ni hekta 49,979,875 na zinazotumika kwa ajili ya malisho hapa ni hekta 26,142,648 na kati ya eneo hilo linalofaa kwa malisho hekta 13,127,286 hazitumiki kutokana na kuwa na mbung’o (tsetse flies) wengi ambao hawaruhusu ufugaji kuendelea katika eneo hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani inajaribu kuonesha kuwa takwimu za Serikali kuhusiana na nyanda za malisho kuwa zinatofautiana, hivyo ni muda mwafaka sasa kuwa na takwimu sahihi za eneo linalofaa na linalotumika kwa mifugo ili upangaji matumizi yake uwe endelevu.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu- Mpango Kabambe wa Mifugo Tanzania- 2017, inaonesha kuwa, Tanzania ina idadi ya ng’ombe milioni 30.5 na asilimia 97 ya ng’ombe hao ni wale wanaofugwa kiasili, mbuzi milioni 18.8 na kondoo Milioni 5.3. Pia, wapo kuku wa asili milioni 38.2.0, kuku wa kisasa milioni 36.6 na nguruwe milioni 1.9.
Mheshimiwa Spika, Wakati huo huo eneo la malisho linazidi kupungua kutokana na matumizi mengine kama vile uchimbaji wa madini, ardhi ya nyanda za malisho kuwa mapori ya akiba, kilimo cha mashamba makubwa n.k. Aidha, ni ukweli kuwa idadi ya mifugo na idadi ya watu zinaongezeka kwa pamoja na hivyo kupelekea kuwa ndio sababu kubwa kwa mabadiliko makubwa ya matumizi ya ardhi. Hoja kubwa inayotolewa na watafiti ni je, Tanzania itaweza kuhimili mabadiliko hayo ya ongezeko la idadi ya watu na mifugo bila kusababisha madhara kwa kundi lolote kati ya makundi hayo? Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa ni dhahiri Tumeshindwa kwani makundi yote yanalalamika na lingine linaonekana ni laana badala ya kuwa ni bahati kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, wafugaji wengi hapa Tanzania wanatumia mfumo wa ufugaji huria ambao hufanywa na wakulima wachungaji na wachungaji wahamaji, ni mfumo unaotegemea upatikanaji wa malisho na maji kwa msimu na matokeo yake husababisha wafugaji kuhamahama. Na ufugaji huu ndio unazalisha nyama takribani asilimia 95 kwa matumizi ya ndani na asilimia kidogo kwa asili ya kuuza nje, sambamba na uuzwaji wa ng’ombe wazima kwenda nje ya nchi. Ufugaji huu ndio unaotoa ajira.
Mheshimiwa Spika,wafugaji wa asilini jamii ya watanzania waishio kwa kutegemea mifugo yao ya asili katika nyanda za malisho na hujipatia takriban mahitaji yao yote kutokana na mifugo. Mifugo hiyo hutegemea malisho ya nyasi, kufikia malisho ya mifugo yao, maji, kukwepa magonjwa ya mifugo na kuruhusu nyanda hizo za malisho kuzalisha malisho mapya mara nyingine wafugaji hulazimka kuhama kutoka katika uwanda mmoja wa malisho kwenda katika uwanda mwingine. Hivyo basi, uhamaji wa wafugaji una tija kwa sababu wafugaji wa asili hutumia eneo moja la kiekologia kwa misimu tofauti na hatimaye kurudi katika eneo la awali kwa kutegemeana na uwepo wa malisho, chumvi, maji na kutokuwepo na magonjwa ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na mfumo wao wa kiekologia kukumbwa na changamoto na kutokana na wafugaji kuondolewa katika maeneo yao ya asili ya malisho, ulazima huo wao wa kuhama umekua mkubwa mno kwa siku za karibuni. Wafugaji wa asili wamejikuta wakihamia katika maeneo yasiyokuwa ya kwao kiasili na hivyo kukumbana na jamii zingine ambazo sio za kifugaji jambo na hivyo kuzuka kwa migogoro ya matumizi ya ardhi ikihusisha wenyeji wanaowakuta katika maeneo hayo. Hivi sasa wafugaji wa asili wameenea Mikoa ya Arusha, Morogoro, Manyara, Mwanza, Shinyanga, Singida, Mbeya, Tanga, Tabora na Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kwamba ufugaji wa asili unaajiri takriban watu 5,000,000; sawa na 10% ya idadi ya watanzania wote. Pia unachangia 97% ya mifugo yote nchini na kuwapatia 98% ya Watanzania nyama na maziwa. Mifugo ya ufugaji wa asili pia inachangia 30% ya uzalishaji wa sekta ya kilimo na 18% pato ghafi la taifa.
Mheshimiwa Spika, ni katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafugaji wa asili ni vyema kukawepo na ramani katika kila wilaya zetu za kuonesha rasilimali ya nyanda za malisho na iainishe mahali na hali ya maliasili (m.f maji, maeneo ya malisho, hifadhi ya chakula cha mifugo), pamoja na eneo ambalo linahitaji hatua za usimamizi maalumu (m.f hifadhi ya malisho ya msimu). “Tija ya nyanda za malisho katika sehemu zenye matatizo” ni rasilimali muhimu ambayo wafugaji wanahitaji zaidi katika kuendeleza tija ya njia zao za kujipatia riziki kulingana na ufugaji wa mifugo yao.
Mheshimiwa Spika, Katika ramani hizo zikionesha Maeneo haya yenye matatizo kwa maana ya migogoro inayotokea mara kwa mara baina ya makundi ya watumiaji mbalimbali ya ardhi yanaweza kuonyeshwa kwenye ramani.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi binafsi za wafugaji zilishauri kuwa katika kuchora ramani hizo zinazoonesha maeneo ya malisho, pia ramani zinaweza kuonesha maswali yanayolenga kwenye maeneo ya malisho ili wahusika waweze kufahamu mapema kabla ya kupeleka mifugo yao kwenye maeneo husika , kwa mfano, ramani inaweza kujumuisha yafuatayo:
NG’OMBE WALIOUZWA KWA KUINGIA MAENEO YASIYOTAKIWA
Mheshimiwa Spika, Kikosi maalum ambacho kinashughulika na zoezi kuondoa mifungo katika hifadhi za taifa kimefanikiwa kukamata ngíombe 970 kutoka kijiji cha Piyaya Tarafa ya Loliondo ambao wamekuwa wakichungwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara. Aidha, ng’ombe zaidi ya 1,332 waliokuwa wanalishwa kwenye maeneo ya hifadhi mkoani katavi wamekamatwa na kutaifishwa.
Mheshimiwa Spika, Ngo’mbe 119 walikamatwa na mamlaka ya wanyamapori nchini ndani ya pori la akiba Maswa mkoani Simiyu wameuzwa katika mnada wa hadhara kwa amri ya mahakama. Mkoa wa Kagera kwa operation iliyofanyika mwaka jana jumla ya ng’ombe 4328 walikamatwa na kunadiwa katika mnada wa Rusahunga, kwa ng’ombe kuuzw kati ya shilingi 250,000 hadi 300,000.
UPIGAJI CHAPA MIFUGO
Mheshimiwa Spika, uchapaji cha wa mifugo ni utaratibu uliowekwa kupitia sheria ya Bunge ya “utambuzi,usajili na ufuatiliaji mifugo wa mwaka 2010 (the livestock identification, registration and traceability Act, 2010)”.
Mheshimiwa Spika, Suala la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo unakwenda sambamba na tasnia ya nyama na maziwa ambayo hivi sasa imekuwa na masharti mengi sana ili kuweza kupata soko la uhakika toka nchi zilizoendelea. Katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji chama mifugo ni lazima pia busara zitumike kuliko nguvu kama vile operation hamisha wafugaji ilivyofanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa dhana nzima ya sheria tajwa hapo awali ni kwamba sheria hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuipatia soko la uhakika bodhaa zitokanazo za mifugo yetu na sio kuwabana wafugaji kufanya shughuli zao katika nchi yao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa angalizo hapo awali kuhusu haina tatizo na dhana inayobebwa na Sheria hiyo. Hata hivyo sasa hivi inaonesha kuwa sheria hiyo inakuwa msingi wa kero kubwa sana kwa wafugaji kutokana na kutokuangalia uhalisia wa hali ya ufugaji katika nchi yetu kwa utambuzi,usajili na ufuatiliaji mifugo badala ya kuwa ni wa kinasaba zaidi unakuwa ni kuhusiana na mfugaji anatokea eneo gani la nchi na kuzuiwa kufanyia shughuli zake katika wilaya nyingine, na kama akiruhusiwa na wilaya husika ni lazima alipishwe fedha kwa kichwa mfugo.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba zoezi hili limeliingizia Taifa fedha nyingi kwa kulinganisha na fedha za Maendeleo zilizokuwa zimetengwa na Serikali katika katika wa fedha 2017/18. Randama uk 6 inatuonesha kuwa zoezi la kupiga liekamilika Machi 2018 na jumla ya ng;ombe 17,390,000 wamepigwa chapa, na bei ya kupiga chapa kwa kila ng’ombe ni tsh. 500/- na hivyo kufanya makusanyo kuwa Tshs 8,695,000,000/- au Tsh. Bilioni 8.7 wakati fedha za maendeleo zilizopitishwa na Bunge ni Tshs bilioni 4 tu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani katika kupitia Randama Jedwali na.3 uk 18 inaonesha kuwa fedha hizo za Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/18 zilizoidhinishwa na Bunge shilingi bilioni 4, hadi kufikia mwezi Machi 2018 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa. Hapa ni kweli sekta ambayo asilimia 50 ya kaya huitegemea katika kuendesha shughuli zake za kiuchumi, sekta ambayo inategemewa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025 inapewa umuhimu kweli? Aidha, Mpango Kabambe wa mifugo (Livestock Master Plan) gharama za utekelezaji wake ni jumla ya shilingi trilioni 1.3, kwa uwekezaji huo wa Serikali wa shilingi sifuri kwa mwaka tutafikia malengo?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Randama inaonesha kuwa mchango wa sekta ya mifugo (Nyama, ngozi, maziwa, mbolea, kwato na mayai) katika pato la taifa unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi trilioni 18 kwa mwaka. Kambi Rasmi ya Upinzani inaomba waheshimiwa Viongozi mfanye ulinganisho baina ya sekta hii na sekta ya usafiri wa anga na kuona ni wapi kunaweza kuleta tija zaidi na kututoa hapa tulipo kwa haraka kama uwekezaji uliofanyiwa utafiti wa kina utafanyika.
UPUNGUFU WA RASLIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya Mifugo na Uvuvi hali ya upungufu wa rasilimali watu ni vivyo hivyo kama kwenye kilimo.Hapa watumishi wenye taaluma ya kuanzia shahada na kuendelea wanaohitajika ni 1,936 waliopo ni 867 sawa na 44.8%. Ngazi ya cheti na Diploma wanaohitajika ni 15,000 waliopo ni 3,904 sawa na 26%. Kwa ujumla sekta inahitaji watumishi wataalam 16,936 lakini waliopo ni 4,771 sawa na 28.1%
Mheshimiwa Spika, maendeleo ya sekta ynatokana kwa kiasi kikubwa na Raslimali watu iliyopo katika sekta hiyo. Kwa kuangalia takwimu hizo hapo juu kama zilizovyotafitiwa na ANSAF ni dhahiri kuwa bado tuna kazi kubwa ya kuifanya sekta hii ya mifuko na uvuvi kuwa endelevu ambayo kila mshirika/mdau itamletea tija sambamba na kwa Serikali kupata kile inachostahili.
SEKTA YA MAZIWA
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya maziwa ni kitovu kikubwa cha uchumi hasa kwa wafugaji wadogo hapa nchini, kutokana na idadi ya mifugo iliyopo ya takriban milioni 28.4. Ni dhahiri kuwa kama uwekezaji wa kutosha hasa katika ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji wetu popote pale walipo, sekta zingine kama vile afya na elimu zitakuwa na maendeleo chanya.
Mheshimiwa Spika, Randama uk.9 unaonesha kuwa Tanzania ina viwanda vya maziwa 81 vyenye uwezo wa kusindika maziwa lita milioni 276.55 kwa mwaka, lakini kwa sasa vinasindika lita milioni 56.25 kwa mwaka sawa na asilimia 20.33 tu. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hii ni kutokana na kutokuwepo na maziwa toka kwa hao ng’ombe milioni 28.4 au kutokana na kutokufahamu ng’ombe walipo ili kukusanya maziwa?
Mheshimiwa Spika, ukiangalia randama uk.27 inaonesha kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2017, Bodi ya Maziwa ilitoa vibali 417 vya kuingiza maziwa ndani ya nchi vyenye thamani ya shilingi bilioni 22.81.
Mheshimiwa Spika, hoja ya msingi ya kuuliza ni kwanini wafanyabiashara wanaamua kuagiza maziwa wakati viwanda vyetu vinazalisha chini ya uwezo wake? Wadau wanatoa jibu rahisi kabisa kuwa ukiritimba wa kimamlaka baina ya asasi zinazohusika (TBS, TFDA, SIDO, BRELA,OSHA, TRA, N.K) na masuala ya uthibiti ni tatizo na hivyo kupelekea wahusika kuona ni nafuu kuagiza bidhaa hiyo toka nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kunakuwepo na mazingira wezeshi kwa wawekezaji/wajasiriamali wadogo kuingia na kufanya kazi katika sekta ndogo hii ya maziwa, kinyume cha hapo tutategemea mitaji mikubwa toka nje wakati hapa ndani kuna mitaji na fursa lakini tunawakatisha tamaa.
UZALISHAJI WA NYAMA
Mheshimiwa Spika, takwimu za Serikali zinaonesha kuwa Tanzania tuna viwanda/machinjio vya nyama 25 na vinauwezo wa kuzalisha tani 626,992 za nyama kwa mwaka, lakini uzalishaji kwa sasa ni tani 81,220 kwa mwaka na hivyo kufanya kuwa vinazalisha chini ya uwezo wake kwa asilimia 87.05 (Operating under capacity for 87.05%)
Mheshimiwa Spika, aidha takwimu zinaonesha kuwa tani 2,165.95 za nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na Punda iliuzwa nje ya nchi, wakati huo huo jumla ya tani 1,224.55 za nyama ziliagizwa toka nje ya nchi, ikiwa tani 506.05 nyama ya nguruwe, tani 711.03 nyama ya ng’ombe n Tni 7.47 nyama ya kondoo.
Mheshimiwa Spika, Uagizaji huo umeongezeka kwa asilimia 37.5 mwaka 2017/18 kwa kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2016/17 cha uagizaji wa tani 890.66; hiyo kutokana na kuongezeka kwa soko maalum. Kambi Rsmi ya Upinzani inauliza, hili soko maalum ambalo linaongezeka na sisi idadi ya mifugo inaongezeka tunakabiliana nalo vipi?
MWENENDO WA BAJETI KWA FUNGU 99-IDARA KUU YA MIFUGO
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2015/16, Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi 60,373,984,500/- kwa wizara ya mifugo na uvuvi (wakati huo ikiwa ndani ya wizara ya kilimo) zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya hizo shilingi 19,398,607,500/- zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, lakini hadi kufikia 31March, 2016 wizara ilikuwa haijapokea hata shilingi 1 kati ya shilingi bilioni19.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 99 ilitengewa na bunge jumla ya shilingi 60,013,252,440.56/- na kati ya fedha hizo shilingi 15,873,215,000/- (fedha hizi zimejumuisha Mifugo & Uvuvi) zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Upatikanaji na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2016/17, sekta hii ya mifugo ilitengewa shilingi 4,000,000,000/- tu (kwa ajili ya huduma ya mifugo, na uzalishaji wa mifugo), kati ya fedha hizi ni shilingi 130,000,000/- tu ndizo zilizotelewa kwa ajili ya shughuli za uzalishaji wa mifugo, sawa na asilimia 3.25 ya fedha zote za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka huo.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi 29,963,524,000.00 kati ya fedha hizo shilingi 25,963,524,000.00 zilikuwa ni kwa matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo zilikuwa ni shilingi 4,000,000,000.00 na katika fedha hizo za maendeleo hadi mwezi machi, 2018 hakuna hata shilingi moja ambayo ilikuwa imepokelewa kutoka hazina.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 wizara kupitia fungu 99 inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 35,362,663,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida shilingi 30,362,663,000.00 na matumizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo wametenga shilingi 5,000,000,000.00 fedha ambazo ni ongezeko la shilingi bilioni 1 kwa kulinganisha na fedha za maendeleo zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2017/18.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia trend ya uwekezaji wa Serikali kwenye sekta ya mifugo ni dhahiri kwamba, sekta hii japokuwa inahudumia takribani asilimia 50 ya kaya zetu lakini inapewa umuhimu mdogo sana. Hivyo basi ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Serikali kufanya utafiti wa kina katika kufanya uwekezaji wake.
Mheshimiwa Spika, ni bora kuanza kuangalia vigezo vingi na Serikali kuanza kufikiria kama Serikali badala ya kufikiria kama vile uhai wake katika kutumikia wananchi ni wa miaka 5 au 10 tu, na kusahau kuwa serikali itaendelea kuwepo miaka yote ijayo. Hivyo uwekezaji unatakiwa uangalie mustakabali wa wananchi hata ambao hawajazaliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sera ya mifugo ya mwaka 2006, kwamba; “Changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa mifugo na mazao yake vitakavyokidhi mahitaji ya soko la kikanda na kimataifa. Kwa hiyo, tasnia hii itashiriki kikamilifu katika biashara ya kimataifa kwa kuongeza uuzaji wa mazao nje ya nchi na kukabili ushindani wa bidhaa zinazoingizwa nchini ambapo ulinzi pekee uliopo kwa viwanda vya ndani ni kuweka viwango muafaka vya ushuru na ubora unaotakiwa. Marekebisho ya kisera ya kuifanya biashara ya mifugo iendane na mfumo wa kisasa wa biashara ya kimataifa yamekamilika na Tanzania a mabadiliko zaidi katika mifumo ya biashara hiyo”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza tunatokaje katika changamoto hizo wakati ambapo Serikali haiwekezi katika tasnia hii?
Mheshimiwa Spika, majigambo ya Serikali hii ya awamu ya tano kwamba; inajenga uchumi wa viwanda na kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati kufikia 2025 ni kejeli na hadaa kwa wananchi wa Tanzania. Hii ni kwa sababu kuna mserereko hasi wa utoaji na utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika wizara hii hasa katika miaka miwili mwanzo wa utawala wa Serikali ya awamu ya tano.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwisho ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne katika mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara hii ilitengewa shilingi 111,958,354,000 kati ya hizo shilingi 33,356,643,000 zilikuwa ni matumizi ya kawaida na shilingi 78,601,711,000 zilikuwa ni matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili, 2015 Wizara ilikuwa imeshapokea shilingi 93,185,222,288 sawa na 82% ya fedha zilizotengwa ambapo shilingi 27,905,758,188 ni za matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 65,279,464,100 ni za matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo ni kwamba; hadi kufikia Aprili, 2015 bajeti ya maendeleo katika wizara hii ilikuwa imetekelezwa kwa asilimia 83. Hii ilikuwa ni hatua kubwa sana ya utekelezaji wa bajeti ya viwanda licha ya ukweli kwamba suala la viwanda lilikuwa halipigiwi upatu na wala halikuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya nne.
Mheshimiwa Spika, mara tu baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii umeyumba sana licha ya mbwembwe na mikogo mingi kwamba ni Serikali inayojenga uchumi wa viwanda. Kwa mfano; katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji ilitengewa jumla ya shilingi 87,470,349,000 kati ya fedha hizo shilingi 52,082,968,000 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 35,387,381,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha ni kuwa hadi kufikia mwezi Machi, 2016, kati ya Shilingi 35,387,381,000 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Shilingi 1,602,111,662 ndizo zilikuwa zimepokelewa na Wizara kutoka hazina, kiasi hiki ni sawa na asilimia 5 tu ya fedha zote za maendeleo zilizokuwa zimepitishwa na Bunge. Aidha, fedha hizi zilikuwa ni za nje tu. Hakukuwa na hata senti moja ya fedha za ndani zilizotolewa kutekeleza bajeti ya maendeleo licha ya Bunge kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 26.588[43] ya fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wizara hii.
Mheshimiwa Spika, ni vema kumbukumbu zikawekwa vizuri kwamba Serikali ya awamu ya tano inayojinasibu kuwa ni ya viwanda; katika mwaka wake wa kwanza wa utawala; ilianza utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kutoa asilimia tano tu (5%) ya fedha zilizokuwa zimetengwa kutekeleza miradi ya maendeleo; na katika fedha hizo hakukuwa na hata senti moja ya fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilidhani kwamba utekelezaji huu dhaifu wa bajeti ya maendeleo katika wizara hii pengine ulitokana na ukosefu wa uzoefu wa kazi ukizingatia kwamba ulikuwa ndio mwaka wa kwanza wa Serikali ya awamu ya tano kuanza kazi.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo; udhaifu huu unaonekana kuendelea hata katika mwaka wa tatu wa utawala wa Serikali hii. Kwa mfano; katika mwaka wa fedha 2017/18 Wizara ilikuwa imetengewa jumla ya shilingi 122,215,109,750; kati ya hizo shilingi73,840,377,000 zilikuwa ni fedha za maendeleo. Lakini hadi mwezi Machi 2018; wizara ilikuwa imepokea fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 7,000,000,000 tu sawa na asilimia 9.47 ya fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa mwenendo huo dhaifu wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni uwiano wa Kauli Mbiu ya “Tanzania ya Viwanda“ na utekelezaji halisi wa shughuli zitakazopelekea Tanzania ya Viwanda. Kwa maneno mengine; Serikali hii ya awamu ya tano imeamua kuwahadaa watanzania kwamba inajenga uchumi wa Viwanda lakini kiuhalisia haitoi fedha za kutosha kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali suala la utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii; Serikali ilijiwekea lengo la kukuza sekta ya uzalishaji (manufacturing)ili kuweza kuchangia asilimia 40 ya pato la taifa kufikia 2025 kama njia mojawapo ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati kiviwanda.
Mheshimiwa Spika, imesaliatakribani miaka 8 kabla ya mwaka 2025, sekta ya viwanda vya uzalishaji (manufacturing) inachangia asilimia 5.2[44] tu ya pato la Taifa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza kuwa ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda ni lazima kila mwaka wa fedha ukiwemo mwaka wa fedha unaomaliza muda wake 2017/2018, sekta ya uzalishaji (manufucturing) inapaswa kukua kwa asilimia 4.35 kila mwaka wa fedha mpaka ifikapo mwaka 2025 ili kufikia lengo la kuifanya ‘manufacturing’ ichangie asilimia 40 ya pato la Taifa na hatimaye Tanzania kuwa ya uchumi wa kati kiviwanda!
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita sekta ambazo zimefanya vibaya kwa kuwa na ukuaji mdogo ni pamoja na sekta ya uzalishaji. Kwa hali hii maana yake ni kuwa azma ambayo iliwekwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano haiwezi kufikiwa kama ukuaji katika sekta ya uzalishaji ni mdogo.
Mheshimiwa Spika, licha ya ukwelli kwamba sekta ya viwanda vidogovidogo ndio chimbuko na chemchemi ya mapinduzi makubwa ya viwanda; sekta hii imekuwa haipewi kipaumbele na serikali jambo ambalo limesababisha sekta hii kuporomoka vibaya na kufifisha ndoto za kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya Ukaguzi wa Kiufanisi (Performance Audit) kuhusu huduma wezeshi kwa viwanda vidogovidgo nchini ya mwaka 2018; ni kwamba; sekta ya viwanda vidogovidogo ni dhaifu na imeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Taarifa hiyo inaonyesha kwamba sekta hiyo haikui kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa sasa sekta ya viwanda vidogovidogo inakuwa kwa asilimia 5.6 wakati kiwango cha kuporomoka ni asilimia 8. Uchangiaji wa sekta hii katika ajira kwa sasa uko katika asilimia 40 tofauti na kiwango kilichopangwa cha asilimia 60. Uchangiaji wa jumla wa sekta hii katika pato la taifa unakadiriwa kuwa asilimia 35 tofauti na kiwango kilichokusudiwa cha asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya CAG inaonyesha pia kwamba; kumekuwa na utekelezaji mdogo sana wa bajeti za maendeleo kwa viwanda vidogovidogo katika ngazi zote za Serikali. Kwa mfano; kwa miaka minne ya nyuma, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imetumia asilimia 16 tu ya fedha za maendeleo zilizopokelewa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogovidogo na vya kati. Hata hivyo, CAG anasema kwamba; bajeti ya maendeleo imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka kunzia mwaka 2013/14. Kwa upande mwingine, Shirika la kuhudumia viwanda vidogo na vya kati (SIDO) ambalo hutumia wastani wa shilingi bilioni 14 kwa mwaka, limekuwa likitenga wastani wa asilimia 30 tu ya fedha zake kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati. CAG anaendelea kusema kwamba; kati ya ofisi tano za SIDO za Mikoa zilizotembelewa ambazo ndio watekelezaji wakuu wa huduma kwa viwanda vidogo na vya kati, zilikuwa zimepokea asilimia 20 tu ya fedha zilizoombwa kwa ajili ya shuguli za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utekelezaji wa huduma ya mafunzo katika sekta ya viwanda vidogo na vya kati; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alingundua kwamba hakuna huduma za mafunzo za kuridhisha. Kwa sasa; huduma za mafunzo ya nje kwa watendaji wa viwanda vidogo na vya kati yanayoratibiwa na SIDO ni asilimia 7 tu ya viwanda hivyo vilivyosajiliwa SIDO. Kwa nchi nzima, huduma ya mafunzo iliyotolewa ni asilimia 0.4 tu. Hata hivyo, mafunzo yaliyotolewa hayakusaidia ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati. Taarifa ya CAG inaonyesha kwamba licha ya mafunzo hayo kutolewa bado asilimia 24 ya viwanda vidogo na vya kati vilivyosajiliwa na SIDO vilishindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, teknolojia sahihi nayo ni hitaji la msingi katika maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati. Taarifa ya CAG inaonyesha kwamba hakuna maendeleo ya teknolojia katika sekta ya viwanda vidogo na vya kati. Kwa sasa vituo vya maendeleo ya teknolojia bado vinatumia mashine zilizofungwa zaidi ya miaka 40 iliyopita, kwa ajili ya uzalishaji wa mashine zinazohitajika na viwanda vidogo na vya kati kwa soko la sasa. Kwa maoni ya CAG, mashine hizo zilizopitwa na wakati haziwezi kuzalisha mashine zenye teknolojia ya kisasa inavyoweza kushindana na teknolojia mpya zinazoingizwa nchini.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali suala la uhitaji wa teknolojia ya kisasa kama chagizo la ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vya kati; hitaji la mikopo ya fedha kwa viwanda vidogo nalo ni la msingi katika ukuaji wa viwanda hivyo. Ukaguzi wa kiufanisi uliofanywa na CAG ulibaini kwamba SIDO haikuwa na huduma ya kutosha ya mikopo kwa viwanda vidogo na vya kati. Taarifa ya ukaguzi huo inaonyesha kwamba; kwa miaka minne ya nyuma; huduma za mikopo ziliongezeka kwa asilimia 9 tu ikiwa ni sawa na ukuaji/ongezeko la asilimia 2 tu kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, wakati uwezo wa SIDO wa kutoa mikopo kwa viwanda vidogo unakuwa kwa kasi ndogo; hitaji la mikopo kwa viwanda hivyo linazidi kuongezeka na hivyo kuifanya SIDO kushindwa kutoa huduma hiyo ipasavyo. Ripoti ya CAG inaonyesha kwamba; kwa miaka minne iliyopita; SIDO haikuweza kutoa hata asilimia 40 ya mikopo iliyokuwa inahitajika licha ya kuipitisha mikopo hiyo, kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha za mikopo.
Mheshimiwa Spika, tatizo jingine linaloikumba sekta ya viwanda vidogo na vya kati ni kukosekana kwa mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathmini. Shughuli za utoaji wa huduma kwa viwanda vidogo hazijapangwa kikamilifu; hazitekelezwi kikamilifu na wala haziratibiwi kikamilifu na wala hazifanyiwi tathmini na Wizara na SIDO ili kukuza sekta ya viwanda vidogo nchini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukaguzi wa kiufanisi wa CAG; ni kwamba; ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo hauridhishi kukidhi vigezo vya kuifanya sekta hiyo kuweza kuchangia katika uchumi wa nchi ambao utaiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kiviwanda kufikia 2025. Na hii ni kwa sababu kasi ya kuporomoka kwa sekta hii ni kubwa kuliko kasi ya ukuaji. Kwa mfano; taarifa ya CAG inaonyesha kwamba katika miaka minne iliyopita wastani wa kasi ya kuporomoka kwa sekta hii ulikuwa ni asilimia 30 wakati kasi ya ukuaji ilikuwa ni asilimia 5.6.
Mheshimiwa Spika, kwa kifupi, sekta ya viwanda vidogo na vya kati ndio moyo wa maendeleo ya viwanda hata katika nchi zilizoe delea. Kudorora kwa sekta hii, kama CAG alivyoonesha katika ukaguzi wake hakutoi taswira njema ya kufikia malengo ya uchumi wa viwanda ifikapo 2025. Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa Serikali kuacha kufanya propaganda za kisiasa kwamba nchi inaendelea vizuri katika ujenzi wa viwanda, wakati sekta ya viwanda vidogo ni dhaifu kiasi hiki.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imekua ikijinasibu mara kwa mara kuwa inajenga uchumi wa viwanda na imekua ikitoa takwimu mbalimbali zikionesha idada ya viwanda vinavyoanzishwa nchini kwa lengo la kutoa taswira kwamba; nchi inaendelea vizuri kiviwanda.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali mpango wa serikali wa miaka mitano ambao umezungumzia kidogo uchumi wa viwanda, Waziri wa Viwanda na Biashara hajawahi kuwasilisha kwenye Bunge lako tukufu mpango wa ujenzi wa viwanda na namna uzalishaji na masoko ya bidhaa utakavyofanyika. Aidha yapo maelekezo yaliyotolewa kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa kila Mkoa unajenga viwanda mia moja kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, haijaelezwa ni viwanda vya namna gani vinaenda kujengwa na kwa tafiti zipi za masoko ya bidhaa zitakazozaliwa na viwanda husika. Taarifa ya jarida la The Economist Intelligence Unitya tarehe 17 Januari, 2018 inaonesha kuwa; pamoja na serikali kueleza kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano kuwa itajikita kwenye uchumi wa viwanda na kutengeneza ajira ongezeko la kodi na kubadilika kwa ghafla kwa mifumo ya usimamizi wa biashara inayofanywa na serikali yameathiri ukuaji wa biashara nchini[45].
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto wanazopitia wafanyabiashara za kodi na maelekezo ya kiutawala na mifumo ya usimamizi wa biashara nchini taarifa za kiuwekezaji zinaonyesha kuwa uwekezaji nchini utapungua kwa kiasi kikubwa pamoja na uwepo wa mipango ya serikali.
Mheshimiwa Spika, katika hali kama hii ni wazi kuwa serikali kuendelea kujinasibu na uchumi wa viwanda ni kauli za majukwaani pekee kuliko hali halisi ya mazingira ya biashara nchini. Ni wazi kuwa huwezi kujenga uchumi wa viwanda bila kuwa na uhakika wa soko, na kama huna uhakika wa soko na hakuna uwekezaji wenye tija unaofanyika ni wazi pia kuwa serikali haiwezi kukusanya kodi.
Mheshimiwa Spika, aidha zipo takwimu tofauti tofauti ambazo zimetolewa kuhusu idadi ya viwanda vilivyojengwa nchini. Rais anapohutubia wananchi kwenye shughuli zake za uzinduzi wa miradi mbalimbali amekuwa akitoa takwimu za idadi ya viwanda vilivyojengwa na vinavyotegemewa kujengwa. Aidha, wakati mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/2019; Kambi Rasmi ya Upinzani ilihoji juu ya utofauti ya takwimu za idadi ya viwanda vinavyojengwa nchini kama ilivyoainishwa kwenye Mpango na idadi ambayo Rais anawatangazia wananchi.
Mheshimiwa Spika, Katika Mapendekezo ya Mpango wa Serikali yaliyowasilishwa na Serikali katika Mkutano wa tisa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji juu ya kauli ya Rais aliyoitoa tarehe 14 Oktoba, 2017 wakati anazima Mwenge, kuwa Mwenge ulizindua Viwanda 148 kwa mwaka uliopita ambavyo vilizalisha ajira 13,370.
Mheshimiwa Spika, katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango takwimu zilionyesha kuwa kulikuwa na viwanda 50 ambapo kati ya hivyo 32 vilianza uzalishaji na 18 vilikuwa vinaendelea kujengwa. Katika hali ya kushangaza miezi mitano baadae Waziri wa Fedha na Mipango wakati akiwasilishwa maelezo yake kuhusu mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19 alisema kuwa kuna viwanda vipya 3,306 kote nchini takwimu ambazo alizirudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa katika ziara Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Spika, Katika taarifa ya Wizara iliyowasilishwa katika Bunge lako tukufu kupitia randama ya Wizara ya Viwanda na Biashara Waziri wa sekta hii hajawasilishwa idadi hiyo ya Viwanda iliyotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango ambayo ilikuja kuungwa mkono na Rais ambayo pia ni tofauti na kilichozungumzwa wakati wa mjadala wa mapendekezo ya mpango wa serikali.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Viwanda na Biashara katika randama ya Wizara kazungumzia zaidi idadi ya Viwanda vidogo na vya kati ambapo pamoja na takwimu na maelezo yake kutokuwa na mantiki jumla yake ni Viwanda 689 ambavyo anasema vimezalisha ajira 1,287[46].
Mheshimiwa Spika, Kama serikali ni moja na Rais ni mmoja, mbona kunakuwa na tofauti ya idadi ya viwanda? Takwimu tofauti zinazotolewa na serikali kwa umma na propaganda za idadi ya Viwanda mnamfurahisha nani? Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kutoa taarifa Bungeni ya aina viwanda na uwezo wake wa uzalishaji pamoja na takwimu sahihi kwa sababu tukiendelea kudanganyana hivi, kama Taifa hatuendi popote
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Shirika la Fedha Duniani ya Januari 2018 kuhusu mapitio ya saba ya Mwongozo wa Sera ya Tanzania[47] imeeleza pamoja na mambo mengine pamoja na pato la taifa kuonekana kukua mazingira ya biashara nchini sio rafiki kwa uwekezaji maendeleo ya biashara.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo ya sasa inaonekana dhahiri kuwa shughuli za kiuchumi ni dhaifu na hivyo kupelekea kushindwa kuzalisha ajira na kupunguza umasikini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kueleza kuwa pamoja na taarifa ya biashara nyingi kufungwa ambayo tulieleza kwa kirefu mwaka uliopita, Waziri wa Fedha alijibu kwa idadi ya biashara mpya zilizofunguliwa na kueleza kwa propaganda kuwa biashara zilizofungwa zilikuwa zinahusishwa na ukwepaji kodi.
Mheshimiwa Spika, kufungwa kwa biashara nchini sio jambo la kushangilia kwa sababu ni dhahiri kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wanalipa kodi, na hivyo kuongezeka kwa makusanyo. IMF wanaeleza kuwa makusanyo ya kodi yameshuka tofauti na jinsi ilivyokuwa inategemewa na hivyo kupelekea utekelezaji wa bajeti ya serikali kuwa dhaifu.
Mheshimiwa Spika, aidha kumekuwa na ongezeko kubwa la mikopo isiyolipika katika mabenki jambo ambalo linaathiri pia mazingira ya ufanyaji biashara kwa sababu kutokana na madhaifu yaliyopo katika mfumo wa sasa kodi na maelekezo ya kiutawala yasioangalia maslahi ya wafanyabiashara, wafanyabiashara wameshindwa kulipa mikopo kwenye mabenki ya ndani.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaeleza kuwa hadi kufikia mwezi Septemba mwaka 2017 mikopo isiyolipika katika mabenki ya biashara iliongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi 12.5. Hali hii ilipelekea mabenki nchini kupata hasara kubwa jambo ambalo halijawahi kuwepo toka mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hatua za Benki Kuu kupunguza kima cha chini cha fedha zinazohitajika kuhifadhiwa na Benki za Biashara nchini ikiwa ni pamoja na kushusha kiwango cha riba bado sekta hiyo ilifanya vibaya na hivyo kuathiri mazingira ya biashara katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, mauzo ya bidhaa kwenda nje ya nchi (export) yalionekana kushuka na pia makusanyo ya ushuru wa bidhaa nayo yalishuka kutokana na wananchi kupunguza matumizi ya bidhaa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuangalia kwa umakini hali ya uchumi wa nchi kuliko kuendelea kutoa kauli za kuwashawishi wananchi kuwa hali ni nzuri wakati katika takwimu hali inaonekana tofauti.
Mheshimiwa Spika, serikali haiwezi kukusanya kodi ya kutosha kama mazingira biashara na sera za kodi ziko hovyo. Aidha serikali haitapiga hatua kama maamuzi ya namna ya kuboresha biashara yanafanywa na serikali kuu bila hata kuzingatia uhalisia wa mazingira ya biashara. Ikumbukwe kuwa serikali imejinasibu kupunguza matumizi ya kawaida kwa ajili ya kubana matumizi, jambo hili ni jema hasa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Spika, kupunguza matumizi kwa sekta muhimu ambazo wafanya biashara walikuwa wanaingia mikataba ya kibiashara pamoja na zabuni za serikali usitegemee kukua kwa biashara nchini kwa sababu serikali ndiyo inayohitaji huduma na kupata huduma na bidhaa ni lazima ishirikishe sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, yapo pia malalamiko ya wazabuni ambao walikuwa na madeni na serikali kwa sababu ya huduma au bidhaa ambazo walihudumia katika taasisi mbalimbali za serikali ambao hawajalipwa na serikali inasema bado inahakiki madeni hayo kama ni halisi. Wahanga wa uhakiki huu ni wafanya biashara ambapo pamoja na kushindwa kuendelea kufanya biashara kwa sababu ya madeni, hata madeni hayo yakilipwa bado hayalipwi kulingana na bei ya soko au kuangalia na thamani ya shilingi yetu ambao bado inasuasua.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inalitaka Bunge kupitia Kamati zake za kisekta zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara nchini kuangalia hali hii ambayo si njema katika mustakabali wa Taifa letu na kuchukua hatua za dharura kuisimamia serikali ili kuepuka anguko la uchumi ambalo linakuja mbeleni.
Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya uwekezaji kwenye reli ya standard gauge (SGR), Mradi wa umeme wa Stiegler’sGorge, bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga na mradi wa Bandari ya Bagamoyo ambao kwa sasa hauzungumziwi sana lakini hakuna mkakati wa wazi wa namna miradi hiyo inagharamiwa.
Mheshimiwa Spika, mara kadhaa Rais John Magufuli anasikika akisema kuwa miradi hiyo inagharamiwa na fedha za ndani za walipa kodi, na wakati mwingine Waziri wa Fedha ananukuliwa akisema kuwa miradi hiyo inagharamiwa na fedha za mikopo mbalimbali. Hata hivyo kutokuwa wazi kuhusu gharama za miradi mikubwa na muda wa kuimaliza kunazua sintofahamu kuhusu uwezekano wa kumaliza miradi hiyo mikubwa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kuwa kama serikali haitashirikisha sekta binafsi kupitia ubia (PPP) wachambuzi wa uchumi wameshauri kuwa deni la taifa litaendelea kukua na kuwa mzigo kwa walipa kodi. Aidha ikumbukwe kuwa serikali imekua ikikopa sana ndani na hivyo kutengeneza ushindani na wawekezaji wa ndani ambao pia wanatumia mikopo kuendeleza biashara zao.
Mheshimiwa Spika, Ushirikishwaji wa sekta binafsi sio utachochea tu mazingira ya biashara na mzunguko wa fedha nchini bali pia itaipunguzia serikali mzigo wa kuwekeza kwenye kila mradi mkubwa jambo ambalo linasababisha ugumu katika kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje na kuepuka serikali kukopa sana ndani kugharamia miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa miaka mitano unazungumzia na kuonyesha ahadi ya serikali kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya ukuaji wa sekta binafsi nchini. Kinachotokea kwa sasa ni serikali kutaka kumkamua Ng’ombe maziwa ambaye hajampeleka kwenye malisho yenye majani ambayo yatamfanya Ng’ombe huyo kuzalisha maziwa ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, Hivi ndivyo serikali inavyofanya kwa wafanyabishara nchini, ambapo serikali inawahimiza kulipa kodi ya maendeleo (jambo ambalo ni jema) lakini haijaweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa biashara hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu urahisi wa kufanya biashara duniani, Tanzania imekuwa nchi ya 137 kati ya nchi 190 duniani na moja ya changamoto zilizotajwa ni pamoja masuala ya kodi ambazo sio rafiki, kufanya biashara kwenye mipaka na ugumu katika uanzishaji wa biashara.
Mheshimiwa Spika, kila wakati serikali hii inapokosolewa Kiongozi Mkuu wa nchi amenukuliwa akisema kuwa wanaotoa ukosoaji huo wanatumwa na mabeberu jambo ambalo linaonyesha kuwa bado tunao viongozi ambao wanafikiria kijamaa kuliko kufikiri katika Nyanja za utandawaza, soko huria na kukua kwa sekta binafsi. Ni lazima serikali ijue kuwa haiwezi kuirudisha nchi kwenye Ujamaa kama walivyozungumza lugha za kijamaa wakati kama Taifa tulishatoka kwenye zama hizo.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya kuanzisha biashara nchini ni magumu, Waziri anaweza kuja na takwimu nzuri za namna Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni alivyosajili biashara kadhaa kwa mwaka huu wa fedha lakini ukweli ni kuwa mazingira ya kuanzisha biashara nchini ni magumu. Mathalani kuanzisha biashara ya kawaida unaweza ukatakiwa kupitia kwenye mamlaka na wakala zaidi ya tano na sehemu zote hizo kuna gharama ambazo lazima uzilipe kama mfanyabiashara kupata vibali au leseni.
Mheshimiwa Spika, hata utendaji wa Mamlaka ya Mapato (TRA) sio rafiki kwa wafanyabiashara. Hii ni kutokana na maafisa kuambatana na vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa ukusanyaji au ufuatiliaji wa kodi jambo ambalo linatia wafanyabiashara hofu na kuamua kufunga biashara zao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutofumbia macho mapungufu haya yaliyopo ya mazingira ya kufanya biashara. Ni vema kama wanahitaji makusanyo mazuri ya kodi watatue changamoto zinazowakumba wafanyabiashara kuliko kujikita zaidi kwenye ukusanyaji wa kodi bila kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kufanya biashara nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa sio kazi rahisi kuanzisha kiwanda kama ambavyo serikali hii imekuwa ikipiga kelele hapa Bungeni na kwenye vyombo vya habari. Hasa ukizingatia kuwa kuanzisha viwanda vikubwa ambavyo huzalisha mathalani kama magari, viwanda hivyo vipya hasa vya “fabrication industries” ni ghali si tu katika kuvianzisha bali hata kuviendesha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na gharama kubwa za kuanzisha na kuviendesha muda wa bidhaa zitakazozalishwa ili kuingia kwenye soko na kukubalika katika jamii ya watumiaji huwa mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, serikali makini duniani kwa sasa huwa jambo la muhimu kwao ni kuanzisha viwanda vya uunganishaji (assembly plants), kama wenzetu wa Kenya walivyofanya au kama inavyofanyika kwa matrekta ya ASUS yanayounganishiwa hapa Tanzania lakini kiwanda mama kipo nchi za nje.
Mheshimiwa Spika, kwa njia hii ni dhahiri tutakuwa tumeepuka gharama kubwa ya matumizi ya nishati umeme, gharama kubwa ya kutangaza bidhaa husika na hivyo bidhaa husika zitakuwa shindani katika soko la ndani na nje. Nchi nyingi za Mashariki ya Kati hutumia teknolojia ya kuunganisha bidhaa kama mbadala wa kuanzisha viwanda vipya kuepuka changamoto ambazo tumeeleza.
Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa zipo pia changamoto za kimazingira ambazo kama nchi tutakumbana nazo katika kile ambacho serikali hii inakiita “uchumi wa viwanda”. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa serikali hii inacheza ngoma ambayo haijafanyiwa utafiti wa kutosha kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika, kuna dalili ya ufisadi katika mradi wa kufufua kiwanda cha matairi cha General Tyre. Hii ni kwa sababu Bunge limekuwa likiidhinisha fedha za kufufua kiwanda hicho lakini ki-uhalisia hakuna kinachofanyika. Awali Bunge lilihoji juu ya kuchelewa kutekelezwa kwa mradi huo jambo lililopelekea kuongezeka kwa gharama za ufufuaji wa kiwanda hicho kutoka shilingi bilioni 45 mwaka wa fedha 2015/2016 mpaka shilingi bilioni 60 mwaka wa fedha 2016/2017. Fedha hiyo ilihitajika kwa ajili kukamilisha ukarabati wa awamu ya tatu na kufanya majaribio ya uzalishaji kabla ya kuanza uzalishaji kamili.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2016/17 ni kwamba Serikali ilitenga fedha kwa ajili tathimini katika mwaka wa fedha 2016/2017, wakati tathmini hiyo ilkwishafanywa na kukamilika katika mwaka wa fedha 2015/2016 kwa gharama ya shilingi bilioni 45. Aidha, kwa mujibu wa Randama ya Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji fungu 44 uk. 131; Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuandaa taarifa ya kina ya upembuzi yakinifu ambayo inaweza kuvutia taasisi za fedha; kuratibu ununuzi wa mitambo na mashine za kiwanda; kutangaza eneo kwa ajili ya kupata wawekezaji na kulipa tozo ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kupata majibu kwa Serikali Ni kwa nini Serikali inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda hiki lakini hakifanyi kazi mpaka sasa? Aidha, ni kwa nini fedha zinazotengwa mara zote ni kufanya upembuzi yakinifu na uratibu lakini hakuna fedha kubwa inayotolewa kwa ili kuhakikisha kuwa kiwanda kinafanya kazi?
Mheshimiwa Spika, kutokana na kusua sua kwa Serikali kufufua kiwanda hiki; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali afanye ukaguzi maalum kuhusu matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Kiwanda hiki na kushauri hatua za kuchukua.
Mheshimiwa Spika; katika mwaka wa fedha 2014/15 Bunge liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuendeleza miradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma; na shilingi bilioni 3. kutekeleza Mradi wa Chuma cha Liganga.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa za Serikali zinaonesha kuwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lilishakamilisha tathmini ya kufahamu wingi na ubora wa makaa ya mawe pamoja na chuma cha Linganga, na kubaini kuwa tuna makaa ya mawe kiasi cha tani milioni 428 na chuma tani milioni 126; na kwa kuwa tathmini ya mazingira ilishafanyika na Serikali kueleza kuwa ujenzi wa miradi hiyo ulitarajiwa kuanza mwaka 2016 na uzalishaji kuanza mnamo mwaka 2019/2020; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni kwanini Serikali isitumie chuma cha Liganga katika kujenga reli ya Standard Gauge badala vyuma vya Uturuki ilhali tuna chuma cha kutosha kwa matumizi ya ndani na hata akiba ya kuuza nje?
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Serikali katika kutekeleza miradi ya Tanzania Mini Tiger Plan katika mwaka wa fedha 2014/15 bunge lilipitisha kiasi cha shilingi bilioni 7.0 kwa ajili ya kulipia fidia eneo la Bagamoyo Special Economic Zone . Hadi kufikia mwezi Februari 2015 kiasi cha shilingi 6.75 bilioni tayari kilikuwa kimelipwa kwa walengwa katika eneo la Bagamoyo SEZ. Hata hivyo, pamoja na kufanyika malipo hayo, bado shilingi 44.25 bilioni hazijalipwa kutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba kuendelea kuchelewa kulipa fidia hizo kuna athari kubwa kiuchumi. Kwanza; muda unavyozidi kwenda ndio thamani ya ardhi inazidi kupanda. Hivyo, kuchelewa zaidi maana yake ni kuongeza kiwango cha fidia kitakacholipwa. Aidha, kuendelea kuchelewa ni kurudisha nyuma kasi ya utekelezaji wa miradi husika ambapo hata gharama ya utekelezaji itapanda
Mheshimiwa Spika, halikadhalika katika mradi wa Tanzania-China Logistics Centre – Kurasini, fidia imekuwa ikilipwa lakini hakuna kinachofanyika. Hadi kufikia mwezi Septemba, 2014 Wizara kupitia EPZA ilikuwa imelipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 53 kwa watu 538. Aidha, kiasi cha fedha kinachodaiwa kumalizia kulipa fidia na malalamiko mbalimbali ya mapunjo yaliyotokana na makosa ya kiuthamini ni shilingi bilioni 3.75.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa, fedha iliyotolewa na Wizara hadi kufikia Machi 2016 ni shilingi 3,048,904,930 tu ambazo zilikuwa zimetolewa na serikali kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa pale Kurasini Tanzania –China Logistic Center na kufanya jumla ya uwekezaji wa shilingi bilioni 56.
Mheshimiwa Spika, ukirejea taarifa ya kamati ya viwanda na Biashara kwa mwaka huo ni kwamba fidia katika maeneo yote yaliyofanyiwa tathmini yaliyopo chini ya EPZ na SEZ kufikia Mwaka wa Fedha 2015/2016; gharama ilifikia Shilingi Bilioni 60.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu za sasa fidia inayotakiwa kulipwa kutokana na kuchelewa kulipwa imeongezeka hadi kufikia shilingi Bilioni 190.9. Fidia hii ni kwa maeneo ambayo tayari yalikwisha fanyiwa uthamini ambayo ni Bagamoyo SEZ hekta 5473, Ruvuma (2033), Tanga(1363), Mara (1360), Kigoma(691), Manyara (530.87), Manyoni-Singida (755). Maeneo ambayo bado hayajafanyiwa tathmini ni hekta 21634.
Mheshimiwa Spika, Tukumbuke kwamba eneo hilo lote waliokuwa wamiliki hadi sasa wamezuiwa kuliendeleza na bado wanateseka na Serikali haifahamu ni lini fidia itatolewa. Huu ni unyanyasaji mwingine wa Serikali dhidi ya Raia wake; lakini pia ni kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya viwanda na biashara.
MWENENDO WA SEKTA YA UTALII NCHINI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na sintofahamu juu ya takwimu zinazotolewa juu ya idadi ya watalii wanaoingia nchini . Sintofahamu hii inatokana na idadi ya watalii ambayo imekuwa ikiripotiwa kwenye hotuba mbalimbali ikiwemo randama ya Wizara fungu 69. Katika Randama inazoonyesha kuwa kwa mwaka 2016 watalii walioingia nchini walikuwa 1,284,279 na kwa mwaka 2017 walikuwa ni takribani watalii 1,327,143. Ripoti hizi zimebainisha kuwa wataliii hao waliokuja kutembelea hifadhi za taifa, mamlaka za hifadhi za Ngorongoro na Zanzibar. Hii ina maana kwamba watalii walioingia kutoa Zanzibar nao wamejumuishwa katika idadi ya Watalii wote walioingia nchini kwa mujibu wa maelezo ya Randama.
Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa masuala ya sekta ya utalii sio masuala ya Muungano. Hivyo kujumuisha idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar kama sehemu ya Muungano kwa mujibu wa Randama ndiko kunakozua mtanziko. Serikali ituambie ni lini hasa imeamua mambo ya utalii kuwa sehemu ya Muungano kama ambavyo serikali imekuwa ikijinasibu na idadi ya watalii inayojumuisha Tanzania Bara na Tanzania visiwani? Jambo hili liliwahi kuhojiwa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na serikali haikutoa majibu.Hivyo basi ni muhimu serikali ikaweka wazi dhamira yake ya kujumuisha Idadi ya watalii ikiwemo ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo taarifa mbalimbali ikiwemo ripoti ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na TANAPA zinaonyesha kwa mwaka 2013/2014 idadi ya wageni waliopokelewa na TANAPA walikuwa 957,702 ikilinganishwa na mwaka 2015/2016 ambapo idadi ilikuwa 957,576, na katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Ilipokea wageni 619,876 kwa mwaka 2014/2015 ikilinganishwa na idadi ya wageni 588,264 kwa mwaka 2016/2017. Hii ikiwa ni pungufu ya takribani wageni 31,612. Ni muhimu serikali ikaeleza ni nini hasa kimesababisha anguko hili? Serikali inapata wapi uhalali wa kusema sekta ya utalii inakuwa huku idadi ya watalii ikionekana kupungua?
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo bado takwimu zinaonyesha Watalii wengi zaidi hukimbilia nchini Kenya kutokana na huduma nzuri na unafuu wa gharama ikilinganishwa na Tanzania. Kwa Mwaka 2016, pekee jumla ya watalii waliotembeea nchini Kenya ni 1,342,899 ikilinganishwa na Mwaka 2017 ambapo idadi ya watalii waliongezeka hadi kufikia 1,474,671[48]. Pamoja na changamoto walizozipata nchi jirani ya Kenya kutokana na shambulio la Bomu mjini Garisa Mwaka 2015 bado nchi hiyo imekuwa na mikakati madhubuti ya kuwavutia wageni na wawekezaji katika sekta hii ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo ya VAT, kuboresha huduma za mahoteli na usafiri hususani usafiri katika nchi ya Marekani na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ambapo nchi hiyo imekuwa mdau mkubwa wa sekta ya utalii Africa ya Mashariki.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa za kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii ambayo imetolea mfano wa nchi kama Botswana ambayo imekuwa na tozo la VAT katika huduma za kitalii kwa sasa wameongeza VAT kutoka 14% kwenda 15% kama mfano wa nchi Barani Afrika zenye mfumo wa VAT , ni vyema serikali hii ikatambua kuwa pamoja na tozo ya VAT kwenye utalii nchini Botswana bado kiwango hicho haijafikia ukubwa wa tozo kama tozo 18% kama ilivyo kwa Tanzania kwa sasa. Pamoja na hilo Botswana itambulike kuwa nchi ya Botswana . Vilevile, ikumbukwe kuwa nchi ya Botswana imepunguza mrundikano wa kodi tofauti na Tanzania yenye takribani kodi 36 kwenye sekta ya utalii pekee. Ukiwa ndio nchi inayoongoza kwa wingi wa kodi katika biashara ya utalii Afrika ya Mashariki.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mazingira mazuri ya kibiashara na faida zake, sekta hii ya utalii inaweza kukua tu pale ambapo nchi inakuwa katika hali ya amani na utulivu. Amani na utulivu huja tu pale ambapo mamlaka zinazingatia haki za kiraia, demokrasia na siasa safi. Katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka 2016/2017 ilitolea mfano wa nchi ya Srilanka. Katika gazeti la New York Times, nchi kama Srilankailiwahi kupata hadhi ya kujulikana kama nchi ya kwanza duniani kwa kivutio cha watalii. Lakini kukandamizwa kwa demokrasia na misukosuko ya kisiasa nchini Srilanka kama inavyotokea Tanzania leo ilipelekea utalii wa nchi hiyo kushuka kwa kasi ya asilimia 43 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuanguka kabisa kwa uchumi wa nchi hiyo.Hivyo, kuanza kusuasa kwa sekta hii ya utalii ni dalili mbaya na isipoangaliwa inaweza kutupeleka katika kile kilichotokea Srilanka.
Mheshimiwa spika, sekta ya Uwindaji ni sekta muhimu katika Utalii. Kuanzia Mwaka 2009-2016 sekta hii ilichangia takribani dola za kimarekani milioni 163,465,077.01 sawa na takribani shilingi bilioni 3.5 za Kitanzania ndani ya sekta. Katika Mwenendo wa biashara ya Uwindaji, inaonekana kuporomoka kuanzia mwaka 2014/15 mpaka mwaka 2017 ambapo makadirio yanaonyesha kuendelea kuporomoka zaidi. Mwaka 2010/11 mapato yalifikia dola 26,399,634 ikilinganishwa na mwaka 2015/16 ambapo mapato yalifikia kiasi 17,406,860 na mwaka 2016/2017 kiasi cha shilingi 18,787,976 tu[49].Hii ikiwa na maana kwamba miaka ya nyuma sekta hii ilifanya vizuri tofauti na ilivyo sasa. Kambi Rasmi inataka kujua ni nini hasa kinasababisha kushuka kwa mapato katika sekta hii tofauti na miaka ya nyuma?
Mheshimiwa Spika, vilevile kutoka mwaka 2013 mpaka kufikia mwaka 2017 jumla ya kampuni 52 zilirudisha vitalu serikalini, vitalu 11 havikupata wawekezaji kabisa na zaidi ya yote mpaka mwishoni mwa mwezi Machi 2018 kampuni nyingine 18 zimerudisha vitalu na hivyo kufikia jumla ya kampuni 71 ambazo zimerudisha vitalu serikali kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuyumbishwa kwa sera, sheria, kuongezeka kwa kodi, ada na tozo mbalimbali, kuporomoka kwa soko la Tanzania na matamko ya kisiasa yanayotishia wawekezaji wa ndani na nje.
Mheshimiwa Spika, Jumla ya kampuni 16 zimefunga biashara ya uwindaji kabisa mpaka sasa ambapo kati ya hizo kampuni 3 ni za kigeni na kampuni 13 ni za Wazawa. Baadhi ya kampuni zimehamishia biashara nchini Afrika ya Kusini ambapo biashara ya Uwindaji inafanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa wastani nchi yetu imekuwa ikipata takribani dola za kimarekani milioni 20,433,134.6 kutokana na shughuli za uwindaji ambazo zinalipwa kama mapato ya serikali[50]. Kutokana na serikali kushindwa kudhibiti biashara ya uwindaji haramu na ujangili, biashara ya uwindaji inaonekana kutafsiriwa tofauti miongoni mwa wananchi walio wengi. Serikali imeshindwa kutoa ajira za kutosha kwa walinzi wa wanyamapori, kushindwa kulinda mazalia ya wanyamapori, kushindwa kufanya tafiti za mara kwa mara juu ya ongezeko na upungufu wa baadhi ya wanyama na viumbe hai, wananchi kutoshirikishwa kikamilifu katika kulinda wanyama wetu na badala yake wananchi wanaoishi kandokando ya hifadhi wamechukuliwa kama maadui wa wanyama. Hii yote ni kutokana na kutokuwapa elimu na mafunzo ya ulinzi shirikishi katika suala zima ya kulinda rasilimali hii (participatory approach), vilevile serikali imeshindwa kuja na mbinu mbadala wa kuhakikisha aina (species) muhimu zinalindwa na kuzalishwa kwa wingi kwa njia za kisayansi, kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 sekta ya utalii ilichangia 17.5% ya pato la taifa (GDP) na takribani25% ya fedha za kigeni (foreign currency). Hii ikiwa ni kati ya sekta tano muhimu zinazichangia zaidi katika pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, takwimu za serikali zinaonyesha sekta hii ya utalii hutoa ajira za mojamoja zipatazo 500,000 na zisizo za moja kwa moja 1,000,000 .[51]Pamoja na hilo, sekta hii ya utalii imekuwa ikichangia kaitka kukuza kipato cha wananchi mmoja mmoja kutokana na manunuzi ya bidhaa katika hoteli zikiwemo vyakula, huduma za samani, vifaa vya ujenzi, malazi n.k
Mheshimiwa Spika, sekta hii ni sekta muhimu kwa kuwa inafungamanisha uchumi wa sekta nyingine. Katika nchi mbalimbali duniani mfano Brazil, Mauritius , Nicaragua na hata hapa kwetu Tanzania katika visiwa vya Zanzibar utalii wa fukwe umekuwa ni kitovu cha kukuza uchumi wao. Vilevile utalii wa Malikale kama vile majumba ya kihistoria , na sanaa za kale, pamoja na utalii wa tamaduni umekuwa muhimu sana katika sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuona umuhimu huu wa sekta ya utalii na mifano ya nchi mbalimbali wanavyonufaika katika utalii wa aina tofauti tofauti bado hapa nchini kwenye sekta hii imekuwa ikisuasua na kutegemea wahisani katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa miradi mingi ya maendeleo katika sekta inategemea wahisani kutoka nchi zilizoendelea na taasisi mbalimbali za kimataifa hususani World Bank, Belgium, German, Norway, Finland, n.k Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali ione umuhimu wa kuwekeza katika sekta hii nyeti ambayo inauwezo wa kutoa ajira zaidi, kuongeza GDP na fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika,mnamo mwaka 2013 serikali ilitangaza kuhuisha vibali vya uwindaji kwa makampuni ya uwindaji ambayo yalifanya vizuri katika kuchangia uchumi wa nchi yetu kupitia biashara ya uwindaji nchini. Tukumbuke kuwa biashara ya uwindaji ndio biashara inayoingizia serikali fedha nyingi zaidi ya kigeni kwenye sekta ya utalii (foreign currency). Kutokana na makampuni hayo kulipa kodi vizuri serikali ilihuisha tena leseni zao kwa kipindi cha miaka mitano yaani kutoka Mwaka 2013 mpaka Decemba Mwaka 2018 kwa kupitia barua ya Waziri iliyokuwa na kumbukumbu Na.CHA.79/519/01/117.
Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 16 Januari 2017, serikali ili tangaza tena mchakato wa kuhuisha ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa muhula wa mwaka 2018-2022. Tangazo hilo lilitoka kwenye barua ya Waziri yenye kumbukumbu namba CHA.79/519/01/138 ambayo ilitoa leseni katika vitalu vya Lake Natron GCA (W),Lukwati Game reserve (South) na Longido Game reserve Controlled Area.
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwaka huo huo wa 2017, Mwezi Desemba, serikali kupitia Waziri wa Malisili na utalii aliandika barua yenye kumbukumbu namba CHA.79/519/01iliyoelekeza juu ya ugawaji mpya wa vitalu (granting allocation of hunting blocks kwa mujibu sheria ya Wanyamapori (Wildlife Conservation Act . Na 5 ya Mwaka 2009) kifungu cha 38 (6) (11) ambapo zoezi hilo lilikuwa limekwisha fanyika tangu Mwezi Januari mwaka huo wa 2017. Jambo la kushangaza ni kuwa barua hiyo ilikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa Wizara imeamua kubadili mfumo wa ugawaji wa vitalu kutoka mfumo uliokuwa umezoeleka kwenda kwenye mfumo wa mpya wa minada ( from admistrative allocation to auctioning). Kwa mujibu wa barua hiyo, serikali ilitoa tangazo la kufuta vibali kwa makampuni yote ya uwindaji na hivyo Wizara ikatoa muda wa miaka miwili kwa makampuni hayo kujiandaa na mfumo huo mpya yaani mpaka tarehe 31,Desemba 2019 ambapo mfumo huo wa minada ungeanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, jambo hili la kushangaza la kufuta vibali kinyume na sheria ya Wanyama ya pori ya Mwaka 2009 ambayo inaeleza wazi taratibu na makosa ambayo yanaweza kusababisha kampuni kufutiwa vibali ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza masharti ya leseni,endapo kampuni imepatiakana na hatia au kushindwa kulipa ada na tozo mbalimbali na sio kufuta vibali kwa ghafla pasipo kufuata sheria na taratibu.
Mheshimiwa Spika, Waziri anatambua wazi kuwa vibali vyote vilivyotolewa mwaka 2018 vinaisha muda wake mwaka 2022. Pamoja na hilo, biashara ya Uwindaji ni biashara ya muda mrefu. Wageni hulipia vibali vyao na safari ya kuja kuwinda nchini miaka 3 mpaka 5 kabla ya safari hiyo ya kuja nchini. Kukatisha vibali kwa sababu zisizo za msingi au za kidharura ni kuonyesha kuwa bado serikali ya CCM haina nia ya dhati ya kutanua wigo wa kibiashara ili kuikomboa nchi yetu kwenye umaskini. Serikali kupitia Wizara hii imekuwa ikikiuka utaratibu mara kadhaa jambo ambalo linaathiri mazingira ya kibishara na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wawekezaji wa ndani na wale wa kigeni.
Mheshimiwa Spika,tuna mifano mingi ndani ya serikali hii ya CCM ambapo nchi inapata hasara kubwa kutokana na maamuzi ya baadhi ya viongozi ya kutokufuata taratibu. Tunakumbuka sakata la meli ya Wachina iliyokamatwa na Samaki maarufu kama ‘samaki wa Magufuli’ ambapo serikali inapaswa kulipa fidia ya meli aina ya Tawariq 1 yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2.3 na samaki waliokutwa kwenye meli hiyo wakiwa na thamani ya shilingi bilioni mbili.[52]Huu ni mfano mdogo tu kati ya mingine mingi ambayo imeigharimu serikali hususani wananchi maskini ambao ndio hubeba mzigo mzima wa kulipia madeni ambayo yamesababishwa kutokana na uzembe na ubabe wa watendaji ndani ya serikali ya CCM.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea tabia ya serikali kuendelea kukandamiza sekta binafsi kwa kufanya maamuzi ya kukurupuka bila kuwasikiliza au kushauriana na wadau wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi na ushirikiano wa kibiashara. Kambi Rasmi ya Upinzania inaitaka serikali itambue mchango mkubwa wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na makusanyo ya kodi yanayotokana na sekta binafsi. Vilevile,Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kukaa upya nawamiliki wa vitalu pamoja na wadau wengine wanaojihusisha na biashara ya utalii na uwindaji ili kufikia maamuzi ya pamoja kwa kuangalia namna bora ya kufanya kazi na kutatua changamoto kubwa na masononeko miongoni mwa wawekezaji katia sekta hii , ili kulinda sifa ya Tanzania iliyojijengea miaka ya nyuma katika soko la Kimataifa la Utalii.
Mheshimiwa Spika, biashara ya uwindaji ni biashara inayohitaji nidhamu kubwa na uaminifu ili kulinda soko ndani na nje ya nchi. Ni biashara inayojumuisha wafanyabiashara wakubwa wenye fedha nyingi duniani ambao huwinda sio kwa sababu ya kitoweo bali kwa sababu ya mashindano mbalimbali ya kidunia ya kuwania tuzo mbalimbali yaani Hunters trophy.
Mheshimiwa Spika, nchi nyingi zilizobarikiwa kuwa na wanyamapori duniani hufanya biashara ya uwindaji kimkakati kwani ndio biashara inayoweza kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni . Mfano nchi kama Africa Kusini kwa mwaka 2015 pekee iliweza kukusanya kiasi cha dola bilioni mbili kutokana na biashara ya uwindaji pekee ($ 2 bil). Hii ni sawa na fedha za kitanzania takribani trillion 4.545[53] fedha ambazo zinazoweza kutosheleza takribani Wizara ya kilimo, afya na maji.
Mheshimiwa Spika, biashara ya uwindaji huhusisha uwindaji wa baadhi ya wanyama dume ambapo baadhi ya sehemu za wanyama kama vile kichwa, ngozi,pembe na kwato hutumika katika mashindano. Mara nyingi nyama hutolewa kama kitoweo katika jamii (local community). Hapa nchini biashara hii haijapewa kipaumbele kabisa kama biashara ambayo ingeweza kukutoa kimasomaso katika umaskini huu wa kutisha.
Mheshimiwa Spika, biiashara ya uwindaji imekuwa na changamoto nyingi sana zinazowakatisha tamaa wawekezaji. Ni biashara inayoelemewa na wingi wa kodi. Mfano, katika sekta hii ndogo ya Uwindaji kuna takribani tozo 21 za kodi kubwa kuachilia mbali zile za biashara ya utalii. Kodi zenyewe ni kama zifuatazo:
MGAO WA LESENI,ADA, KODI NA TOZO SEKTA YA UWINDAJI NCHINI
Aina ya Kodi | Kiwango (USD) | Kiwango (TZS) | Muda |
Tala A | 5,000 | 11,000,000 | Kwa mwaka |
Tala B | 1,000 | 2,200,000 | Mwindaji Mtaalamu (Professional Hunter-PH)kwa Mwaka |
Leseni ya Biashara | 3,000 | 6,600,000 | Kwa mwaka |
Leseni ya PH | 3,000 | 6,600,000 | Kwa Mwaka |
Kibali cha kazi | 1,000 | 2,200,000 | Kwa Mwaka |
Kibali cha Ukazi A | 2,050 | 4,510,000 | Kwa kichwa kwa mwaka |
Kibali cha Ukazi B | 3,050 | 6,710,000 | Kwa kichwa kwa Mwaka |
Leseni ya Kuwinda | 4,600 | 10,120,000 | Kwa leseni ya mteja kwa kichwa |
Category 1 | 60,000 | 132,000,000 | Kwa mwaka |
Category 11 | 30,000 | 66,000,000 | Kwa Mwaka |
Category 111 | 18,000 | 39,000,000 | Kwa Mwaka |
Category 1V | 10,000 | 22,000,000 | Kwa Mwaka |
Category V | 5,000 | 11,000,000 | Kwa Mwaka |
Observer Tax | 100 | 220,000 | Kwa siku |
Hunter Conservation Tax | 150 | 330,000 | Kwa siku |
Riffle Import permits | 120 | 264,000 | Per firearm on application |
Trophy handling fee | 500 | 1,100,000 | On application |
Mchango wa kijamii | 5,000 | 11,000,000 | Kwa kitalu kwa mwaka (Ni lazima) |
Maombi ya kitalu ya mara nyingine (renewal) | 5,000 | 11,000,000 | Kwa kitalu (Non-refundable) |
Ada ya kuhamisha kitalu | 50,000 | 110,000,000 | Kwa kitalu |
Maombi ya kuhamisha kitalu | 5,000 | 11,000,000 | Kwa kitalu |
Mheshimiwa Spika, hizi ni baadhi tu ya tozo katika sekta ndogo ya Uwindaji nchini. Katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 iliainisha takribani kodi 36 katika sekta ya utalii pekee ukiachilia mbali sekta hii ndogo ya Uwindaji. Mfumo mzima wa kodi katika sekta ya uwindaji na utalii nchini una kasoro nyingi za kiutendaji kwani ili mwekezaji au mfanyabiashara apate leseni ya biashara ni lazima awe amelipia leseni ya TALA na masharti hayohayo yanahitaji ili kupata leseni ya TALA lazima uwe na leseni ya biashara. Huu ni mkanganyiko usiovumilika katika biashara na unaleta usumbufu mkubwa sana kwa wawekezaji.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa takribani 40% ya wafanyabiashara ya uwindaji wamerudisha vitalu vyao serikalini kutokana na kushindwa kutimiza masharti magumu ambayo ni mwiba wa kuua kwa makusudi sekta ya utalii au pengine kuacha mwanya kwa watu wachache waweze kumudu biashara hiyo kwa manufaa yao wenyewe huku wengine wakifunga biashara.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa na wawekezaji wamekuwa wakipata changamoto hizi bado wamekuwa wakijitoa sana katika shughuli za kijamii ikiwemo masuala ya kuzuia biashara ya ujangili na kulinda makazi ya wanyama.Ambapo kwa mwaka 2013-2015 takribani dola milioni 9.8 zilichangwa japo hata mchanganuo wa matumizi yake haukuonekana[54]
Mheshimiwa Spika, ifike mahali sasa serikali ya CCM ijitathimini na itathimini adhma yake ya kulikomboa taifa hili kiuchumi. Sekta ya utalii ni sekta isiyohitaji uwekezaji mkubwa ukilinganisha na sekta nyingine mfano sekta ya viwanda au madini.Lakini ni sekta inayoweza kutukomboa endapo serikali itawekeza kimkakati. Kwa mujibu wa ripoti ya Uchumi ya Dunia -The World Economic Forum Report ya mwaka 2015, Nchi kama Afrika Kusini, Ushelisheli (Sychelles),Kenya ,Botwana ziliongoza katika kuvutia wawekezaji katika sekta ya utalii huku Tanzania ikishika nafasi ya 93 duniani huku ikiwa ndio nchi yenye vivutio vingi na vyenye upekee zaidi duniani.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeyazungumza haya mara nyingi ikiwemo kuangalia upya mchanganuo wa kodi ndani ya sekta mabadiliko ya ghafla ya kisera na athari zake, pamoja na ubadhirifu wa fedha kama ilivyoelezwa kwenye matumizi ya fedha za kupambana na ujangili yaangaliwe upya. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Bunge lako liunde kamati teule ichunguze matatizo yanayohusu sekta ndogo ya uwindaji hususani suala la utoaji wa vitalu na kodi ambayo yamekuwa sugu na yenye kuwaumiza wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje katika sekta ndogo ya uwindaji nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni ya tozo za Maendeleo ya Utalii, kifungu cha 4(2) ya Mwaka 2013 inamtaka Mkurugenzi wa utalii kupeleka mapato ya maswala ya malazi ya watalii kwa kila Mwaka wa Fedha husika katika Mamlaka ya Mapato nchini yaani TRA.
Mheshimiwa Spika, fedha hizo huwekwa katika akaunti ya tozo za Maendeleo ya Utalii. Jambo la kushangaza ni kuwa kiasi cha shilingi 8,248,083,588 (Bil 8.248) zilizokuwa zimekusanywa kama makusanyo ya kila mwezi ya TRA hazikuhamishwa kwenda kwenye akaunti ya Tozo ya Maendeleo ya Utalii kama kama kanuni ya 4(2) ya Tozo za Maendeleo ya utalii inavyosema.
Mheshimiwa Spika, kuna takribani shilingi bilioni 6,357,529,854 ambazo hazikutolewa katika kipindi cha Mwaka 2015/2016 kutoka TRA kwenda kwenye tozo za Maendleeo ya Utalii. Kutokupeleka fedha katika akaunti ya Tozo ya Maendeleo ya utalii inaathari za moja kwa moja katika utendaji kazi ndani ya Wizara. Mpaka sasa Wizara hii imekuwa ikitegemea zaidi wahisani na hivyo kuendelea kukwamisha jitihada za Wizara .Kutokuhamisha fedha kwa wakati maana yake ni kuifanya wizara kushindwa kutekeleza majukumu yake lakini pia ndiko hasa kunaporuhusu matumizi mabaya ya fedha kuanza kujipenyeza.
Mheshimiwa Spika, Mpaka sasa kuna miradi ndani ya Wizara imeshindwa kutekelezeka ikiwemo mradi wa Theme Park (Utalii Dar es Salaam) kutokana na kukosekana kwa fedha. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini hasa fedha hizi hazikupelekwa Wizarani?Na kwa vile hazikupelekwa basi serikali ituambie fedha hizo ziko wapi na zinafanya nini?
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 serikali ilitenga kiasi cha shilingi 250,000,000 (mil 250) kwa ajili ya upembuzi yakinifu ili kufanya Mji wa Dar es salaam kuwa Mji wa kitalii. Serikali ilikuwa na dhamira ya kujenga hoteli za kitalii, viwanja vya michezo, maeneo ya kupumzikia na bustani za wanyamapori katikati ya Jiji.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 iliishauri serikali kutenga eneo la Msitu wa Pande kuwa sehemu ya Bustani ya Wanyamapori ili kupunguza gharama za kujenga eneo jingine litakaloweza kushabihiana na mazingira ya kuishi wanyama ikiwa ni pamoja na eneo la mazalia ya wanyamapori ndani ya Jiji la Dar es Slaam.
Mheshimiwa Spika, kutokutolewa kwa fedha hii iliyotengwa kunaonyesha wazi kuwa bado serikali inaweka mipango ambayo haina uwezo wa kuitekeleza. Hii yote inaonyesha serikali imeshindwa kufanya usimamizina ufatiliaji wa mipango yake inayojiwekea. Endapo mpango wa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa sehemu ya muhimu kwa utalii ungetekelezwa ungeweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana, kuchochea uchumi ikiwemo kufunguliwa kwa biashara nyingi zaidi zenye kutoa huduma kwa watalii, kuongezeka kwa mzunguko wa fedha za kigeni na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kama miundombinu mfano usafiri wa anga na barabara, uvuvi, sanaa, sekta ya nyumba na hata viwanda.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha zilizotengwa, badala ya mfumo wa sasa unaotumiwa na baadhi ya wanasiasa wa kufanya matumizi ambayo hayajatengwa wala kuidhinishwa na Bunge jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Bajeti. Pamoja na hilo Kambi Rasmi inataka kujua uwepo wa taarifa ya mabasi yaliyonunuliwa kwa ajili ya kutoa huduma za kutembeza watalii katika vivutio mbalimbali Jijini Dar es Salaam ? Je, mabasi hayo yaliyonunuliwa ni sehemu ya mradi huu? Je,gharama yake ni shilingi ngapi? Na Je, mabasi hayo ni mangapi?, Je ni vivutio vipi tayari vimeshabainishwa ndani ya Jiji ?
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo sugu la migogoro baina ya serikali na wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi za wanyapori kwa muda mrefu sasa. Pamoja na jitihada mbalimbali za kuizungumzia na kushauri hatua stahiki za kuitatua bado hali inaonyesha migogoro hii imekuwa na nguvu kubwa kuliko uwezo wa serikali kuitatua.
Mheshimiwa Spika, migogoro hii imedumu muda mrefu ambapo imegharimu maisha ya wananchi wengi, tumepoteza wanyama ambao ndio fahari yetu na chanzo cha mapato, migogoro hii imesababisha kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na wanyamapori, mifugo na hivyo kuathiri afya za binadamu na wanyama wa kufugwa na wale wa porini. Mfano, kwa mujibu wa taarifa ya kamati takribani viboko 158 walikufa ndani ya Mwezi Agosti na Septemba pekee mwaka 2016 ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa ugonjwa wa kimeta na takribani watu 322 waliugua Kimeta kati ya Mwezi Octoba 2015 na Novemba 2015.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Mwaka 2013 Bunge liliteua kamati ndogo ya tathimini ya operesheni tokomeza, kamati ile ilibaini kuwa kuna baadhi ya maeneo migogoro imekuwa ya muda mrefu kutokana tuhuma kuwa kuna baadhi ya mapori ya akiba na hifadhi hupanua mipaka yake bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika. Mifano iliyotolewa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Bunda yanayopanaka na Pori la Akiba la Grumeti, vijiji vya Kegonga na Masanga , pia maeneo ya Ulanga vijiji vya Iputi na Lupiro yakiwa ni baadhi tu ya maeneo ambayo migogoro imesababishwa na Mamlaka za Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Idara ya Wanyamapori ilibainika kukosa vitendea kazi kwa kuwa zana nyingi za ulinzi zilichukuliwa kutoka kwenye baadhi ya halmashauri kwa ajili ya Operesheni Tokomeza na hivyo kuathiri sana shughuli za kiulinzi ikiwemo kuwadhibiti wanyama waharibifu kama vile tembo wanaovamia mashamba ya wanavijijini. Uvamizi unaofanywa na wanyama waharibifu umesababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwauwa wanyama hao ili kuokoa mazao yao.
Mheshimiwa Spika,pamoja na hayo, serikali imekuwa ikiwakumbatia baadhi ya wawekezaji ambao wamekuwa chanzo au sehemu ya migogoro sugu ya wanavijiji wanaoishi maeneo ya hifadhi. Mfano, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 ilizungumzia kwa kina sana Historia ya mgogoro wa Loliondo uliodumu kwa takribani miaka 26. Mgogoro huu uliwahi kuundiwa kamati mbalimbali ili kutafuta suluhu mfano; kamati iliyoongozwa na Mheshimiwa Ndugai ilifuatilia mgogoro huu japokuwa taarifa yake haikusomwa Bungeni, na hivi karibuni kamati ya Waziri Mkuu iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambayo ilirudisha mrejesho kwa serikali pasipo wananchi kujua kinagaubaga na hatua mahususi zilizopendekezwa.
Mheshimiwa Spika, mifano hii inatoa picha ya wazi kuwa migogoro mingi imeendelea kuwepo kutokana na ripoti nyingi kuwa za siri na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo katika maamuzi. Ripoti hufanywa kuwa mali ya watu wachache badala ya mali ya umma. Mfano, katika ripoti mbalimbali za serikali, mashirika na taasisi binafsi pamoja na hotuba mbalimbali za Kambi Rasmi ya Upinzani zimezungumzia kwa kina watuhumiwa wakubwa wa mgogoro wa Loliondo ambapo kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC) ambayo imetuhumiwa kwa muda mrefu kuwa sehemu kubwa ya chanzo cha mgogoro katika Bonde Tengefu la Loliondo mpaka sasa haijatatuliwa kutokana na wananchi wa maeneo hayo kutoridhishwa. Kampuni ya Greenmile Co.Ltd imekuwa na kashfa nyingi na kuwa sehemu ya migogoro,kampuni ya Thomson Safaris imekuwa ikituhumiwa kama sehemu kuu ya mgogoro katika vijiji vilivyo ndani ya hifadhi ya Serengeti n.k
Mheshimiwa Spika, Pamoja na tuhuma nyingi za wazi dhidi ya baadhi ya wawekezaji ikiwa ni pamoja na kujenga uwanja mkubwa wa ndege katikati ya hifadhi, kujenga majengo ya kudumu katika mapitio ya wanyama, kuwa na mtandao binafsi wa simu kwa ushirikiano wa Arab Etisalat Emirates na kujichukulia sheria mkononi ambapo vipo vifo kadhaa viliwahi kuripotiwa kutokea kutokana na mgogoro ndani ya Pori hili Tengefu la Loliondo, uuwaji wa wanyama bila kuzingatia sheria za nchi na haki za wanyama n.k.
Mheshimiwa Spikajambo la kushangaza bado serikali haijaweza kuziwajibisha kampuni hizi. Hii ni mifano midogo tu kati ya migogoro mingi inayoendelea nchini ambapo serikali imeshindwa kuja na majibu na mikakati ya kudumu jambo ambalo linazua shaka kubwa na ari ya kutaka kujua ni nani hasa mnufaika wa migogoro ya namna hii? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha inaweka wazi ripoti zote za kamati maalum za zilizowahi kushughulikia migogoro hii, ili kutoa fursa kwa wawakilishi wa wananchi kujadili kwa uwazi ripoti hizo na hata kutoa mapendekezo. Jamii pia inapaswa kujua mambo yaliyo katika ripoti hizo na hatua stahiki zitakazochukuliwa. Mara nyingi tumeshuhudia ripoti nyingi zikiwa zimeghubikwa na usiri mkubwa na hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kujua yale yaliyo ndani ya ripoti hizo za kamati huku fedha nyingi zikitumika katika uchunguzi.
Uwekaji wa vigingi kama sehemu ya utatuzi wa migogoro
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu katika kutatua migorogo baina ya hifadhi na wananchi wanaoishi kandokando ya hifadhi ilikuwa ni kuweka vigingi (beacons) katika mipaka. Wizara ilipanga kuweka vigingi 27,942 ambapo mpaka sasa vigingi vilivyotolewa ni 9,357. Kati ya vigingi hivyo zaidi ya vigingi 324 tayari vimeng’olewa na watu wasiojulikana.
Mheshimiwa Spika, kung’olewa kwa vigingi hivi kunaonyesha wazi kuwa pengine wananchi hawajaridhika, au kushirikishwa katika ulinzi wa maeneo hayo. Vilevile, kuna uwezekano kukawa na watendaji wasio waaminifu. Hivyo basi, serikali ituambie mpaka sasa imebaini ni nani hasa mhusika wa uhujumu wa zoezi hilo ili sasa watu hawa wasiojulikana waliohamia mpaka kwenye sekta ya utalii waweze kujulikana.
Mheshimiwa Spika, suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu sana kwa ikolojia ya misitu,bahari, mbuga zetu kwani uwepo wa maji, hali nzuri ya hewa na udongo vinapekea mimea na wanyama kuzaliana na kuwa katika hali bora zaidi.
Mheshimiwa Spika, sote tunatambua umuhimu wa kutunza ikolojia na madhara makubwa yanayojitokeza nchini kwa sasa kutokana na kuharibu ikolojia ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi, kukauka kwa vyanzo vya maji, kuharibika kwa ardhi, kuongezeka kwa hewa ya ukaa n.k. Kwa kutambua madhara haya makubwa kwa binadamu na mimea serikali iliamua kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya kulinda mazingira pamoja na kuweka sheria na sera za kulinda mazingira nchini.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha na fedheha kubwa kwa serikali hii ya awamu ya tano kuwa mstari wa mbele katika kuyafuta yale mazuri tuliyoyaridhia kama taifa ili kulinda mazingira ya sasa na ya vizazi vijavyo. Nayasema haya kwa kuwa serikali hii ya awamu ya tano mapema mwaka jana ilifanya upembuzi katika kile walichokisema ni mpango wa serikali wa kuanzisha mradi mkubwa wa kuzalisha nishati ya umeme yaani Stiegler’s Gorge katika pori la akiba la Selous kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, hakuna mtu yoyote mwenye akili timamu asiyejua umuhimu wa Pori la Akiba la Selous na umuhimu wa kuilinda kwa wivu mkubwa ikolojia ya eneo hilo ambalo kwa kupitia mto Rufiji imekuwa ni chanzo kikubwa cha maji yanayotegemwa na binadamu, mimea, wanyamapori, samaki na mifugo. Pamoja na serikali kusema imefanya upembuzi yakinifu, ni vyema ikaamua kufanya mkakati wa tathimini ya mazingira kwa miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Spika, endapo chanzo hiki cha maji kitaharibiwa basi tujue hata umeme unaotaka kuzalishwa hautakuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo. Tunatambua umuhimu mkubwa wa upatikaji wa nishati ya umeme nchini , lakini serikali hii ya awamu ya tano itambue umuhimu mkubwa wa kuhifadhi vyanzo vya maji hususani chanzo hiki muhimu kwani bila maji hakuna uhai, bila maji hakuna umeme, bila maji hakuna chakula.
Mheshimiwa Spika, bado nchi yetu ina namna nyingi ya kuzalisha umeme katika maeneo mengi ambayo athari zake za kimazingira sio makubwa kama itakavyotokea kwenye chanzo hiki cha mto Rufiji. Pori la Akiba la Selous limekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya wananchi na ajira kutokana na utalii wa Southern Circuit. Mpaka sasa Pori hili limeorodheshwa katika maliasili zilizo hatarini kupotea kwa mujibu wamkataba wa Urithi wa Dunia kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya tembo na kuharibika kwa mapitio ya wanyama. Na endapo mradi huu utalazimishwa kufanyika basi tutambue athari kubwa ya kimazingira huko mbeleni nap engine kuweka kabisa kwa pori hili kwani uendeshaji wa mitambi hiyo ya umeme unaotumia maji husababisha joto la maji jambo ambalo ni hatari kwa baionuai .
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo mengi ambayo wananchi wamefukuzwa na wengine kuhamishwa kutokana na kulinda ikolojia ya maeneo hayo. Mfano, mpaka leo jamii ya Wamasai wanaoishi katika Pori la Serengeti, Ngorongoro na Pori tengefu la Loliondo wamekuwa katika mgogoro mkubwa na serikali na wawekezaji kutokana na kutakiwa kuhama katika maeneo yao ili kulinda baionuai na ikolojia ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuangalia upya mikakati ya kimazingira ya muda mrefu kabla ya kuanza kwa mradi huu. Serikali ikumbuke makosa makubwa iliyofanya katika kujenga mradi wa stesheni ya mabasi yaendayo kwa kasi (DART) ambao kwa sasa inaigharimu serikali kutokana tu na kufanya miradi ya namna hii bila kuangalia athari za muda mrefu za kimazingira.
Mheshimiwa Spika, sekta ya ufugaji wa nyuki imekuwa haifanyi vizuri kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokupewa kipaumbele ipasavyo. Miradi mingi inayoanzishwa na serikali imekuwa haifanyi vizuri na mingi imeshindwa kuendelea kutokana na kutotunzaji vizuri na ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG serikali ilitoa kiasi cha shilingi 104,072,000 (mil 104) kwa wafugaji 7 kwa kipindi cha miaka miwili lakini cha kushangaza mizinga mingi haina nyuki na miradi hiyo imesimama. Mfano, katika mizinga 150 iliyowekwa Manispaa ya Dodoma ni mizinga 7 tu yenye nyuki, katika halmashauri ya Kishapu mizinga 150 imewekwa mahali ambapo sio mazingira sahihi kwa mazalia ya nyuki na hivyo hakuna nyuki. Mradi huu wa Kishapu umegharimu takribani milioni 40. Katika halmashauri ya Misungwi kati ya mizinga 150 ni mizinga 14 tu ndio ilikuwa na nyuki kwa kipindi cha miaka miwili hivyo mizinga 136 haikuwa na nyuki huku mradi ukigharimu takribani shilingi milioni 20. Hii ni baadhi tu ya mifano mingine mingi ambapo fedha nyingi hutumika huku matokeo yakikosa tija kabisa.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri nchi yetu inakabiliwa na matatizo mengi sana ikiwepo ujinga, umaskini na maradhi. Matatizo haya yote tumeshindwa kuyatatua tangu tulipopata uhuru. Hivyo kuendelea kupoteza fedha nyingi kiasi hiki katika miradi isiyo na rudisho la faida (positive returns) maana yake ni kuendelea kuwaumiza Watanzania ..
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzania Bungeni inataka kujua ni hatua gani stahiki zimechukuliwa kwa uzembe huu mkubwa wa upotevu wa fedha za umma katika miradi inayogharimu mamilioni bila kuwa na faida yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Randama ya Wizara Fungu 69 ya Mwaka 2016/2017 fedha za miradi ya Maendeleo zilijumuisha 15,746,682,000 fedha za ndani na 2,000,000,000 fedha za nje. Kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 fedha za ndani zilizotolewa zilikuwa shilingi 11,353,250,489 na fedha za nje ni shilingi 16,593,530,813 hii ikiwa na maana kwamba fedha za ndani zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinaungua . Hii inaonyesha wazi kuwa makusanyanyo ya Wizara hii yanapungua kwa kuwa hata makadirio ya bajeti ya Mwaka wa Fedha 2018/2019 fedha za ndani zinakadiriwa kupungua kwani Wizara ina mpango wa kutenga shilingi 3,000,000,000 kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, hili ni tishio kubwa kwa Wizara kwani kuzidi kutegemea misaada kutoka kwa wahisani hakuwezi kamwe kunyanyua sekta hii. Tumekuwa tukisikia matamko mbalimbali ya Rais akisema kuwa hatutagemea wahisani. Ila hali halisi ni kuwa bajeti yetu imezidi kuwa tegemezi kwa takribani zaidi ya 50%. Na hii inaonyesha kuwa bado serikali haijakubali kuwekeza ipasavyo kaika sekta hii.
Mheshimiwa Spika, nashauri sote tutafute makala iliyoandikwa na Yende Nsizwazonke kutoka Africa Kusini inayosema “Natural resources: Are we blessed with a curse or cursed with a blessings?Maneno haya mazito yanaonyesha dhahiri tunahitaji taasisi imara (Strong institutions)ambapo mifumo ya utendaji kazi ndani ya Wizara inakuwa imara katika utendaji na sio kila wakati anapopewa nafasi kiongozi fulani hubadili sera na taratibu kwa kufuata matakwa yake binafsi. Kujenga taasisi zenye mifumo imara itasaidia kuvutia wawekezaji wengi zaidi, itapanua soko la utalii ndani na nje ya nchi, mapato ya ndani yataongezeka na hivyo tutakuwa tumepanua wigo wa fedha nyingi zaidi katika miradi ya maendeleo nchini.
[1]Tazama taarifa ya hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2017
[2] Fedha ya kitanzania imekokotolewa kwa kutumia viwango vya kubadilisha fedha (exchange rate) ya dola ya kimarekani kwa shilingi ya tanzania ambayo kwa sasa ni shilingi 2,200 kwa dola moja ya Marekani.
[3] Tazama Jedwali la Sura ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19
[4] Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG kuhusu Ukaguzi wa Fedha za Serikali Kuu ya Machi, 2018; Shilingi 4,421,750,000,000/= ni sawa na asilimia 4.14 ya Pato la Taifa ambalo kwa sasa ni shilingi 106,867,000,000,000/= ( trilioni 106 na bilioni 867).
[5] Tazama Hotuba ya Waziri Mkuu akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19 uk.9 aya ya 16.
[6] Ripoti kuu ya mwaka ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali, kuhusu taarifa za fedha za Taasisi za Serikali Kuu kwa mwaka unaoishia Tarehe 30 Juni ,2016. Machi 2017, uk.76
[7] Rejea Hotuba ya Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, wizara ya fedha 2017/18. Ofisi ya Msajili ya Hazina juu ya hali ya Kampuni ya Ndege.
[8] Hotuba ya waziri wa fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (MB), Taarifa ya Hali ya uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2017/18
[9] Hoja ya kutenga 1% ya GDP kwa shughuli za utafiti ililenga kupatia ufumbuzi maswali kama haya.
[10] How can Tanzania move, From poverty to prosperity? Edited by L.A. Msambichaka- J.K .Mduma – O .selejio- O.J Mashindano, pg 173
[11] Benki hii ilianzishwa kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia mapinduzi ya Kilimo . Uanzishwaji wa benki hii ilikuwa moja ya maazimio kumi ya KILIMO KWANZA yaliyofikiwa mwaka 2009.
[12] India ina diaspora wanaokadiriwa kufikia milioni 20 wanaoishi katika mataifa mbalimbali 70 duniani.
[13]https://www.mcc.gov/news-and-events/release/stmt-032816-tanzania-partnership-suspended
[14]http://www.mwananchi.co.tz/Marekani-yaipoka-Tanzania-Sh-1-4-trilioni/-/1596774/3139372/-/ewa7s1z/-/index.html
[15]https://tz.usembassy.gov/tanzania-at-the-crossroads/
[16] Mpango wa pili wa miaka mitano, aya ya 5.4.4.4
[17] National Five Year Development Plan 2016/17- 2020/21 uk 88,89 ,90
[18] Nationa five year development plan 2016/17 – 2020/21 pg 91- Tax revenue
[19] Haki Elimu-Education Budget Analysis Report, November 2017
[20] The Tanzanian Fisheries Sector-Challenges and Opportunities, September 2016
[21] Tazama Randama ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) uk. 110 – 113.
[22] Tazama Randama ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) uk.121 – 161
[23]http://www.businessinsider.com/the-us-military-is-responsible-for-almost-all-the-technology-in-your-iphone-2014-10?IR=T
[24] https://www.ippmedia.com/en/news/govt
[25]https://habarileo.co.tz/index ).
[26] Tazama Randama ya Wizara ya Afya Fungu 52 uk 51.
[27]http://www.mwananchi.co.tz/habari/Wilaya-vinara-kupima-VVU-kwa-hiari/1597578-3471102-5txvow/index.html
[28]www.avert.org/professionals/hiv/around-world/sub/saharan-africa/tanzania.
[29] Mpondo B, Gunda D, Kilonzo S. (2017): HIV Epidemic in Tanzania; The possible Role of the key population – TZ.
[30] Oloo S.(2010), Influence of sanitary towels on girls child performance in primary schools.A case of girl child in Tana River Nairobi.
[31]http://www.thecitizen.co.tz/magazine/success/How-lack-of-sanitary-pads-affects-school-girls/1843788-4274452-cfs9uhz/index.html
[32]Tazama Randama ya Wizara (fungu 52) uk. 193 ambapo Matumizi ya Kawaida ni shilingi 304,473,476,000/= na Matumizi ya Maendeleo ni shilingi 561,759,999,000/=
[33]http://www.thecitizen.co.tz/News/Business/works/Real-estate-business-has-come-a-long-way/3956094-4258346-3fusvo/index.html
[34] Ministry of Lands, Housing and Human Settlement, Habitat III National Report, 2016
[35] Ripoti ya Ufanisi ya CAG kuhusu usimamizi na utoaji wa viwanja ya Machi, 2018
[36]Lugoe. F, Dr; Esrf- Discussion paper No. 35- 2011, aligning and harmonizing the livestock and land policies of tanzania
[37]1. Tafiti elekezi – Daima, 2. Chanzo: PMC, SUA, Usaili – Julai 2012; 3. Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB (Framework Paper: Programme for Post –harvest Losses Reduction in Africa, 2010 – 2014) FAO/WB Workshop on Reducing PHL in grain supply chains in Africa: lessons learned and practical guidelines, FAO Hqrts. Rome, Italy, March 2010, 4. Uzoefu wa Tanzania wa kuelimisha wakulima wadogo jinsi ya kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa, Idara ya Uchumi na Biashara ya Kilimo – SUA, Oktoba 2012
[38] Construction Industry Policy-2003
[39] Ewura- Downstream Petroleum Sub Sector Performance Review Report for Year 2016
[40] MEM News Bulletin, toleo No. 24, Julai 11-17,2014
[41]IMF Country Report No. 18/11
[42] Gazeti la Mwananchi :Bulyamhulu yapunguza wafanyakazi 2,000
[43] Tazama Jedwali Na. 1 katika Randama ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Fungu 44) ya mwaka wa fedha 2016/17 uk. 21
[44]Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (National Five Year Development Plan, 2016/17 – 2020/21
[45] Economist Intelligence Unit report, generated on 17th January, 2018 uk. 5.
[46] Randama uk. 103
[47] IMF Country Report No. 18/11 The Seventh Review Under The Policy Support Instrument.
[48] BBC Swahili 20, Februari 2018
[49] Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na utalii
[50] Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii
[51] Rejea Randama ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2017/2018
[52] Gazeti Mtanzania tarehe 4,Septemba 2017
[53] BBC News 21st August 2015 Why Big game hunting is big business in South Africa.
[54] Rejea ripoti ya TAHOA tarehe 16-01-2018